Tuesday, May 13, 2014

Mimi ni Polisi: Kisa cha Mke wa Waziri Part II

Mimi ni Polisi: Kisa cha Mke wa Waziri 

2008, November

Kwa ufupi tu: Nilibahatika kupata ruhusa ya kwenda masomoni mwaka 2006. Nilikuwa nimeomba kwenda kusoma masomo ya Uhasibu na kukubaliwa kujiunga na chuo cha uhasibu cha Arusha (IAA). Niliomba ruhusa kazini na kukubaliwa kuhamia mkoani arusha.

”Hallo mentor” Nilipokea simu kutoka kwa lecturer wangu wa Business Mathematics. Kipindi hiki nilikuwa mwaka wa tatu wa masomo yangu na kwa kuwa nilikuwa na masomo machache muhula huo mwalimu huyu alikuwa akipenda sana kuniomba nimsaidie kusahihisha mitihani/tests za wanafunzi wa mwaka wa kwanza. Kwa kweli nilipenda hesabu na kufundisha hivyo sikuona shida, nikawa namsaidia.

Aliendelea, “Aisee, nimeamka sijisikii vyema kidogo naomba uende darasa langu la first year ukawasaidie kufanya masahihisho ya test ya juzi.”

“Ok sir!” Niliitikia na kwenda kwanza kuangalia ratiba nijue kipindi chake ni saa ngapi na kinafanyikia darasa gani.

Ile kuingia tu darasani, hamadi! Macho yangu yakagongana ana kwa ana na sura ambayo kwa wakati ule sikukumbuka ni wapi niliwahi kuiona. Kalikuwa kabinti karembo na kamekaa dawati la mbele kabisa mwa darasa. Hadi leo nakumbuka kalikuwa kamevalia jeans shirt ya blue na jeans nyekundu. Kichwani alikuwa na weave ila ya kwake ilimpendeza. Nililipotezea lile wazo ovu la kumtamani mwanafunzi wa mwaka wa kwanza na kuendelea na kilichonipeleka darasani pale. Baada ya kufanya masahihisho niliwaambia kama kuna atakayekuwa na shida atanitafuta na kuwaachia namba yangu ya simu ubaoni.

Ama hakika msema kweli mpenzi wa Mungu, namba ile niliiandika makusudi kwa kuwa akili yangu ya kibazazi ilikuwa bado ikimuwaza binti Yule. Sikuwa na njia nyingine ila kuamini kuwa labda ataichukua na kunitafuta.

<Na hapa sijisifii> Ila hazikupita siku mbili nilipokea simu kutoka kwa namba ngeni. Alisema anaomba nimfundishe statistics kwani hakuwa akielewa vyema. Tulikubaliana tukutane jioni darasani na ndivyo ilivyokuwa.

Alikuwa ndiye, yule yule binti mrembo aliyekuwa amekaa siti ya mbele darasani. Na wakati namfundisha ndipo nilipogundua kuwa hakuwa mwingine bali Tinna, binti wa mke wa waziri. Moyoni nilifurahi kuona Tinna yule aliyekuwa akiambiwa asiposoma atakuja kuwa kama mimi ndiye huyu ninamfundisha 'Statistics'. Ila pia nilijiambia lazima nimlipizie mama yake kwa kupitia yeye.

Ilikuwa kazi rahisi sana kumfanya Tinna aangukie katika mtego wangu. Kwa muda wa miezi kama sita hivi nilimfanya Tinna aamini kuwa kwangu amempata mwanaume. Ila sasa alianza kuniganda na kunizuia mimi kufurahia maisha yangu na watoto wa Arusha. Rafiki yangu alipenda kuwaelezea kwa kusema, “They are very beautiful, until they smile (if you know what I mean)”.

Nilipanga kumpotezea Tinna (ambaye hadi wakati huu hakuwa akijua kuwa mimi ni askari wala kuwa namfahamu ni binti yule wa waziri aliyekuwa akilia kwa kutokutaka kwenda shule). Nilianza kwa kumpotezea taratibu na kutokujibu sms zake wala kupokea simu. Akaanza kulalamika na kutuma meseji ambazo nilikuwa nishazizoea kama, “Mentor, kama kuna kitu nimekukosea, nisamehe tafadhali”

Baada ya wiki mbili niliona haachi kunisumbua ikabidi nihamie plan B. Nilianza kwa kumweleza kuwa mimi ndiye niliyemkosea na ndiye niliyetakiwa kumuomba msamaha. Hakunielewa hadi siku nilipoamua liwalo na liwe, nikamuomba tukutane kwa maongezi.

09 – 15 July, 2006, Nairobi

Ilikuwa wiki ya kawaida sana ukiachia kuwa nilikuwa nje ya kituo changu cha kazi. Nilikuwa nimechaguliwa kwenda semina ya ‘Post Traumatic Stress Disorder’ na jinsi ya kuwasaidia watu kama hao. Ilikuwa semina nzuri yenye mafundisho mazuri hasa kwa wataalamu wa usalama na matukio yanayotokea duniani. Semina hii ilifanyika chuo cha Catholic University of Eastern Africa huko eneo la Rongai katika viunga vya jiji la Nairobi.

Siku ya kwanza ya kujiandikisha nilikutana na binti mmoja ambaye naye alikuwa mwanafunzi wa chuoni hapo. Aliitwa Catherine. Alikuwa akipenda sana kunitania kwa kuniongelesha Kiswahili ambacho kwa kweli sijui nani aliwaambia sisi huongea hivyo. “Habari yako ndugu!” “Naomba nikuombe twende tukanywe chai” “Naomba nikusalimu!” etc etc Well, kwa ajili ya kumfurahisha nami nilikuwa nikimjibu kama atakavyo.

Jumamosi, 15 July

Siku ya Jumamosi ya tarehe 15 tulitoka kwenda kutembea walau tulijue jiji la Nairobi kiasi kabla hatujarudi makwetu kesho yake. Alinionesha vyema maeneo ya katikati ya jiji hilo ambako kuna msongamano wa watu na magari mengi hadi unashangaa. Tulianzia huku chini railway, tukapanda kwa miguu kuelekea club maarufu ya F2, kisha tukaingia Kimathi street, tukaenda mpaka Odeon na kuchepuka kuelekea river road. Tulipata mahali tukakaa na kupata mlo wa mchana ambapo kwa mbele yetu kulikuwa na kiji hotel kama sikosei kaliitwa EXPATRIATES & DIASPORA HOTEL.

Nilimtania kuwa itabidi niingie pale walau kwa nusu saa tu maana na mimi ni expatriate. Kimzaha mzaha tukajikuta tumo ndani ya hoteli ile na haikuwa hadi mida ya saa kumi na mbili jioni ndipo tulipotoka kurudi chuoni. Tuliamua kutokuliongelea kabisa lililotokea mule ndani kwani hakuna aliyekuwa amepanga litokee wala kujua madhara yake muda huo.

12 April 2009, 2335hrs …Arusha

Baby I know that you like me, you my future wifey
Soulja Boy Tell 'Em, yeah
You can be my Bonnie, I can be your Clyde
You could be my wife, text me, call me


Ilikuwa ni ringtone ya simu yangu. Ndiyo kwanza nilikuwa nimepanda kitandani ili nilale. Nilinyanyuka na kuchukua simu lakini kabla sijaipokea nikaangalia na kukuta ni namba nisiyoifahamu. Kuangalia vyema zaidi haikuwa hata ya Tanzania. Ilianza na +254.

Kwa wasiwasi niliipokea, “Hello!”

“Hi! Mentor” Iliitikia sauti ya pili.
Alikuwa Catherine.
Mh! Kwani bado alikuwa na namba yangu? Miaka yote hiyo? Mbona hakuwahi kunitafuta? Kwa kiasi moyo ulifurahi kusikia sauti yake na kujua kuwa bado kumbe ananikumbuka. Ila yalioendelea baada ya hapo yalinifanya nikachanganyikiwa kabisa, sikuelewa, sikuamini sikujua nifanyeje, nikatamani nisingeipokea simu ile.

Catherine alinikumbushia siku ile pale EXPATRIATES & DIASPORA HOTEL na kwamba tendo lile ambalo tulilifanya mule ndani bila vizuizi vyovyote lilipelekea yeye kushika mimba na tarehe 17/04/2007 alijifungua mtoto wa kiume, Nelson.

Aliendelea kuniambia eti, hakutaka kuniambia kabisa na hata hivyo ameniambia tu kwa sababu wazazi wake wamemlazimisha. Alijua sikuwa na nia ya kumpa mimba hivyo pia sikuwa tayari kulea na huenda ningeikana mimba ile kama angeniambia. Ndiyo maana aliamua kukata mawasiliano kabisa ili nisifahamu chochote kuhusu yeye. Sikukumbuka hata kumuuliza alipoipata namba yangu ya simu maana sikumbuki kumpatia kipindi kile.

Sikujua nifurahie habari zile au nisikitike au nifanyeje, kifupi nilichanganyikiwa. Nilishindwa cha kumwambia ila ilinibidi na mimi kuwaeleza wazazi wangu ambao (hasa mama yangu) walisikitika na kukasirika sana. Walisema jambo hilo kamwe haliwezi kuongelewa kwenye simu. Itanibidi kupanga safari mimi na Catherine wote twende Moshi tukalizungumzie hilo swala akiwepo na mtoto, Nelson.

“We Mentor! Acha uongo! We unaaminije kuwa ni wa kwako! Huo ni uongo! Yani miaka yote hiyo mtu ana mtoto wako asikuambie! Mentor unanidanganya! Miaka mitatu ni mingi sana kutokumwambia mtu! “ alidakia Tinna kwa maswali mengi.
Na kabla sijamjibu akaendelea, “Ulikuwa unampenda huyo dada? Kwa hiyo ukikuta ni wako utaamuaje? Utabaki na huyo dada? Kwahiyo ndo unamaanisha nini? Mentor mi siamini hata kidogo, haiwezekani. Kwa nini asikuambie miaka yote hiyo…”

Tinna alikuwa na kila sababu ya kulalamika na kutokuamini hadithi ile kwani kwa upande mmoja ni kweli haikuwa na mashiko. Ila nilidhamiria kuisimamia kama vile ni ya kweli. Nilimwambia tu kuwa nilichanganyikiwa sana kupata habari zile ndiyo maana akawa ameona mabadiliko yale kwenye mawasiliano yetu.

“Hapana Mentor! Mi siamini!” Alilalamika Tinna.

Maneno haya yalinifanya nihamie Plan C kwani nilihisi uongo wangu haujajitosheleza kumfanya Tina aniamini na aniache kwa amani. Kwa kuwa tulikuwa peke yetu chumbani kwangu nilianza kutoa machozi huku nikimweleza jinsi ambavyo mimi mwenyewe nilikuwa nimechanganyikiwa kwa habari ile. Hadi leo siamini kama ni mimi niliweza kulia vile. Nilionesha wazi kuwa nimechanganywa sana na habari ile na nilichomuomba Tina ni kuniacha tu peke yangu niwaze na pia niende Moshi nitakapofika na kujua hali halisi ndipo nitakapoweza kufanya maamuzi. Ilimbidi sasa Tinna aanze kunibembeleza mimi kwani aliona jinsi nilivyoumizwa na kuathiriwa na hali ile.

Nilimuomba Tinna tuwe tu tunawasiliana kama marafiki kwa kipindi kile hadi nitakapojua mustakabali wangu na Kate, mama Nelson. Hofu yangu kubwa ilikuwa kuleta drama/scene kubwa kiasi cha kuharibu cover yangu maana hakuna mwanafunzi aliyekuwa akijua kuwa mimi ni askari na pia kwa kufahamu yeye alikuwa binti wa waziri, ingeweza kuniletea shida si tu shuleni, bali hata kazini.

Nilifanikiwa kumaliza chuo salama salimini huku tukiachana na Tinna kwa amani. Nilirudi kituoni kwangu mkoani Arusha ambapo nilihamishwa kikosi kutoka FFU kwenda kazi za kawaida ambapo nilikuwa nikifanya ofisi ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD) kama mhasibu wa wilaya.

2010, July

Bahati nyingine iliniangukia miezi michache baada ya kumaliza masomo yangu. Kutokana na elimu yangu na utendaji wangu wa kazi (tangu kuajiriwa sijawahi kupatwa na shitaka lolote la kiutendaji/nidhamu), nilichaguliwa kwenda kozi ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi almaarufu kama 'makirikiri' na baada ya kozi nilibaki kuwa mhasibu wa Polisi wilaya ya Arusha. Mara mojamoja nilikuwa nikienda vituoni ili na mimi nijifunze kazi za Polisi kwani ukweli ni kwamba huwezi kukaa tu ofisini kila siku mwishowe utakuwa kiongozi na hujui chochote.

No comments:

Post a Comment