Tuesday, September 21, 2021

Huyu Ndiye! (Sehemu ya Pili)

 

Huyu Ndiye!

Sebastian:

Mimi alikuja siku moja jioni, baada ya chakula akaniambia, “Mume wangu! Ninajua nimekukosea, nisamehe. Nimekuwa na mahusiano ya kimapenzi na mfanyakazi mwenzangu. Niko tayari tuachane.”

Mh! Kwanza tukashtuka. Mbona Seba amebadilisha topic haraka hivi? Hata Morris hakuwa amemaliza hadithi yake vyema.

Mimi haikuwa rahisi hivyo.”  Aliendelea Seba.

Kwanza nikiwa Shule ya Msingi Kibo tulifahamiana na binti mmoja alikuwa akisoma Shule ya Msingi Kilimanjaro. Tulifahamiana kwenye michezo ya UMITASHUMTA. Nilipenda michezo lakini kukutana na Sia kuliongeza furaha ya wazo la kwenda kwenye michezo ile. Alikuwa akicheza mpira wa pete. Tulikuwa marafiki tukapendana kwa akili zetu za utoto. Tulimaliza shule ya msingi na mimi nilipangiwa Shule ya Old Moshi na yeye alipangwa Mawenzi. Sote ni kama tulikuwa shule ya kutwa kwani Old Moshi pamoja na kuwa ya bweni tulikuwa huru sana kutoka. Lakini pia tuliendelea kuwa kwenye timu za shule, mimi mpira, yeye mpira wa pete na sasa ni ngazi ya UMISETA. Uzuri, tulikuwa tukifanya vizuri pia kwenye masomo. Moyoni nilijua sikumpenda thabiti lakini tulikuwa watoto tuliodhani tunapendana. Baada ya kumaliza kidato cha nne, nilimpa Sia ujauzito na kwa bahati mbaya kwa kuwa baba yake Sia alikuwa Polisi pale CCP alihamishwa hivyo sikuhusishwa tena kwa suala la malezi ya mtoto yule wala kuonana na Sia.

Niliendelea na maisha na masomo na sikuwa na hamu na mahusiano tena. Nilikuwa nikiishi tu.

Tukiwa Chuo mwaka wa mwisho, wa nne, siku moja tulitoka kwenda klabu Posta, Billicanas. Tukiwa huko tulikutana na mabinti kadhaa na kuna ile hali mnajikuta mnapatana tu, tukawa tumekaa pamoja wote tunapiga stori huku tukisindikizwa na mziki. Binti huyu mmoja alikuwa akiongea na rafiki yangu zaidi. Baadaye tulikuja kugundua walikuwa wanafunzi wa chuo cha Ardhi, jirani zetu kabisa.

Siku moja tulikutana na huyu binti maeneo ya Chuo na kukaa kwenye vimbweta kuzungumza. Nakumbuka alisema, “yaani kuzungumza na wewe ni rahisi, ni kama nimekufahamu miaka mingi wakati ni mwezi uliopita tu tulifahamiana.”

Sikuchukulia maneno yale kwa uzito. Kwanza sikuwa na wazo la kuwa na mahusiano kabisa pamoja na kuwa nilikuwa ninamaliza Chuo mwezi unaofuata. Nilikuwa nampotezea ingawa alijitahidi kuwa ananitafuta.

Hata baada ya kumaliza Chuo nilibaki Dar es salaam. Nilikuwa natamani kuanzisha kampuni yangu ya elektroniki. Wakati huo pia nilianza kujifunza ‘computer programming’ ili kuongeza wigo wa kazi nitazoweza kufanya. Kwa kuwa wazazi hawakuwa na uwezo sana sikuweza kuwategemea hivyo ilinibidi nitafute kazi ya kuajiriwa, mahali pa kujishikiza wakati ninatafuta mtaji wa kampuni yangu.

Nilikuwa ninaishi nyumba ya kupanga. Siku moja nilishangaa Polisi wamevamia nyumbani na kulazimisha kunisachi kwamba wamepata taarifa kuwa kuna mali za wizi kwenye hiyo nyumba. Baada ya kuwaruhusu wakague na kunichukua maelezo niliwabembeleza sana wasinipeleke kituoni usiku ule kwani ingemaanisha kesho yake nisingeweza kwenda kazini.  Bado nilikuwa na hofu kuwa pamoja na kuwa hawakukuta chochote cha wizi nyumbani kwangu, mwajiri wangu akipata taarifa hizi anaweza kunifukuza kazi. Baada ya kuwabembeleza na kukataa kuniachia hivi hivi, niliomba kupiga simu.

Nilinyanyua Motorola yangu na kumpigia mtu wa kwanza kunijia kichwani kwangu, yule binti, ambaye pamoja na kumpotezea alikuwa akinitafuta mara kwa mara. Alikuja mara moja nilipokuwa nimepanga na kuwatoa askari wale. Mpaka leo sijawahi kujua aliwapa kiasi gani kwani alikataa kuniambia ili nimrudishie fedha yake baadaye. Baada ya pale ndipo nilikumbuka kuwapigia wazazi wangu na kuwalezea mkasa ule.

Alipofika yule binti, hofu yote iliniondoka. Ghafla nilipata amani na nilijua mambo yatakuwa shwari.

Miezi michache baadaye nilimchumbia na hatimaye kuoana. Alikuwa kwangu msaada na mfariji. Nilijisikia amani kama siku ile, siku ambapo mama yangu alifariki kwa ajali nikiwa na miaka 30. Miaka mitatu baadaye alikuwa pembeni yangu baba yangu alipofikia mwisho wa vita yake na kansa, ugonjwa ambao ulimsumbua kwa muda mrefu na kwa akili za binadamu tulidhani angefariki kabla ya mama. Kwa kila tukio kubwa lililonikuta, alikuwepo pembeni yangu.

Oh hadi wakati ninaenda kumchukua mwanangu Joel kutoka kwa mama yake alikuwa na mimi. Hii ilikuwa baada ya kumueleza na yeye ndiye aliyefuatilia hadi kupata mawasiliano na kujua walipokuwa.

Alikuwa pembeni yangu kwenye kila hatua ya maisha na kazi, akinisapoti bila kulalamika wala kupiga kelele hadi siku moja aliporudi nyumbani kutoka kazini na kuniambia kuwa amekuwa na mahusiano ya kimapenzi na mfanyakazi mwenzake na alikuwa tayari, asingenilaumu, kama ningempa talaka.

Niliumia. Sikuwahi kuwaza kama kuna siku mwanamke huyu atatamka maneno haya kwangu. Sikuwaza ambavyo ningeishi bila huyu binti wa watu ambaye sasa tulikuwa na familia naye. Ghafla nikakumbuka nyakati zote nilipopatwa na simanzi na hofu, mtu pekee aliyeweza kunifanya nijisikie nafuu ni mtu huyu huyu aliyesimama mbele yangu akiuponda moyo wangu.

Nilijua kuwa nilikuwa sehemu kubwa ya uharibifu uliotokea kwenye nyumba yangu. Nilikuwa nikifanya kazi mbili; ya kuajiriwa na kuendesha kampuni yangu. Wakati huo huo nilikuwa nafundisha kwa muda wa ziada chuo cha DIT Posta. Mke wangu kwa sehemu kubwa ni kama alikuwa ‘single mother’. Ukiacha kuwa nilikuwa ninatoa fedha za matumizi nyumbani, sikuwa na mchango mwingine wowote. Sikuwa mlevi au mkorofi ila sikuwa nashinda nyumbani.

Sikumjibu chochote usiku ule. Nilienda kitandani nikitafakari sana, nililia pia. Upande mmoja wa moyo ulimkasirikia mke wangu kwa kile alichokifanya na upande wa pili ulinizodoa kuwa mimi mwenyewe ndiye chanzo cha yote haya. Nilijua maamuzi yake hayakuwa asilimia mia makosa yake.

Kesho yake nikiwa kazini nilimpigia simu na kumueleza kuwa naelewa maamuzi aliyoyafanya na hisia alizopitia kufikia maamuzi yale. Pamoja na kuwa nisingetamani aondoke lakini sikuwa na cha kufanya kuhakikisha familia yangu inabaki pamoja bila yeye kuridhia kubaki. Niliishia kumuomba anifundishe kupika maana ni jambo alilokuwa akilifanya peke yake.

Msicheke lakini hadi wakati ule sikuwa najua kupika chakula chochote zaidi ya chai. Aliitikia lakini nilihisi kama ninayechelewesha matokeo tu na kwamba hakuna kitakachobadilika. Siku ile nililala kwa Edwin yule rafiki yangu aliyegoma kuoa.

Wiki moja baadaye nilirudi nyumbani na kukuta kikaratasi chumbani kwangu – wiki hii yote kila mtu alikuwa akilala chumba chake. Aliandika kuwa anatamani tujaribu kuijenga familia yetu tena. Baada ya wiki mbili tulijikuta sote tumerudi chumbani kwetu na hali imekuwa hivyo mpaka sasa.

Wakati Seba anamalizia mkasa wake - maana sio jibu tena, muda ulikuwa umeenda sana na tulitakiwa kwenda kupumzika kwa ajili ya shughuli ya siku iliyofuata. Hatukupata hata muda wa kumsikiliza Kelvin, bwana harusi mtarajiwa, atueleze nini hasa au wakati gani alijua kuwa Barbara, mke wake mtarajiwa, ndiye aliyedhamiria kufunga naye pingu za maisha.

Leo, 20 Septemba 2021 saa 7:14 usiku

Nimekumbuka miaka saba iliyopita na kuwaza kama nilipata jibu nililokuwa ninalitafuta kutoka kwenye hadithi zao. Huenda kwangu itakuja tofauti. Lakini sitamani yawe kama Seba. Mtu yule yule aliyekuwa bega lako kukushikilia ulipopatwa ma maswaibu ndiye mtu yule yule aliyekuvunja na kushusha chini kabisa. Akili yangu mara nyingi inaenda miaka saba iliyopita na inaumia. Haikumbuki hadithi ya Morris wala ya Phillip. Bali pamoja na yote yaliyompata Seba alimalizia kwa kusema hawazi kumbadilisha mke wake na mwanamke mwingine yeyote na kwamba ‘huyu ndiye’. Ndiye mwanamke anayemfanya awe mume, baba, na mwanaume bora kila siku.

Wasalaam wapendwa,

Mentor.

No comments:

Post a Comment