Kisa cha Mfalme na Maskini
Mimi: Hadithi! hadithi!
Helena: Hadisi njoo, uongo ndoo, tamkolea (ndivyo ambavyo binti yangu Hellena hutamka)
Mimi:
Hapo zamani za kale mwanangu, zamani hizo ambazo nchi zote zilikuwa zikiongozwa na wafalme, palitokea masikini, masikini wa kutupwa. Maskini huyu hakuwa na chochote zaidi ya nguo kuukuu alizokuwa amezivaa na mfuko wa mchele usiozidi kilo tano uzito wake. Aliishi katika kibanda cha kuezekwa kwa mchanganyiko maalum wa makuti, maboksi na takataka nyingine alimradi siku zisonge. Kama kuna mtu hutamani kufa, basi maskini huyu aliitamani sana siku hiyo ifike kwani kuishi kwake kulikuwa kwa shida kuliko picha aliyokuwa nayo juu ya kufa.
Maskini huyu alikuwa akitembea na mfuko huo wa mchele kila mahali anakokwenda. Ndicho chakula pekee alichokuwa amebakiwa nacho. Kila siku alikuwa akipika kiasi kidogo tu ale atulize njaa na kusubiria tena siku inayofuata. Maisha haya yaliendelea kwa muda mrefu kiasi.
Siku moja, maskini alipata taarifa kuwa mfalme wa nchi hiyo angepita karibu na eneo alilokuwa akiishi maskini kuelekea mji mwingine. Maskini alifurahi sana. Alihisi huo ndiyo mwisho wa shida zake. Alipanga kuwa angeamka asubuhi na mapema siku hiyo na kuwahi barabarani kumngojea mfalme. Mfalme atakapopita, maskini angemsimamisha amuombe japo msaada wowote ambao mfalme angependa kumpa.
Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani siku ilipofika, maskini alidamka asubuhi na mapema akakamata mfuko wake wa mchele kisha akatoka kuelekea barabara ambayo mfalme angeitumia katika safari yake. Alifika mapema sana na akatulia kusubiri. Alikuwa na uhakika kuwa mfalme angepita, na bila hiyana angemsimamisha na kumuomba chochote.
Masaa yalipita na jua likajitokeza na mfalme hakupita. Lakini maskini hakukata tama. Taratibu jua likaanza kuzama na hata hapo mfalme naye hakuwa amepita. Kwa kawaida, kama binadamu, maskini alianza kukata tama. Kila wakati alijiambia, ‘nitahesabu hadi mia, kama hajafika nitaondoka.’ Alihesabu mara kadhaa na pale ambapo uvumilivu wake ulikuwa unakaribia kumshinda akajiambia tena kwa mara ya mwisho, ‘Nitahesabu hadi mia, kama mfalme hajatokea basi nitajiendea zangu nyumbani nikapike mchele wangu uliobakia kisha nisubirie siku yangu ya kufa nife’
Ni wakati anamalizia kuweka nadhiri hiyo ndipo alipoanza kuzisikia kelele kwa mbali. Alikuwa ni mfalme. Ghafla akaona watu wengi wakija na kabla ya muda mrefu alishangaa kuona watu wamejaa barabarani bila kujua walipotokea. Walimsonga mpaka akaingiwa na hofu huenda hatopata nafasi ya kumuona mfalme na kumueleza shida yake. Alijitahidi kujipenyeza katikati ya watu akiwa na mfuko wake wa mchele kwani mfalme alikuwa amekwisha kufika na hakuwa mbali na mahali alipo. Masikini alijitahidi na kwa bahati nzuri, baada ya kujipenyeza na kusukumana, alijikuta akisukumwa kuelekea barabarani ambapo aliangukia hatua chache kutoka mahali farasi aliyembeba mfalme alipokuwa.
Bila kujali nani kamsukuma au la, bila kujali aibu au fedheha, bila kujali kadhia ambayo labda walinzi wa mfalme wangempa, maskini yule alinyanyuka tena bila kujipangusa, akageukia alipo mfalme na kusujudu. Alisujudu huku kainamisha kichwa na kuunyosha mkono wake mbele kana kwamba anaomba kitu. Alikaa hivyo kwa takribani sekunde ishirini bila kusikia chochote kikiwekwa mkononi mwake. Alinyanyua uso taratibu na ndipo alipogundua kuwa umati wote ulikuwa kimya ghafla kuangalia kile kilichokuwa kikiendelea kati yake na mfalme.
Kumbe, wakati amenyoosha mkono kuomba kwa mfalme, mfalme naye alikuwa amenyoosha mkono wake vilevile kana kwamba kuomba kitu kutoka kwa maskini yule. Masikini alizidi kuchanganyikiwa. Alijiuliza maswali mengi, ‘kwa nini mfalme kunifanyia hivi?’ ‘Mfalme anategemea nini kutoka kwangu?’ ‘maskini mimi wa kutupwa, ni nini niwezacho kumpa mfalme?’ Kwa ufupi, alichanganyikiwa.
Basi, katika hali ya kukata tamaa maskini yule aliingiza mkono katika mfuko wake wa mchele na kisha kutoa punje moja ya mchele na kuiweka katika mkono wa mfalme. Mfalme aliipokea na kuamuru msafara uendelee.
Maskini alibaki na sintofahamu ya nini kilichotokea pale. Alirudi nyumbani kwake akiwa na majonzi makubwa kwani alisikitika kupoteza siku yake nzima kumngojea mfalme ambaye alitegemea sana kupata msaada kwake na matokeo yake amerudi nyumbani kwake na punje moja pungufu ya mchele katika kile kidogo alichokuwa nacho.
Alijiambia moyoni mwake, ‘Na nipike tena kiasi cha mchele huu uliobaki, nile, nisogeze siku nikisubiria siku mchele huu uishe nami nife’ Ndipo alipoufungua mfuko ule kwa minajili ya kuchota mchele.
HAMADI! Alishtushwa na kitu alichokiona. Kulikuwa na kitu king’aacho ambacho ama kwa hakika hakikuwa mchele wala chuya ila kilikuwa na umbo na ukubwa ule ule sawa na punje ya mchele. Alikiokota na kukiangalia kwa makini. Kumbe! Ilikuwa ni punje ya dhahabu.
Ndipo ilipomuingia akilini mwake na kukumbuka mkasa wa siku hiyo. Punje ile moja ya mchele aliyotoa na kumpa mfalme iligeuka na kuwa punje moja ya dhahabu. Maskini akaanza kujilaumu kwa kusema, ‘Laiti ningetoa zaidi!’ Lakini haikuwezekana tena. Mfalme alikwisha kuondoka katika eneo lile.
Mimi: Hellen mwanangu, umejifunza nini kwenye hadithi hii?
Mimi: Hellen, Hellen!??
Oh mwanangu huyu…huwa anapenda sana kuhadithiwa hadithi. Tatizo lake anajikuta amekwisha kusinzia kabla sijamuuliza amejifunza nini kutokana na hadithi hiyo. Akiamka tena nitamuuliza.
Wasalaam wapendwa,
Mentor.
No comments:
Post a Comment