Mazoea Huzaa Tabia: My Confession
Nililitumikia Jeshi la Polisi kwa miaka 25 kabla ya kustaafu kwa hiari. Nilipofikisha muda wa miaka 22 kazini nilikaa chini siku moja tumetoka kwenye tukio la ujambazi ambapo yaliyotokea huko yalinifanya kubadilisha mawazo yangu juu ya kusubiri kustaafu kwa umri wa lazima.
Ni tukio ambalo kila ninapolikumbuka hunifanya vinyweleo vya mwili wangu kusisimka. Sikuwahi kuogopa kufa kama siku ile. Hapana, hakuna siku niliyokiona kifo kwa ukaribu katika maisha yangu yote kama siku ile.
Ilikuwa ni mwaka 2008 katika pori la Nzega mkoani Tabora huko maeneo ya Bukene au Mwakalundi kama sikosei. Majambazi ambayo tulikuwa tumeyafuatilia toka mkoani Shinyanga yalielekea huko, nasi ili tusiwashitue hatukutoa taarifa mkoani Tabora ili tuongezewe nguvu.
Tuliwafuata kimya kimya hadi walipoingia kwenye pori hilo. Sitoelezea sana ila kulitokea majibizano ya risasi ambapo wenzetu wawili walijeruhiwa vibaya (mmoja kwa bahati mbaya alifariki hospitali). Katika majibizano hayo ilifika mahali risasi zangu zikaniishia. Ilinibidi kugeuka kurudi mahali tulipoficha gari nikaongeze risasi.
Kosa la kwanza, tulikuwa tumevaa kiraia, hivyo kutufanya tufanane na wale majambazi. Nashukuru tu Mungu yule askari aliyebaki kulinda gari alifuata sheria hivyo alinilenga kwenye bega ili kunipunguza nguvu. Kumbe, wakati ananipiga risasi kulikuwa na jambazi maeneo ya karibu na hapo ambapo aliposikia mlio ule alikuja haraka na kunikuta nimeanguka huku nikiugulia maumivu.
Alipogundua sikuwa mwenzao alinyanyua mtutu wa bunduki yake na kuuelekeza kwangu. Jasho, machozi, mkojo na vitu vyote vitokavyo mwilini mwa binadamu vilinitoka siku ile. Akafyatua risasi ambapo kumbe pasipo kujua zilikuwa zimeisha kwenye bunduki yake. Akiwa bado ameuelekeza mtutu wa bunduki yake kwangu alitoa ‘magazine’ ili aweke nyingine yenye risasi. Hali yangu ilizidi kuwa mbaya. Niliuona mwisho wangu. Sikuwa na nguvu ya kupigana kutokana na maumivu yale ya mkono niliyokuwa nayo. Niliuona mlango wa Mbinguni na malaika wakishuka kama kuja kunichukua.
Alipomaliza kuweka ‘magazine’ mpya, akakoki ili risasi iingie chemba. Ule mlio wa risasi kuingia chemba ulikuwa mkubwa kiasi kwamba nilihisi alikoki na kupiga papo hapo. Akilini mwangu niliwaza kama bado nipo hai au nilishakufa. Kabla sijafungua macho nikasikia kitu kinaniangukia na kunigonga kichwani. Kwa dakika mbili nzima nililala pale nikigugumia maumivu na kutokujua kama hivyo nilivyo nipo hai au nimeshakufa. Nilikuja kushtushwa naamshwa na mwenzangu huku damu nyingi zikinitoka mdomoni.
Kumbe askari yule alipogundua kosa alilolifanya alijificha na wakati yule jambazi anaweka risasi chemba, mlio ule mkubwa uliotoka ulikuwa wa yule mwenzangu alipompiga jambazi risasi ya mgongo. Bunduki aliyokuwa ameishikilia ilimuanguka na kunigonga mdomoni ambapo hadi leo nina jino moja lililomegeka kama ukumbusho wa tuliko lile.
Baada ya tukio hilo nilishindwa kuendelea na kazi za nje kwa muda hivyo nilirudishwa kituoni nifanye kazi nyepesi.
2012
Hali yangu kiafya ilikuwa imeshatengemaa na bega lilirudi kama kawaida. Hata kisaikolojia kwa kiasi fulani ile hali ilikuwa imeanza kunitoka. Ndipo nikaanza kupewa kazi ndogondogo za nje za upelelezi.
Ni wakati huu ndipo nilipofanya tukio ambalo pamoja na kukiri katika maelezo haya, bado siombi msamaha!
Nikiwa kama mpelelezi wa zamu kituoni nakumbuka ilikuwa siku ya Ijumaa usiku.
Aliwasili bibi mmoja akiwa na binti mdogo kwa makadirio ya haraka alikuwa na miaka nane hivi. Nilimpokea na kumsikiliza. Bibi yule alikuwa akilia kwa kwikwi (hysterically) ambapo ilikuwa shida kidogo kuweza kuongea tukasikilizana. Ilinibidi nifanye kwanza kazi ya kumbembeleza ndipo aanze kunielezea kisa cha yeye kulia vile. Bibi yule alianza kunielezea;
Kwanza aliniambia kwamba binti yule ni mjukuu wake ambaye kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake binti yake alipojifungua alikuja akamwachia na kisha kuelekea pasipojulikana. Kwa mwaka mmoja tangu amlete mtoto alikuwa akifika na kuacha fedha na nguo na vimahitaji kidogo kwa ajili yao. Lakini sasa ni miaka mitano hajui binti yake huyo alienda wapi na wala baba wa huyo mtoto ni nani.
Siku hiyo binti huyo alikuwa ametoka shule jioni alipanda daladala lililomshusha kituo cha karibu na nyumbani. Kipindi hiki ndicho kipindi bodaboda zilianza kushamiri jijini hapa. Kwa akili zake za utoto alimfuata dereva bodaboda aliyekuwa eneo lile na kumuomba lift ampeleke nyumbani kwao na kwamba angempa shilingi mia tano aliyokuwa amebakiza kama nauli. Yule dereva boda boda alikubali pamoja na kwamba haikuwa nauli halali kwa safari ile.
Basi binti Yule aliifanya ile kama tabia na kwa wiki kadhaa walikuwa walifanya hivyo. Alizoea lift ya Yule kaka kiasi kwamba akirudi asipomkuta, aidha atatembea kwa miguu kwenda nyumbani au atamsubiria hapo kituoni.
Ilitokea siku moja binti Yule alirudi nyumbani na alipofika kituoni alijisachi na kujikuta hana fedha. Hakujua aliidondoshea wapi lakini kwa kuwa alikuwa ameshazoeana na dereva bodaboda Yule alimfuata na kumueleza kuwa siku ile hakuwa na nauli na hivyo alimuomba kama angeweza kumpeleka. Bodaboda Yule bila hiyana alimpakiza kwenye pikipiki yake kisha kumpeleka nyumbani kwake. Hapo ndipo mchezo wake ulipoanzia.
Alimlawiti binti Yule.
Kitendo cha siku moja kikageuka kuwa cha kila siku na kama wahenga walivyosema, “Mazoea huzaa tabia”. Sasa ikawa binti mwenyewe anamtafuta dereva bodaboda kila akitoka shule naye bila hiyana anaendelea kumlawiti na kumharibu binti Yule.
Sasa ikawa binti halipi tena nauli ya boda boda kwa fedha anailipia kwa fadhila ya kulawitiwa.
Wahenga walisema, “za mwizi ni 40”! Siku ya siku bibi alimwona mjukuu wake amekaa upande. Kila akimwambia akae sawa anakaa sekunde mbili kisha anarudi kukaa upande, kwa tako moja. Halafu mbaya zaidi wakati akiendelea kumsemesha binti akajisaidia haja kubwa pale pale. Hapo ndipo bibi alipopata mshituko kuhusu mjukuu wake.
Alitaka kumchapa kwa nini mpaka umri ule bado anashindwa kujizuia kutoa haja kubwa. Alimshika na kumtoa kwanza nguo ya ndani ndipo alipoona jambo lililomshitua moyo wake. Mjukuu wake alikuwa ameharibika.
Nashindwa kuelezea maana nami nilikuwepo wakati daktari anamkagua ili kuweza kuandika ripoti tutakayoitumia kuthibitisha kuwa kweli binti Yule alilawitiwa. Nilishindwa kuzuia machozi. Daktari aliniangalia akacheka, akaniambia, “Afande! Ndo binadamu hawa” Nilimkatalia.
Yule binti alikuwa ameharibika ‘beyond repair’. Daktari alituthibitishia kuwa hatakaa arudie hali yake ya kawaida tena. Na itambidi kuishi na hali hiyo milele. Niliumia sana usiku ule. Nilimuuliza maswali mengi binti yule ambayo majibu yake yalizidi kunitia hasira kwa kweli.
Uchunguzi wa daktari ulionesha kuwa njia ya mbele haikuwa imeguswa kabisa! Dah! Nilimuuliza aliwezaje kujizuia shuleni asijisaidie darasani na alinijibu alikuwa akilazimisha kutoka darasani kama amebanwa hata ikibidi kuja kuchapwa na mwalimu atakaporudi.
Nilimuuliza tena, kama alikuwa anaumia na alinijibu ndiyo. Je, kwa nini bado ulikuwa ukienda kwake? Naye alinijibu, “Alikuwa ananitishia nikisema ataniua lakini wakati mwingine nilikua nasikia kuwashwa, namfuata namwambia kisha ananifanyia hivyo naacha kuwashwa.”
Nikamuuliza tena mbele ya daktari kujua yule bodaboda alikuwa akitumia nini kulainisha njia ili amuingilie? Naye alijibu alikuwa akitumia tu mafuta ya kujipaka na baada ya yeye – binti – kuzoea alikuwa akitumia mate tu!!!! Dah uso ulijaa machozi ndipo daktari akasema kwa hali hiyo itabidi apimwe kama ana maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwemo virusi vya UKIMWI. Nilimuona bodaboda yule kama muuaji…muuaji! kwani binti yule alikutwa ameambukizwa virusi vya UKIMWI na fangasi za kutosha kutokana na kutokujisafisha vyema.
Kazi ilianza ya kumtafuta bodaboda yule na nilijiapiza kutokugusa kesi nyingine yoyote hadi nimpate. Niliwafuata bodaboda wenzake na kumuulizia na mwanzoni walimficha. Sikutaka kuwaambia sababu ya kumtafuta kwangu. Ilinichukua siku mbili wananizungusha kuwa akija watanijulisha. Siku ya tatu nikiwa nimechoka kumfuatilia kote alikofahamika kuwa anaishi nilirudi nikawaambia wale bodaboda wenzake kuwa nawapa siku mbili tu wamlete wenyewe la sivyo nitawarudia niwashitaki wao wote kwa kosa la kumficha mtuhumiwa. Ilinibidi kutumia mbinu ile kwani nilijua wazi walifahamu alipo ila hawakutaka kuniambia.
Na kweli, kesho yake tu walimleta wamemfunga kamba mpaka kituoni na kunikabidhi. Alikuwa kijana wa miaka 25 hivi. Nilimwangalia kwa hasira. Nilimchukia kuliko jambazi Yule aliyetaka kuniua mkoani Tabora. Niliwaza mengi muda ule…akipelekwa mahakamani huyu atahukumiwa kifungo gani zaidi ya miaka 30 tu jela?
Ili kuondoa ushahidi sikumweka mahabusu hadi ukaguzi wa mahabusu ulipokamilika. Na hata nilipomwingiza nilimshawishi askari aliyekuwa zamu asimuandike kwenye kitabu. Usiku wa siku hiyo nilimtoa mahabusu nikamweka kwenye gari langu dogo na kwenda naye kusikojulikana…
Wasalaam wapendwa,
Mentor.
No comments:
Post a Comment