NAKUMBUKA
Genesis 2:24 “Therefore a
man leaves his father and his mother and cleaves to his
wife, and they become one flesh.”
Kijijini...1961
Nakumbuka enzi za
mwalimu! Ndiyo kwanza tulikuwa tumepata uhuru nami ndiyo nilikuwa najiunga na
darasa la kwanza. Hayakuwa maisha marahisi kwani pamoja na kubahatika kwenda
shule bado kulikuwa na majukumu mengi nyumbani.
Kabla ya kutoka
nyumbani ni lazima ukamue ng’ombe, utoe samadi na kuwalisha ng’ombe na mifugo
yote mliyonayo kisha uondoke nusu saa kabla ili kufika shule.
Shule ilikuwa mbali
na nyumbani kiasi kwamba nyakati za mvua mara nyingi tulishawishika kutoroka
shule. Kwa bahati mbaya tangu nikiwa darasa la nne nilikuwa mtunza stoo ya
shule hivyo kunifanya nishindwe kutega au kutoroka shule.
Sitosahau siku
madaftari yangu yalipodumbukia mtoni wakati nikienda shule. Mvua ilikuwa
ikinyesha hivyo njia ilikuwa ikiteleza hasa ukizingatia hatukuwa tukivaa viatu.
Nilifika kwenye daraja ambalo lilikuwa ni mbao moja ndefu nyembamba. Kutokana
na waliopita awali kutolea matope kwenye mbao ile sikujua hasa upana wake hivyo
kujikuta nimekanyaga sehemu yenye tope na kuteleza. Nilibahatika kujishika
mwenyewe na bahati mbaya kuyaachia madaftari yangu na yakaangukia mtoni. Sijawahi
kulia maishani mwangu kama siku ile.
Ukitoka shule unafikia
kukata kuni kwa ajili ya kupikia ikiwa ni pamoja na kupika chakula cha jioni
kama ni zamu yako au kwenda kukata majani au kukamua na kulisha ng’ombe
kutegemea na zamu yako. Ulikuwa na bahati kama mlizaliwa wengi.
Nakumbuka tulikuwa
tukibeba mahindi ya kukaanga tunayafunga vyema kwenye jani la mgomba
kisha tunaenda kuyaweka pembeni ya mto ambapo maji hayapiti mengi. Basi saa nne
– muda wa mapumziko – utaona kila mtoto akikimbia kuelekea kunako mto. Mahindi
yale yanakuwa yamekwisha kulainika na yanakuwa matamu sana.
Safari moja
ikaanzisha nyingine nami nikachaguliwa kwenda shule ya upili. Maisha yalikuwa
ya dhiki ingawa kwa kipindi kile tuliona sawa tu. Ni bahati kuchaguliwa
kujiunga na shule ya upili maana watu walichaguliwa kulingana na idadi ya shule
zilizokuwepo kwani waliofaulu walikuwa wengi kuliko shule zilizokuwepo.
Tulijitahidi kusoma
sana tuwapo shule maana wakati wa likizo tulikwenda nyumbani kwetu na wazazi
hawakuelewa wakikuona unashika kitabu. Ungeweza kusoma usiku kama kuna mbalamwezi
kwani wasingeruhusu umalize mafuta ya taa kusoma magazeti (baba yangu alikuwa
akiita madaftari yangu magazeti).
Nilibahatika kufaulu
vizuri na kuchaguliwa kwenda kusoma shule ya upili ya Azania kwa ajili ya
kidato cha tano na sita.
Azania Sekondari, Dar es salaam
Kutoka kijiji
nilichozaliwa, ni vijana watatu tu ambao tulibahatika kufikia ngazi hii na
kutoka shule niliyotoka ni vijana 10 tu tulioweza kuchagulia kuendelea na
masomo. Nilijiapiza kutokuipoteza nafasi ile. Ndiyo nilikuwa na akili lakini
pia nilitambua kuwa wengi wa waliobaki walikuwa sawa na mimi ila uhaba wa shule
ndio uliofanya wao wabaki na mimi niendelee.
Ni wakati wa vipindi
vya UKWATA ambapo tuliungana na shule ya jirani ya Jangwani.
Nilimuona binti!
Alikuwa ni wale
wadada viongozi wa UKWATA na kwaya na hakuna jinsi ungeweza kumweleza lolote kuhusu
mahusiano akakukisiliza, lakini alikuwa mzuri, ukweli na usemwe.
Nilijitahidi
tukazoeana na ilibidi niridhike na cheo nilichopewa cha ‘kaka’. Kwa kuwa pia
tulikuwa tumetokea mkoa mmoja mimi ndiye nilikuwa nikiwasindikiza kwenda mjini
au sehemu nyingine nje ya shule ili wasipate shida. Kwa kipindi kile
niliridhika na kufanya yote hayo ili tu niwe karibu na dada huyu. Sikuwahi kuwa
na mahusiano yoyote na binti wa kike hasa ukizingatia malezi yetu nyumbani na
kanisani.
Nilikuwa na suruali
moja tu – ukiacha sare ya shule – ambayo ndiyo nilikuwa nikiivaa tunapoenda
mjini au kwenye matukio yoyote nje ya shule, na shati langu lekundu lakini
nilijitahidi sana kuwa msafi. Nilikuwa nikizifua kila ninapotoka kwenye
mizunguko kisha kuzikunja vyema na kuziweka chini ya godoro langu hadi wakati
mwingine wa mtoko.
Maisha yalienda
haraka na miaka miwili iliisha na kumaliza elimu yangu ya sekondari.
Kipindi hiki
ulitakiwa kwenda JKT kwa mwaka mmoja kisha mwaka mwingine ufanye kazi ndipo
uende chuo kikuu. Nilipangiwa Kambi ya Makutupora, Dodoma.
Kutokana na kufanya
kazi nyingi nilipokuwa nyumbani, kijijini, nilipata wakati mwepesi sana
nilipokuwa kambini hapo kwani walipotaka fundi waashi nilikuwepo, wajenzi, kazi
zote za mikono na hata Sanaa nilikuwepo. Hivyo mara nyingi watu wawapo kwenye
gwaride au kazi za ‘mahovyohovyo’ mimi nilikuwa bize napaka rangi Ikulu ya
Chamwino.
Tulikuwa pia tukifanya
kazi binafsi kwenye nyumba za maafande hivyo kuweza kupata kipato cha ziada
ingawa nakumbuka bado tulikuwa tukipewa fedha tulipokuwa kambini.
Nilimuona binti!
Huyu alikuwa binti wa
‘saa-meja’ yaani RSM wa kambi yetu ya Makutopora. Alikuwa kidato cha tano
kipindi kile ila alikuwa mrembo sana. Alikuwa akisoma shule ya kutwa.
Tulionana siku ambayo
nilikuwa nikirekebisha mfumo wa umeme nyumbani kwao ambapo alitoka shuleni na
kunikuta sebuleni peke yangu. Tulisalimiana kwa aibu – yeye kwa kuwa ni binti wa
kike na mimi kwa sababu ya uzuri wake, aisee kalikuwa karembo kweli kweli na
kalikuwa kameanza kujipodoa basi kalikuwa kanang’aa kweli kweli. Ingawa alikuwa
ndiyo ametoka shule lakini alikuwa msafi utadhani alikuwa ndiyo anaenda, na
sketi yake ya marinda, daah nakumbuka vyema.
Tuliendelea kuonana
mara kwa mara kwa kuwa mara nyingi kama tulikuwa tunaenda kufanya kazi kambini
ni lazima tukapige ripoti kwa RSM kisha atupeleke. Jambo moja nililompendea RSM
ni hakuwa akichukua pesa zetu, alitupa fedha zote kama tulivyopatana na afande
tuliyemsaidia kazi yake – alikuwa mzee mmoja mwaminifu sana.
Nakumbuka RSM alikuwa akitamka maneno ambayo yalikuwa yakituchekesha sana, “Kila mtu avae green vesti ya kijani!”
mara nyingi alikuwa akitumarisha kabla hatujaenda kambini.
Maisha yalienda
haraka na tulikaribia kumaliza mafunzo yetu na kurudi kijijini kwetu. Ni wazo
hili ovu lililonifanya kuruka hatua kwani nilihisi baada ya mimi kuondoka
sitokuja tena kukutana na binti yule mtoto wa RSM. Nilijisemea moyoni, japo tu ‘nimuonje’
walau hata nikiondoka basi nisiwe nimekosa vyote.
Hivyo wiki za mwisho
za mafunzo nilijitahidi kuongeza ukaribu na yeye na kumuonesha nilikuwa
nikimpenda kweli. Ilikuwa muhimu kwangu kumuonesha nampenda kwani ingerahisisha
uongo/ushawishi wangu kuwa ili kuonesha kuwa naye ananipenda basi anipe ‘salome’
wake.
Sitaelezea kwa kina
lakini ilikuwa ni siku ya passing-out na kwa kuwa mimi nilikuwa mtu wa kukaba
chaka – ingawa nilikuwa vyema kwenye vitengo vyote vya kijeshi - sikuwepo
kwenye gwaride la kufunga mafunzo ambapo baba yake alikuwa ndiye RSM wa gwaride…
Baada ya mwaka mmoja wa
JKT nilichaguliwa kuendelea na kozi ya JKT. Hivyo nilibaki kambini pale na
kuendeleza mahusiano yangu na binti huyu ambapo tuliahidiana mengi sana hasa
atakapomaliza shule. Tulipanga akimaliza shule tukajitambulishe kwa wazazi wetu
na kwamba wakiridhia basi nimuoe kabisa.
Tuliingia kwenye
uhusiano wetu kwa kupitia mlango usio lakini kwa kulazimisha tulifunga –nilifunga
– macho na kuendelea. Kumbe mwenzangu hakufurahishwa na jinsi tulivyoanza
uhusiano wetu. Hivyo wakati mimi namaliza mwaka mmoja wa kuwa JKT nikiwa sasa
Lance Koplo, alihitimisha mahusiano yetu.
Ingawa niliumia sana
kwani nilikuwa nikimpenda alinirahisishia maamuzi yangu juu ya maisha yangu. Tulikuwa
tumeahidiwa kuwa tutapelekwa shule na Jeshi kama tukiridhia kubaki. Kutokana na
maumivu niliyokuwa nayo niliamua kutokuendelea na Jeshi na kwenda Chuo Kikuu.
Chuo Kikuu cha Dar es salaam
Nilifika chuoni
nikiwa fedha za kutosha hivyo ukiongezea na kwamba tulikuwa tukipewa kila kitu
maisha yangu yalikuwa nafuu kuliko wenzetu wengi.
Sasa nilikuwa na
suruali na mashati ya kutosha kubadilisha na nilikuwa sasa kijana barobaro
kweli kweli.
Kwa muda nilisahau
nilikotoka na kuendekeza anasa za mjini. Ingawa nilikuwa nikienda bado kwenye
vipindi vya dini lakini dhamira yangu haikuwa kamili. Room mate wangu hasa
alichangia mimi kwenda kwenye vipindi hivyo ingawa yeye alikwenda kwa nia moja
tu. Watu walikuwa wakituita mapacha watuonapo ingawa mioyoni tulijua jinsi
ambavyo tabia zetu zilikuwa kama Kaskazi na kusi…nakumbuka sana nikimpiga ‘exile’.
Ukitukuta kwenye
vipindi utasema hawa ndio vijana wa Bwana. Tulikuwa tukikaa mbele wakati wote.
Kuna kipindi wadada ilibidi watuulize, “Jamani
nyie kina kaka, ina maana hamtuoni?” Tulipowauliza kwanini walisema hivyo
walijibu, “Yani nyie mkija mnakaa mbele
tu na mkipiga makofi mnaangalia juu tu.”
Itoshe kusema
nilifanya mengi yasiyopendeza. Kwa kipindi kile nilisingizia kuumizwa na mtoto
wa RSM hivyo sikuona umuhimu wa kuwa na mahusiano ya kudumu. Sikuwa na hofu ya
kuchelewa kuoa au kukosa mtu wa kumuoa kwani nyumbani wazazi walikuwa
wamenichagulia binti wa kumuoa.
Ingawa sikuwa
nikimpenda lakini nilijua yupo tu. Kwa bahati mbaya alikuwa ni kati ya wale
watatu tuliofaulu kwenye sekondari na baada ya hapo alikwenda shule ya ualimu
na kurudi kufundisha shule ya msingi pale kijijini.
Nakumbuka nikiwa
mwaka wa mwisho nilikutana na binti mmoja aliyekuwa ndiyo kwanza anaanza mwaka
wake wa kwanza wa masomo. Huyu alinivutia kwanza kwa umbo lake matata lakini
kadri nilivyozidi kumfahamu niligundua hata tabia yake ya ndani ilikuwa ya
kuridhisha japo kwa kuanzia.
Sikumlazia damu
nikaona japo nijaribu huenda akawa ndiye. Kama kawaida yangu ya kutokuwa na uvumilivu,
naye pia nilitumia mlango usio sahihi kuanza naye mahusiano.
Mahusiano yetu
yalikuwa na kwa kiasi room mate wangu alipumua maana alikuwa amezoea kukutana
na wadada tofauti tofauti chumbani.
Ni hadi wakati
nilipokaribia kumaliza masomo yangu ndipo binti huyu alipoanza mikasa yake
naye. Sikujua shida hasa ni nini lakini kidogo kidogo alianza kubadilika.
Sikugundua hili mapema nikajitahidi kuvumilia.
Siku moja, Jumapili
moja.
Baada ya kutoka
kanisani nilirudi chumbani kwangu na baada ya kufanya usafi na maandalizi
madogo madogo nlielekea chumbani cha rafiki yangu huyu. Mwenzake wanayeishi
naye chumbani alikuwa amekwenda kuwasalimia wazazi wake maana yeye kwa bahati
nzuri alikuwa mwenyeji wa jijini hapa.
Baada ya kuandaa chai
tulikaa tukinywa huku tukiongea haya na yale kuhusu maisha na masomo. Baadaye
tulikubaliana tutoke tukatembee na kupata chakula cha mchana nje kisha ndipo
turudi.
Kabla ya kutoka
nakumbuka alikuja rafiki yake kipenzi ambaye walitoka naye kijiji kimoja. Baada
ya salamu alimwambia kuwa kaka yake alikuwa amekuja kumtembelea na alitaka aje
kumuona. Tulimjulisha kuwa kwa kuwa tunashuka chini basi tutapitia chumbani kwake
kumsalimia.
Tulitoka kwenda
kutembea na kisha kurudi baadaye jioni. Ilikuwa ni siku njema ambayo
haikustahili kuisha jinsi ilivyoisha.
Nakumbuka akitoa nguo
zake ambazo alipanga kuzivaa kesho yake darasani huku akilalamika gauni lake
alipendalo lilikuwa limefumuka kwa pembeni. Wakati akinieleza hayo, rafiki yake
yule alirudi tena na kumuita nje.
Baada ya maongezi yao mafupi alirudi ndani na
kuniambia kuwa kaka yake amelalamika kuwa tumemchomesha mahindi kutusubiri
(kumsubiri) na hakwenda.
Nikamuuliza kama alimwambia kuwa tulipitia kwake
wakati tunakwenda na hata wakati tunarudi na hawakuwepo. Akanijibu ‘ndiyo’. Hivyo nikamwambia akae atulie
maana si makosa yake.
Baada ya dakika
chache tena mlango wake uligongwa na akatoka nje kuongea na mgeni mpya ambaye
sikumjua kwa kipindi hicho.
Kwa kuwa nilibaki
ndani peke yangu nilijihisi mpweke hivyo kutaka kujiweka busy nilichukua uzi na
sindano na kuanza kurudishia sehmu ile iliyofumuka ya gauni lake. Haikuwa kazi
rahisi maana lilikuwa gauni lile la utelezi lenye layer nyingine kama mbili
ndani.
Ni hadi aliporudi
ndani ndipo nilipogundua kuwa alikuwa ametoka kwa zaidi ya dakika 50. Sikuwa
nimewaza lolote baya hadi nilipomtazama machoni. Sikuhitaji kuuliza sana ili
kugundua alikotoka hakukuwa na jema lolote. Hata hivyo nlikuwa mpole kijana wa
kiume wa Kimachame mimi na kumsikiliza.
Ningelikuwa sijasoma,
au Mkurya (sina maana mbaya) basi ile siku ingekuwa mbaya sana kwake.
Mwaka mmoja baadaye…
Nikiwa sina hili wala
lile nikuwa nikisoma kitabu cha I Married
You – Walter Trobisch. Nanukuu;
SEX IS NO TEST OF
LOVE
If a couple
want to use the sex act in order to know whether they love each other, one has
to ask them:
“Do you
love each other so little?”
If both of them think: “Tonight
we must have sex - otherwise my partner will think that I don't love him or
that he does not love me,” the fear of a possible failure is sufficient to
prevent the success of the experiment.
Sex is no test of love, for it is precisely the very thing that one
wants to test which is destroyed by the testing.
Try to observe yourself when you
go to sleep. Either you observe
yourself, then you don't fall asleep. Or
you fall asleep, and then you haven't observed yourself. The same is true about sex as a test of
love. Either you test, then you don't
love. Or you love, then you don't
test. For its own sake, love needs to
wait with its physical expression until it can be included in the dynamism of
the triangle.
This waiting is usually harder
for the young man than for the girl.
Therefore, the girl has to help the young man here, who, because of his
natural impetuousness, is more tempted to aim short of the goal. The first help she can give him is to
learn how to say 'no' without wounding, how to refuse without breaking
off. This is an art.
Kwa majonzi nilijiona
mimi. Jinsi nilivyojitahidi kuingia kwenye mahusiano mengi kwa kupitia mlango usio
sahihi wa ‘sex’. Nikaelewa kuwa kumbe si makosa yao yaliyofanya tuachane, au makosa
yangu...lakini ni kwa kuwa tulikosea msingi wa kuingilia.
Nakumbuka nikimfuata
pacha wangu ambaye kwa bahati tulikuwa wote tukifanya kazi sehemu moja na
kumueleza nilichokisoma na kwamba nilikuwa na nia ya kubadilika.
Alikuwa na furaha
kuliko maelezo na sikujua sababu hadi aliponyanyuka na kuingia chumbani ambapo
alitoka na bahasha ambayo ilikwisha kufunguliwa.
Ilikuwa imeandikwa
majina yetu mawili.
Niliifungua na kuanza
kuisoma kimya kimya;
S.L. P. **,
Morogoro.
Kaka Mentor,
Nakusalimu kwa jina la Bwana wetu mpendwa Yesu
Kristo.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea vyema na
kumtumikia Bwana katika maisha yako.
Nimefurahi kupata barua yako ambayo uliniandikia
ingawa nilichelewa kuipata kwani nilihama kazi. Kwa sasa nipo mjini Morogoro.
Ingawa ni zaidi ya mwaka tangu uniandikie nitajitahidi kukujibu kama Roho
atakavyoniongoza.
*
*
*
*
Pamoja na kukujibu barua yako nilipenda kukufahamisha
kuwa mwezi wa tisa tutakuja Dar es salaam kwa ajili ya semina fupi. Nitafurahi
kama tutapata nafasi ya kuonana.
Wako katika Upendo,
Yule wa Jangwani Sec.
1 Wakorintho 6:20
Ingawa barua ile
haikuwa na maneno yoyote ya mapenzi lakini ilinifanya nimkasirikie sana rafiki
yangu kwa nini hakuinipa barua ile awali kwani ilionesha yeye aliipata miezi
miwili kabla na ule ulikuwa mwezi wa nane, yaani mwezi mmoja tu kabla hawajaja.
Alinisihi nikae chini
anielezee na aliniambia ni kutokana na tabia yangu mbaya aliyokuwa akiifahamu
iliyomfanya asinipe barua ile na kama si kuja kumueleza mabadiliko yangu
alipanga kutonipa kabisa barua ile.
Alinieleza aliumia
alipowaza kuwa nitamharibia maisha binti yule (maana alimfahamu pia tangu tukiwa
sekondari) akaona njia pekee ni kutokunipa barua ile.
Ilinibidi niwe mpole
kwa maelezo yale na kugundua kumbe nilikuwa najinyima fursa mwenyewe.
Septemba 21, 2016
Itoshe kusema kuwa
sasa mimi ni baba wa watoto watatu na leo imenikumbusha siku ile Ijumaa ya Septemba
21, 1984 nilipokaa na shemeji yenu na kuongea kwa kina kuhusu mustakabali wa
maisha yetu na mwaka mmoja baadaye kufunga pingu za maisha.
Bado nakumbuka…
Wasalaam wapendwa,
Mentor.
No comments:
Post a Comment