Tuesday, June 9, 2015

Mimi ni Polisi: Leo Halali Nyumbani

Mimi ni Polisi: Leo Halali Nyumbani
Leo, 09/06/2015, nimekumbuka matukio mawili makubwa yaliyonikuta kwa kufuatana na ambayo si mazuri hata kuyakumbuka. Miaka kama kumi na mbili hivi iliyopita nilikuwa nimeoa. Tulijaaliwa mtoto mmoja, Felix. Kipindi hicho nilikuwa ni Koplo wa Jeshi la Polisi, kijana machachari, mtanashati wa kikosi cha Trafiki.

Enzi zetu zile, ili kuchaguliwa kwenda kikosi cha Trafiki ilikuwa lazima uwe msafi, nadhifu. Tulikuwa tukishindana kung’arisha viatu na kunyosha nguo zetu nyeupe kiasi kwamba nzi akikosea njia akajigonga na upanga wa nguo yako, basi ni lazima akatike. Ah, enzi zile…

Kutokana na haiba yangu ya uchangamfu niwapo kazini, nilizoeana sana na madereva wengi wa barabarani kiasi kwamba ilifika hadi wakati unashindwa kumpiga faini mtu kwa kosa lililo wazi kabisa. Ila maisha yalisonga hivyo hivyo. Mwaka 2000 Nilienda koplo kozi huko chuo cha polisi, Moshi ambapo nilikutana na binti mmoja wa Kinyaturu. Alikuwa askari pale kituo kidogo cha polisi, Majengo.

Nilienda pale kuwasalimia wenzangu ambao nilimaliza nao depo. Ndipo nilipokutana na Elizabeth. Binti mdogo mzuri kwa kweli. Ni hadithi ndefu lakini baada ya muda si mrefu, Liz alikuwa mke wangu halali wa ndoa.

Labda nilioa mapema sana. Labda sikuwa nimemaliza mambo ya ujana. Labda, ni tabia ilikuwa imeshakomaa. Labda, labda, labda…lakini kila nikikumbuka enzi zile, sipati jibu kwa nini pamoja na kuamini kuwa nilimpenda Liz kwa dhati, bado nilichepuka. Na mke wangu alikuwa kifaa hasa...waliomjua wangeweza kuthibitisha haya nisemayo.

Mara nyingi sikuwa nikipenda kufanya hivyo, lakini nilijikuta tu nimeshaingia nyumba ya wageni na mwanamke mwingine. Wengi wa wanawake hawa walikuwa wateja wangu niliokutana nao barabarani. Nilijitahidi kufanya kwa siri bila mke wangu kipenzi kufahamu. Nilionesha mapenzi kwake na kamwe hakuhisi kama nilikuwa nikifanya chochote nyuma yake.

Mke wangu alinipenda sana. Alikuwa akijisifu na kunisifu mbele ya rafiki zake. Kila walipokuwa wakikutana kwenye vikao vyao vya wanawake alikuwa akijisifu jinsi alivyopata mume mwaminifu anayempenda na kujali familia. Wale waliokuwa wakifahamu nyendo zangu walimsikitikia kimoyomoyo huku wengine wakimwambia bila kificho kuwa, “mumeo kama waume zetu!” Ila kamwe hakuwasadiki…#nisamehe-mke-wangu.

Mara nyingi nilikuwa nikitumia kazi kama kisingizio cha michepuko yangu na ile hali ya sisi kuwa vituo tofauti ilisaidia kufanikisha mipango yangu kwa kipindi kile. Mara nyingi nilikuwa nikitumia kisingizio cha kwenda doria naye aliamini kabisa. Lakini, za mwizi…

Katika michepuko yangu, kulikuwa na mmoja ambao ulikuwa ukitokea mkoa wa jirani. Mawazoni mwangu nilijua hakuna aliyekuwa akimfahamu kwani alipokuwa akija huenda moja kwa moja hadi sehemu tunapokutana na kufanya yetu kisha mimi huondoka usiku na kurudi kwangu nikisingizia ndio tumetoka doria ya usiku.

Kumbe dunia hii haina siri. Wahenga wanasema, siri weka na jiwe. Watu walikuwa wanatuona na kutupuuzia. Labda kwa kuwa sikuwa nikiingilia maisha yao.

Siku hii ya siku kama kawaida dada yule alifika mkoani kwangu na kuelekea moja kwa moja sehemu ya kukutania. Naam ilikuwa ni Ijumaa ama Jumamosi kama sikosei. Nami niliendelea na kazi huku akili yangu yote ikiwaza muda wa kazi uishe nikajirushe na mchepuko wangu. Madereva waliokutana na mimi siku ile walipata raha maana muda wote nilikuwa nimekaa kivulini natunza nguvu kwa ajili ya mtanange wa jioni. Akili yangu ilikuwa tayari chumbani, ni mwili tu ndio ulibaki pale.

Naam, niliwahi kurudi nyumbani na kusingizia kuchoka hivyo nikaomba kuachwa nipumzike kidogo maana jioni yake nilitakiwa kuingia doria. Hata mke wangu aliporudi kutoka kazini alinikuta nimelala na baada ya kuuliza alipewa maelezo hayo kuwa nimepumzika nikijiandaa na kwenda doria baadaye jioni.

Naye kwa upendo kabisa aliniacha niendelee kulala hadi saa kumi na moja hivi. Niliamka mwenye nguvu mpya na kuanza kujiandaa harakaharaka bila mke wangu kuniona kwani ndani ya sare zangu za kazini nilikuwa nimevaa na nguo nyingine za kiraia.

Niliaga na kuelekea mjini kunako kituoni kwangu. Niliingilia mlango wa mbele na kuwasalimia waliokuwepo pale na kutaniana nao kidogo kisha huyo nikatokea mlango wa nyuma kuelekea alipofikia mchepuko wangu.

Shughuli yenyewe ilianza mida ya saa moja zajioni na kuendelea.

Saa nane na nusu usiku:

Ghafla nikasikia mlango ukigongwa kwa nguvu. Nilishituka kutoka usingizini na kuuliza waliokuwa wakigonga kwa nguvu ni kina nani wao. Walijitambulisha kuwa wao ni askari Polisi na walitaka kuzungumza na mimi kidogo. Kwa kuwa niliwafahamu hasa kwa sauti zao sikupatwa hofu sana. Nilifungua mlango na hamadi nikakutana na sura ya mke wangu. Ndipo nilipogundua kosa nililolifanya. Nilinogewa na mchepuko nikasahau kurudi nyumbani katika muda niliopanga ili mke wangu kipenzi asije kugundua.

Lakini je, alifahamuje nilipo? Sikuwa na jibu kwa wakati ule. Tukio la kwanza nililolikumbuka leo ni siku kama hii miaka kumi na iliyopita niliingia mahabusu kwa mara ya kwanza. RPC alikuwa ameagiza nitafutwe popote nilipo niende mahabusu kisha asubuhi ndipo atasikiliza kesi yangu. Nilizidi kuchanganyikiwa nikiwaza, imekuaje tena hadi RPC kuhusika na ishu yangu? Niliwaza huenda mchepuko wangu huu unahusika na uhalifu sehemu fulani na mimi nilikuwa nikitumiwa kama chambo. Niliona dalili mbaya mbeleni. Mahabusu kipindi kile kulikuwa na ubabe mwingi sana. Kilichosaidia ni kwamba niliwekwa mahabusu ya kituo nifanyiacho kazi.

Asubuhi ya kesho yake, alikuja mke wangu akiwa analia sana na macho yamemvimba. Hakutaka kunisalimia wala kunieleza lingine, aliniambia tu, “Siwezi tena kuishi na wewe!” Sikuwa na muda wa kujitetea.

Niliwauliza wenzangu ni nini kilitokea mpaka nikafika pale ndipo nikaelezewa. Ilikuwa hivi;

Mchana wa hiyo siku mke wangu alikuwa kwenye vikao vyao vya wanawake. Ghafla alipita yule mchepuko wangu. Wale wanawake wengine waliokuwepo pale walikuwa wakimfahamu isipokuwa mke wangu. Kwa umbea na kushindwa kujizuia wakamuambia tu, “Mumeo leo halali nyumbani” Mke wangu hakuelewa na kwa vile alivyokuwa akinipenda alihisi ni wivu tu wa wale wanawake. Aliendelea kunisifu bila kujua #dah

Aliporudi nyumbani na kunikuta nimelala aliamini kuwa wanawake wake walikuwa wafitini tu hata alipoambiwa nimepumzika nikijiandaa na kwenda doria bado haikumuingia akilini kunihisi jambo lolote baya.

Shida ilifika pale ilipotimu saa tano ya usiku huku mke wangu mwaminifu akiwa nyumbani, macho, akiningojea mumewe nirudi nyumbani kutokea doria. Saa sita, saa saba…kimya!

Ndipo mke wangu alipoamua kwenda kituoni kuulizia kumetokea nini sijarudi nyumbani. Alishtushwa alipoambiwa kuwa sikuwa nimeingia doria siku hiyo. Walikagua hadi vitabu vya kazini bila kuona sehemu yoyote niliyoandika kuingia kazini. Hapo ndipo hofu ilipoanza kumuingia, akaenda hadi kwa mkuu wa kituo, kisha mkuu wa polisi wilaya ndipo taarifa zilipomfikia RPC. Kwa hasira RPC ndipo akaagiza nitafutwe popote nilipo niwekwe mahabusu.

Unapodhani watu hawajui uyafanyayo subiri hadi wanapokuja kukugongea mlango hapo uyafanyapo. Ndivyo yalivyokuwa kwangu, sikuwa najua wanajua mahali nilipokuwa na mchepuko wangu. Hivyo kazi ya kunisaka ikawa rahisi kabisa na kujikuta mahabusu.

Tukio la pili lililonitokea maishani mwangu lilinifika asubuhi hiyo baada ya kutolewa mahabusu. Nilifika nyumbani na kukuta mke wangu amefungasha nguo zake na mwanetu na wanaondoka.

Nilishindwa kulia, nilishindwa nifanye nini. Kuomba msamaha pia nilishindwa. Alikuwa akiniamini sana mke wangu, Liz, mama Felix. Aliniacha na michepuko yangu.

Sasa mimi ni RSM mkoa mmoja huku nyanda za juu kusini, na bado sijaoa.

Wasalaam wapendwa,
Mentor.

No comments:

Post a Comment