...NAKUMBUKA...
Psalm
37:25 “I was young and now I am old, yet I have never seen the righteous forsaken or their children
begging bread.”
…IDM Mzumbe…
Nakumbuka enzi za Mwalimu! Wakati huo tukisoma
ADCA (Advanced Diploma in Certified Accounting). Elimu ilikuwa nzuri, chuo
kilikuwa kikiheshimika. Tulikuwa tukila vyakula vizuri sana; chai ya maziwa,
mayai, siagi, jam, mikate, karanga, chakula mboga saba na kikikosekana kimoja
tu, tunagoma.
Ghafla vikaanza kupungua kimoja kimoja. Zilianza
jam, siagi, karanga, maziwa. Hayati baba wa taifa, Mwalimu J. K. Nyerere
akasimama akalihutubia taifa akasema, “Tufunge
mikanda” adui alikuwa ametuvamia na hatukuwa na budi kuhamisha rasilimali
nyingine kwenda kwenye vita. Mpaka leo, na bahati mbaya amefariki, hatujaambiwa
tufungue mikanda.
Nilimfahamu binti mmoja, maji ya kunde, mfupi,
mwenye uzuri wa asili. Nikisema uzuri wa asili namaamisha kuwa hata nywele, kucha,
na kujipamba kwake kulikuwa kwa kawaida kabisa hivyo ni rahisi kuuona urembo
wake wa asili.
Tulimaliza chuo na yeye kwenda kufanya kazi Morogoro,
kwenye kiwanda cha ngozi, Morogoro Tanneries kama mhasibu.
Viwanda vilikuwa vingi kipindi hiki. Viwanda
hivi vya ngozi kwa wakati huo vilikuwa vitatu tu; Morogoro, Mwanza na
Kilimanjaro. Hiki cha Kilimanjaro kilikuwa ndicho kiwanda cha kwanza kabisa cha
ngozi nandiyo maana kiliitwa Tanzania Tanneries.
Kulikuwa na kiwanda binafsi cha ngozi pia mkoani
Kilimanjaro, Himo Tanneries. Sikumbuki kilikuwa ni cha nani, na hadi leo bado
kipo ingawa hivi vingine vyote – vya serikali – vilikwisha kufa.
Kazi ilikuwa nzuri na alikuwa mwaminifu sana kazini
hata ilipotokea nafasi ya kwenda IFM kusoma Post Graduate Diploma ya Uhasibu
kwa mwaka mmoja, yeye alichaguliwa kwenda. Ilikuwa ni kawaida kusikia
tukiambiwa, “mbona hamjitumia kama huyu dada jamani?”
Akiwa huko ilikuwa ni jambo la kawaida sana
wanafunzi kuchanga na kununua mitihani. Alikuwa na hofu ya Mungu. Hakutaka
kushiriki katika hilo. Wenzake walimcheka na kumdhikahi na kumuambia, “Utafeli wewe!” Alijiwazia moyoni mwake,
“Sina cha kupoteza. Cha maana sana hapa
nasoma ili nipate notisi za kufanya mitihani ya bodi ya NBAA.”
Mwaka mmoja si mrefu, hatimaye muda wa mitihani ukafika.
Alikuwa anafahamu sana somo la Financial
Management. Ila somo la Accounting lilikuwa likimpiga chenga. Wakati tunasoma
Mzumbe, tulifundishwa kwa kutumia mfumo wa Muingereza ilhali masomo ya huko IFM
ilikuwa kwa mfumo wa Mmarekani.
Nakumbukua mfano mmoja. Alikuwa akichanganywa na
maneno haya, “accounts receivable and
accounts payable”. Hakujua yalikuwa sawa tu na kusema “debtors and creditors.”
Siku kadhaa kabla ya mtihani wa mwisho
walimletea maswali ya Financial Management awasaidie na aliwasaidia kuyafanya.
Alikasirika sana alipoingia kwenye mtihani na kukuta maswali yaleyale. Aliamini
kweli walinunua mitihani.
Kwa bahati mbaya, hakupata mtu wa kumfundisha
Accounting maana kila mtu alikuwa na majibu tayari, hakukuwa na haja ya kusoma
tena. Waliendelea kumkejeli kuwa atafeli. Alirudi chumbani kwake akamkuta
mwenzake akifanya maswali yao yakununua, alikuwa ni mja mzito. Mwenzake
akamwambia, “toa hela wewe upewe mtihani,
utafeli!” Akamjibu, “tena ninaomba
nifeli ili niwaoneshe Mungu wangu ninayemtegemea ni wa namna gani.”
Matokeo yalipotoka alifeli mtihani ule wa
Accounting hivyo alirudi kazini Morogoro bila cheti.
Kazini kwake walimsimanga
na baadhi waliopata kusikia alichofanya huko walimkejeli kuwa amekataa kununua
mtihani akakosa cheti.
Baada ya miaka michache, binti yule aliolewa na
kuhamia mkoani Kilimanjaro kumfuata mumewe. Alitoka kuishi kwenye nyumba ya
hadhi ya juu huko Kingalu, Morogoro hadi kwenye nyumba ya kupanga Moshi. Nyumba
isiyo na ceiling board. Kwa bahati nzuri, Moshi nako kulikuwa na kiwanda cha
ngozi hivyo aliendelea na kazi kwenye kiwanda hicho hicho.
Wakati wote huu aliendelea kushikilia msimamo
wake wa uaminifu na hofu kwa Mungu. Wengi walimcheka kwani wakati ule ilikuwa
rahisi kwa wahasibu kuiba bila kugundulika kirahisi. Walimkuta na kumuacha -
kiuchumi. Lakini yeye hilo halikumghasi usingizi.
Huku nyumbani hali ya maisha ilikuwa ya kawaida
sana. Kwa nyakati zile familia zetu hizi, ukienda shule unakuwa ndiyo tegemeo
la ukoo mzima. Ndugu wa mume na wa kwako wote watakuja kwako kuomba msaada. Kwa
hofu ya Mungu waliyokuwa nayo, hawakuweza kumfukuza mtu. Hii ndiyo iliyofanya,
pamoja na kupata mishahara ‘nafuu’ haikuwa ikiwatosha. Iliwalazimu kuwalisha
watoto mchicha kila siku na maziwa nusu lita kwa watoto wawili. Nakumbuka kuna
kipindi watoto walifikia hadi kuharisha.
Siku moja mhasibu mkuu alimwita ofisini kwake
akamwambia, “Wewe binti nataka nikupe
dili! Hapa nimepiga milioni 20 kutoka kwenye OC sasa wewe kwa kuwa hutaki
rushwa na ulokole wako hata nikikupa pesa utakataa, basi nenda shule mimi
nitakulipia.”
Yule binti aliuliza maswali mengi juu ya fedha
zile na kwamba atagundulika lakini mhasibu mkuu alimthibitishia kuwa hilo
halimhusu, yeye aende shule na kwamba atalipiwa na ofisi. Wakati ule sehemu
pekee kwa kanda hii iliyokuwa inatoa masomo ya kujiandaa na mitihani ya CPA
kilikuwa ni chuo kipya cha IAA, Arusha. Alikubali akaenda.
Wakati huo binti huyu ni mama wa watoto wawili.
Alisoma kwa bidi masomo yake yale ya kujiandaa. Kipindi kile CPA ilikua
ikitolewa kwa awamu mbili; CPA 1 na CPA 2. Binti huyu alifanya mitihani minne
kati ya sita ya CPA 1 na kufaulu yote. Hata hivyo hakuruhusiwa kuendelea na
sehemu ya pili bila kufanya kwanza mitihani ile miwili na kupita, enzi hizo
walisema ‘ku-clear’.
Alienda hadi ofisini kwa mwenyekiti wa bodi ya
wahasibu (NBAA) na kumuomba aruhusiwe kufanya mitihani yote kwa wakati mmoja.
Mwenyekiti alimkatalia ila baada ya kumsumbua sana alikubali ila akamtaka
aandike barua ya kujifunga kuwa kama atafeli mtihani wa sehemu ya kwanza kati
ya ile miwili aliyobakiza, hata kama atapita ile ya sehemu ya pili basi
hataruhusiwa kuhesabika amefaulu, akakubali.
Alirudi kusoma tena kujiandaa na mtanange wa
pili. Wakati huo huo alikuwa na uja uzito wa mtoto wa tatu. Alidhamiria kusoma
hivyo hivyo na kumaliza kwa wakati.
Alienda tena kuripoti chuoni Arusha na mkuu wa
chuo alipomwona na jinsi alivyodhamiria, alimwonea huruma na kumwambia atafute
tu dada wa kumsaidia kazi. Hivyo aliendelea kusoma hadi akajifungua. Alikula
yeye na dada wa kazi kwa ada ile ile moja hadi anamaliza chuo.
Wakati anasoma, aliona masomo marahisi maana
alikuwa bado na notes za kipindi kile akiwa IFM kwenye kozi aliyofeli kwa kuwa
alikataa kununua mtihani. Wakati huo alielewa tayari kilichokuwa kikimtatiza
kwenye Accounting. Alikuwa vizuri zaidi kwenye Finance maana ndiyo kazi hasa
aliyokuwa akiifanya kazini kwake.
Wakati anakaribia kujiandikisha kufanya mtihani,
mwanaye alikuwa mgonjwa. Mkuu wa chuo alimshauri asijiandikishe kufanya mtihani
kwani aliona jinsi alivyojituma asingependa kumuona akifeli wakati yeye
alifahamu ana uwezo mkubwa. Hakumsikiliza, alijiandikisha hivyohivyo.
Mkuu wa chuo bado hakukata tamaa, alijua
akimzuia kufanya mitihani hatajaziwa matokeo yoyote walau atakuja kufanya
mitihani wakati mwingine. Binti yule alikuwa na mawazo mengine tofauti kabisa,
“Mungu wangu nimekutegemea wewe tangu
utoto wangu, ninakutegemea wewe hata sasa!” aliomba.
Wakati wa mitihani, mkuu wa chuo alikuwa akiingia
chumba cha mitihani na kukagua ambapo alijiridhisha hayupo. Kumbe! Binti
alikuwa amejificha na pindi tu mkuu wa chuo anapotoka ukumbini yeye alikimbia
na kuingia ndani ya chumba cha mtihani na kuendelea. Alijitahidi kuingia kabla
nusu saa hazijaisha baada ya mtihani kuanza. Mitihani sita, mkuu wa chuo
alikuwa akiingia na kukagua. Mitihani sita alikuwa akijificha na kuingia baada
ya mkuu wa chuo kutoka. Hatimaye alimaliza mitihani yake.
Baada ya mitihani alirudi nyumbani na kazini
kuendelea kulea watoto na kulitumikia taifa. Hakujua linaloendela hadi siku
mtoto wake wa tatu alipoamka anaumwa. Ametokwa na jasho kali na ana joto mwili
mzima. Aliharakisha kwenda hospitali ambapo mtoto alilazwa.
Asubuhi ya siku iliyofuata, alichanganyikiwa
alipomuona mumewe anakuja na tabasamu kisha anamuambia, “hongera”. Hakuelewa hadi alipomuambia kuwa amepigiwa simu na rafiki
zake na kumuambia kuwa ame ‘clear’. Hakuamini!
Alilia huku akiwaza kwa nini rafiki zake walimfanyia
vile. Hawakujua yuko hospitali na mtoto halafu wanamtania na kumdanganya tena
kupitia kwa mumewe kuwa amefaulu masomo yote? Haiwezekani! Watu huwa hawafaulu
CPA kirahisi hivyo. Alijua lazima kuna somo atakuwa alishindwa ku-clear.
Hakuhitaji kusumbuka sana ili kuthibitisha hilo kwani mumewe alimuahidi kwenda
hadi Dar es salaam kwenye bodi ya NBAA kumuangalizia matokeo.
Mumewe alipofika alilakiwa na msururu na kelele
za watu kila mmoja akisema la kwake. Wengine wakilia, wengine wakilia na
kucheka maana wamefaulu baadhi na kufeli baadhi. Wengine walikuwa wakiulizana,
‘huyu mwanamke ni nani?’
Alisogea hadi kwenye mbao ya matangazo na kuanza
kutafuta jina la mkewe. He he he, ni kama ulijua, alianza kutafuta chini
kuelekea juu. Baadaye akagundua yamepangwa kwa alfabeti. Alipeleka macho mahali
alipojua jina la mkewe litakuwepo. Hakuliona, hakikuwa kazi rahisi kuamini,
kwani mahali ambapo palikuwa – au palipotakiwa kuwa – na jina la mkewe palikuwa
na alama za michoro ya kalamu mpaka jina hilo halikuonekana.
Alijongea hadi ofisini na baada ya kujieleza
alishangaa anapewa hongera na kuulizwa huyo binti yuko wapi? Aliwaeleza yupo
hospitali Moshi. Alirudi na furaha kuliko ile ya mwanzo na kumueleza kuwa
alikuwa amefaulu masomo yote aliyokuwa amefanya. Na kama hiyo haitoshi, kati ya
watahiniwa 77, ni watahiniwa 3 TU waliopita masomo yote bila kurudia na kati ya
hao watatu basi wa kike ni yeye pekee. Aliyemaliza chuo miaka 10 kabla ya
kufanya mitihani hiyo. Mumewe alitembea kifua mbele kama vile yeye ndiye
aliyepata hiyo CPA (T)!
Baada ya wiki moja binti yule alirudi kazini na
kuendelea na majukumu yake kama kawaida.
Nakumbuka siku moja asubuhi na mapema, akiwa
nyumbani kwake bado kwenda ofisini, alishtushwa na mlio mkali wa honi ambapo
alipotoka nje alikuta gari aina ya land cruiser nyeupe na mbaba mfupi, mweupe
akiwa ameliegemea.
“Hujambo
binti?” alimsalimia. Na binti aliitikia salamu ile na kuijibu kwa heshima
aliyostahili. “Wewe ndiye mrs. ****
mwenye CPA?” aliendelea kuongea mzee yule. “Je, unajua kufundisha?”
Bila kujijua alichokuwa akikijibu, alikubali.
Binti aliambiwa aandike barua ya kuomba kazi na mwezi mmoja tu baadaye alipata
kazi katika chuo kimoja hapo Moshi akiwa mmoja kati ya walimu wanne tu wakati huo wenye CPA.
Walihama kutoka kwenye nyumba isiyokuwa na
ceiling board kwenda kwenye nyumba yenye vyumba vitatu vya kulala na mengine
mengi.
Nakumbuka akiulizwa, “Unajiona ukifika wapi?” naye akajibu, “Mungu anajua…”
Nakumbuka…
Nakumbuka…
Mentor.
No comments:
Post a Comment