Monday, July 14, 2014

Kuelekea Fainali za Kombe la Dunia

Haya Lala Mwanangu

13 Julai 2014, 2200hrs

Miaka mingi iliyopita, zamani sana. Miaka hiyo binadamu aliweza kuongea na wanyama na wakaelewana. Miaka mingi kabla binadamu hajaanza kufikiria kujenga mnara wa Babeli uliosababisha, sio tu kutokuelewana na wanyama, bali kumfanya binadamu kushindwa kuelewana na binadamu mwenzake.

Hapo zamani za kale, binadamu alikuwa akiishi na wanyama wote kwa amani. Ndiyo, kuku aliendelea kutumika kama kitoweo na kadhalika, lakini walikuwa wakiongea na kuelewana. Panya naye alikuwa panya yuleyule mharibifu.

Baada ya ukame wa muda mrefu, mvua zilinyesha tena katika eneo hilo aliloishi binadamu huyu na kufanikiwa kuvuna magunia machache tu ya mpunga. Ndipo binadamu alipopata wazo la kulima kwa wingi na kuhifadhi kwa ajili ya nyakati kama hizi huko mbeleni. Alijenga ghala na kuanza kuhifadhi nafaka.

Siku moja, panya alifanikiwa kuingia palipo ghala yalimohifadhiwa magunia ya mpunga na kutoboa na kula huku mwingine akiumwaga tu. Binadamu alipoamka asubuhi na kukuta yaliyofanywa na panya alikasirika sana. Aliamua kuweka mtego wa panya karibu na lango la ghala ili afanikiwe kumkamata panya mharibifu.

Kesho yake jioni panya alipita tena penye ghala lile ajipatie mlo wake wa jioni ndipo alipokutana na mtego ule. Kwa haraka haraka aliweza kuugundua kabla hajategwa. Aliwaza sana jinsi ya kuutegua lakini baada ya kugundua hatoweza akaamua kutafuta msaada.

Katika pitapita akakutana na kuku. Panya akamuomba kuku amsaidie kwenda kufyatua mtego ili aweze kupata chakula. Kuku akamjibu, “Huo ni mzigo wako wewe panya, mimi nachakura jalalani nala mabaki na wadudu, wewe unayekula vya watu utakoma.” Kuku akaondoka huku akitingisha mkia wake.

Baadaye akakutana na mbuzi na kumuomba akamsaidie kutatua shida yake, ategue mtego ili panya apate kula. Mbuzi naye akamjibu, “shauri yako! Mie nala majani, mpunga unanihusu nini mimi?”

Kidogo kabla jua halijazama alikutana na ng’ombe na kumuomba vile vile. Ng’ombe naye alimjibu kuwa yeye hula majani na pumba hivyo hahusiki na mpunga. Kwa ufupi wote walimuacha panya na shida yake wakiamini haiwahusu.

Baadaye jioni hiyohiyo katika pitapita zake, nyoka alijikuta katika shamba la binadamu huyu na katika ghala lile lenye mtego wa panya. Baada ya kuuona alijiwazia moyoni mwake, ‘Mtego huu kawekewa panya. Kwa namna yeyote hapa kuna panya, hivyo nitajificha hapa karibu akinaswa tu namtoa namla’ Katika kujigeuza, kwa bahati mbaya mtego ule ukamnasa nyoka.

Baada ya kusikia mlio wa mtego ule, binadamu alifurahi akijua amemnasa panya aliyekula mpunga wake. Hivyo aliondoka kwa haraka kuelekea ghalani. Kumbe, mtego ulivyofyatuka ulimbana nyoka mkiani hivyo binadamu alipoenda kuugusa alimgusa nyoka na kuumwa. Kwa bahati mbaya binadamu alikosa msaada wa haraka na kufariki.

Ndugu walipokuja kwa ajili ya kupanga taratibu za mazishi iliamuliwa akamatwe kuku, achinjwe, watu wapate kula. Hivyo kuku mwenye kuchakura jalalani na kula makombo na wadudu, kuku asiyehusika na mtego wa panya akakamatwa na kuchinjwa akawa kitoweo kwa ajili ya ndugu waliokuja kwenye msiba wa binadamu mwenzao.

Wakati wa mazishi, walikuja watu wengi zaidi. Hivyo ikapendekezwa mbuzi, mbuzi alaye majani tu tena asiyehusika na mtego wa panya, achinjwe. Hivyo mbuzi alichinjwa na watu wote waliokuja kwenye msiba wakala wakashiba wakamzika ndugu/jamaa/rafiki yao binadamu aliyefariki kwa kugongwa na nyoka aliyenaswa bahati mbaya kwenye mtego wa panya.

Siku arobaini baadaye, ndugu wote na wale waliokuwa mbali na kwa namna moja ama nyingine hawakuweza kufika kwenye msiba wa binadamu waliwasili kwa ajili ya kumsomea arobaini ndugu yao. Hivyo iliamuliwa ngo’mbe – ng’ombe alaye majani na pumba - achinjwe ili wapate kula na kumswalia ndugu yao kisha kuvunja tanga.

Mimi: “Mwanangu, umejifunza nini kwenye hadithi hii?”

Mimi (kwa kunong’ona): “Hellen! Hellen!”

Oh binti yangu Hellen alikuwa keshasinzia tayari. Alikuwa amekataa katakata kwenda kulala. Ilinibidi kumbembeleza na nimsindikize kwenda kitandani akalale kwani alitakiwa kuwahi kuamka asubuhi kwenda shule. Kiukweli, sababu kubwa ilikuwa tu nipate nafasi ya kutoroka kwenda kuangalia fainali za kombe la dunia na kama Hellen binti yangu angekuwa macho, basi angelazimisha aidha kwenda nami au kunifanya nibaki hapo nyumbani niangalizie mechi sebuleni na mke wangu mwenye maswali mengi yasiyo na kichwa wala mguu.

Nilitamani kweli kujua amejifunza nini kwenye hadithi hii lakini nilifarijika kuwa amesinzia…nitamuuliza siku nyingine…


Wasalaam Wapendwa,
Mentor.

No comments:

Post a Comment