10th January, 2014,
Ijumaa
“Mwizii,
mwiziiii, mama mwiziiiii, kaniibiia mwiziiiiiiii….nisaidieniii kaniiibia,
mwiziiiiiiiiiiiiiiiiiiii” Niliisikia sauti ya kike ikiita kwa nguvu. Haikuwa
ikitokea mbali na nilipo. Nikageuka kuona huyu mwizi yuko wapi nami nione kama
nitaweza kumsaidia mrembo huyu.
Niliona
vijana kadhaa pembeni yangu wakiokota mawe. Ghafla, nilihisi kitu kizito
kikinipiga maeneo ya kichwani….
26th October, 2012,
Ijumaa
Ngo
ngo ngo…Mlango wa ofisini uligongwa.
Mimi:
“Karibu”
(huku
akifungua mlango) “Asante” iliitikia sauti nyororo, nyepesi, laini ambayo kwa
zile flash-seconds chache kabla sura haijajitokeza, kichwani kwangu nilikuwa
tayari nimeshatengeneza sura na umbo la mhusika hata bila ya kumuona.
Aliingia
binti mmoja mweupe, mrefu wa wastani. Alivalia blauzi nyeupe ambayo ukiikazia
macho utaona vyema muundo wa tochi mbili zilizosimama vyema kifuani pake zikiwa
zimeshikiliwa na bra ya buluu mpauko ambayo ilivaliwa zaidi kama urembo kuliko
kutimiza kazi yake. Chini alivaa sketi nyeusi ndefu iliyoshuka vyema na mwili
wake mwembamba lakini uliojengeka sehemu stahiki hadi kuja kuungana na kiuno
chembamba kilichoonekana dhahiri kutokana na kuchomekewa kwa ile blauzi.
“Habari
ya saa hizi kaka”
“Nzuri,
karibu, karibu ukae” (huku nikimuonesha kiti cha pembeni na kumkaribisha)
Kwa
kweli hapa nilikumbuka mafundisho yote ya huduma kwa mteja na nilijitahidi
kuweka na madoido mengine kuhakikisha kuwa mteja wangu huyu anaridhishwa na
huduma yangu hadi atakapoondoka ofisini pale. Kabla sijaanza kumuuliza shida
yake alianza kuongea.
“Naitwa
Asha Daudi, natokea Kikulacho Company.
Tunatangaza bidhaa zetu za king’amuzi hiki cha Kikulacho (huku akitoa
makaratasi na kunikabidhi). Ni king’amuzi kizuri, and we offer competitive
prices. Ukikubali kununua na kujiunga nasi basi utafungiwa king’amuzi chako
bure na kupewa huduma ya matengenezo kwa miezi mingine mitatu kama kutatokea
tatizo lolote.” Nilivutiwa na jinsi mrembo huyu alivyokuwa akiongea.
“Asante
sana dada, tena ni kama bahati maana siku za hivi karibuni nilikuwa nachagua
kipi king’amuzi bora kwa nyumba yangu.” Nilijitahidi kutupia macho kwenye
karatasi alizonipatia Asha. Akili yangu ya kibazazi ilikuwa ishawaza pengine.
“Ooh
naona hapa premium ndo mnaonesha na channel za michezo eeh.” Niliuliza
vimaswali vya hapa na pale ambavyo ilimbidi asimame na kuja kunielekeza kwa
ukaribu zaidi. Ni hatua zisizozidi sita kutoka kiti alichokuwa amekalia kuja
nilipo lakini alizitembea kama vile yupo kwenye mashindano ya ulimbwende.
Alikuja na kuinama mbele yangu huku akiacha sehemu ya kifua ikiwa wazi na
kunifanya hata nisimuelewe alichokuwa akikisema.
“…ndo
hivyo iko, wewe ulikuwa unafikiria kipi hasa?” Ndicho nilichobahatisha
kumsikia.
Ilibidi
nijibaraguze na kazi hivyo nikamuomba aniachie karatasi zile nifanye maamuzi
baadaye kwani nina kazi ‘pressing and urgent, running towards its deadline’
nilitakiwa kuifanya kwa ajili ya ‘final presentation’ kwa ‘board of trustees’
hivyo nisingeweza kutafakari na kufikia uamuzi kwa wakati ule. Alinishukuru na kuaga kuondoka.
“Errr…samahani!”
(Nilimwita kabla ya kufungua mlango)
“Bila
samahani kaka” (aliitika kwa tabasamu la mbali lililonifanya nipaliwe kwa
kumeza fundo kubwa la mate ya tamaa)
“Niandikie
namba yako hapa kwenye karatasi yako basi tutaongea baadaye nikipata nafasi ya
kuangalia hizi karatasi in case nitakuwa na swali” (nilijibaraguza na maelezo)
Alirudi
na kuniandikia namba zake kisha akaniaga na kuondoka huku nyuma akiniachia
simanzi la moyo na akili ilianza kutafakari ni mbinu gani nitatumia kumpata
binti huyu, Asha!
Haikuchukua
siku nyingi kwani Jumapili tu nilimpigia simu Asha na kupiga naye stori mbili
tatu. Nilimjulisha kuwa ningependa kufahamu jinsi ya kulipa na vitu kama hivyo
na aliniahidi kuwa angepita tena ofisini siku inayofuata kunipa malekezo zaidi.
Haikuwa
hadi Jumatano ambapo Asha alikuja nami nikamuomba kwa kuwa sikuwa na kazi
nyingi basi twende tukapate chakula cha mchana pamoja. Kwa shingo upande
alikubali kwani alisisitiza kuwa anatakiwa kwenda ofisini kurudisha majibu ya
kazi za siku hiyo. Ushawishi wangu pia haukuwa haba hivyo alikubali. Tuliongea
mengi yasiyohusu kazi na ndipo nilipofahamu kuwa alikuwa amemaliza shahada yake
ya kwanza ya masomo ya utawala wa rasilimali watu. Tatizo kubwa lilikuwa kupata
ajira kwa fani aliyosomea hivyo wakati akisubiria kuitwa kwenye usaili wa kazi
alizo-apply hakuwa na budi kujishikiza hapo kwenye kampuni ya ving’amuzi ya
‘Kikulacho.’
Kwa
kifupi alitangaza dhiki. Ndipo ubazazi wangu ukajua njia ya kupitia kutimiza
adhma yangu kwa Asha. Tulimaliza kula na kabla ya kuagana nilimpatia elfu
hamsini na kumsisitizia kuwa itamsaidia kusogeza siku kwani nafahamu kuwa
commission anayolipwa haitoshelezi mahitaji yake. Alinishukuru sana. Tukaagana
na kuendelea na shughuli zetu kila mmoja.
Tuliendelea
kuwasiliana sana kwa simu huku akiulizia lini nakuja kulipa king’amuzi. Hakujua
kuwa hata mpango wa kulipia king’amuzi sikuwa nao. Tulizoeana mpaka kufika
wakati alikuwa akija ofisini jioni baada ya muda wa kazi tunaenda Mary’s, au
breakpoint tunapata mbili tatu huku tukipiga stori za hapa na pale tukingojea
foleni zipungue. Alikuwa tayari amenichukulia kama rafiki yake na akilini
mwangu nilishaamua kuwa ni muda wa mashambulizi.
Nilimchombeza
kuwa Ijumaa moja twende zetu Kigamboni (kipindi hiki nilikuwa bado nikiishi
Gongo la Mboto, Kitunda). Mwanzoni alitaka kusita lakini baada ya ushawishi
mwingi na ahadi za uongo za ‘sitofanya lolote usilopenda nifanye’, alikubali.
Baada
ya wikiendi ile, Asha alifanya kosa kubwa…alijihalalishia uchumba! Alikuwa
akiwafahamu baadhi ya rafiki zangu ambao mara nyingi tulikuwa tukikutana jioni
nikiwa naye. Na kama kawaida yetu kila utakayekuja naye wao wanamuita, ‘shem!’
Asha hakulifahamu hilo, alidhani alikuwa ‘shem’ peke yake. Niliendelea kujilia
vyangu kiulaini kwani sasa ameshakuwa shem wao.
Tatizo
lilianza kuja nilipotaka uhuru wa kufanya ‘yangu’. Asha alishakolea kwangu
kiasi kwamba akataka kuninyima uhuru. Ulikuwa ni wakati wa kukata kamba. Kwa
mantiki hyo kulikuwa na haja ya kusitisha mkataba haraka iwezekanavyo kwani
kulikuwa na wateja wengine in-line wakingojea kuhudumiwa nami. Kwa uzoefu wangu
nilijua mbinu pekee ya kumuacha Asha ilikuwa kukatisha mawasiliano haraka
iwezekanavyo.
Kwanza
nilijipa safari ambapo huko ‘safarini’ hakukuwa na mtandao ila sasa hizo baby
na honey kwa kweli zilinikera. Alikuwa akiota ndoto za mbali sana. Nilirudi
‘safari’ ila niliendelea kukaa kimya hadi alipoona mwenyewe hapa niliuziwa
cover la ‘Olympus has Fallen’ ilhali ndani kuna CD ya King Mzee Majuto.
Baada
ya ukimya usio na maelezo na meseji zisizojibiwa, alijikatia tamaa. Kama
kawaida alinitumia ujumbe mfupi wa vitisho kuwa lazima atalipiza kisasi siku
moja kwa niliyomfanya.
“Ha
ha ha” nilijichekea moyoni kwani kama ni visasi basi hakika ningekuwa na kijiji
cha watu wenye kutaka kulipa kisasi kwa orodha ya niliowapitia na kuwaacha
kwenye mataa. Nilifarijika zaidi nilipopata habari kuwa Asha amepata kazi
mkoani Dodoma na hivyo hatutakutana tena jijini hapa hata kwa bahati mbaya.
Maisha
yalisonga mbele…
10th January 2014,
Ijumaa 1550hrs
Nilifunga
ofisi mapema kwa matarajio ya kuwahi nyumbani kujiandaa na safari ya Morogoro
kesho yake. Ilikuwa safari ya kikazi lakini pia nilikuwa na miadi na Clara,
mwanafunzi wa Mzumbe ambaye tulikutana juzi juzi Dar walipokuwa likizo za
Christmas na mwaka mpya. Niliipania sana safari hii.
Ni
kwa sababu hiyo niliamua kuacha gari ofisini ili kesho yake nisipange foleni ya
kungojea pantoni niwahi tu safarini. Hivyo nilijikuta nikitembea kuelekea
ferry. Kutokana na matengenezo yanayoendelea ya barabara za mabasi ya BRT eneo hilo
kuna vumbi sana hivyo inakubidi kutembea ukiwa umefungua macho kwa mbali.
Nikikaribia
kabisa pale ambapo pikipiki na bajaji nyingi hupaki niliiona sura ambayo
ilinivutia macho. Binti mmoja mrefu wa wastani, mweupe, amevalia sleeveless top
ya pink na suruali ya buluu. Nilijikuta nikibadili uelekeo ili walau nimfikie
binti yule. Alikuwa katika msongamano wa watu waliokuwa wametoka kwenye pantoni
wakielekea mjini. Akili yangu iliwaza jambo moja tu, ‘nikifanikiwa kumsalimia
tu…’
Kwa
bahati macho yetu yaligongana, na ni kama alikuwa amesoma mawazo yangu kwani
naye alijitahidi kupenya kwenye msongamano ule kunielekea mimi. Nilitabasamu
moyoni. Tulielekeana huku nikimkazia macho yenye tabasamu la mbali. Alikuwa
ameyakaza macho yake kwangu kwa jinsi ambayo kwa wakati ule sikuwa nimeelewa
sababu.
Ha!
Haikuwa sura ngeni! Oh maama…alikuwa Asha Daudi!!!! Katika hali ile ya mshituko
sikujua hasa lengo langu lilikuwa kumpa mkono au kumkumbatia, ila na yeye
alikuja hadi kunigonga kabisa. Ndipo ghafla nikazisikia zile kelele…
“Mwizii,
mwiziiii, mama mwiziiiii, kaniibiia mwiziiiiiiii….nisaidieniii kaniiibia,
mwiziiiiiiiiiiiiiiiiiiii” Niliisikia sauti ya kike ikiita kwa nguvu. Haikuwa
ikitokea mbali. Nikageuka kuona huyu mwizi yuko wapi nami nione kama nitaweza
kumsaidia mrembo huyu. Alikuwa ni Asha anapiga kelele za kuibiwa. Sikuelewa
ameibiwaje na mimi nilikuwa karibu naye kabisa na nisimuone mwizi yule.
Ni hadi
aliponyoosha mkono kunielekea ndipo nilipoelewa…alikuwa amedhamiria, alipanga!
17th January, 2014
Ni
leo nimeruhusiwa kutoka hospitali kwa kipigo cha mbwa mwizi nilichokipokea siku
ile. Kama sio askari waliokuwepo karibu na mahali pale, basi leo ningekuwa na
jina lingine. Nimeambiwa natakiwa kwenda kujibu kesi mahakamani. Nashindwa
kuelewa kama hakimu ataniamini nitakapomueleza hadithi hii.
Wasalaam
wapendwa,
Mentor.
No comments:
Post a Comment