Monday, January 27, 2014

Nakungojea

Nakungojea...




Ngoja niombe kalamu, nitume zangu salamu,
kwa mtoto wa Kilamu, uzuri we ka tunda damu,
mwingine simfahamu, yeye tu anipa hamu,
kwake naziba fahamu, anipavyo nafahamu!

Wangu wa moyo kipenzi, uzurio nauenzi,
si kwamba hauna wenzi, ndo maana natunga tenzi,
wajapo wengi wakwezi, si wote wataka nazi,
wakileta upuuzi, watimue waziwazi!

Najua fimbo ya mbali, kamwe haina makali,
na sisi tulivyo mbali, penzi usilibadili,
nipende kwa kila hali, siku moja tule wali,
na nyama yake fahali, matunda ya kujijali!

Pendo la kweli hungoja, vumilia bila hoja,
hushinda vyote vioja, vya wale waso na tija,
kimbia wanapokuja, kasema dada mahija,
upendo ni namba moja, vingine vyajikongoja!

Si mwingi muda nadhani, utakuja wewe hani,
na siri iwe hewani, waelezwe na wageni,
"walopendana kifani, leo wako harusini,
waliitunza imani, sasa wamo furahani!"



Wasalaam wapendwa,
Mentor.


"At the touch of love, everyone becomes a poet." - Plato

No comments:

Post a Comment