.
.
Amini kwamba mi ni wako, we ni wangu, sitofanya chaguzi nyingine,
mi Mfalme we malkia wangu, sitowapa nafasi wengine,
We mwanga moyoni mwangu, mtamu kama senene,
Tanesco wakate kwangu, sitaki bili pengine!
.
.
Nasinzia nikikuwaza, ulipo u hali gani,
Naamka kwa kujikaza, ndotoni sipati amani,
Ni lini utaniliwaza, uitwe wangu mwandani,
Waseme kwa viambaza, yule kaka kapewa nini!
.
.
Lije jua ije mvua, we ndo kwangu kivuli amini,
Hata wakijisumbua, siwapi sukari yamini,
Hakika nasubiria, kwa hamu siku yakini,
Uwe mama familia, na kwangu mke makini!
.
.
Ni mengi ya kutamka, moyoni nayahifadhi,
Usiku nikiamka, naanza kuomba radhi,
Kabla pumzi jakatika, (nam)shukuru muumba ardhi,
Kunipa wewe hakika, kutibu yangu maradhi!
.
.
Unyayo naweka chini, wino nikautafute,
Niende hata porini, nisiandikie mate,
Nitapanda na mtini, niwajuze watu wote,
Mliyeuliza ni lini, leo amevishwa pete!
No comments:
Post a Comment