Monday, August 11, 2014

Mama Hellen: Kiapo cha Ndoa

Mama Hellen

Alikuwa ni binti niliyemfahamu vyema. Nilimfahamu tangu akiwa sekondari shule ya upili ya Arusha. Tangu akiwa kidato cha pili nilianza kufuatilia nyendo zake. Ilinichukua miaka miwili kuweza kupata walau salamu yake. Alikuwa serious mno na masomo yake kiasi kwamba hakukuwa na njia nyepesi ya kuweza kuonana naye. Wakati huo akiwa kidato cha nne nilikuwa niko chuoni nikianza mwaka wangu wa kwanza wa masomo. Alinifahamu tu kama kijana tuliyekuwa tukiishi mtaa mmoja na sifa zangu zote mbaya (hili nilikuja kulifahamu baadaye) alikuwa akizifahamu.

Nakumbuka kuongea naye mara ya kwanza alipita karibu na nyumbani kwetu. Nilikuwa likizo fupi. Nilimwita kwa kupiga mbinja ambapo aliniangalia kwa kunipandisha juu kisha chini na kuamua kuja. Wahenga wanasema ‘Kubali wito kataa neno’. Nilitupa mistari yangu miwili mitatu na jibu nililopokea kama ni mtu mwingine basi lingemtosha kusitisha mipango yoyote ya kuendelea kumfuatilia binti huyu. Aliniambia, “Sikiliza Mentor, unachojaribu kufanya ni sawa na kutaka kukamua maji kutoka kwenye kipande cha chuma. Hutofanikiwa

Nilijipa moyo kuwa uzoefu wangu hauwezi kuishia hapo. Nilirudi chuo ambapo kama kawaida yangu niliendelea na ubazazi wangu (kwangu ulikuwa ushujaa..nilifanya kama mazoezi ya kwenda kumtokea mama Hellen nirudipo likizo). Ilikuwa rahisi. Nilijifunza tabia nyingine nikiwa chuo, ulevi. Kwa kweli kama ni kupiga vyombo nilikuwa stadi. Alhamisi kwangu ilikuwa Ijumaa, nilianza kunywa na kubazazi mabinti wa watu hadi Jumapili. Na Jumatatu nilikuwa niko vizuri kuhudhuria vipindi darasani.

Kufupisha hadithi…


2000

Ilifika kipindi sasa Mentor nikajiona ni muda wa kujipatia jiko. Ni miaka mitano baada ya kumaliza chuo na kwa kiasi nilikuwa nimejijenga. Katika kulitafakari hili, nikaanza kujiuliza ni nani kati ya mabinti ninaowafahamu angeweza kufuzu kuwa mama wa wanangu. Hakukuwa na jina lingine kichwani kwangu zaidi ya jina la mama Hellen.

Alitosheleza vigezo vyote vya mke mwema. Na zaidi ni binti ambaye nimemfahamu tangu akiwa binti mdogo. Haikuwa kazi ngumu kumpata kwani alikuwa naye amemaliza chuo na kupangiwa kazi mkoani Arusha ambapo nami nilikuwepo. Ni kwa bahati mbaya kuwa siku niliyokutana naye nilikuwa nimetoka kutupia maji ya dhahabu kiasi hivyo nilikuwa na harufu kwa mbali. Kumbe mama Hellen alikuwa ameokoka bana. Alinitolea nje papo hapo.

Baada ya kuendelea kumfuatilia sana aliniambia tu kuwa kweli hawezi kunikubali kutokana na tabia yangu na kama nikitaka anifikirie basi nijitafakari njia zangu na maisha yangu ya kiroho, atakapoona mabadiliko ndipo atakaponipa jibu.

Nilianza kubadilika. Ukweli nilipunguza kwa kiasi kikubwa unywaji wangu. Niliacha kabisa uhuni. Nikaanza kuwa mwenyeji wa nyumba za ibada. Kipindi hicho nilikuwa nikiishi eneo la Kijenge mijini Arusha. Alifurahi sana siku ya kwanza kuniona kanisani. Nilidhamiria kufanya lolote lililo ndani ya uwezo wangu kumpata mama Hellen.

11 August 2001, Jumamosi

Ni siku ambayo nilifunga pingu za maisha na mama Hellen wangu. Hatimaye alikuwa wangu. Nilifurahi sana kwani alikuwa ni zaidi ya mke. Wazungu wanasema ‘a woman and a half’. Nikianza kuandika sifa zake hapa itakuwa ni sawa na kuanza hadithi nyingine.

Miezi mitatu tu baadaye, uzalendo ulinishinda. Nilianza kupatwa na kiu ya ghafla. Kidogo kidogo na kwa kujificha nilianza kurudi kwenye kunywa. Mwanzoni nilianza kunywa bia moja moja nitokapo kazini lakini baadaye nilishindwa kujizuia na kuanza kurudi nyumbani nimelewa. Mama Hellen alianza kulalamika. Nilikuwa nikirudi na kumkuta akisali wala nisiguswe kabisa. Nakumbuka kuna siku nilimjibu kuwa, ‘nilikuokokea wewe!’ Lilikuwa pigo la kiimani kwake. Nilianza kabisa kuwa nakuja na bia nyumbani na hali yangu ya ulevi haikuwa siri tena.

Kwenye bar niliyokuwa ninapendelea kwenda nilijizolea jina maarufu la ‘Askofu’. Kuna siku katika kulewa nilizungusha ofa za kutosha na muda ulipofika sote tuliondoka bila kulipa bili. Asubuhi kama ya saa tatu hivi nilikwenda eneo lile na kumkuta meneja akimgombeza sana mhudumu kwa kumuingizia hasara. Ni hadi nilipomfuata meneja kumuambia nimekuja kulipa bili ya jana ndipo walipoanza kunipa jina hilo. Na kama kupalilia moto kwenye ulevi wangu nilipewa ofa ya bia moja kila siku nitakayoenda pale.

Mama Hellen kwa upande wake alizidi kusikitika lakini cha zaidi alimlilia sana Mungu kwa maombi kuhusu mabadiliko haya ya tabia ya mume wake kipenzi. Sikuwa tena na muda wa kwenda kanisani.

11 August 2014, Jumatatu

Leo ni mwaka wa 13 tangu nimuoe mama Hellen. Nikimuangalia, nakumbuka, nakumbuka visa vyote nilivyowahi kumfanyia lakini bado alibaki pembeni yangu na hakuniacha wala kukata tamaa. Nakumbuka zaidi kisa kilichonifanya niache pombe kabisa. Miaka mitano baada ya ndoa yetu.

2006

Wakati huu, ulevi wangu ulikuwa umekithiri. Nilikuwa nimeshaitwa nyumbani kwenye vikao si chini ya mara tatu na mara zote niliishia kuomba msamaha kwa mke wangu. Tukirudi Arusha nilianza moja. Ila kamwe hakuwahi kunisema kwa wazazi au ndugu zake. Ingawa baadhi walifahamu.

Alinipeleka kwa mchungaji kuombewa na wakati mwingine walikuja hadi nyumbani kwangu. Sikuwa mtu wa fujo lakini kila niliporudi na kuwakuta niligeuza na kurudi bar. Nilikuwa radhi kulala huko na asubuhi ningerudi mapema naoga na kuelekea ofisini. Nilianza kumuona mama Hellen kama kizuizi cha starehe zangu. Niliona ni afadhali nisingekuwa nimeoa kwani alikuwa zaidi kama kero kwangu. Hakuwa akinivutia tena kama zamani. Yaani nilikuwa nikiiwaza chupa kubwa ya yule jamaa aliyekunja mikono na kumuwaza mama Hellen, wazo la chupa lilinipa tabasamu kuliko wazo la kurudi nyumbani kwangu.

Siku hii Ijumaa moja ya mwanzoni kabisa mwa mwaka 2006 nilirudi nyumbani mida ya saa tatu usiku. Tayari nilikuwa nimeshalewa. Nilimkuta mama Hellen akiwa amepiga magoti sebuleni akisali. Sikuwa mtu wa fujo…kwa hilo namshukuru sana Mungu. Nilimwamsha alipokuwa amepiga magoti na kumuambia, “We mwanamke! Naona sasa inatosha…mimi natoka, nikirudi nisikukute hapa! Chukua chochote (R) chochote ukitakacho lakini nikirudi nisikukute” Zaidi ya hapo kwa kweli sikumbuki kingine ila kutoka na kufunga mlango kwa nguvu kurejea kunywa.

Nilishtuka mida ya saa tatu hivi asubuhi nikiwa nimelala kwenye kitanda ambacho kwa hakika hakikuwa cha nyumbani kwangu. Niliangalia juu kwenye dari, dari ambalo lilikuwa likipenyeza miale ya mwanga wa jua kwa kutoboka. Nilishtuka na kukaa kwanza kitandani nikijaribu kuvuta hisia za mahali nilipo. Sikuweza kufahamu. Niliangaza macho huko na kule chumbani hapo labda ningeweza kubaini ni wapi nilipo. Nilifanikiwa kuona pochi ya mke wangu ikiwa imewekwa juu ya kikapu kikubwa pembeni mwa kitanda. Jambo ambalo kwa wakati ule nilikuwa na uhakika nalo ni kuwa mahali pale palikuwa kijijini.

Ghafla nikaelewa! Mke wangu alikuwa amenileta kwa mganga. Alichoka na tabia yangu na kuona maombi yameshindwa kujibu hitaji lake. Hofu kuu iliniingia kwani niliamini tayari nimeshafanyiwa uganga na uchawi. Niliamka haraka kutaka kutoka kitandani, ndipo nilipogundua jambo la pili; nguo nilizokuwa nimezivaa zilikuwa zimelowa matapishi na mkojo. Kumbe mama Hellen alikuja kunichukua bar? Sikuwahi kulewa namna ile kiasi cha kusahau kabisa kilichotokea hadi mimi kujikuta pale.

Nikiwa katika tafakuri hiyo, mama Hellen aliingia chumbani. Nilitaka kuanza kumgombeza lakini nikawaza heri niwe mpole nimbembeleze huenda wakawa bado hawajanifanyia uchawi wao. Aliniomba niamke twende nimfuate. Bila maswali zaidi nilinyanyuka na nguo zangu zilezile zinazonuka na kumfuata mke wangu.

Sikuamini nilichokiona! Walikuwa wamekaa mezani wazazi wake na mama Hellen pamoja na ndugu zake na wajomba wawili. Ndipo kumbukumbu za nyumba ile ziliponirudia. Nilishawahi kufika kwenye sebule ile kipindi fulani. Palikuwa ni nyumbani kwa wazazi wa mke wangu. Aibu, hofu, hasira vyote vilinijia kwa wakati mmoja. Aibu kwamba wakwe wangu waliniona katika hali ile. Hofu ya kwa nini nipo pale (nilijua sasa mke wangu anataka talaka). Hasira ya kulazwa kwa wakwe. Mila zetu sisi wachaga ni MWIKO a.k.a taboo a.k.a KIWICHO; ni dhambi kulala kwa wakwe.

Kwa upole na aibu nyingi nilisalimia, na baba mkwe kunitaka nikae kwenye kiti ili mke wangu aelezee kisa kilichotokea. Ndipo alipokumbushia usiku wa jana yake niliporudi na kumtaka awe ameondoka nitakaporudi.

Kumbe nilirudishwa na wasamaria wema usiku huo huo mida ya saa nane nikiwa sijielewi. Nilizima kiasi cha kwamba hata maji hayakuweza kuniamsha. Waligonga mlango na mke wangu aliwafungulia. Walitaka kunishusha kwenye gari lakini mke wangu aliwaambia waniache humo humo. Aliingia ndani akachukua pochi yake na fedha kidogo akafunga nyumba. Alirudi kwenye gari akawashukuru vijana walionileta na kuwaaga. Aliendesha gari kutoka Arusha mjini usiku ule ule hadi nyumbani kwao Sanya Juu, kwa wazazi wake.

Alisema (huku machozi yakimtoka), “Mume wangu, uliniambia nichukue chochote nikitakacho. Kwa kweli kulikuwa na vingi ambavyo ningeweza kuvichukua ambavyo vingenisaidia sana kiuchumi. Lakini niliangalia vyote nikaviona havina thamani. Nilimuomba sana Mungu anipe jibu la jaribu hili. Nikiwa katikati ya maombi ndipo honi ya gari lako ilipopigwa na nilipoenda kufungua mlango - tayari kwa lolote kutoka kwako, kupigwa au lolote, maana nilishadhamiria kuwa sitoondoka – nikakuta umepakizwa ndani ya gari umelewa hujielewi. Ndipo nikakumbuka ulivyoniambia kabla hujaondoka. Nami katika vitu vyote vilivyokuwemo mule ndani hakuna kilichokuwa cha thamani kwangu zaidi yako. Niliamua kukuchukua wewe na kuja nawe kwetu ndiyo maana upo hapa mida hii.

Sitaki kuelezea aibu niliyojisikia na kuipata kwa tukio lile. Ilikuwa ni siku ndefu kuliko zote maishani mwangu.

Tulirudi nyumbani pamoja na mke wangu siku ile. Ni mwaka wa nane sasa tangu siku ile sijawahi kuitamani wala kuona kiu ya kinywaji kile.

11 August 2014

Kama sio upendo alionionesha mama Hellen wangu, mke wangu, sijui leo hii ningekuwa wapi. Leo ni miaka 13 kamili tangu siku ile kanisani pale Kijenge niliposema “Mimi Mentor nakubali na ninaweka ahadi ya kuoana na wewe kuwa mke wangu kwa maisha yetu yote niwe nawe tangu leo hii, katika mema na mabaya, katika utajiri na umaskini, katika ugonjwa na hali ya kuwa na afya; nikupende nikutunze mpaka kifo kitakapotutenganisha kufuata agizo takatifu la Mungu. Hii ndiyo ahadi yangu ya kweli mbele yako na mbele ya Mungu na usharika huu.

Nakupenda mama Hellen wangu, uliyeanza kunionesha wewe maana halisi ya kiapo hicho.

Wasalaam wapendwa,
Mentor.

No comments:

Post a Comment