Mimi ni Polisi: Kisa cha Ashura wa Kahama
18th February 2014
Pamoja na mengi yaliyonitokea ambayo nitayasimulia siku nyingine, leo nimekumbuka kisa kilichonitokea miaka sita iliyopita.
29th December 2007 06:40am, Mbeya
“Kundiiiii sawa!”
“Mguu pande!”
“Mwili regeza”
…alikuwa ni meja wa kambi, RSM, afande Ruta. Kipindi hiki nilikuwa nikifanya kazi kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) mkoani Mbeya. Nilibahatika kuwa kati ya askari wachache ambao tulitoka nchini Marekani kwa mafunzo maalumu ya kuzuia ghasia sehemu zenye milipuko. Mfano ni kama sehemu zenye migodi ambapo kukitokea fujo labda wafanyakazi wake wanaweza kutumia milipuko kushambulia raia ama hata Polisi.
“Hiiiiiiiit!!!” Alipayuka afande Ruta na kutushitua wote ambao tulikuwa tumekusanyika uwanjani asubuhi kwa ajili ya maelekezo na ukaguzi kabla ya kuelekea kazini. Amri hii iliashiria wote tukae tayari kwa amri itakayofuata.
“Wote sawa! Tulia kabisa…”
Aligeuka nyuma kiukakamavu ndipo tulipomuona mkuu wetu wa kambi (OC FFU) akiwasili uwanjani hapo. Mara nyingi wakati wa ukaguzi wa asubuhi afande wetu huyu huwa hafiki na akifika ujue kuna jambo siriazi sana anataka kuongea.
Alitukumbusha sana walimu wetu wakuu enzi za sekondari. Ilikuwa ukimuona mwalimu mkuu anakuja paredi asubuhi lazima kuna mtu atafukuzwa hiyo siku.
Afande RSM Ruta aligeuka na kupiga saluti kisha akaendelea, “Timamu afande, Beta-kenda-nne-kenda -nane sajini meja Ruta…. ” Aliendelea kutoa ripoti ya asubuhi na kisha kumkaribisha afande kuongea.
“Askari, Habari ya asubuhi” Alitamka afande OC kwa sauti nzito yenye amri.
“Nzuri afandeee!” Nasi tuliitikia kwa ukakamavu kabisa.
“Imekuja amri ya uhamisho kutoa Makao Makuu, “ aliendelea. “Wale askari waliotoka kozi wamepangiwa mikoa mingine ili kusaidia kufundisha na wengine waliyoyasoma. Hivyo RSM atawasoma majina na mkimaliza mje ofisini kuandikiwa vibali vya safari. Amri hii ni ya mara moja.”
Katika watu waliopangiwa kuhama nilikuwa mmojawapo. Nilisikitika sana kwani pale mkoani Mbeya nilikuwa nimepapenda sana kutokana na hali ya hewa na urahisi wa maisha hasahasa vyakula…hasa maharage (sina maana hiyoooooo!) Lakini pia nilisikitika kwani mkoa niliopangiwa sikuwahi kuufika kabisa wala kupita tangu nizaliwe. Nilipangiwa mkoa wa Shinyanga.
08th January 2008
Niliwasili mkoani Shinyanga na kwenda kuripoti kwa Afisa Mnadhimu wa mkoa. Nilielekezwa kwenda Kahama ambapo ndipo kwenye kambi nitakayoishi kwa wakati wote nitakaofanya kazi Shinyanga. KWa kweli baada ya kuuzoea mkoa wa Shinyanga ndipo nilipokuja kugundua kuwa Kahama pamechangamka kuliko hata Shinyanga mjini penyewe.
Nilipelekwa Kahama badala ya kukaa kambi ya FFU Shinyanga Mjini kwani nilitakiwa kuwafundisha askari wa pale baadhi ya masomo ya kule. Walikuja askari wengine kutoka mikoa mingine jumla tukawa sita. Kutokana na kambi ya askari Kahama kuwa na eneo kubwa ilikuwa rahisi kukusanya askari waliochaguliwa kutoka wilaya za Kishapu, Maswa, Bariadi na nyinginezo kwa ajili ya kozi hiyo.
Maisha yaliendelea hadi siku nilipokutana na Ashura. Mtoto maashallah! Kitendo tu cha kutia macho yangu juu yake moyoni nilishawishika kuwa huyu ndiye. Ni katika wale mabinti ambao pamoja na kujisifu kote kwa ujuzi wangu wa kuongea na wanawake, ukikutana naye moyo unaenda moyo na kukosa maneno ya kusema…kigugumizi!
Ashura alikuwa akiishi maeneo ya jirani na kambi ya polisi Kahama hivyo nilitokea kuwa namuona kila mara. Alininyima usingizi lakini ndo hivyo nilikosa kabisa ujasiri wa kwenda kumwambia. Siku moja nilikutana naye barabarani nikiwa nimevaa sare zangu za kazi nikamsimamisha. Huwa nikiwa nimevaa uniform zangu na ukute ni Jumatatu hivi nimeng’arisha pua ya buti hadi najiona, sare yangu ya ‘jungle green’ (raia wanaziita ‘zile nguo za fidi fosi’) imepigwa pasi ya mkaa vizuri imenyooka na kunata na mwili napata ujasiri wa ajabu kama vile dunia yote ni yangu.
Aligeuka akaniangalia kwa jicho la upande akasema, “Siongeagi na mapolisi mimi.” Duh! Nilikosa pozi kabisa ila nikajikaza nikamwambia sawa dada. Nilirudi kambini na mawazo sana kichwani jinsi gani hata nitaweza kumfanya Ashura akanisikiliza walau.
Haikuwa hadi miezi miwili baadaye nilipokutana naye stendi akitoka kwa Shangazi yake huko Bariadi. Na mimi nilikuwa nimetoka Shinyanga mjini. Nilimwendea na kumsalimia ambapo aliitikia japo baada ya kunikumbuka tabasamu lake lilipotea. Alikuwa na mizigo ambapo nilijitolea kumsaidia na kwa kuwa ilikuwa mingi na asingeweza kuibeba mwenyewe ilimbidi kwa shingo upande akubali.
Ni mwendo wa dakika kumi hadi kumi na tano tu kutoka Stendi hadi aishipo Ashura lakini nilizitumia vyema kuhakikisha Napata kidate na Ashura. Tulikubaliana kukutana jioni karibu na kanisa katoliki.
Jioni tulikutana na kwa kuwa alikuwa ameshanikataa mwanzoni nikaingia kwa gia nyingine hivyo nilimwomba twende Pine Ridge ‘for drinks’. Tulienjoy sana kuwa pamoja na ukiachia upolisi wangu, Ashura alionesha kufurahia kuwa na mimi. Ila tangu mwanzo alisisitiza yeye haamini maaskari.
Ilinichukua muda kumshawishi Ashura kuwa maaskari hatuko hivyo anavyotudhania lakini hakuelewa. Baada ya kuzoeana kwa muda nilimtamkia kuwa ningependa kumuoa. Ashura alikataa katukatu kusikia hiyo habari. Aliniambia maaskari ni wahuni na malaya wa kutupwa na atakuwa kipofu kumkubali askari.
Sentensi yake iliniuma lakini nilijipa moyo na kupiga moyo konde kwani hakuna mkate mbabe mbele ya chai. Niliendelea kumchombeza bibi Ashura anikubali lakini inaonesha alishalishwa sumu ya umalaya wa mapolisi. Nilijiwazia nyakati ninafanya kazi Dar es salaam, Mbeya, Kilimanjaro au nilipokuwa ulinzi wa mipaka kule Kigoma. Ni kweli kulikwa na vishawishi vingi tena kwa kijana ambaye hajaoa vingetosha kuwa visingizio vya kudumbukia kwenye ubazazi. Nakumbuka hata wale maafande waliokuwa wameoa iliwabidi kufanya vile ili kupunguza msongo wa protini mwilini. Ingawa sikumwambia lakini nilimhakikishia kuwa akinikubali yote hayo yatakuwa historia na mimi si kama hao aliowaona. Ashura alikataa katukatu.
Ashura alinisimulia walivyokuwa wadogo. Nyakati wanakuwa ukitaka msichana alie walikuwa wakimwambia, “Utaolewa na polisi” Yani anaweza kulia mpaka asubuhi. Hivyo ndivyo alivyokuwa akijua mapolisi ni wahuni na kwa kuwa alikuwa akiishi karibu na kambi ya Polisi (kwa maneno yake) aliwaona walivyokuwa wakifanya.
Nilibahatika kufahamiana na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Kahama, Afande Mayala, ambaye kwa bahati mbaya au nzuri alipangiwa kufanya kazi kwa ndugu zake kabisa hapo. Aliniambia, “Bhangosha, utawaweza hawa ndugu zangu wewe? Kama hujala donna hapa unaweza ukafia kitandani.” Alisema kiutani lakini mimi nilimhakikishia kuwa Ashura nimempenda na nilimwomba anisaidie kusema naye ndugu yake huyo akubali kuwa mke wangu. Niliamua Ashura ndiye! Kwanza alionekana mwenye adabu na kalelewa vyema.
Afande Mayala alijitahidi kuongea na Ashura na kumwelewesha kuwa mwenzake Mentor nimefika kwake. Ashura alisimamia msimamo wake kuwa mapolisi ni Malaya! Baada ya muda mrefu wa kumuomba alimwambia afande Mayala, “Labda tukapime kwanza kabla hata sijakubali. Lakini haimaanishi ndo nitamkubali…tukapime kwanza Sezae!”
Afande Mayalla alinipigia simu na kunieleza kuhusu hilo suala. Kiukweli nilimpenda Ashura ila lilipokuja suala la kupima ndipo akili yangu ilipogota. Ni kweli sikuwa na dalili zozote za kuukwaa ugonjwa huu na kweli mimi wakiitwa wahuni ninaweza kuwa mtu wa mwisho mstarini, lakini hata pale nilipoteleza vipi palikuwa salama? Nilihisi kijasho chembamba cha kukata tamaa kikinipitia. Nilitaka kumwambia yaishe lakini nilijipa moyo kuamini kama kupata UKIMWI ni hadi ulogwe.
Tulienda kupima Desemba 1, 2008 siku ya kuazimisha siku ya UKIMWI duniani. Nakumbuka kama mtu angeniangalia vyema angehisi kuwa tayari nimeshapokea majibu na mimi ndiye niliyeathirika. Ashura alikuwa anajiamini sana ambapo kwa kiasi niliongeza upendo kwake kwani nilijua hapa nimempata mke.
18th February 2014
Leo nimepokea taarifa kuwa Ashura amefariki kwa maradhi ya Upungufu wa Kinga Mwilini nimekumbuka jinsi alivyonikataa kwa kuamini mimi Polisi ndiye niliyeathirika. Natumaini kabla hajafariki alikuja kugundua upolisi haumaanishi umalaya na kwamba kila mtu ni malaya kama alivyo moyoni mwake na si kama akiwa Polisi.
Mungu ailaze roho ya mrembo Ashura (na hakuwa Polisi!) mahala pema peponi, Amina.
Wasalaam Wapendwa,
Mentor.
No comments:
Post a Comment