Wednesday, August 3, 2022

UPENDO NI TABIA (LOVE IS A BEHAVIOR)

 

UPENDO NI TABIA (LOVE IS A BEHAVIOR)

Tuanze na mfano:

Siku moja nilikuwa bar na wenzangu tunajipongeza kwa kazi nzuri za wiki. Meza ya pembeni yetu kulikuwa na mwanaume ambaye kwa mazungumzo yake ilionesha ni mtu mwenye familia. Katika mazungumzo yao alisema, “Nawapenda wanangu kufa.” Halafu baada ya kusema hayo akaendelea kuwaagizia wenzake vinywaji tena kwa kuwasisitizia waongeze na kwamba yeye atalipa. Aliagiza na nyama ya kuchoma. Alionesha kuwa na furaha siku ile. Muda mchache baada ya hayo niliyoyashuhudia kwake, niliona akisoma ujumbe kutoka kwenye simu yake kisha  akanza kulalamika. Alisema, “Argh wanawake wengine bwana, kwani watoto wakila maharage kila siku kuna shida gani. Walale njaa basi!” Wenzake walicheka. Kumbe ujumbe ule ulitoka kwa mkewe akihitaji fedha kwa ajili ya chakula.

Mara nyingi tukiwa kwenye mahusiano, tunavumilia mengi tunayofanyiwa na wenza wetu kwa kujiaminisha “Najua ananipenda!” Huwa hatujiulizi kwa nini ananifanyia haya anayoyafanya as long as “alisema/nahisi/aliniambia - ananipenda.”

UPENDO ni neno gumu kiasi kwa maana linatumika kwenye maeneo na vitu vingi. Tunasema tunaipenda YANGA au SIMBA. Neno hilo hilo tunalitumia tukielezea upendo wetu kwa pilau au siku hizi biryani. Halafu sasa tunatumia neno hilo hilo kuelezea tunavyowapenda watoto wetu na wenza wetu.

Unakumbuka kwenye Jiografia tuliwahi kufundishwa aina ya mawingu? Ziko aina 10 za mawingu zenye majina yake tofauti  kutegemea na aina ya wingu lililopo. Huenda tungetafuta neno tofauti kwa kila aina ya upendo tunaouongelea.

Lakini kwa kuwa hili linaweza lisiwezekane, hebu tujaribu kuwaza kama tungeutazama upendo kama TABIA kuliko hisia. Kwa sababu, kama upendo ni hisia, basi ni ngumu kufahamu wakati gani upendo ni wa kweli kwa kuwa huna njia ya kutambua hisia za mtu. Unaweza tu kufahamu mtu ana hisia gani kwa kuangalia tabia yake kwako. Kama ndivyo, kwa nini tusiende moja kwa moja kutumia neno upendo kama TABIA? Hivyo, mtu akikuonesha upendo kwa TABIA yake, basi inamaanisha anakupenda. Kama anaonesha TABIA mbaya, hakupendi. Na uzuri wa tabia, sio TENDO la siku moja, au wakati fulani.

Ukiwaza kwa njia hii, ni ngumu sana kudanganywa, kutumiwa, au kuumizwa. Ni rahisi mtu kusema upendo lakini kutenda tabia ya upendo huwezi.

Vivyo hivyo katika Biblia, 1 Wakorintho 13, inaongelea upendo. Ukisoma sifa zilizotajwa za upendo, zote zinaonesha ‘TABIA’ (behavior). Hivyo ukitaka kujua mwenza wako anakupenda angalia kama ana tabia zilizoainishwa.

Kuna mtu aliwahi kusema, kama una mwenza wako, chukua Biblia kisha fungua 1 Wakorintho 13:4-7. Kila penye neno UPENDO, weka jina la mwenza wako. Kwa mfano, mimi ninaitwa MENTOR, ikiwa mwenza wako ana jina kama langu fanya hivi;

Mentor <weka jina la mwenza wako> ni mvumilivu (patient),

Mentor ni mfadhili (kind),

Mentor hana wivu,

Mentor hana majivuno,

Mentor hana kiburi,

Mentor hadharau wengine,

Mentor hajipendelei,

Mentor hakasiriki upesi,

Mentor hakumbuki mabaya,

Mentor hafurahii mabaya,

Mentor hufurahia ukweli,

Mentor protects, trusts, hopes, perseveres!!!

Ikiwa katika TABIA zote hizi, kuna ambayo utaguna, basi jua Mentor hana uwezo wa kupenda kweli. Huenda anatamani kukupenda, lakini kama hajajifunza kuwa na tabia hizi kwa watu wengine, hawezi kuwa na tabia hizi kwako tu. Hakuna mtu mwenye upendo kwa mtu mmoja tu, kumbuka, upendo ni tabia. Zitazidi kwako, lakini utaiona hii tabia yake hata kwa jinsi anavyochangamana na wengine katika jamii.

UPENDO NI TABIA. Unaweza kupimwa kwa kuangalia TABIA ya mwenza wako kwako. Ukijiaminisha ni hisia (feeling), au maamuzi (decision), basi utaumizwa sana kwa kuwa hutakuwa na njia ya kupima hisia wala uamuzi wa mwenzio hata kama mdomoni anakuambia anakupenda.

Wasalaam wapendwa,

Mentor.

No comments:

Post a Comment