Sunday, December 29, 2013

Nimempata Asiyebadilika...

NIMEMPATA ASIYEBADILIKA…

DECEMBER 29, 2013, Kanisani

(singing) NIMEMPATA ASIYEBADILIKA,
YESU HAWEZI BADILIKA (repeat)

Kwa hali ya kushitua nilijikuta natokwa na machozi ambayo kwa kweli sikufahamu kama ni ya furaha au huzuni. Nilifurahia wimbo na ujumbe uliokuwepo kwenye pambio lile. Ghafla nikajikuta katika dimbwi la mawazo na kumbukumbu ya ile siku nilipompata wangu..wangu wa moyoni…asiyebadilika…

September 19, 2012 Chelsea vs Juventus
Kwa mbali niliikumbuka siku hii nikiwa na hisia mbilimbili. Moja ya hasira kwani pamoja na kutoa draw ya goli mbili tulishindwa kufuzu kuendelea hatua nyingine ya mtoano katika kombe la UEFA Champions League.

Mechi hii nilienda kuiangalia sebuleni (baa iliyopo karibu na unapoishi...kimjini tunapaita sebuleni). Katika kushangilia kulikuwa na kundi kubwa la watu ingawa kama kawaida wengi wao hawakuwa mashabiki wa Chelsea bali timu nyingine pinzani tena wakiwa wamevalia jezi za timu zao. Mbaya zaidi mechii hii ilichezwa wakati ambapo timu kama Manchester United, Manchester City na Arsenal tayari zikiwa ama zimeshajihakikishia ushindi kwa kucheza tayari au zilikuwa na uhakika wa kupita hata kwa kutoa suluhu.

Tuliendelea kushangilia mechi hasa baada ya goli alilolifunga Oscar Emboaba Dos Santos Jr. Ni wakati Juventus waliposawazisha ndipo nilipojua kuwa kuna hadi wadada ‘haters’! Dada huyu alikuwa amevalia top ya Arsenal iliyomshika vyema mwilini na jeans ya buluu mpauko. Katika ile furaha aliyokuwa nayo ndipo kwa bahati mbaya akanimwagia kinywaji alichokuwa amekishika kikiwa ndani ya glasi.

Kusema ukweli kabisa, angekuwa ni mwanaume amefanya vile ingekuwa ni kesi isiyoisha. Ila nilipogeuka na kumuona, kwanza ulimbwende wake ulinishtua, nilishindwa kukasirika kwani mbali na kufungwa goli lililotuondoa kwenye mashindano yeye na jezi yake ya Arsenal alikuwa akishangilia.
Kwa bahati na yeye alikuwa mstaarabu akaacha ghafla kushangilia na kuomba samahani huku akitafuta tissue ili anifute. Nami nilimuacha anifute huku nikimfanyia ‘body appraisal’. Kwa kweli alikuwa anavutia. Nikamtania kuwa itabidi anipe namba zake nimtafute kesho yake anifulie jeans yangu. Kiutani akakubali huku washikaji pembeni nao wakisapoti hilo na kama mzaha vile nikatoa simu yangu akaniandikia namba yake. Nikamsave kama ‘Arsenal’.

September 22, 2012 Jumamosi
Nilimpigia simu kumsalimia na kufahamu kama angekuwa sebuleni jioni hiyo tukaangalie wote mechi. Pia nilimtania kuwa nitamletea jeans yangu aifue. Alicheka, tukaendelea na hadithi mbili tatu kisha nikakata simu baada ya kupata uhakika kuwa tutakuwa wote jioni ile.
Kama kawaida alikuja na jezi yake ya Arsenal. Hii ilikuwa zile za njano ila za kwake ni zimeshonwa kama top.

Mentor: “Mh! Wardrobe yako yote ni jezi nini?”

Arsenal (akicheka): “hamna hujaniona siku nyingine ndiyo maana”

Mentor: “Na kweli..hiyo siku nyingine naomba iwe kesho”

Arsenal: “Kesho kuna nini?”

Mentor: “Aaah…nothing specific! Ila tunaweza kuipa jina tu…our own public holiday”

Arsenal” “Hahah haya bwana! Jeans yangu iko wapi?”

Mentor: “Nitakupa, ipo kwenye gari”

Basi tuliendelea kupiga stori huku tukingojea mechi zianze ambapo kama kawaida utani uliendelea hasa kila walipokuwa wakimuonesha Arsene Wenger akitweta kwa kutokujua lipi zaidi afanye dhidi ya timu pinzani. Mechi ziliisha na kila mtu alielekea kwake. Tulikubaliana kukutana kesho yake twende ufukweni kuogelea.

Huyu dada aliishaanza kuniingia akilini kidogo hasa kwa ulimbwende wake. Alipendeza sana alipovaa top zake za Arsenal…zilimkaa vyema mwilini mwake zikionesha vizuri miinuko ya wastani maeneo ya nyanda za juu kifuani na utambarare wa nyanda za kati tumboni huku kwa chini ikionesha vizuri muanzio wa umbile zuri la namba nane. Ile hali pia ya yeye kuwa shabiki wa Arsenal, timu ambayo ina miaka mingi haijachukua ubingwa wowote, ilinifanya niamini atakuwa binti mmoja mvumilivu.

Tuliendelea kuonana mara kwa mara huku akili yangu ikigombana yenyewe kati ya kuwa a good boy au naughty Mentor. Upande mmoja ulitaka nipige na kusepa ilhali upande mwingine uliniambia kuwa umri sasa umenitupa mkono na ni wakati wa kutafuta mtu wa kutulia naye. Hili wazo hunijia kila ninapokutana na binti mrembo ila huwa haikai sana kwa kuwa nikishapata nilichokitaka hamu ya kuendelea na mahusiano inakufa. Kwa huyu mlimbwende ilikuwa tofauti. Nilitaka kufanya jambo la tofauti. Nilifahamu fika kuwa nikisha*** huo ndiyo utakuwa  mwisho wa mahusiano yetu, Hivyo nilijiapiza kutomgusa mpaka siku ile.

Nakumbuka ilikuwa siku ya kumbukumbu ya kufariki kwa hayati baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, nilipofunguka kwake na kumueleza lengo langu kwake. Alionesha kushituka kwani alishahisi kuwa sina interest naye zaidi ya ushabiki wa mpira. Tuliongea mengi sana nikamueleza mpango wangu wa kutaka kufunga ndoa ifikapo mwisho wa mwaka 2013, tena nilimwambia hadi tarehe nilishaipanga kuwa ni jumamosi ya 14/12/2013 kwani ingekuwa pia kumbukumbu ya ndoa ya wazazi wangu. Nilitamani sana iwe hivyo…

Nilimueleza pia kuwa nisingependa kumgusa kabisa hadi siku ile ya ndoa kwani –ingawa hili sikumuambia- nilihisi tu nikishafanya naye ngono ndiyo itakuwa mwisho wa hadithi. Alifurahi kusikia hivyo na kunishukuru kwa kuonesha upendo wa kweli na kumuhakikishia kuwa nina mpango kweli wa kuwa naye. Wengi walishajaribu kumtongoza ila hata kabla hawajakubaliwa walishatangaza nia ya kutaka kuonja tunda hivyo alishakata tama na wanaume walio serious na ndoa kabisa.

Nilimuhakikishia kuwa mimi ndimi, na nitahakikisha kuwa hata kama Arsenal hawatachukua kombe (which was so obvious), basi mimi nitampa zawadi ya pekee.

Nilikuja kufahamiana na rafiki zake ambao wengi wanafanya naye kazi NSSF. Walikuwa wanapenda sana kuja kuogelea hivyo wikiendi nyingi tulikuwa nao. Wengi walikuwa na magari na niliona hilo kama jambo linalomsumbua hivyo nikawa nimemuambia kuwa nitatengeneza la kwangu nimuachie awe anaendesha mimi nitakuwa ninatumia gari la ofisini. Na kwa kuwa wikiendi tutakuwa wote tutatumia hilo moja. Alifurahi nami nililiona kama jambo jema. Kwa muda mfupi tuliokuwa tumefahamiana, alionesha kuwa mtu mwaminifu nami moyoni nilianza kujiambia kuwa sasa nimempata binti…mrembo, anayenipenda, mwenye tabia njema…tena asiyebadilika!

Nilikuwa na Honda CRV ambayo niliinunulia engine ya Starlet (hehe..mafuta budget!) na mpango ulikuwa kuipaka rangi na kubadili seats ndipo nimkabidhi siku ya birthday yake 09/03/2013. Nilitamani kutumia mshahara wangu kufanya jambo lile haraka, ila  moyo ulikataa kufanya vile kwani si vyema kutumia mshahara kuwekeza kwenye ‘liabilities’. Niliamua kama ni kupenda nioneshe upendo wote asipate kijisababu chochote cha kuwa na wasiwasi juu yangu.

November 29, 2013, Hindu Mandal Hospital
Mawazo yaliruka hadi wodi ya wazazi hospitali ya Hindu Mandal nilipoenda kumsalimia na kumjulia hali kwa kujifungua watoto mapacha, na sio wa kwangu.

December 29, 2013, Jumapili leo Kanisani

(singing) Mahali nimefika nimeona wema wako,
na sasa ninasema wewe ni Ebenezer (repeat).
Ni wimbo huu ulionishitua kutoka katika dimbwi zito la mawazo na haraka nikafuta machozi yaliyokuwa yakijitokeza kwa mbali na kuendelea na ibada.

Najipa moyo Mentor bado nitampata yule asiyebadilika, wa kuwa naye ambaye nitampa moyo wangu bila kuwa na wasiwasi wowote. Yule ambaye hatutakubaliana moja akafanye lingine. Ambaye labda nitajua akitakacho…ila kwa sasa bado nipo nipo.

Wasalaam wapendwa,
 
Mentor.

No comments:

Post a Comment