Tuesday, June 2, 2015

Ndege wa Pelikana: Hadithi ya Bibi



NDEGE WA PELIKANA: HADITHI YA BIBI

Mimi na mama yangu tuna kitu kimoja tunachofanana. Sote tuna jino moja lililomegeka. Tofauti – kubwa – huja pale tutakiwapo kuelezea sababu ya kumegeka huko. Nikiwa mdogo nakumbuka nilikuwa nikimuuliza kwa nini jino lake limemegeka. Alinijibu kuwa alitaka kufanana na Nyerere vile alivyochonga meno yake. Niliziangalia picha za Nyerere na kuona kweli ni kama alichonga meno yake ya mbele. Alikuwa akipendeza.

Nami nilitaka kuwa kama mama, tatizo sikujua ni jinsi gani alilichonga la kwake na kwa nini yeye alichonga moja. Kila nilipokuwa nikimuuliza alikataa kunijibu. Alisema nikiwa mkubwa nitaweza.

Siku moja niliamua liwalo na liwe na nikaamua na mimi nitamega jino langu kuwa kama la mama. Nililigonga na jiwe! Maumivu niliyoyapata siku ile siwezi kuyaelezea lakini ilimchukua hadi bibi kunibembeleza. Aliniuliza kwa nini nilijigonga na jiwe na baada ya kumwelezea akaniambia ninyamaze anielezee kisa.

Bibi: “Hapo zamani za kale, palitokea ndege mmoja aliyeitwa ‘pelikana’. Ndege pelikana alipenda kuishi kando kando ya maji kwani chakula chao kikubwa kilikuwa samaki na mazao ya majini. Alitotoa mayai yake kipindi cha kiangazi na kuyahifadhi juu kabisa ya mti kwa usalama wao.

Kwa bahati mbaya, kiangazi kile kilizidi na kuwa ukame. Mvua hazikunyesha kwa muda mrefu. Hata makinda yalipototolewa mama pelikana alikuwa akipata shida kusafiri umbali mrefu majini kutafuta chakula kwa ajili ya wanae. Kwa kuwa walikuwa wengi hakuweza pia kuwabeba wote ili wahame kutafuta eneo lenye chakula.

Mama pelikana alijitahidi kukusanya wadudu kidogo waliokuwepo wakati ule kwa ajili ya wanae. Hata hivyo ukame ulizidi, samaki wote walikufa. Makinda wake walianza kudhoofu kwa kukosa chakula. Mama pelikana akakosa mbinu mbadala ya kuwalisha wanae.

Alianza kwa kujidonoa hadi akatoka damu kisha akawapa wanae. Aliendelea kujidonoa kisha kuwalisha wanae nyama ile itokayo mwilini mwake. Baada ya muda mfupi alikufa. Makinda yale bila kujua walianza kuudonoa mwili wa mama yao na kuula. Kwa kuwa alikuwa mkubwa sana makinda yale yaliendelea kuula mzoga wa mama yao hadi ulipokwisha.

Kwa bahati nzuri mzoga ulipoisha makinda yale yalikuwa yameshakua na kuwa ndege pelikana kamili. Mvua nazo zilianza kunyesha hivyo kukawa hakuna tena tatizo kupata chakula.

Wale ndege pelikana walianza kuruka huku na huku wakimtafuta mama yao huku kila wanayekutana naye wanamwambia mama yao aliwakimbia. 

Mimi: Lakini bibi, si mama yao walimla wenyewe?

Bibi: Hawakujua kama walimla wao.

Bibi aliniuliza,“Unajua kwa nini nimekuambia hadithi hiyo?”

Mimi: “Sijui bibi”

Bibi akaendelea kunisimulia,
“Wakati wewe bado u mdogo sana, ulikuwa mtundu! Ulikuwa ukipenda kugusa kila kitu. Siku moja katika utundu wako uliingia jikoni na kwa bahati mbaya ulivuta sufuria iliyokuwa juu ya meza. Kwa kuwa hukuweza kuifikia ulitumia kitambaa kilichokuwa chini ya sufuria ile. Kwa bahati nzuri mama yako alikuwa karibu na alipoona kuwa sufuria ile inakaribia kuanguka alikurukia na kukusogeza mbali na ile sufuria. Ni wakati huo ndipo alipojigonga na mlango wa kabati na kwa bahati mbaya jino lake likavunjika. Ndani ya sufuria ile kulikuwa na maziwa ya moto sana ambayo ndiyo kwanza alikuwa ameyaepua kutoka jikoni. “

Ghafla maumivu ya jino yakanianza upya ikabidi tukatishe hadithi tuanze kubembelezana tena.

Wasalaam wapendwa,
Mentor.

No comments:

Post a Comment