KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA
DAYOSISI YA DODOMA
USHARIKA WA BETHELI - IPAGALA
BIDII YA VIJANA - MAFANIKIO YA KANISA
JUMAPILI JULAI 07, 2024
Sala:
Mungu, Baba wa Bwana wetu
Yesu Kristo. Wewe uliyetupa kibali cha kuiona siku ya leo. Wewe uliyetupa Neema
ya kushiriki ibada hii asubuhi ya leo. Tunakushukuru. Sema nasi kupitia neno
lako. Roho wako Mtakatifu akazungumze na Msharika mmoja mmoja juu ya lile
limpasalo kufanya katika maisha yake ya Ukristo kupitia neno hili. AMINA.
Bwana Yesu Kristo Asifiwe!
Muongozo wa Kanisa unasema kijana ni Msharika yeyote yule kuanzia anapomaliza kipaimara hadi miaka 40. Haya, Vijana wote tuliopo, Bwana Yesu Asifiwe!
Nimekuwa nikifurahishwa (na kuguswa) ninapowaangalia Wachungaji na Watumishi wengine wanapokuja kushiriki ibada na sisi wakitokea sharika na mikoa ya nje ya hapa. Wanapokuja mbele kujitambulisha husema, “Mimi ni Mtumishi XYZ, ninatokea Mkoa wa Arusha, usharika fulani. Ni mume wa mke mmoja na watoto watatu. Ninaleta kwenu salamu za upendo kutoka kwa Mchungaji wangu Kiongozi na familia yangu, wanafahamu nipo hapa na wanawapenda sana. Bwana Yesu asifiwe.”
Nilitamani sana siku moja nijitambulishe kwa namna hii. Lakini kwa leo, itoshe kujitambulisha kama Paulo; Mimi Ni Eben-ezer Exaud Mwende, mtumwa wa Yesu Kristo niliyepewa kibali na Neema kwa siku ya leo kusimama mbele yenu kuihubiri Habari Njema ya Mungu. Ni msharika wa hapa Betheli.
Bwana Wetu Yesu Kristo Asifiwe sana!
Neno tulilopewa kutafakari siku ya leo linatoka katika kitabu cha Mithali 21:5. Nitaomba nilisome tena kwa utaratibu;
“Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu,
Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji.”
[The plans of the diligent lead surely to plenty, but those of everyone who is hasty, surely to poverty]
Kwa lengo la uelewa wa pamoja, nitaomba kutoa tafsiri ya baadhi ya maneno mawili yaliyomo kwenye mstari huu;
Bidii (diligence) - Kufanya jambo ulilolipanga vyema kwa kujituma licha ya changamoto utakazokutana nazo (ikiwemo kukatishwa tamaa). Bidii si kuchapa kazi tu.
Bidii = Mipango thabiti + Kuchapa kazi (Proper Planning + Hard work)
Pupa (hasty) - kufanya mambo bila kufikiria vizuri
Bidii ukiweka kihesabu ili kuzaa mafanikio/utajiri;
Maono + Bidii [Mipango thabiti + Kuchapa kazi] = Mafanikio/Utajiri
Maono + Pupa = Hasara/Umaskini
Maisha ya Mwanadamu, ya Mkristo, yanaundwa na maeneo makubwa manne ya utajiri - Kimwili, Kijamii, Kiuchumi na Kiroho. Wale wa duniani wanaishia kwenye haya matatu ya mwanzo.
Uchumi: Kiuchumi, ni rahisi kulielewa na kulitafsiri neno hili la leo. Kwamba ukiwa na wazo bora (maono), ukilifanyia kazi kwa bidii, utapata utajiri. Ukikurupukia kazi/jambo utapata umaskini. Simple! Na sote tunajua hii ndiyo kanuni ya mafanikio kiuchumi au kifedha.
Mwili: Tumezoea kusikia kuwa Afya ni Utajiri! Au Utajiri wako wa kwanza ni afya yako! Infact, ili kuupata utajiri huu wa juu (uchumi) ni lazima kuanza na utajiri huu wa afya. Au kuufaidi utajiri huu wa uchumi, ni bora kuhakikisha unao utajiri wa afya; ya mwili na akili.
Neno la Mungu linasema miili yetu ni hekalu la Roho mtakatifu. Kwa maana hii, tuna wajibu wa kuitunza na kuhakikisha kwa kadri ya uwezo wetu tunakuwa na afya njema na nguvu za kufanya kazi.
Bidii kwenye eneo hili, ni kwenye kuhakikisha kila wakati tunajitunza. Kwa mfano kufanya mazoezi, kula vyakula vyenye afya, kupumzika vya kutosha, kutojihusisha na vitendo hatarishi kwa miili yetu, na kuhakikisha afya yetu ya akili iko vizuri. Na kwa kuzingatia maana tuliyoisema mwanzoni, kufanya hivi kila wakati licha ya vishawishi au changamoto tunazoweza kukukutana/kuwa nazo. Mathalan, ni rahisi kusema, ‘sasa kuna baridi sana aisee, siwezi kufanya mazoezi’ na kusahau kuwa unaweza kufanya mazoezi ya kutosha hata ukiwa ndani ya nyumba yako ikiwa umedhamiria tu.
Jamii: Mtu ni Watu! Au Utajiri wa Mtu ni Watu maana Binadamu si Kisiwa.
Kanuni yetu ni ile ile; ili kuupata utajiri wa jamii inayotuzunguka, hatuna budi kuweka bidii kuyatunza mahusiano yetu na jamii. Familia, Washarika, Wafanyakazi na Majirani. Tusiwe wepesi kusema, ‘mimi ndivyo nilivyo, mnizoee tu’ Tunakumbushwa kuweka bidii katika kuwa wanajamii bora. Tushiriki kwenye mambo ya kijamii bila kukosa na kujitoa kwa hali na mali. Tushiriki jamani;
ni suala la ulinzi - shiriki,
kikao cha mtaa - shiriki,
kazini - shiriki,
kanisani - shiriki...kwa bidii!
Kwa kadri ya Neema Mungu atakayokupa.
Kiroho:
Hivyo vitu vyote hapo juu vina kanuni zake ambazo ukizitilia bidii utaupata utajiri wake. Kanuni ambayo kwanza inaweza kuchukua siku nzima kuelezea kimojawapo tu; lakini pia ninaweza nisiwe na utaalamu wala mamlaka ya kuiongelea. Kuna shule tofauti tofauti pia juu ya hatua zake kwa kulingana na mtu mmoja mmoja.
Ni kweli, hatua za mkulima kufikia utajiri ni tofauti na za mwajiriwa. Hatua za mtu mwenye utapiamlo kufikia utajiri wa afya ni tofauti na ambazo mimi ninapaswa kuzifuata kuufikia utajiri wa afya.
Kiroho, na katika maisha yetu ya Ukristo, Bidii ya Mkristo inajengwa na kanuni zinazopatikana kwenye Kitabu kimoja TU - BIBLIA! Hakuna Rich dad-Poor dad, Hatua 7 za Mafanikio, au masharti ya Dr. Janabi.
Na Utajiri tunaoutazamia katika maisha yetu ya kiroho ni Kuuona Ufalme wa Mungu.
Bwana Yesu Asifiwe.
Ni utajiri usioharibika, usioibika, usioathiriwa na hali ya miili au uchumi wetu. Huo ndio utajiri mkuu tunaoitiwa kuweka bidii katika kuutafuta.
Ili uupate ule utajiri wa mwisho, wenye thamani kuliko mwingine wowote - sharti uweke bidii katika kumfahamu Yesu Kristo.
Hapa ndipo tunarudishwa kwenye neno la Zaburi la leo;
Kumfahamu Yesu Kristo ni kulifahamu Neno Lake;
Kumfahamu Yesu Kristo ni kulitii Neno Lake,
Kumfahamu Yesu Kristo ni kuliweka Neno Lake Mioyoni mwetu tusije tukamtenda dhambi,
Kumfahamu Yesu Kristo ni kuweka bidii katika kutenda wema;
Ni kuweka bidii katika kumcha Mungu;
Ni kuweka bidii katika kufuata maagizo yake;
Ni kuweka bidii katika kukuza na kutumia vipawa alivyokupatia katika kumtumikia na kuhudumia wengine;
Ni kuweka bidii katika upendo!
Taifa la Israeli wakati Mfalme Sulemani anaandika Methali hizi lilikuwa katika mafanikio na hali nzuri kiuchumi. Ni katika kipindi hiki Mungu alimruhusu mfalme Sulemani kumjengea yeye hekalu (1 Chr. 29)
Ukiangalia taifa la Israeli katika vitabu vya Wafalme na Mambo ya Nyakati na Waamuzi utaona mafanikio yake yalikuwa yanakuja na kuondoka kulingana na maamuzi ya viongozi na wana wa Israeli wenyewe. Viongozi na wananchi wakimtii Mungu na kutenda kama alivyowaelekeza, taifa lilibarikiwa. Viongozi na Wana wa Israeli wakigeuka na kuabudu miungu mingine, taifa liliharibikiwa.
Je, Mungu alikuwa Mungu Bado katika vipindi vyote viwili? Ndiyo! Bado alikuwa ni Mungu wa Israeli. Mungu alikuwa Mungu wakati wote ila mafanikio yao yalitegemea utayari wao wa kushirikiana na Mungu waliyesema wanamtegemea.
Mungu anashughulika na mambo yetu yote. Anatamani kutubariki, ameahidi kutupa utajiri wa hapa duniani na Mbinguni kama tukiweka bidii katika kumtumikia yeye.
Hakuna njia mbadala! Kama tunataka kufurahia mafanikio ya PSSF basi hatuna budi kufanya wajibu wetu na kuufanya kwa bidii. Ukifanya mapenzi yake utegemee Baraka zake kwenye kila utakaloweka mkono wako juu yake kulifanya.
Ninatamani ukitafakari maisha yako, uone mkono wako kwenye mafanikio yako? Usiwe tu umefanikiwa kwa sababu ya wema wa Mungu peke yake. Iwe ni Mungu alifanya kazi pamoja na wewe.
Pamoja na mapungufu yetu, bado anatubariki. Tumekuwa mashahidi wa neema, rehema, na huruma zake mara nyingi kuliko tunavyoweza kuhesabu. Lakini, kwa hili tusiujaribu wema wake kwa kuendelea kupuuzia neno lake, matakwa yake na njia zake; halafu bado tuendelee kutegemea Baraka zake kuja kwetu.
Kristo anatuita kuwa wafuasi wake na tunapokubali wito huo, kuuishi kwa bidii. Bidii hii ina sura ya;
- Jinsi unavyoishi binafsi: wewe ukiwa ndani kwako peke yako, mahali ambapo hakuna mtu anayekuona; unawaza nini? Unafanya nini? Unasema nini? Unaweka bidii kwenye kujiboresha kiakili na kiroho?
- Jinsi unavyoishi katika jamii inayokuzunguka (mtaani, kazini, kanisani, familia): Kristo anaonekana katika maisha yako? Unaweka bidii katika kuisafisha njia yako ili iwe na matunda yenye kuwavutia wengine kwa Kristo?
HATA HIVYO, kuishi kwa bidii katika Ukristo wetu hakumaanishi utafichwa usionekane, usikutane na changamoto, usikatishwe tamaa au usione ya dunia yenye kutamanisha macho na mwili, lakini kutaongeza uwezo wako wa kufanikiwa kuyashinda majaribu (Ps. 119:11).
Neno hili la leo, ni Methali iliyokaa kama sentensi ya jumla kwamba ukitenda kwa bidii utapata utajiri na ukitenda kwa pupa utakuwa maskini. Lakini tumeona wengi wanaofanya kazi kwa bidii wakipata hasara kwenye kazi zao na tumeona waovu, wavivu na watu wasio na mipango wakifanikiwa.
Jibu moja tunalipata 1 Petro 3:13 Ikiwa unajaribu kwa bidii kutenda mema, ni nani atakayetaka kukudhuru? Lakini hata ukiteseka kwa sababu ya kutenda yaliyo haki, unazo Baraka za Mungu (unayo heri). Sina maneno mazuri zaidi au matamu zaidi ya kukufariji unapokutana na vikwazo au majaribu au uhitaji na umetenda kwa bidii - lakini neno hili litutie moyo kuwa kuna eneo ambalo basi tukitia bidii hatutakaa tukwame.
Jibu la pili lipo katika mistari tofauti tofauti kwenye Biblia - Ayubu 9:24, Zaburi 17:14 na Zaburi 92:7; kwamba wa duniani wameshaupata utajiri wao hapa duniani, lakini sisi utajiri wa ufalme tuutazamiao ni wa thamani kuliko fedha na dhahabu ipoteayo.
Kuna kwaya waliimba wimbo unaoitwa ‘Fondogoo’. Kiitikio cha wimbo huo kitukumbushe juu ya hili;
♫♪Nani aonea wivu maendeleo ya wapendao dhambi,
Nazo raha walonazo wenye kudhulumu wasiojiweza,
Siwaangalie, wala usiwaige hata kuutamani ukwasi walonao,
Maana ujira washaupata, kwa kutafuta mambo ya ulimwengu,
Mwanadamu, mfu asiwe kioo chako,
Kielelezo ni Yesu Jemedari,
Tumwelekezee macho, mwanadamu situdanganye! ♪♫
…
Kanuni inayojirudia katika Kitabu cha Methali ni kwamba wale wanaochagua bidii katika kumtii na kumfuata Mungu watabarikiwa kwa njia nyingi: kwa maisha marefu (9:11); ustawi (2:20-22); furaha (3:13-18); utajiri (21:5); na wema wa Mungu (12:21). Wale wanaomkataa Yeye, kwa upande mwingine, watapata umaskini, aibu na kifo (21:5; 3:35; 10:21).
HITIMISHO:
Huenda upo hapa kanisani siku ya leo na umetafakari na kugundua moja kati ya yafuatayo kupitia neno hili;
- Umegundua hauna mahusiano na Kristo licha ya kumfahamu na kulifahamu neno lake
- Umegundua umeipenda dunia na/au umesongwa na mambo yake
- Umegundua kuwa haujafanya kwa bidii katika eneo mojawapo kati ya tuliyoyajadili;
o Hujaweka bidii kutunza afya na mwili wako kwani ni hekalu la Roho Mtakatifu
o Hujaweka bidii kujenga mahusiano na jamii inayokuzunguka - familia, ndugu, majirani, na wafanyakazi wenzako kiasi kwamba hawamuoni Kristo katika maisha yako
o Hujaweka bidii kwenye uchumi wako - hujamtolea Mungu iliyo haki yake, umepata mali zako kwa njia zisizo halali na kuilisha familia yako mapato ya udhalimu, umefuja mali, hujatumia kipawa alichokupa Mungu kadri ya uwezo wako,
o Lakini zaidi hujaweka bidii katika kumjua Mungu, kumtii na kulifuata neno lake
Mungu anasema na wewe leo, anasema kuwa “dunia inapita na tamaa zake zote zinapita”, anasema ni wakati sasa wa kuacha kufanya kwa kuzitegemea akili zako mwenyewe zinazopelekea kuchoka haraka, anataka kuwa na mahusiano kamili na wewe.
TAFAKURI:
Mstari wa mahubiri wa leo ni mfupi sana, ni rahisi kuukumbuka, “Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu, Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji.” Tumejua sifa za kumfanya Mkristo kuwa mwenye bidii na kuzaa matunda katika Kristo Yesu. Kila mmoja kwa nafsi yake, na mimi mwenyewe, ninajua mahali nilipopungukiwa. Usijilinganishe na mtu mwingine, jirani, mfanyakazi, ndugu. Unajua mahali unapopungukiwa, hujafanya bidii, hasa katika maisha yako ya Kiroho.
Ninaomba kwa leo, ibada hii tusimame sote. Naomba upige note za wimbo wa TMW 351 “Nataka Nimjue Yesu”, kila mmoja kwa dakika moja aseme neno kwa kinywa chake - anayetaka kumpokea Kristo, anayetaka kurekebisha mwenendo wake, anayetaka nguvu ya Roho Mtakatifu katika maeneo aliyoyaona anapungukiwa - ili sote tukaufikie utajiri ule usioharibika, Ufalme wa Mungu.
Sala:
Asante Mungu Baba kwa neno lako. Asante Mungu Baba kwa kusema nasi. Asante kwa Msharika yule anayesema anataka kuanza maisha mapya na wewe leo. Asante kwa Msharika yule anayetambua kuwa bila nguvu ya Roho Mtakatifu wako bidii yake ni bure. Asante kwa Msharika yule aliyepo hapa na ana eneo analokiri amepungukiwa hajafanya bidii kwalo. Ninakuomba Bwana Yesu, utusaidie. Roho Mtakatifu wako aendelee kusema na mioyo yetu na kutubadilisha mienendo yetu. Tukaenende kama wana wa Ufalme wa Mbinguni, tukiufurahia utajiri wa hapa duniani na ule wa ulimwengu ujao. Tusamehe pale tulipofanya kwa pupa, kwa uvivu au kutokufanya kabisa. Rejesha mahusiano nasi, tukujue vyema na kuweka bidii katika kuutafuta utajiri usioisha, usioharibika.
AMINA!
No comments:
Post a Comment