Wednesday, December 11, 2013

LLB

LLB (Elimu ya Watu Wazima)

04:29AM…

Alarm yangu iliita kuashiria ni muda wa kuamka na kuianza siku mpya. Kwa kawaida mimi hupenda kuamka mapema ili nipate muda wa kufanya mazoezi kidogo na sala ya asubuhi (morning devotion). Nilijinyoosha kivivu huku kisauti chembamba kikiniambia niendelee kulala japo kwa sekunde chache tu.

Kwa kupitia upenyo wa mlango uliokuwa wazi niliipata harufu nzuri ya kama chakula kitamu kilichopikwa na mpishi anayeijua vyema kazi yake. Ndiyo, ilikuwa ni harufu ya maandazi au jamii hiyo. Nilinyosha mkono kupapasa pembeni mwa kitanda na kukuta nipo peke yangu. Ndipo nilipogundua kuwa harufu ile haikuwa ikitokea mahali pengine ila jikoni kwangu na si mwingine bali mke wangu kipenzi ndiye alikuwa akikarangiza vitu vya kunukia namna ile.

Sikutaka kuwaza kwa nini aliamua kuamka mapema hivyo kuanza mapishi hayo ila moyoni nilifurahia. Niliamka kwa kunyata kuelekea jikoni. Nilimkuta mke wangu kipenzi ndani ya mtandio mwepesi (sio khanga) wa rangi ya udhurungi. Kusema kweli, mke wangu ni mzuri. Rangi yake ya maji ya kunde na umbo zuri lenye kung’aa. Michirizi myembamba ilishuka kiuchokozi nyuma ya goti na nywele ndefu nyeusi zilizoshuka vizuri kichwani mwake.

Nilimuangalia kwa jicho la kumtamani nikakumbuka kipindi tunakutana. Nilikuwa nimeenda Zanzibar kikazi na pamoja na kwamba alikuwa amejisitiri, uzuri wake ulionekana bado. Aliniambia anaitwa Fetty. Alipoongea nami tu nilijua moyoni kuwa huyu ndiye. Niliapa kwa juhudi zozote lazima nimpate. Na kama ilivyokuwa miaka miwili baadaye ndiye huyu mbele yangu – beautiful as ever - akikarangiza maandazi kwa ajili ya familia yetu changa ya mtoto mmoja.

Nilimfuata nikamkumbatia na kumbusu shingoni. Nilimwona alivyoshtuka na kusisimka hadi kutoka vipele vya msisimko akanigeukia akitabasamu. “Weeewe umenishtua ujue” alisema nami nikamuomba msamaha na kumuambia uzuri wake ulivyonichanganya nikashindwa kujizuia. Nikamuuliza kisa cha kuamka mapema vile na kuniacha kitandani mwenyewe akaniambia amejisikia leo kupika maandazi ya Pemba kwani ameyamiss na akaniambia nikiyaonja kila siku nitakuwa namdai anipikie. Nilimjibu haihitaji kuyaonja kwani ile harufu tu ilitosha kuniambia utamu wa maandazi yale.

Nilirudi chumbani nikiwa na tabasamu kwa mbali ila tabasamu lile lilipotea ghafla baada ya kukumbuka kuwa siku ile ilikuwa ya mwisho kubaki nyumbani. Nilitakiwa kurudi chuo UDSM kuendelea na masomo yangu ya sheria. Ah! Hii elimu ya ukubwani hii..nilijiwazia moyoni huku nikichukua taulo langu na kueleka bafuni. Nilirudi na kukuta chai ikiwa tayari mezani tukanywa huku nikipiga hadithi za hapa na pale na mke wangu. Ilinibidi kuondoka mapema kwani kuna mambo nilitakiwa kufanya mchana huo kabla sijaenda kuripoti chuoni.

Maisha yaliendelea vyema chuoni na nyumbani hadi nilipoingia semesta yangu ya sita chuoni, yaani mwaka wa tatu semesta ya pili. Kwa kweli masomo haya ya sheria yalikuwa magumu na nilikuwa nimejiapiza kuwa lazima nimalize na daraja la kwanza na si vinginevyo. Hivyo nilikuwa nabaki chuoni wikiendi nyingi nikijisomea. Pamoja na yote hayo nilijitahidi kupiga simu nyumbani karibu kila siku na kuwajulia hali. Fatma, mke wangu, ama mama Brighton, alinitia moyo kuwa nisome kwa bidii na kwamba wote wapo sawa.

Niliipata nafasi hii ya kusoma nikiwa kazini na kwamba ambaye angepata nafasi hiyo angelipiwa kila kitu ikiwa pamoja na mshahara wake kuendelea kulipwa. Kwangu mimi ilikuwa kama bahati ya mtende nikaomba kwenda kusomea kozi hiyo ili kuongezea diploma yangu ya sheria niliyoipata chuo cha Lushoto.

“We mangi kwani siku hizi kujenga imekuwa siri?” Ni swali aliloniuliza rafiki yangu Kaluse tulipokutana kwenye kamgahawa kamoja tukipata moja moto moja baridi.

“Mh! Mimi nijenge kweli ndugu yangu saivi kwa pesa ipi tena iliyobaki?” Nilijitetea.

“Haya bwana…” Aliitikia kishingo upande na tukaendelea kupata kinywaji huku kila mmoja akiwa ameshasau topic hiyo.

Miezi mitatu baadaye nilikutana tena na bwana Kaluse katika mgahawa uleule na jambo la kwanza aliloniuliza lilikuwa lilelile la ujenzi, “Mentor! Mentor! Yani unajenga kisirisiri hivyo bila kuambiana kwani umeiba pesa mangi!??”

Nilicheka kwani nilihisi kuna mtu ananichanganya naye na si mimi. Ila nilimuomba anielezee kwa nini yeye husema hivyo kila mara.

“Juzi tena nimemuona shemeji, mama Brighton, akija kukagua ujenzi unajifanya huelewi?”
“Nani, Fatma mke wangu?”

“Ndiyo nani mwingine. Yani unajifanya mjanja kumbe unajenga pembeni yangu bana. Sisi ndiyo majirani inabidi tufahamiane mkuu”

“Ah!” Ndilo neno pekee lililoweza kutoka mdomoni mwangu. Kengele ya hatari ililia kichwani. Nilitaka kuamini kuwa amemfananisha Fetty wangu lakini hapana anamfahamu fika. Ilinibidi kumuomba Kaluse anielezee vyema. Ndipo akaniambia mbona kila mwisho wa wiki mke wangu huja pale na ‘dereva’ (alidhani ni dereva kwani hakuwa akishuka kwenye gari kila wanapokuja) na kukagua ujenzi wa nyumba ‘yetu’.

Kwa kweli nilishindwa kuamini kuwa Fetty wangu angeweza kufanya yale niliyokuwa nikihadithiwa. Nilidhani ni ndoto tu au pombe zilizokwisha mkolea bwana Kaluse lakini hapana. Nilimuomba anipeleke hadi hapo anaposema mke wangu huja kukagua ujenzi na kuniahidi tungeenda wikiendi iliyofuata. Nilikubali na kurudi chuoni huku nikiwa na mawazo tele. Kama kawaida yangu sikuacha kupiga simu nyumbani na kuwajulia hali. Kwa jinsi nilivyompenda mke wangu, alivyo mzuri na mtoto wetu niliomba sana habari ile isijekuwa kweli.

Wikiendi hiyo tulikutana na bwana Kaluse kuelekea maeneo ya Chalinze ambapo na yeye pia anajenga huko. Tulifika na kukuta wafanyakazi wakiendelea na kazi yao. Tulipaki gari eneo la mbali kidogo na kusubiri. Tulikaa pale kuanzia asubuhi ile ya saa tatu hadi saa tisa jioni bila mtu yeyote kutokea. Nilitaka kufurahi moyoni ila Kaluse aliniambia tuje tena wikiendi inayofuata na ama hakika tutamkuta. Nilitamani kumpuuzia lakini rafiki yangu huyu hawezi kutunga hadithi tu kama ile.

Niliwaza sana wiki hiyo na hata darasani nilikwenda tu kuonekana ila sikuwepo kiakili. Niitamani jumamosi ifike mapema na ilipofika wala sikusubiri kukumbushwa na Kaluse bali nilimpigia simu mwenyewe na kumkumbusha. Aliniomba nimngojee kidogo kwani alitakiwa kununua saruji kupeleka kwenye eneo lake la ujenzi.

Mida kama ya saa nne tulikuwa tumeshafika eneo la tukio tayari kumngojea Fatma mke wangu. Na siku hii kweli alifika akiwa ndani ya gari aina ya double cabin lenye vioo vyeusi (tinted) hivyo kwa haraka sikuweza kumuona dereva wa gari lile. Alishuka na kwenda kuongea na mafundi na baada ya kama nusu saa ya kuangalia tukio lile kwa uchungu aliondoka na kuingia kwenye gari. Ni hadi alipogeuza gari na kuondoka ndipo akili iliporudi na kugundua gari lile halikuwa la mtu mwingine bali la jirani yetu Dr. Chrispin.

Tulienda kuongea na mafundi wale kuwadodosa zaidi kama walimfahamu mwenye nyumba wanayoijenga. Walitujibu kuwa ni mtu na mkewe na kuwa wao huja kukagua eneo hilo kila wikiendi. Moyoni uliniuma sana kusikia habari ile.

Jumatatu nilikatisha masomo na kurudi nyumbani Morogoro na kuitisha kikao cha dharura cha wazazi. Niliwaeleza wazazi wake juu ya suala lile la mke wangu kujenga nyumba bila mimi kuwa na taarifa. Mwanzoni alitaka kukataa ila nilikuwa nimejizaititi na ushahidi wa kutosha..thanks to masomo ya sheria niliyokuwa ninayasoma.

Nilitaka kujua tu kwa nini hakunitaarifu na pesa za ujenzi wa nyumba ile alizitoa wapi. Wazazi wake walipomtaka ajitetee alisema kuwa ni pesa yake ya mshahara alikuwa ameweka na kwamba alitaka kunifanyia surprise. Kimbembe kilikuja alipotakiwa kutoa hati za kiwanja na za ujenzi wa nyumba ili kuona majina yaliyoandikwa. Nilishituka kukuta majina yaliyoandikwa ni ya mama yake. Kwa kweli ilikuwa surprise ya aina yake.

Niliondoka na wazo moja tu ni mwisho wa ndoa yangu na Fatma mke wangu. Niliwaonesha ushahidi wa kutosha kuwa mke wangu huyu alikuwa akitoka na jirani yetu Dr. Chrispin.

10th December 2013, Jumanne

“Kaka Mentor! Leo huendi kazini?” Ilikuwa ni sauti ya jirani yangu Lucy akinigongea mlango. Nilishituka usingizini na kuangalia saa yangu. Ilikuwa ni saa moja kasoro kumi asubuhi. Kumbe nilipitiliza usingizini asubuhi ile alarm ilipoita 4:29am na harufu ile ilikuwa ya mama wa jirani ambaye huamka asubuhi na kupika maandazi kwa ajili ya kuuza kwa wateja watakaopita hapo asubuhi kuelekea makazini.

Fatma? Mama Brighton? Nilishusha pumzi ya faraja baada ya kugundua kuwa licha ya kutokuwa na mtoto kumbe Mentor hata bado sijaoa…ilikuwa ni ndoto tu. Nilifunga macho na kumshukuru Mungu kuwa ni ndoto tu ila nikaomba hayo yasinitokee.

Ni saa tatu sasa nimefika kazini, naomba niendelee na majukumu ya kulijenga taifa. Ndoto nyingine mbaya jamani.

Wasalaam wapendwa,
Mentor.

No comments:

Post a Comment