Msomali
Inasemekana katika mataifa barani
Afrika yenye wadada wenye ulimbwende wa asili basi mataifa haya
matatu; Eritrea, Ethiopia na Somalia, kamwe hayawezi kukosekana
katika namba za juu kabisa.
2016, Chuo Kikuu
Nilikwenda pamoja na baadhi ya wenzangu
chuoni hapo kutoa mada juu ya soko la ajira kama njia ya kujitoa
kwenye chuo kilichotulea wakati tukisoma huko. Tulikutana wengi
tuliokuwa tumesoma mwaka mmoja na wengine wa miaka ya nyuma na mbele
yetu. Ilikuwa siku nzuri sana maana tulikumbushana mambo mengi ya
ujana tuliyofanya tukiwa chuoni hapo.
Wengi sasa walikuwa na familia zao –
ndiyo, isipokuwa mimi – na wale ambao walibahatika kuwa na wake zao
ambao nao tulisoma wote chuo hicho walikuja nao kuturingishia sie.
Ilipendeza sana walipokuwa wakiwaambia wanafunzi kuwa wao walikuwa
wapenzi miaka kumi na iliyopita na sasa ni familia moja. Waliwatia
moyo wanafunzi kuwa kama wanapendana haimaanishi kuwa wakimaliza chuo
ndiyo mapenzi yataisha. Niliamua kujiondoa kwenye mjadala huo maana
ulinikumbusha machungu tu.
Nilitoka ukumbini na kuanza kutembea
bila kuwa na lengo maalum la nilipotaka kwenda isipokuwa tu kwa lisaa limoja lijalo
nisiwepo ukumbini kule kwenye mada ya 'ujana na mahusiano'.
Nilitakiwa kurudi tena kutoa mada ya 'Morality in the Workplace: How
university experience can shape you'.
Nilijikuta nimesimama ghafla baada ya
kuisikia sauti, sauti ambayo sikujua kama bado ningeweza kuikumbuka.
Nilijua hii sauti nilishawahi kuisikia, miaka mingi iliyopita.
Nilitembea kwa kunyata na kuchungulia kuthibitisha sauti ile ilikuwa
ya yule niliyemdhania.
“Mentor huyu huyu ambaye ndiyo
ameteuliwa kuwa Mkurugenzi pale TIRA? Wewe msomali ulipoteza
bahatiee...” ilikuwa sauti ya binti mmoja.
“Ndiyo huyo huyo” ilijibu sauti
ile. “Lakini hilo sio la maana.” aliendelea.
2002
“Tulikuwa mwaka wa pili na penzi letu
lilikuwa ndiyo kwanza linaanza kuchanua. Nilimpenda Mentor na yeye
alionesha kunipenda sana. Alikuwa ni wale wakaka wapole unajua, wao
ni kitabu na mpira tu. Hata alivyokuja kunitongoza nilibaki najiuliza
alinioneaga wapi?
Basi bwana tukaenda hivyo hivyo hadi
hii 2003 wakati tumeenda kwenye mazoezi kwa vitendo (field).
Nikakutana na mkaka ambaye yeye alikuwa
anafanya kazi pale. Alikuwa mzuriiii! Basi yeye kila siku anavaa suti
tu. Ni wale tunawaita; tall-dark-handsome, halafu anavaa miwani yake
full kutabasamu. Halafu hana hata miaka mingi hapo tayari
keshapandishwa cheo mara mbili tangu aajiriwe.
Kidogo kidogo akaanza kunizoea, mara
akipita kwenye meza yangu aniguse bega, siku nyingine aniletee
chocolate, mara biskuti, ali mradi hakosi kitu cha kunishtua kila
siku.
Mwanzoni nilikuwa namchukulia poa maana
nilikuwa na Mentor lakini kadri siku zilivyoenda nilizidi kumzoea.
Alinifanyia mpango hata baada ya kumaliza field niwe naenda kazini
kwa masaa machache na ilinisaidia sana kupata uzoefu. Kidogo kidogo
hata muda wa kukaa na Mentor ukaanza kupungua maana kule kazi, shule
na vimtoko vya kuibia na huyu mpya.
Siku ya siku, bwana yule akanitamkia
wazi kuwa ananipenda, anataka kunioa nitakapomaliza tu chuo. Ilibidi
nimueleze tu kuwa nina mpenzi mwingine. Akanisisitizia ari yake
lakini akanipa wiki moja nimpe jibu.
Nilitaka niwe nao wote maana kila mmoja alikuwa na sifa yake tofauti na mwenzake. Lakini baada ya muda nilikaa nikatafakari
nikaona ninachofanya si kizuri, sikulelewa hivyo mimi. Nikatafakari
kati ya hawa wawii ni nani nilikuwa nampenda zaidi. Hivyo nikamfuata
Mentor nikamueleza kuwa sitaweza kuendelea naye tena kwani nimempata
mwanaume mwingine. Nilimuomba msamaha sana maana nilijua nilimuumiza
lakini ilibidi nimueleze ukweli.
Ulikuwa ni mwezi mrefu sana kwangu
maana ndiyo tulikuwa tumeingia mwaka wa tatu sasa. Mentor kichwani
kwake alijua tukimaliza chuo tu ndiyo ndoa. Nakubali nilikuwa
nikimpenda Mentor lakini baada ya kukutana na huyu kaka niligundua
sikuwa nikimpenda vva kutosha.
Mentor alinisumbua sana akitaka hata nimpeleke kwetu akaongee na wazazi wangu kama shida ni ndoa. Alikuwa tayari kwa lolote maskini kaka wa watu.
Hata hivyo baada ya muda alikubali
kushindwa nami nikaanza penzi jipya na huyu mwingine. Maisha yalikuwa
nusu mbingu nusu dunia. Alikuwa mtaratibu mno, mcheshi na zaidi
alipenda kuzungumzia mambo magumu magumu ya maisha. Alinifanya kila
siku nijifunze jambo jipya niangalie habari kiasi kwamba hata masomo
yangu yalipanda maana nilikuwa ninasoma mambo hayohayo.
Wakati nikimalizia mwaka wangu wa
mwisho nilipata fursa ya kuomba kwenda kufanya kazi makao makuu ya
Umoja wa Mataifa maana tukiwa chuo nilikuwa mhudhuriaji mkubwa wa
makongamano na miradi yao. Hiyo nafasi hiyo ilipojitokeza wale
wawezeshaji (facilitators) wa upande wa Tanzania walinihimiza kuiomba
nafasi hiyo na walinithibitishia wataongeza neno lao na nitapata
nafasi hiyo.
Ilikuwa kazi ya muda/mkataba wa miaka
mitatu tu lakini niliiona kuwa ni fursa nzuri sana. Nilimueleza
mpenzi wangu na alifurahi sana. Aliahidi kunisaidia katika mchakato
mzima.
Huku shule ikielekea ukingoni, nami
nilikuwa namalizia viambatanisho vya mwisho vya maombi yangu. Kama
sio yeye sidhani kama ningemaliza maana mambo yalikuwa mengi mno.
Siku moja nikiwa natoka darasani, miezi
miwili kabla ya kufanya mitihani ya mwisho, nilisikia kichefuchefu
ghafla na nilitapika. Wala bila kuuliza nilielekea duka la dawa na
kununua vihusika na kama ilivyokuwa nilikuwa na ujauzito.
Nilipata mawazo mengi; shule, kazi,
nyumbani. Mambo haya yalinipa msongo wa mawazo maana kiukweli
sikutarajia kupata ujauzito wakati huu. Nilitaka nami nijifungue
ndani ya ndoa. Katika msongo wote huo wa mawazo kitu pekee
kilichonipa tabasamu ni kumfikiria baba mtoto maana siku zote alikuwa
akinitania, “Yani mtoto wetu atatoka mzuri balaa kama shombe wa
Kisomali!”
Nilitabasamu maana nilimuona
anavyofurahia kumuona mwanetu. Nilisahau hata nitawaelezaje wazazi na
ndugu zangu maana Msomali mimi ndiyo nilikuwa mfano wa ndugu na
wadogo zangu. Kila kitu kizuri lazima Msomali nitajwe kama mfano wa
kuigwa. Nilisahau kazi ambayo niliiomba na itakuwaje kwenda huko na
ujauzito. Nilisahau yote hayo, nilitoka chooni nikiwa na tabasamu
kama vile nimeambiwa Yanga na Chelsea wameshinda ligi! Hahah
Nilichukua simu na kumpigia ili kumtaka
kuongea naye baadaye jioni. Alikubali na kama tulivyoongea jioni
alikuja na maua mazuri ambayo alinikabidhi, bado nilikuwa
nikitabasamu.
Nilimueleza kuhusu ujauzito wangu na
hapo ndipo nilipona maajabu. “Hapana Msomali! Siko tayari na kulea
mtoto kwa sasa..hapana! Ulipataje sasa na wewe ulisema ulikuwa siku
salama? Hapana msomali.”
Hata nilipojaribu kuomba msaada kupitia rafiki zake na baadhi ya ndugu alinitukana, alinisema vibaya. Alionesha
dhahiri hataki kusikia juu ya mimba wala mtoto.
Kwa jioni ile aliondoka bila kusema
zaidi ya hapo na nilijifariji kuwa huenda ni ule mshituko wa kuwa
baba. Niliamua kumpa muda ajitafakari na baadaye atatulia.
Hali haikuwa kama nilivyotarajia maana
kadri siku zilivyoenda ndivyo alivyozidi kuwa mkali. Alifikia hadi
hatua ya kuniambia niitoe mimba. Niliumia sana. “Mimba au mimi”,
ndiyo zilikuwa chaguzi zangu.
Kumbe wakati mimi naandika maombi yangu
ya kwenda kufanya kazi naye alikuwa anafanya maombi ya kwenda shule
nchi ile ile ambayo nami nilikuwa naenda kufanya kazi. Kwa bahati
nzuri yeye alikuwa ameshapata na majibu kuwa amekubaliwa na
angeondoka mwezi Novemba mwaka huo. Alikuwa ameiweka kama siri ili
aje kuniambia baadaye. Sikuwa nimefahamu hadi siku moja kabla
hajaondoka ambapo alinipigia kuniambia kuwa anaondoka kesho yake.
Lengo hasa la simu yake halikuwa
kuniaga ila kisingizio kutaka kujua kama niliitoa mimba ile au la
maana tangu aniache siku ile hatukuwa tumeonana tena.
Nilimaliza chuo huku nikitafakari sana
kuitoa mimba ile lakini nashukuru Mungu nilipata rafiki wazuri
walionishawishi kutoitoa mimba ile. Siwezi kuelezea yote
waliyoniambia ila somo liliniingia nikaamua nirudi nyumbani kwa
wazazi wangu niwaeleze lililotokea. Kinyume na matarajio yangu,
nyumbani walinipokea vizuri sana tena wazazi na ndugu waliojua mkasa
ule walinionea huruma sana. Niliendelea kubaki nyumbani hadi Novemba
hiyo aliyonipigia simu.
Baada ya kukata simu yake ndipo nami
nikakumbuka maombi yangu niliyoyatuma. Nilifahamu kuwa kwa taratibu
za huko hata kama mtu umekosa nafasi ni lazima wakuambie. Hivyo
niliingia kwa mategemeo ya kukuta barua pepe yenye kunijulisha
nimekosa. Sikuwa nimeingia tena huko tangu jioni ile nilipoachwa
maana pia vitu vingi alikuwa akivifanya yeye. Alikuwa na nywila
yangu.
Niliangalia barua pepe zote mpya na
sikuona yoyote ya kuhusu hilo hadi nilipoangalia vyema na kukuta moja
ambayo ilikwishafunguliwa kumaanisha aliiona na hakuniambia. Ilikuwa
ikihitaji mimi kuongeza 'referee' mmoja zaidi maana nilikuwa
nimeandika wawili tu. Niliumia sana kwamba hakuniambia na hata
nilipoenda kwenye 'portal' yao hakuwa ameongeza chochote. Kigezo
hicho kimoja, kikawa kimenikosesha kazi, niko nyumbani na ujauzito na
siwezi kwenda kuomba kazi mahali kwa hali ile. Nahisi nilikuwa na
miezi sita hivi.
Maisha yalienda kama kawaida,
nikajifungua vyema mtoto wa kike ambaye nashukuru Mungu alifanana na
mimi karibia kila kitu. Sasa yeye ndo alikuwa shombeshombe, msomali, wa ukweli.
Nilitamani nimueleze baba yake lakini nilijizuia maana hakutaka kujua
chochote kuhusu mwanaye.
Nakumbuka wakati mmoja kabla hajarudi
nilijikuta tu nikimtumia picha za mwanaye, walau amuone tu. Nahisi
aliona nataka kumuomba pesa au kurudisha mahusiano hivyo aliipuuzia
barua ile.
Baada ya muda moyo ulianza kupoa hasa
baada ya hasira za kutelekezewa mtoto na hisia za mapenzi kwake
kuisha.
Nilianza zangu kazi miezi sita tu baada
ya kujifungua na maisha yamekuwa yakiendelea kama kawaida. Sasa hivi
nimeolewa na mume wangu tunaishi vyema kabisa na wala sifahamu huyo
jamaa yuko wapi.” alimalizia kusimuliza Msomali.
Niligeuka na kuendelea kunyata kurudi
ukumbini maana niliyoyasikia yalitosha, yalitosha kunikumbusha miaka
zaidi ya kumi iliyopita ambapo nilimpoteza binti niliyempenda.
Niliiangalia saa yangu na kugundua nimebakiza dakika kumi kabla muda
wangu ufike wa kutoa mada yangu. Niliamua kujikaza kutokukuonesha hisia zozote maana kwa
vyovyote vile, lazima maisha yaendelee...
Wasalaam wapendwa,
Mentor.
Nice Post thanks to you for this attractive informationāšThanks for the tips.
ReplyDeletei99bet