Monday, April 13, 2015

Baba Wawili



BABA WAWILI

September 2005

“Sikuambii ili umchukie baba yako,” alianza kunieleza mama yangu, “nakueleza ili uchukie alichokifanya,” aliendelea.

Nilikuwa kidato cha sita. Nilirudishwa nyumbani na kupewa adhabu ya kutokwenda shule kwa muda wa mwezi mzima. Mama yangu alilia machozi nilipofika nyumbani na kumueleza sababu ya kurudishwa kwangu. Nilirudishwa nyumbani kwa kosa la kumtorosha mwanafunzi wa kike wa shule ya jirani. Waalimu walinionea tu huruma kwa kuwa nilikuwa kidato cha sita lakini tabia yangu hii walikuwa wakiifahamu na iliwakera. Changamoto za balehe ndio zilikuwa zikianza kuonekana kwangu. Sikuwa nikitulia nionapo sketi.

Mama aliniita chumbani, akanikalisha, kisha akaanza kunielezea kisa ambacho kwa muda mrefu nilikuwa nikimsumbua anieleze. Nililelewa na baba wawili. Baba wa kwanza ndiye niliyekuwa nikimfahamu na kumuita baba. Tangu nipate ufahamu, ndiye aliyenilea na nilizoea kumuita hivyo. Nilianza kuona tofauti wakati nimeandikishwa darasa la kwanza. Nilikuwa nikitumia majina ya pili na ya tatu ambayo ni tofauti na majina niliyoyafahamu ya baba huyu aliyeko nyumbani.
Nikiwa darasa la pili pia nakumbuka kurudishwa nyumbani kwa kugoma kupeleka kuni na kisha kuiba maandazi ya mwalimu shuleni na kutakiwa kuja na mzazi kesho yake. Siku hiyo nilipelekwa shule na ‘baba wa nyumbani’ ambapo ilimchukua dakika kadhaa kumwelewesha mwalimu kuwa yeye ni baba yangu pamoja na tofauti ya majina yetu.

Nilirudi nyumbani baadaye na kumuuliza mama. Sikumbuki siku hiyo alinipa jibu gani, lakini, kadri nilivyozidi kukua nilikuwa nikimsumbua aniambie baba yangu ni nani na kwa nini mimi na wadogo zangu tunatumia majina tofauti.

March 1985

“Mwaka huo ndiyo kwanza nilikuwa nimeajiriwa kama katibu muhtasi katika halmashauri ya mji wa Morogoro,” aliendelea kunielezea mama. “Siku moja nilitakiwa kuandaa kikao cha maafisa watendaji wa halmashauri mbalimbali kutoka mikoa ya jirani na Morogoro ikiwemo Mbeya, Iringa, Dodoma na Singida.

Bosi wangu alinitaarifu kuwa nami ningetakiwa kuhudhuria kikao hicho kama mwanakamati wa kamati ya maazimio.
Anaitwa Edwin. Alikuja kumuwakilisha bosi wake. Alinichangamkia kuanzia siku ya kwanza. Hakuwa mtu mzima kama wengine ingawa alinipita miaka kama mine hivi. Kwa kweli alinipa company kiasi kwamba nilijikuta kwa wiki ile moja aliyokuwepo pale nikifurahia kikao kile tofauti na matarajio yangu.

Wiki ya pili, walibaki wachache ambao tulikuwa nao kwenye kamati ya maazimio. Edwin naye alikuwa mmojawapo. Ni katika kipindi hiki ndipo tulipopata muda mwingi wa kuwa pamoja. Mara nyingi baada ya kumaliza kazi tulikuwa tukitoka wote kuelekea mjini na wakati mwingine nilimkaribisha kwangu kuongea au hata kwa chakula cha jioni.

Aliondoka baada ya wiki mbili zile na tuliendelea kuwasiliana kwa simu za ofisini. Mawasiliano yalikuwa kwa haraka hatimaye tukawa tukiongelea mahusiano na uwezekano wa sisi kuwa wapenzi. Kwa mara ya kwanza nilisita kwa kuzingatia umbali kati yetu akini alinihakikishia hilo halitakuwa kizuizi kwake. Kuthibitisha hilo, mwezi wa nne alikuja tena Morogoro kunitembelea. Alikuja ingawa kwa wikiendi tu lakini ilinifanya niamini nia yake kwangu.

Mwezi uliofuata, Mei, nilipata safari ya kwenda Mbeya. Nilimtaarifu kuwa ningefika Mbeya siku moja kabla ya sikukuu ya Mei Mosi na kuwa ningekaa huko kwa wiki nzima. Nilifikia hotelini licha ya kuwa nilitarajia angenikaribisha kwake. Kwa kipindi hicho, hilo sikulijali.

Wiki mbili baada ya kuondoka Mbeya nlimtaarifu Edwin kuwa nahisi mwezi huo nisingeona siku zangu. Alinijibu kimzaha kwani hakuamini kuwa nilichokuwa nikimuambia nilikuwa na uhakika nacho.

Kama nilivyotarajia, baada ya mwezi mmoja nilienda kupima na kujikuta kweli nina ujauzito. Nilienda ofisini na kunyanyua simu kumpigia. Alizidi kushtuka na kuonesha kutokuamini. Nilimuuliza maswali mawili tu ambayo kwa kipindi kile niliamini yangenipa Amani ya moyo. Nilimuuliza; ‘Je, unamtaka huyu mtoto?’ na ‘Je, upo tayari kumlea?’ Kwa maswali yote hayo alinijibu NDIYO. Sikutaka kuongelea kuhusu mahusiano yetu kwani niliamini yale tuliyokuwa tukiyaongelea yangekuja kutimia hapo baadaye. Nilimuamini.

Mwanzoni mawasiliano yalikuwa ya kawaida hadi mimba ilipofika miezi mitatu. Ghafla mawasiliano yakaanza kupungua. Alianza kusingizia majukumu mengi kazini. Ilifika kipindi hata wiki ingepita bila kunipigia wala kunijulia hali. Na ilipobidi mimi kumpigia alikuwa akinigombeza kuwa ninamsumbua.

Alibadilika ghafla. Hakuwa Edwin yule niliyemfahamu. Ni kweli sikuchukua muda mrefu wa kumjua lakini hakuwa tena yule mchangamfu, mwenye tabasamu la bashasha na sauti tamu niliyemfahamu. Alibadilika na kuwa mkali, mkorofi, na mgomvi. Mwishoni aliamua kuwa kimya kabisa. Nipigapo simu ofisini kwake hakuwa akipokea tena n ahata akipokea mtu mwingine nikaacha ujumbe anitafute wala hakuwa akifanya hivyo.

February 10, 1986

Miezi tisa ilipotimia nilimwachia ujumbe ofisini n ahata nilipoenda kujifungua wala hakuja kunijulia hali. Niliamua kuwa nitamlea mwanangu na kuishi mwenyewe bila yeye wala mwanaume mwingine yeyote. Niliwachukia wanaume wote.

December, 1986

Christmas ya mwaka huo nilienda retreat jijini Dar es salaam na mwanangu amabpo tulikutana na wengine ambao tulimaliza wote chuo miaka hiyo. Tulifurahia sana wakati huo na nilifurahi sana kukutana na marafiki zangu tuliopoteana.
Nilikutana na mwanaume. Alikuwa kama organizer kwenye retreat ile. Alionesha kuwa karibu sana na mwanangu, na mwanangu alimfurahia.alijaribu sana kuwa karibu na mimi lakini nilikuwa nimeufunga moyo wangu. Sikutaka kabisa mazoea na mwanaume. Moyo ulikuwa umeumizwa.

Haikuwa hadi miezi miwili baadaye nilipopokea zawadi ya kuzaliwa kwa mwanangu kutoka kwake. Kumbe alikuwa bado akinifuatilia! Sikuwa nikifahamu hilo. Nahisi hapo ndio ulikuwa mwanzo wa mazoea yangu naye. Kidogo kidogo tulizidi kuzoeana na kumfahamu. Nilikuja kugundua kuwa naye alikuwa na mtoto ila alinieleza kuwa mama wa mtoto (aliyekuwa mkewe) alifariki kwenye ajali miaka kama mine iliyopita. Nilipata hofu kuwa na mahusiano kama hayo yasijetokea yale ya, “Baba Mentor, mtoto wako na mtoto wangu wamempiga mtoto wetu.” Hata hivyo hofu hiyo haikudumu kwani ilifunikwa na sifa zake nzuri.

Nilivutiwa sana na upendo wake kwa mwanangu na vile ambavyo wanetu walipendana ghafla kama vile walikuwa ndugu wa siku  nyingi. Alimjali mwanangu kama baba yake. Nakumbuka alikuwa akimhimiza amuite ‘baba’ badala ya ‘anko’.
Mwishoni mwa mwaka huo wa 1987, aliniomba tufunge ndoa mimi na yeye. Kwa kweli sikuwa na pingamizi. Alikuwa ameonesha sifa zote za mwanaume niliyekuwa nikimtaka tangu mwanzo. Mpole na mcheshi na alinipenda kwa maneno na matendo.

Tulifunga ndoa mwaka huohuo na kuanza maisha kama mume na mke.

Hapo ndipo vitimbi vilipoanza.

Edwin alianza kunisumbua. Alianza kwa gia ya kutaka kumuona mwanaye. Ni zaidi ya mwaka na miezi hakuwa amejishughulisha na mwanaye ila baada ya kusikia naolewa ndipo alipoanza makeke yake. Alitaka kuwa ananipigia simu muda wowote atakao au kuja nyumbani muda atakao yeye. Mume wangu hakufurahishwa na hilo. Baada ya usumbufu wa mara kwa mara ambao ulipelekea hadi kutaka kupigana aliitisha kikao kati yetu na Edwin.

Siku hii nilizidisha mapenzi kwake kwa busara aliyoionesha. Alimtaarifu kuwa muda wake kwangu uliisha. Alimwarifu kuwa sasa mimi ni mke wa mtu na mtu huyo ni yeye hivyo ana mamlaka yote kwangu. Alimtaka Edwin kuwa kuanzia siku hiyo mawasiliano yote kuhusu mwanae yapitie kwake na sio kwangu, maana alianza tabia ya kujifanya ananipigia kujua hali ya mtoto kumbe ananitongoza.

Mume wangu alimwambia pia akitaka kuja nyumabni ni lazima awepo na amtaarifu kabla hajaja. Kwa kifupi alimpa masharti ambayo yaliweka mipaka yakinifu baina yangu na yeye na kumfanya kushindwa adhma yake ya kunitongoza au kunisumbua kisa mwanaye…”

Sasa nilikuwa nimeelewa kwa nini niliitwa Mentor Edwin na sio jina la baba niliyezoea kumuita baba. Nilimwona mama akijifuta machozi na mimi moyo ukaniuma sana.

Nilielewa hasa maana ya yeye kuchagua wakati ule kunielezea kisa kile. Alitaka kuniepusha kuja kuwa kama baba yangu. Nilimuomba mama msamaha na kumuahidi kuwa nitakuwa kijana mwema na kuacha uhuni ambao ungenisababishia majuto mbeleni kwa matokeo ambayo sikuyapanga wala kuyatarajia kwani wengi wa hao wasichana wala sikuwa nikiwapenda, ni tamaa tu za ujana.


Wasalaam wapendwa,
Mentor.

 

No comments:

Post a Comment