KWA HERI BARIADI…KWA HERI TEDDY
2014, September 28th
‘Men are from Mars and Women are from Venus’ ukurasa wa 154. Nikiwa nimepumzika nyumbani kwangu nikijisomea kitabu hicho katika lengo langu la kutaka kuupanua wigo wangu wa uelewa wa mahusiano. Ghafla baada ya kufikia ukurasa huo ndipo nikajikuta mawazo yakisafiri kuelekea njia moja ya vumbi inayochepuka kutokea mkoani Shinyanga mjini kuelekea mji wa Bariadi kupitia wilaya ya Maswa. Ilikuwa ni safari ndefu kutokea Dar es salaam ambapo ndipo nilikuwa nikifanyia kazi kabla ya kuhamishiwa Simiyu.
Asikuambie mtu uhamisho - pamoja na kwamba nilikuwa naenda kushika wadhifa mkubwa kuliko niliokuwa nao hapo kabla - ni jambo lenye kusumbua sana. Nilibahatika kumpata mfanyabiashara mmoja ambaye alikuwa akipeleka mizigo yake Bariadi hivyo kukubali kunibebea vimizigo vyangu nilivyopanga kuhama navyo.
2010, October
Ulikuwa ni msimu wa masika hivyo nilikuta watu wa huko wakiwa katika harakati za kilimo. Wengine karanga, mpunga, mahindi na wengine pamba. Ali mradi kila mtu alikuwa katika harakati moja au nyingine kuhakikisha mvua zile hazimpiti bure.
Nilifikia mahali panapoitwa Ntuzu wilayani Bariadi na kuendelea na kilichonipeleka huko. Siku moja katikati ya mvua kubwa nilikutana na jambo nisilolitarajia. Nilikuwa nimesimama kwenye kibanda kimojawapo mjini kusubiri mvua ipungue nirudi nyumbani kwangu. Kuna ule msemo wa ‘a diamond in the dust’. Msemo huo bado hautoshi kuelezea uzuri wa binti aliyekuwa akipita mbele yangu kajifunga khanga iliyoandikwa ‘HATA KWETU WAPO’ akiwa na kikapu kichwani. Hakuwa mchafu, nguo zake zilikuwa safi (ingawa si mpya/nzuri).
Moyo ulinilipuka baada ya kumuona. Alikuwa akitabasamu huku akikaza mwendo kuelekea alikokuwa akienda. Tabasamu lake angavu lilipambwa vyema na meno meupe kama yaliyotiwa nakshi. Mweupe wa haja, na mwili ulijaa na kuumbika vyema. Mtoto wa kisukuma haswa.
Nilitupa macho mbele yake na kumuona kijana mmoja kwenye duka la pembeni aliyevalia jinsi na jezi la Manchester united lekundu la ‘vodafone’. Alikuwa akitabasamu zaidi ya binti yule. Kwa kujipa moyo nilijisemea atakuwa ni kaka yake hadi pale alipomkimbilia na kumkumbatia kwa nguvu huku akimpa mabusu ya shavuni. Nilipatwa na wivu. Alionesha alikuwa ni mpenzi wake.
Siwezi kuuelezea uzuri wa binti yule lakini moyoni na akilini mwangu nilianza kumuundia picha akiwa kajisafi, kajipamba yuko nyumbani kwangu. Ama hakika picha ile ilinivutia machoni. Nilimuuliza muuza duka kuhusu binti yule na kuniambia kuwa alikuwa amemaliza kidato cha sita mwaka huo. Teddy ndo jina lake. Alinielekeza hadi kwao. Kisha akaniambia huyo kijana ninayemuona naye ni rafiki yake kipenzi ambaye sasa yupo Bugando akisomea masomo ya afya mwaka wa kwanza. Walianza urafiki wao kuanzia kijana alipokuwa kidato cha nne na binti cha tatu. Pale kijana alikuwa ametoroka chuoni kidogo kuja kumsalimia binti ambaye muuza duka aliniambia baba yake ni mkali balaa.
Nilimsikiliza kwa makini huku nikihifadhi taarifa zile kwa matumizi ya baadaye.
Sikulaza damu nikaanza kumfuatilia kwa makini Teddy. Nilihisi kumpenda, alinivutia. Nilitamani kujua kama tabia yake ni nzuri kama ilivyo sura na umbo lake. Kidogo kidogo alianza kunifahamu ingawa kila alipokuwa akiniona/tukikutana alikuwa akinipa ‘shikamoo kaka’!
Nilijitahidi nikafahamiana na baba yake na kaka yake mkubwa kwa kutumia mgongo wa kazi yangu hivyo ikawa rahisi zaidi mimi kwenda kwao au kuzungumza naye bila hofu ya kuwaziwa mabaya na wazazi au majirani. Yeye pia alianza kuwa huru kuongea nami. Akanihadithia kuhusu rafiki yake huyo wa kiume (hakuweza kuzungumza hayo na kaka yake wala baba). Aliniambia jinsi gani anampenda na wana mipango ya kuja kuoana baadaye wakimaliza shule. Hakujua jinsi gani alikuwa akiniumiza moyoni. Kila siku nilizidi kumfahamu, na ndivyo nilivyozidi kuvutiwa naye. Sijui kama nilimpenda, ila nahisi nilipenda wazo la kumpenda. Yaani picha niliyoiunda kichwani kwangu.
Wahenga walisema, ‘Fimbo ya mbali haiui nyoka’ nami nilihakikisha usemi huu wa wahenga haubatilishwi. Nilianza kidogo kidogo nikitumia gia ya kile akitakacho kusikia…shule! Hakuwa amepata alama nzuri sana lakini zilimtosha kuanzia ngazi ya diploma ila baba yake hakuwa na uwezo sana hivyo ilimbidi kusubiri mwaka mmoja nyumbani ndipo mwakani aanze shule. Nilikuwa nikimtia moyo kuwa asijali na siku moja atakwenda shule na kufanikiwa kama mimi. Nilimpeleka outing mara kwa mara ila mara nyingi tulipendelea sana kwenda Rogmark hotel na alivutiwa sana kwani aliniambia hakuwahi kutarajia kufika hoteli kama ile.
Nilimwambia utakapoenda shule usome kwa bidii, sehemu kama hizi – na zaidi - zitakuwa jambo la kawaida sana kwako. Nilimpeleka kwangu ambapo wala hakukuwa na vitu vingi kwani vingi niliviacha Dar es salaam wakati nahama. Alikuwa akimaliza kazi zake za nyumbani anakuja kwangu na mdogo wake wanakaa kuangalia miziki au movie na siku nyingine nikiwa vizuri nawapeleka Rogmark. Ndiyo hoteli pekee yenye hadhi iliyokuwepo Bariadi kipindi hicho.
Kufupisha hadithi…
Kwa siri kubwa na kwa ushawishi wa hali ya juu nilifanikiwa kumfanya Teddy amsahau ‘rafiki’ yake na kuhamishia mapenzi kwangu. Alizidi kunivutia. Nilivutiwa na tabia yake, na kwa kuwa nilikuwa nikimpa fedha alikuwa akivutia sasa kwani hakuwa akivaa tena kanga na nguo kuukuu. ‘rafiki’ yake aliumia sana siku aliporudi na kumkuta mpenziye na mimi nyumbani kwangu. Alijiondokea kwa huzuni nami sikujali.
Matunda ya uvumilivu wangu niliyala wakati namsindikiza kwenda Dar kujaza fomu za kujiunga na chuo cha CBE mwaka 2012 mwanzoni. Nilichukua likizo ya dharura ya siku saba nikamwambia mzee wake kuwa nitamsindikiza. Lengo langu lilikuwa limetimia. Tulirudi Bariadi na binti wa watu akaanza tabia ambayo sikuipenda, ‘kujimilikisha kuwa mke wangu’ kisa tu tuli***
2012
Ilianza kama mzaha. Alikuwa anakuja kwangu na kuanza ‘kupanga’ vitu jinsi alivyokuwa anataka yeye. Nilimwambia asifanye hivyo lakini ukweli ni kuwa sikuwa nikipanga vitu vyangu kama ninavyotakiwa kuvipanga. Siku moja nikiwa natafuta kitu ambacho nilijua nilipokiweka ila sikukikuta ndipo nilipozidisha hasira kwake. Alipokuja kwangu jioni sikuanza hata kuhoji kilikuwa wapi nilimpokea na kibao kimoja cha shavuni.
Mwili unanisisimka hata kuandika nilichokifanya. Sikuwa nimepanga kufanya hivyo, sikujua hali ile ilinitokea wapi. Nilijiogopa kuwa na mimi ninaweza kumpiga mtu vile…tena wa kike! Niliomba msamaha kwani kutoka moyoni ile ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kumpiga mwanamke.
Alilia na kuniomba msamaha kuwa alijua nimemuudhi kwani nilishamwambia asiguse vitu vyangu ila hakusikia. Moyoni kikaniingia kiroho fulani kuwa hiyo ndiyo suluhisho la chochote nitakachomwambia.
Naomba nikiri kuwa, ninapoandika kisa hiki, chozi la huzuni linanidondoka. Sijivunii kitendo kile.
Kuna siku nilimwambia aje kulala kwangu, akawa anakataa kwani aliogopa atamuambiaje baba yake. Wikiendi iliyopita tu alikuwa kwangu kwa kisingizio cha kwenda kwa bibi yake Itilima. Kwa kuwa bibi hakuwa na simu na alikuwa na tatizo la kusahau ilikuwa rahisi kuaminika. Akilini nikawaza njia pekee ya kumfanya anitii ni moja tu. Nilimpiga binti wa watu vibao kama vitatu vya haraka huku nikimtuhumu kuwa hanipendi tena na kama ananipenda basi afanye hivyo na wikiendi hiyo aje kwangu. Alilia nami kama kawaida yangu nikajibaraguza kumuomba msamaha. Nilimwaminisha kuwa nilifanya vile kwa kuwa nampenda sana na nina wivu juu yake.
Ni visa vingi nilimfanyia, kwa kisingizo cha upendo. Alikuwa akiomba msamaha kila mara. Nilidhani nilikuwa nikimpenda lakini sikujua ni nini kilichokuwa kikinifanya nitende vile dhidi yake. Kama tumepishana kauli, au kuna jambo tuna maoni tofauti, au nikijua nimekosea, njia pekee niliyojua ya kumfanya anyamaze na kunitii mimi kama mwanaume ilikuwa hiyo. Najua nilikuwa nakosea, lakini niliendelea. Hadi siku nilipopitiliza kipimo.
2012, October
Ni msimu tena wa masika nilikuwa nimejificha eneo la posta nikisubiri mvua ipungue. Hii tabia ya kutembea bila mwamvuli kumbe imeanzia mbali. Ghafla nikamuona Teddy akija uelekeo wa posta. Alikuwa yupo nyumbani likizo. Alikuwa na mwamvuli hivyo nikashindwa kujua alikuja kufanya nini. Ndipo nilipoona mkononi ameshika bahasha. Nilitembea kuelekea eneo la kuwekea barua ili kumsalimia. Alishtuka aliponiona na akaongeza hatua kuelekea kwenye boksi la kutumbukizia barua. Machale yalinicheza kwani nilidhani baada ya kuniona angenisalimia kwanza. Nilimuwahi kabla hajaidumbukiza nikamnyang’anya. Ilikuwa barua kwa ‘rafiki’ yake wa Bugando.
Nilishikwa na hasira na kuanza kumtukana maneno ambayo sikuwa nimewahi kumuambia. Nilimvuta kwa nguvu hadi kwangu na kuanza kumpiga. Sikutaka kujua barua ile ilikuwa na nini. Nilijua tu walikuwa wameanza kuwasiliana. Nilitaka nirudishe heshima yangu, niliamini kwa kumpiga kule ningerudisha hofu kwangu kama ambavyo ilikuwa ikifanya kazi hapo kwanza. Katika vitu vilivyokuwa karibu, ulikuwepo mkanda wangu wa suruali. Niliuchukua na bila kuangalia ni wapi ninapiga nilimshushia hivyohivyo.
Nakumbuka kilichofuata ni taarifa kuwa natafutwa na Polisi. Nilikuwa nimemuumiza binti wa watu. Nilikimbia na kwenda kujificha Meatu kwa rafiki yangu. Sikuweza tena kuvirudia vitu vyangu. Niliambiwa baba yake alikuja kuchukua kila kitu mule ndani akahamishia kwake pamoja na vitisho vya kuniloga.
Potelea mbali niliamini uchawi hauwezi kunipata hivyo nilifanya mpango wa kurudi tena Dar bila kuwaambia nini hasa kilichokuwa kinanihamisha Bariadi.
Baada ya kurudi Dar nilimtafuta tena chuoni, nilimuomba msamaha alikataa kunisamehe. Alikataa kurudiana nami. Huwa namuona mara moja moja, anazidi kupendeza. Amemaliza Diploma yake mwaka huu na kufanikiwa kupata nafasi ya kujiendeleza. Ni mrembo, tena zaidi ya alivyokuwa kule Bariadi, mpole! Sijui kama bado nampenda au ni majuto.
Wakati mwingine huwa nakaa na kujiuliza kama nitampata tena binti mzuri kama Teddy. Nimeshakutana na wengi baada yake, lakini hakujawahi kuwa na aliyefikia uzuri na tabia ya Teddy.
Ngoja niendelee kusoma kijitabu changu huenda nikajifunza mengi kuhusu mimi…
Ukurasa wa 154
“1. Fight: This stance definitely comes from Mars. When a conversation becomes unloving and unsupportive some individuals instinctively begin to fight. They immediately move into an offensive stance. Their motto is ‘the best defense is a strong offense.’ They strike out blaming, judging, criticizing, and making their partner look wrong. They tend to start yelling and express lots of anger. Their inner motive is to intimidate their partner into loving and supporting them. When their partner backs down, they assume they have won, but in truth they have lost.”
Wasalaam wapendwa,
Mentor.
No comments:
Post a Comment