SITAKI DAWA
Jumamosi,
25/06/2016
Nawaza nianzie wapi kuelezea kilichonikuta
nashindwa, lakini hasa ni kukosa maneno ya kukielezea. Nimetamani nikae kimya,
nisiseme, maana ninafahamika na wengi na itaniharibia picha yangu kwenye jamii.
Nimetafakari sana kuchukua maamuzi magumu lakini nfasi yangu haikuumbwa hivo,
nimeshindwa. Labda ningezaliwa Mhehe, lakini Mchagga mimi hata vidonge vya 'piriton' vilikuwa shida kumeza.
Lakini nimeamua nitasema. Sijui baada ya kusema
nini kitatokea, sijui jamii itanichukuliaje, ndugu jamaa na marafiki watasemaje
au labda watanitenga…lakini nitasema.
Wazazi wangu – MNISAMEHE! Zaidi ya yeyote yule, nimewaangusha. Mlikuwa na mategemeo makubwa juu yangu. Mmenisomesha kwa gharama
kubwa na mlikuwa na matumaini ya mimi kufika mbali.
Mlioniita Mentor – MNISAMEHE! Najua ni wengi
walioniona kama kijana wa mfano, kaka na ndugu…mnisamehe kwa kuwaangusha.
Sitamsingizia shetani wala mtu mwingine yeyote kwa kosa langu.
NIMEATHIRIKA! Na sijivunii…
July,
2015
Naamini ni wakati huu. Kulitangazwa nafasi za
masomo nchini Uingereza chini ya ufadhili wa Commonwealth (Commonwealth
Scholarships 2015). Nami nilikuwa nimejiwekea malengo kuwa hadi mwaka 2016 ni
lazima nikasome masomo yangu ya Uzamili (Masters Degree) hata ikibidi kwa kujilipia.
Nilitembelea tovuti tofauti tofauti nikitafuta ufadhili kwa ajili ya masomo
yangu. Hakuna tangazo lililotolewa ambalo sikuliomba. Fulbright, Mwalimu
Nyerere, DAAD, World Bank, IMF, n.k n.k niliomba zote. Nilikuwa na malengo ya
kwenda kusoma masomo ya Usimamizi wa Miradi au Sera za Umma na Utawala. Ndoto yangu
ilikuwa moja tu: SIKU MOJA NIWE KATI YA
WAFANYA MAAMUZI KATIKA NCHI HII.
Nilichoka kuwa mtu wa kutengeneza mifumo ya TEHAMA (programmer) kila
siku halafu aidha fedha zinaliwa au mifumo inawekwa kwenye makabati. Nilichoka
kuhusishwa kwenye miradi isiyo na kichwa na miguu, miradi isiyoangalia
vipaumbele vya Taasisi au Nchi. Nilichoka! Nikasema nitaachana na masomo yangu
ya Sayansi ya Kompyuta nikasome masomo yatakayonifanya niwe mtunga sera na mtoa
maamuzi. FUCK ME!!!! (mnisamehe am so mad at me)
Wakati huu ndipo kulipotangazwa nafasi hii ya
Commonwealth. Nakumbuka nililiona tangazo kupitia tovuti ya TCU na ilikuwa
imebaki wiki moja au mbili hivi kabla ya tarehe ya mwisho kwa hapa kwetu.
Nilijipinda ofisini kuandika insha kama tatu kuelezea kwa nini mimi niipate
nafasi hii na si mwingine. Niliandika kutoka moyoni. Nilifanikiwa kumaliza
mapema nikatoa nakala kama walivyoelekeza; za kupeleka Wizara ya Elimu na za
kutuma kwa barua pepe.
Siku, wiki na miezi vilipita nami nikaitwa
kwenye usaili, nikaenda kufanya mitihani ya Kiingereza ya IELTS pale ubalozi wa
Uingereza, nikafaulu vizuri.
Alhamisi,
23 Juni 2016 - Juzi
Nilipewa majibu kuwa nimechaguliwa pamoja na
wenzangu wawili kwenda Uingereza (Chuo sitokitaja) kwa ajili ya masomo ya
Uzamili katika Usimamizi wa Miradi kuanzia mwezi wa tisa. Nilifurahi sana,
nikapiga magoti ofisini nikamshukuru Mungu kuwa mwaminifu kwangu. Nilimuomba
mwaka huu niende shule na amenijibu. Tena kaniongezea baraka kwa kuwa ninapewa
ufadhili wa asilimia mia (100%). Hakuna hata senti yangu nitakayotumia katika maosomo yangu
hayo.
Jana asubuhi nilitumiwa mkataba wangu pamoja na
fomu za afya ambazo nilitakiwa kuzijaza na kuzirudisha ubalozi wao Jumatatu kwa
ajili ya mipango mingine; visa na kuomba ruhusa kwa Katibu Mkuu Kiongozi
(serikali ya awamu ya tano hii!)
Kwa ile hamu niliyokuwa nayo wala sikuweza
kubaki tena ofisini nikajiondoa kuelekea Mnazi Mmoja maana nilijua hilo sio
suala gumu. Nilishazoea kibongobongo hakuna kufanya vipimo na kwa kuwa
nilishaulizia kuhusu visa za Uingerea nilifahamu huwa hawafanyi vipimo vya afya
vingine zaidi ya kile kilichoandikwa kwenye ile fomu. Hivyo niliamini wala lile
zoezi lisingechukua zaidi ya nusu saa. Niliingia kwenye ATM ya bwana Kimei pale Posta nikachukua fedha ya kutosha kwa ajili ya kumshukuru daktari atakayenisainia
fomu zangu.
Nilimkuta mmama mmoja!dah nikamsalimia na
kumueleza kilichonipeleka pale. Nilishangaa alipochukua kikaratasi chake na
kuanza kujaza vipimo ambavyo nilitakiwa kwenda maabara kupima kabla hajanijazia
fomu yangu. Nilitamani kuondoka lakini nikakumbuka ameshaichukua fomu yangu na
alijua ninataka kuondoka akaiweka kwenye droo na kunikabidhi kile kikaratasi
nielekee maabara. Nilijaribu kumuomba kwamba nimetoroka kazini anisainie tu na
kupiga muhuri nami ningemshukuru vizuri tu. Alikataa na kunitaka niende kupima.
Niliondoka huku nikisoma kile kikaratasi ila
nilipofika kwenye hili neno PITC nikashtuka kidogo. Ufadhili (scholarship)
nautaka na vipimo sivitaki nifanyeje sasa, ikanibidi nielekee maabara.
Nikaelekezwa kwenye dirisha la kulipia nikalipa (nilisahau kabisa kwamba nina
bima ya afya hiyo jana). Nikarudi kwenye kiti changu kusubiri wakati wangu wa
kuitwa.
Palikuwa na makelele na kulikuwa na nesi mmoja
anaita watu majina. Namkumbuka kwa kuwa alikuwa na sauti kubwa kuliko mwili
wake.
“MAGRETH!
MAGRETH!” aliita kwa nguvu. –kimya
Akaendelea kuita jina lingine, “JACKLINE!” “JACKLINE!”
Mh! Haya majina mawili kwa pamoja yakanikumbusha
Changanyikeni.
Sikumbuki
siku kamili!
Nilikuwa na rafiki yangu tuliyeshibana sana toka
utotoni, Arnold. Huyu jamaa ndiye aliyenifundisha ule msemo wa KUPATA UKIMWI MPAKA UWE UMELOGWA. Nami
niliuamini maana michezo niliyoicheza ujanani tena pekupeku sikuwa
nimeathirika, kweli mpaka uathirike ni lazima ulogwe.
Ndiyo, kuna nyakati nilijua sijaathirika kabisa
kwa kuwa mara nyingi mabinti niliokuwa nao kwenye mahusiano walikuwa
wakiniambia. Nakumbuka huyu mmoja ambaye alinifuma nikiwa choo cha klabu na
mwanamke mwingine ambaye hata jina sikuwa nikimfahamu. Alinikuta nikifanya naye
mapenzi pasi na kinga. Nilikuwa nimeshazoea.
Huyu ndo alinifumbua macho siku moja miezi
michache baada ya kuachana nami kuwa kitu cha kwanza alichoenda kufanya baada
ya usiku ule ni kwenda kupima ambapo alipojikuta hakuathirika alishukuru sana.
Ndipo nami nikagundua kumbe sikuathirika. Niliifanya kama mchezo kwamba kila
binti niliyeachana naye; kumuacha au mara nyingi yeye kuniacha, baada ya miezi
michache nitamuuliza kama amepima na mara nyingi huniambia wako poa. Nami hujua
niko vizuri.
Ah!
Jacky na Mage
Nakumbuka ilikuwa siku niliyotoka ubalozi wa
Uingereza ambapo niliambiwa nimepita usaili na nijiandae tu kwa ajili ya
mitihani ya Kiingereza. Baada ya kufanya utafiti mfupi niligundua mitihani ile
si migumu na kwa watu wote tuliopita usaili mimi nisingeweza kukosa ufadhili
ule kwa kamtihani kale karahisi ka kiingereza.
Nilimpigia simu Arnold na kumuambia
tukasherehekee. Tulienda Samaki Samaki ambapo tulikutana na Jacky na Mage,
tulisoma nao O-Level huko Moshi. Tulipiga stori sana na kwa kuwa nilikuwa nasherehekea
mimi ndo nilikuwa mnunuzi. Walikunywa vya kutosha kiasi kwamba wakati wa
kuondoka wale mabinti hawakuweza kwenda peke yao. Ilikuwa kazi rahisi sana
kuwashawishi twende kwangu Changanyikeni kwa kuwa pia ilikuwa ni siku ya
Ijumaa. Tuliingia kwenye kausafiri changu hao mpaka Changanyikeni.
Safari moja
ikapelekea nyingine na yaliyotokea kule – sijivunii – na sitayaelezea na
hatukuwa na kinga yoyote. Na wala siwezi kusingizia ulevi maana mimi huwa
situmii kilevi chochote.
“Mentor!
Mentor!”
Sauti ya nesi yule ikiniita ilinishtua kutoka
kwenye dimbwi la mawazo. Ulikuwa ni wakati wangu kwenda kwenye vipimo.
Nilinyanyuka na kuelekezwa kwenye chumba kingine
ambapo nilipoingia sikukuta hata dalili za sindano. Kumbe ilikuwa kwa ajili ya
vipimo vingine vilivyokuwa kwenye karatasi ile. Nilipima uzito, urefu,
pressure, na mengine kama hayo kisha nesi akaniambia nirudi kukaa kwenye
benchi.
Hapo akili yangu ikaniambia kuwa kinachofuata
sasa ni Ukimwi. Nilikaa nikitafakari kama kweli ninaweza kuwa nimeathirika. Akili
yangu ikakataa.
Usiku
wa Mwaka mpya 2016
Najua wengi mnaonifahamu hamtaamini mkisoma hapa
– MNISAMEHE! Wengi walinifahamu kama kijana Mkristo safi ninayeenda kanisani
kila Jumapili. Hata kanisani kwangu ni mmoja wa viongozi wa vijana – nafasi
ambayo niliitumia vibaya kuendeleza tabia yangu mbaya chini ya kapeti.
Nilienda kwenye mkesha wa mwaka mpya. Tuliimba
na kusherehekea sana na moyoni mwangu nilijiwekea malengo kuwa mwaka huu mpya
nimtafute binti mmoja nitakayempenda na kutulia naye maana umri nao
haunisubiri.
Nilidhamiria kupunguza kwa kiasi kikubwa tabia
zangu mbaya hasa ukizingatia mema mengi ambayo Mungu amekuwa akinifanyia bila
kustahili kwangu. Ni katika kuwaza huku ndipo macho yangu yalipodondoka juu ya
msharika mmoja. Hadi wakati tunatoka ibada usiku ule tulikuwa tumeshafahamiana
vya kutosha.
Itoshe kusema tu kuwa hatukufanikiwa kwenda
kwenye ibada asubuhi ya tarehe 01/01/2016 kutokana na sababu zilizo nje ya
uwezo wetu. Na hatukutumia kinga. Ni katika kuwaza huku ndipo nilipokumbuka
kuwa juzi juzi tu alikuwa akiumwa na hakutaka kuniambia anaugua nini. “Atakuwa ameathirika?” nilijiuliza.
Lakini nikajifariji kuwa KUPATA UKIMWI NI HADI ULOGWE. Ni nani wa kuniloga mimi
Mentor, mtu wa watu, kwa kosa lipi nililomfanyia?
Jina langu liliitwa tena na kwenda kwa ajili ya
vipimo vingine vilivyohusisha damu kuchukuliwa.
Nilitamani kuondoka pale kwani sikuwa nimeomba
ruhusa ofisini lakini pia nilitakiwa kuondoka na fomu zile. Ilinibidi
kusubiria.
Akili yangu ilikuwa ikisafiri mbali. Nilijiuliza
maswali mengi kuhusu afya yangu ambayo sikuwa nimewahi kujiuliza kabla.
Nilifanya mambo yangu mengi kwa siri kiasi kwamba ni vigumu mtu yeyote
akihadithiwa haya kuyaamini. Lakini kwani UKIMWI unawapata waliofanya kwa wazi?
Lakini hapana mimi siwezi kuwa nimeathirika. Kutoka kwa nani labda?
Nikamkumbuka Amina, huyu alikuwa mdada wa usafi
ofisini. Kama tabia yangu nimezoea kusalimia kila mtu na huyu dada tulikuwa
tukikutana asubuhi wakati naingia ofisini hakukosa salamu yangu.
Pamoja na tabia yangu ya kupenda kuwahi ofisini hakuna
siku niliyowahi kwenda ofisini nisikute ameshafika. Tukazoeana sana. Nami
kidogo kidogo nikaanza kumzoea na kumchokoza kwa vimaneno vya hapa na pale.
Kuna zile siku unaamka mapema, unajisikia
vizuri, unaoga unavaa unaingia kwenye gari unaondoka kwenda kazini mapema
ukitegemea kutakuwa na foleni kubwa kumbe unapofika barabarani unatumia robo
saa tu kufika ofisini. Hii siku ilikuwa hivyo. Na nilipofika saa kumi na mbili
kasoro bado nilikuta Amina amekwishafika. Na kwa bahati zaidi alikuwa akifanya
usafi ofisini kwangu.
Sitaki kuelezea zaidi lakini itoshe kusema usafi uliishia
palepale. Na hatukutumia kinga. Baadaye Amina alikuja kuzushiwa maneno kuwa
anatembea na mabosi wangu wengine na eti ameathirika hivyo akafukuzwa na
sikumuona tena. Sikuweza kumuuliza kama alipima au la!
Lakini hapana, wakati ninakutana na Amina
nilikuwa na rafiki wa kike, Hamida, na Hamida tulipoachana alienda kupima na
hakukutwa na virusi. Nilitabasamu kugundua kuwa niko vizuri.
Lindi hili la mawazo lilikatishwa tena na nesi yule
yule aliyeniita nyakati zilizopita. Niliiangalia saa yangu iliyonionesha kuwa ni
saa mbili zimepita tangu nifike pale.
Niliingia kwenye chumba ambacho nilijua tu ni
kwa ajili ya ushauri. Nilimwomba nesi aniandikie majibu yangu kwenye kile
kikaratasi pamoja na yale majibu mengine niwahi kwa daktari maana natakiwa
kurudi ofisini. *sasa ndio naelewa* maana aliniangalia kwa huruma sana huku
akivikusanya vikaratasi vile na kuondoka navyo huku akiniambia nisubiri.
Alienda kumuita yule daktari aliyeniandikia vipimo.
Jumamosi,
25 Juni 2016
Nimeikatisha ndoto yangu mwenyewe kwa umalaya
wangu. Nakumbuka siku ya usaili yule mzungu aliangalia fomu zangu baada ya
kunisikiliza na kusoma insha zangu aliniambia, “Young man! If what you have written and have just told us comes from
your heart, then I wish you all the best.”
Nimeikatisha ndoto yangu kwa kuishi maisha
mawili. Nakosa hata ujasiri wa kutubu kwa Mungu. Nakosa ujasiri wa kwenda
kanisani kesho. Ni nani aliyeniloga?
Pamoja na kupewa ushauri mwingi jana, nimeamua
sitokunywa dawa! Nipo tayari kutumikia adhabu niliyojitakia.
Nilirudi ofisini na kujifanya kama hakuna
kilichotokea. Baadaye jioni nilijilazimisha kwenda kuangalia filamu pale LAPF
Tower (Movie Night) na kwa maumivu makubwa filamu ile ilikuja wakati wa
kuchelewa sana maishani mwangu. Inaitwa ‘God’s
Compass’.
Baada ya kutoka na kuagana na walionialika tena tofauti na siku
zote nilikataa kuwapa lift kwenye gari langu na kuwalazimu wajazane wote kwenye
gari lingine la mwenzao na kurudi makwao. Nilirudi kwenye gari langu ambapo
nilikaa kwa zaidi ya lisaa limoja pale nikilia jinsi maisha yangu yalivyofikia
mwisho haraka.
Nimejitahidi kujifanya kama kila kitu kiko sawa
kwenye maisha yangu lakini nimeshindwa, nimeishia kulia machozi siku nzima ya
leo. Kwa nini Mungu ameruhusu hili linitokee mimi? Kwa nini asingeninyima
scholarship na kunipa afya yangu, ningejilipia mwenyewe. Nilikuwa nimeshapanga
kuwa kama ningekosa scholarship ningeenda kujilipia pale IFM nisome masomo ya
jioni na kwa hakika ningemaliza masomo yangu.
Hii inaweza kuwa hadithi yangu ya mwisho –
sikutaraji ingekuwa hii ndiyo hadithi yangu ya mwisho, na iwe ni ya kweli!
Lakini niwaombe wote msamaha. Sikuwahi kuamini kama nami ningekuja kuathirika,
walikuwa na afya zao, hawakuonekana wameathirika.
Kwa wadada wote mtakaopima na kukutwa
mmeathirika kwa sababu yangu – MNISAMEHE.
Wapendwa, hiki ni kisa changu cha ukweli na ndio
maana nimetaja baadhi ya vitu/sehemu za ukweli ili walau muone uhalisia. Kama
yote niliyowahi kuyaandika humu yatakosa maana kutokana na nilichokifanya basi
naombeni neno langu la mwisho mlizingatie…UKIMWI UPO, NAMI MENTOR NIMEATHIRIKA.
Tafadhali msifuate mfano wangu.
Wasalaam na kwaherini,
Mentor.
...you must be joking Mentor!!
ReplyDeleteHuu ni lazima ushuhudia usomaji na kila mtu, nipo hapa kuruhusu ulimwengu wote kujua kuhusu mtu aliyeokoa uhusiano wangu na mtu huyu mkuu anaitwa Dr IZOYA. Hakika alifanya kazi nzuri kwangu kwa kumrudisha mpenzi wangu wa zamani ambaye aliniacha na kuahidi kamwe kurudi kwangu tena. Kwa hili, nimekuja kutambua kuwa kutoa maelezo ya Dk IZOYA kwa ulimwengu utafanya mengi mazuri kwa wale walio na nyumba zilizovunja au uhusiano kwa ajili yake ili kukusaidia kurekebisha uhusiano huo uliovunjika au ndoa yako. Unaweza kumfikia kupitia anwani yake ya barua pepe: drizayaomosolution@gmail.com au kumwita moja kwa moja kwenye [+12098373537]. Kuwasiliana naye na kuona jinsi tatizo lako litatatuliwa ndani ya 24hours. Pia mtaalamu katika mambo yafuatayo ...
ReplyDelete(1) Unataka kurudi nyuma yako.
(2) Unataka kukuzwa katika ofisi yako.
(3) Unataka wanaume / wanawake kukufuate.
(4) Unataka mtoto.
(5) Wewe ni mjasiriamali na unataka kushinda mikataba
(6) Unataka mume wako awe wako milele
(7) Unahitaji msaada wa kiroho.
(8) Umeshambuliwa na unataka kupona fedha zilizopotea.
(9) Weka talaka
(10) Kualika kwa mila ya fedha
(11) Chagua uchaguzi