Mimi ni Polisi: Kisa cha Mke wa Waziri
“Yanyukwe....Yakobolewe” (hii iliashiria kupiga makofi)“Ipo siku moja nitarudi nyumbani, kwa baba na mama nikiwa kamanda… (repeat)”
Weka changer…
“Mama nipokee, nimechoka zangu na safari, nimetoka zangu Msumbiji na bunduki yangu mkononi mama..(rudia kiitikio)”
“Malela! Malela! Malela (Malela)…Malela! Malela wangu namtafuta! Nimesikia Malela yupo Tabata, Malela! Malela! Malela wangu namtafuta”
Badilisha CD hiyo hatujafiwa hapa…
“Isamawela, isamawela..Isamawela Isamawela (isamawelaaa);
Tutamaliza, tutamaliza..tutamaliza, tutamaliza… (huu wimbo una-emotion jamani)”
“Ugonile ndaga (ugonile ndaga fijo) ugonile ndaga (ugonile ndaga fijo)
Ugonile ndaga fijo (ugonile ndaga fijo)
Wanyakyusa wosa (ugonile ndaga fijo)..ugondile ndaga fijo (ugonile ndaga fijo)
NA wapare/wachaga/wakurya/wajita/wasukuma/insert tribe (ugonile ndaga fijo)…ugonile ndaga fijo (ugonile ndaga fijo)”
“Mama Jeniii mamaa (mama Jeni), Mama Jeni (mama Jeni) ouoo (Mama Jeni)…;
Mama Jeni nitarudi (Mama Jeni), Mama Jeni (mama Jeni) ouoo (Mama Jeni)…”
“Mama bonge (eeh), hebu sikia (eeh) mwanao bonge (eeh) anavyolia;
Alizoea (eeh) chipsi mayai (eeh) soda bagia (eeh) na mishikaki;
Akaja depo (eeh) kuamka sa nane (eeh) ugali harage (eeh) bila kuungwa;
Na sasa boongeee..;
Bonge analia bonge (jamani bonge) bonge analia bonge…”
Ilikuwa tarehe 31/12/2011 usiku tukiupokea mwaka mpya wa 2012 tukiwa porini huku kuruta wakiendelea mafunzo yao ya kujiunga na Jeshi la Polisi (recruit course) mimi nikiwa kama Mkufunzi. Ulikuwa ni mkesha bila kupenda. Hapo kuruta walipiga disko kuanzia saa moja jioni hadi mwaka ulipoingia.
Nakumbuka mchana wa siku hiyo kuruta walipikiwa pilau ambayo kila mtu alitamani wangekula tu ugali kwani liligombaniwa na wala hawakushiba. Sisi tu waalimu kuwasimamia ilikuwa kama fatiki, hawazuiliki.
Mida ya kama saa nne niligundua wameanza kuchoka na sauti zinafifia nikawaambia wanyamaze nikawahadithia kisa kilichonikuta miaka ya mwanzo wa ajira yangu.
07th August 2001, Dar es salaam
Baada ya kumaliza depo nilipangiwa kufanya kazi mkoa wa Dar es salaam. Nilikuwa kikosi cha FFU na hivyo kazi yangu kubwa ilikuwa malindo na kuzuia fujo, ingawa kwa kipindi kile nikiwa Dar sikupata kushiriki sana kwenye kazi hiyo ya kuzia fujo. Moyoni nilikuwa natamani sana ningebahatika kwenda maana nilikuwa natamani niwapige virungu wale waliokuwa wakituita sisi ‘darasa la saba’.
Mimi nilijiunga na Jeshi la Polisi kwani ndiyo ilikuwa ndoto yangu. Tangu nikiwa mdogo nilikuwa napenda sana sare zao na magwaride yao na kwa kuwa nilikulia maeneo ya Moshi nilihakikisha nahudhuria sherehe zote za kipolisi ambazo zilifanyika pale CCP.
Nilifanikiwa kujiunga na Jeshi hili mara baada ya kumaliza kidato cha Sita. Nilipata daraja la pili katika masomo yangu ya ECA hivyo nikakosa fursa ya kusomeshwa kwa mkopo wa serikali. Kwa bahati mbaya wazazi wangu pia hawakuwa na uwezo wa kunilipia ada ukizingatia nilikuwa nikipenda sana kusoma masomo ya uhasibu.
Kwa ufupi ilinibidi nijiunge na Jeshi la Polisi ila moyoni sikukata tamaa nikajiambia ipo siku nitakuja kusoma masomo hayo ya uhasibu.
Maisha yaliendelea hadi siku hii ya tarehe 07/08/2001. Nilipangwa lindo kwa Waziri mmoja ambaye kwa minajili ya maadili ningeomba nisimtaje jina wala wadhifa.
Kupangwa lindo kwa viongozi kulikuwa na faida na hasara zake. Kulikuwa na viongozi waliokuwa na utu sana. Kama mmepangwa jioni mtaandaliwa maji ya kunywa au juisi, chakula cha jioni na mnakuta chumba chenu cha ulinzi (centry box) kimepulizwa dawa ya mbu na kufanyiwa usafi na asubuhi mnapewa chai kabla hamjaondoka. Mara nyingi huwa tunafika kabla kiongozi hajarudi nyumbani kutoka kazini na kama nilivyosema, kwa wale waliokuwa na utu basi baada ya kufika aidha angetusalimia kutujulia hali palepale getini au akishafika ndani angetoka kuja kuzungumza nasi japo maneno mawili matatu. Hakukuwa na lazima kufanya hivyo, lakini bado naamini ni utu na jambo jema la busara.
Sitaongelea kwa waziri mmoja hivi ambaye ukifika kwake hata salamu haji kuwapa, hakuna huduma yeyote mnayopewa na anawapita kama hawaoni. Ila sasa uchelewe kufika lindoni kwako kwa dakika moja tu, kesi yake utaisimulia. Alikuwa akipenda kutugombeza hata kwa mambo bayana yaliyokuwa nje ya maamuzi yenu. Kwa mfano, kwa kuwa sote tulikuwa tukitumia lori moja kwenda malindoni, haikuwa ajabu sisi kufika lindoni tukiwa tumechelewa. Hata hivyo, kwa kuwa wale tunaokuwa tunawapokea wanakuwa wanasubiria lori hilohilo kurudi kambini, hakuna kipindi lindo lingebaki wazi.
07/08/2001…Jumanne
Siku hii nilipangwa lindo kwa mheshimiwa waziri huyu. Ilikuwa lindo la asubuhi. Kama kawaida na sheria, inatubidi tufike eneo la lindo robo saa kabla ya muda wa lindo. Na kawaida yangu nilikuwa napenda sana kutunza muda. Hata askari wenzangu walikuwa wakijua na wengi walikuwa wakifurahi ukipangwa lindo ambalo Mentor ndiyo anakuja kuku-leave unafurahi kwani una uhakika wa kuondoka kazini kwa wakati.
Tulifika nyumbani kwa waziri saa 05:45 asubuhi na kukabidhiana lindo na kisha kuanza kuzunguka kuhakikisha kote ni salama.
Ni hadi ilipofika saa kumi na mbili na nusu asubuhi niliposikia kelele za mtoto akilia. Alikuwa ni mtoto Tina. Tina alikuwa darasa la sita na asubuhi hiyo kama asubuhi nyingi ambazo nimewahi kuwa lindo kwa waziri huyo alikuwa akilia kwa kutokutaka kwenda shule. Mama yake alisikika akimkaripia kuwa avae haraka asijeachwa na basi la shule.
Kalikuwa na akili lakini kalidekezwa sana. Ni wale watoto waliorushwa madarasa kwani pamoja na kuwa darasa la sita alikuwa ameruka darasa la kwanza na la tatu hivyo kihalisia alikuwa mdogo.
Tinna alitoka nje huku akilia; hajavaa tai, viatu, hajabeba begi wala kuchukua ‘lunch box’ yake. Nilimuangalia anavyolazimishwa kwenda shule nikakumbuka wakati nipo kijijini. Nilimuonea wivu kwa bahati anayoipata ya kuweza kwenda shule kwa starehe vile. Nilitamani bahati ile ingeniangukia mimi. Nilishindwa kuendelea na shule kwa kuwa mama yangu mjane alishindwa kunilipia ada ya chuo baada ya kushindwa kupata daraja la kwanza hivo kuwa vigumu kupata mkopo wa kusoma chuo.
Mama Tinna alimwita Tinna nje mkononi akiwa amebeba viatu vyake. Tinna alikataa kuvaa viatu akisema hataki kwenda shule.
Ndipo mama yake Tinna alipotamka maneno ambayo hadi kesho hayatokaa yafutike akilini mwangu. Mama Tinna alimshika Tinna kwa nguvu na kisha akamwambia (huku akininyoshea kidole), “Ukikataa kwenda shule utakuja kuwa kama Yule pale.”
No comments:
Post a Comment