Bado natibu majeraha
Simu
yangu iliita nami nilipoitoa mfukoni nilikuta ni rafiki yangu
tunayefanya naye kazi pamoja kwenye kampuni moja ya mitandao hapa hapa
mjini, sema yeye yupo upande wa utawala. Ni rafiki yangu pia kwa kuwa
tunaishi wote jirani.Mentor: “Oyo niambie”
Fredy: “Uko wapi, nina mzigo wako”
Mentor: “Nipo data centre ya floor ya nne”
Fredy: “Poa nakuja, Nina mzigo wako”
Nikakata simu na kuendelea na kazi zangu huku nikimngojea. Alifika na kunikabidhi simu huku akiniangalia kwa jicho la kutaka kuelezwa nini zaidi. Ni simu ile ile niliyokuwa nimemnunulia baby G (wifi/shemeji yenu alipenda kuitwa hivyo)
22 February 2013, Ijumaa – JNIA
Nilikuwa narudi kutoka kozi fupi ya mawasiliano ya kimitandao jimbo la Guangzhou, China. Baby G alikuja kunipokea uwanjani pale, kipenzi changu G. Ilikuwa furaha isiyo kifani kwani kwa takribani miezi minne tulikuwa tukiwasiliana kwa kupitia facebook pekee tena akiwa ofisini kwani hakuwa na hizi ‘smart phone’. Tulirudi hadi chumba nilichopanga huku akiwa na shauku ya hadithi za yaliyojiri pindi nilipokuwa huko China. Tuliongea mengi sana pamoja na kumuonesha picha hadi mida ya usiku sana ambapo tulilala kutokana na uchovu wa safari.
Asubuhi na mapema nilimwamsha G na kumzawadia zawadi ya simu Samsung SIII niliyomnunulia wakati nipo nchini China. Ilikuwa pia ni kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa. Alifurahi sana nami pia nilifarijika kuona ameifurahia zawadi ile. Ulikuwa ni mwisho wa kuwasiliana kwa sms za kawaida na kuelekea kwenye ulimwengu wa dijitali. Sasa tunaweza kutumiana hata picha, jambo ambalo lilikuwa likinipa huzuni wakati nipo mbali naye kwani unatamani kuona hata picha yake lakini ndo hivyo tena anatumia Nokia Jeneza!
Maisha yaliendelea na siku zikageuka wiki na hatimaye miezi tangu nirudi bongo.
May 2013
Kwa muda mrefu, mpenzi wangu huyu alikuwa na tabia ya viuongo vidogo vidogo ambavyo mimi kwa kweli vilinikera na ama hakika nilikuwa nikimwambia kila nikivigundua. Viuongo ambavyo havikuwa hata na haja ya kuvisema maana havibadili chochote.
Kuna siku tulikutana na rafiki yake mmoja wa kike. Katika kupiga soga zao nikamsikia akimwambia, ‘Yani wewe G hujaachaga tu uongouongo wako!’ Nilishtuka ila moyoni niliendelea kutafakari nini mustakabali wa uongoungo wake.
Ilifika kipindi tulikubaliana kuwa kila atakapotaka kwenda atakuwa ananitaarifu kabla ya muda ili kumuepusha yeye kunidanganya inapotokea nampigia simu na kumuuliza. Hii ilitokea baada ya mwenendo wake wa uongo kuwa mwingi na mimi kugundua nyakati zote bila yeye kufahamu nimegunduaje.
Ukweli ni kuwa, wakati nimeinunua simu niliyompa baby G nilikuwa nimeifanyia ‘settings’ zote kupitia barua pepe yangu. Nilifanya pia ‘backup’ kwenda kwa barua pepe yangu, mambo ambayo baby G hakuyafahamu. Hivyo, wakati akifanya yote hayo na kunidanganya, nilikuwa nikijua na kwa hiyo ninapomuuliza na kumbana anashindwa kukataa.
May 2013, 10th…Alhamisi
Jana yake baby G alinitaarifu kuwa tarehe ya leo angeenda kumsalimia mama yake mkubwa huko Mikocheni kwani alifiwa na baba mkwe na hakuwa ameenda kumsalimu. Nilimwambia itakuwa sawa na amsalimie akifika.
Jana yake hiyo hiyo, baby G alianza kuwasiliana na mume wa rafiki yake. Walikuwa wakipanga mipango ya kukutana leo. Kwa nilivyokuwa nikifahamu, huyu bwana ameoa na mkewe alikuwa safarini mkoani Mbeya alikokwenda kujifungua. Nilikaa kimya kama sifahamu chochote.
Alianza safari mida ya saa tatu asubuhi kuelekea kwa mama yake mkubwa. Alinitaarifu kuwa yupo njiani huku ujumbe huo huo ukitumwa kwa ‘mchepuko’ wake huo. Walianza kuelekezana jinsi ya kufika safari ambayo kupitia google map nikiwa ofisini ilichukua njia ya Kilwa road.
Akiwa huko kwa mama mkubwa nilimwomba tu anitumie picha ya mandhari ya kwa mama mkubwa naye bila hiyana alimwomba ‘mama mkubwa’ ampige picha kisha nikatumiwa. Picha hii niliitaka kama ushahidi atakapokana kuwa hakuwa kwa ‘mama mkubwa’ bali alikuwa kwa mama mkubwa.
Kufupisha mkasa…
Mida ya kutoka kwa mama mkubwa iliwadia ambapo alinitaarifu. Nilimtega kumuuliza kama angepitia barabara ya Morogoro au Ali Hassan Mwinyi. Alinijibu kuwa angepitia Ali Hassan Mwinyi. Kimshale kwenye kompyuta yangu nacho kikaanza kusonga kutokea huko Kilwa road kilipokuwa kimesimama kwa takribani masaa sita kuelekea Posta.
Akiwa safarini nilimwomba akifika kituo cha Red Cross kukaribia Posta aniambie. Hapo ndipo ugomvi ulipoanzia. Alianza kulalamika kuwa amechoka na alitaka kupitiliza kwenda nyumbani. Nilimwambia kuwa akifika kituoni hapo ashuke kwani nilikuwa nikimngojea twende wote nyumbani. Baada ya kutoa visingizio vingi vilivyoshindikana hatimaye alikata tama kuendelea kubishana na kuamua kukubali kuja.
Alifika kwa pikipiki kituoni hapo nilipokuwa nikimngoja na nilipoanza kumuhoji kisa cha kuja na pikipiki ulianza ugomvi mwingine wa “Unafanya yote hayo kwa kuwa huniamini tu”. Nilikuwa nina hasira sana juu yake lakini nilijitahidi kuzizuia. Kama kuukoleza moto, tukiwa katika kubishana uliingia ujumbe kwenye simu yake. Nilimpokonya simu na kuusoma. Ulitoka kwa yule ‘mama mkubwa’ wa Kilwa Road ukisema, ‘Umemuwahi huyo mchepuko wako?’
Nimekuwa peke yangu tangu wakati huo.
Wasalaam wapendwa,
Mentor.
NB: Mwezi mmoja baadaye ilikuja kugundulika kuwa hata yule mtoto aliyezaliwa hakuwa wa ‘mama mkubwa’ wa Kilwa Road na baba halisi wa mtoto alikuwa huko huko Mbeya mama mtoto alikokwenda kujifungua.
No comments:
Post a Comment