Tuesday, May 27, 2025

Rushwa ya Ngono Mashuleni

 

Vita Dhidi ya Rushwa ya Ngono Mashuleni

Siku za nyuma, mwaka 2024, kulizuka mjadala mkubwa sana kwenye mitandao ya jamii hasa twitter. Mjadala huu ulihusu rushwa ya ngono vyuoni baada ya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kukutwa na mwanafunzi hotelini. Sikubahatika kuiona hiyo video mpaka sasa lakini tukio hilo limeniwazisha na kuninyima amani kwa muda mrefu.

Wengi walitoa maoni yao kwenye mitandao hiyo na mimi nilijaribu kutoa ya kwangu hadi kufikia kutukanwa. Nilishtushwa na kusikitishwa kwa mambo mawili; kwanza, aliyenitukana ni mtu niliyekuwa nikimheshimu kitaaluma kama Mwanasheria na wakili msomi na niliheshimu maandishi yake, walau mtandaoni, maana kiuhalisia hatufahamiani. Lakini pili, ni kwa jinsi ambavyo hakutaka mjadala wa kistaarabu na kuishia kunitukana.

Hata hivyo, wahenga wanasema, ‘kuvunjika kwa koleo si mwisho wa uhunzi’. Mjadala huu bado umeendelea kuniwazisha.

Wapo waliosema kuwa lawama wapewe wahadhiri 100%, wapo waliosema lawama wapewe wanafunzi 100%, wapo waliokuwa na mtazamo wa 80/20% kila upande, na wapo waliosema ni 50/50%. Na kila kundi lilikuwa na sababu zake.

Ningependa kuanza na mfano aliotoa mmoja wa wachangiaji huko twitter, alisema, “Hawa wahadhiri wa kiume mnaowaona na kuwasema humu mitandaoni wanaonekana kama maharamia, wanapitia mambo magumu sana kwenye hii kazi ya kitaaluma hususani linapokuja suala la mwanafunzi wa kike, yasikieni tu. These girls of nowadays wana technicalities nyingi mno kwenye haya mambo.

Mwingine akaandika, “’Hawa mabinti usiwaone hivi aisee, kuna siku niliwahi letewa ofisini kwangu mashati mawili, saa, soksi, na suruali za kadeti za bei mbaya tu, halafu akaachiwa secretary wangu na maelezo kuwa akija Sir mpatie mzigo wangu’ jamaa yangu mmoja mhadhiri aliwahi nisimulia hii issue

Rushwa ya ngono mashuleni inalelewa na kukuzwa na wahadhiri wenyewe na si wanafunzi. Na hapa naomba niweke kumbukumbu sahihi kuwa rushwa ya ngono inafanywa na wahadhiri wa jinsi zote mbili, wa kiume na kike.

Voltaire, mwanafilosofia, aliwahi kusema, “With great power comes great responsibility.” Winston Churchill alirejea msemo huo pia akisema, “The price of greatness is responsibility.” Tafsiri sisisi inaweza kuwa, “Kwa kila mamlaka/ukubwa kuna wajibu wake.”

Kwa kusimamia maneno haya, ni dhahiri kuwa hakuna sababu inayomfanya au kumruhusu mhadhiri kuwa mwathirika (victim) wa rushwa ya ngono. Rushwa yoyote inatokana na mojawapo ya sababu zifuatazo;

-    Mtoaji wa rushwa kuwa na hitaji la kupewa kipaumbele dhidi ya wengine wenye sifa sawa au zaidi yake,

-    Mtoaji wa rushwa kutaka kuharakishiwa jambo,

-    Mtoaji wa rushwa kutaka upendeleo asioustahili, au

-    Mtoaji wa rushwa kutishiwa kunyimwa haki/stahiki yake asipotoa rushwa.

Kwa upande wa mpokeaji, atapokea tu endapo anachopewa kina manufaa kwake kwa wakati huo lakini hakimpi haki au faida yoyote ya moja kwa moja na kazi yake.

Kwa misingi hii, rushwa ya ngono mashuleni hutokea kwa; Mwalimu kumtaka mwanafunzi kimapenzi bila ridhaa ya mwanafunzi na hivyo mwanafunzi kushawishika kukubali kwa aidha kuchoka usumbufu, kutishiwa aidha kufeli au kupunguziwa alama za mitihani, AU mwanafunzi kumshawishi mhadhiri kuwa akimsaidia jambo lake lihusulo masomo yake, basi atamzawadia mwili wake kama shukrani.

Hivyo basi, tukitaka kutokomeza rushwa ya ngono vyuoni ni lazima tuwatake walio na mamlaka kuwajibika zaidi ya wanavyowajibika sasa. Tusimbebeshe lawama mwanafunzi kwa kuwa tu, alimpelekea mhadhiri zawadi. Kwa mamlaka aliyonayo alipaswa kukataa zawadi zile kwani alijua zina lengo gani. Tusimbebeshe lawama mwanafunzi eti kwa kuwa ‘inajulikana mwanafunzi mwenyewe ni malaya’. Kwani malaya akibakwa inaondoa kosa la jinai la kubaka kisa tu ni malaya? Tusipeleke lawama kwa mwanafunzi kuwa angekataa kwani angebakwa? Mimi ninajua mabinti waliopunguziwa alama kwenye mithani yao kwa kuwa tu walikataa kulala na Mwalimu. Tusimbebeshe mwanafunzi lawama eti kwakuwa ana zaidi ya miaka 18 hivyo ni makubaliano ya watu wazima.

Ni ukweli kuwa mtoaji na mpokeaji wa rushwa wote wana makosa.  Lakini tukianza kuwatengenezea visingizio wahadhiri hawa, tutakuwa tunadhoofisha vita hii. Tutakuwa tunataka kuhoji na kumfanya mwanafunzi kuwa mkosaji. Tuchukue kipimo cha Mwalimu Nyerere kuwa Mtumishi wa Umma hutakiwi hata kushukiwa kujihusisha na vitendo viovu kwenye jamii.

Tutengeneze njia nzuri na salama za wanafunzi wanaoombwa rushwa za ngono na walimu kuweza kutoa taarifa na taarifa hizo kufanyiwa uchunguzi usio na uonevu wala upendeleo dhidi ya malalamiko yao na itakapobainika kuwa ni kweli basi tuwe na sheria madhubuti kuhakikisha mhusika anaadhibiwa vikali ili iwe funzo kwake na wengine wenye tabia kama zake. Hii itaondoa hofu ya mhadhiri kuhisi atasingiziwa lakini pia itaondoa hofu ya mwanafunzi kuona kama atachukuliwa kama mkosaji akitoa taarifa (victimized). Zaidi sana italinda utu wa wote wawili tofauti na kinachoendelea sasa hivi cha kufumaniana kwenye vyumba vya hoteli.

Kwa namna yoyote, siondoi umuhimu wa elimu kwa vijana wetu wa vyuoni kuelimishwa juu ya kujikinga na vishawishi hivi kwa kufanya nafasi yao kwenye masomo yao, kuweza kusema hapana inayomaanisha hapana, na kujua njia sahihi za kutoa taarifa endapo itahitajika. Na elimu hii pia ianzie chini; kuwafunza watoto wetu kuwa waaminifu, kuwafundisha watoto wetu kukataa rushwa, kuwafundisha watoto wetu kujithamini, kujiheshimu, na kuwa na maadili yawapasayo kuyaishi endapo watakuwa wanafunzi au Wahadhiri au Watumishi mahali popote na kukumbwa na vishawishi kama hivi.

Mjadala huu uliibua maoni ya watu wengi kwenye sekta nyingine za kazi hasa sekta ya afya jambo ambalo hata mimi sikuwa nikilifahamu.  Lakini bado mtazamo wangu ni ule ule; tutengeneze njia salama ya kutoa taarifa na kuzichunguza kisha tuwe na sheria madhubuti zenye kutoa adhabu kali kwa wahusika wa rushwa hizi za ngono.

Hakuna, na narudia, hakuna kisingizio cha Mhadhiri, Mwalimu, Askari, Daktari, Mtumishi wa Umma kusema alishawishiwa kupewa rushwa ya ngono (na rushwa nyingine) na kwamba agawane lawama na mtoaji. Kwa kukubali nafasi na mamlaka uliyonayo, unao wajibu mkubwa zaidi kuitetea nafasi hiyo na kuitumikia kwa heshima na nidhamu kubwa.

Tukikubali kumtengenezea visingizio mhadhiri, basi tusimseme mtumishi mwingine yeyote anayeshawishika kupokea rushwa - ya aina yoyote ile - kwani nao kama walivyo wahadhiri, ni binadamu wenye tamaa za mwili na wanaweza kushawishika kwa fedha au kingono.

 

Wasalaam wapendwa,

Mentor.

No comments:

Post a Comment