Wednesday, November 27, 2013

Nanasi Lililoozea ndani...



Nanasi lililoozea ndani…



“We tutusa, niaje?”

“Poa tu mbe niambie”

“Umeshasikia habari za Nicas?”

“Hapana sijasikia, kuna nini?”

“Upo dunia ya ngapi?”

“Aaa si uniambie mkuu, kuna nini?”

“Nicas kanywa sumu, yupo KCMC inasemekana hali yake ni mbaya sana”

“WHAT!??” “Haiwezekani…yule jamaa na ujanja wake wote nini kinaweza kuwa kimemzingua namna hiyo?”

“Hatujajua hadi sasa, ila ndo hivyo”

“Duh! Basi imekuwa bahati nipo Moshi, jioni nitaenda kumcheki”

Ni maongezi kati yangu na rafiki yangu Aggrey. Kwa kweli nilibaki nimeshtuka sana kwani katika watu nisiotarajia kunywa sumu, Nicas alikuwa mmojawapo.

Labda nianze kwa kuelezea tulipotoka na Nicas...

Chuo cha Ushirika, Moshi…1990’s

Mimi, Aggrey na Nicas tulikulia pamoja maeneo ya Chuo cha Ushirika. Na kipindi hicho kilikuwa hasaa Chuo cha Ushirika. Enzi hizo chuo kilikuwa na miradi mingi. Mifugo na vitu vingine. Kilikuwa kiki-reflect maana halisi ya chuo cha biashara. Nakumbuka jinsi tulivyokuwa tunaenda kupiga stori na wafanyakazi kule chini mabandani kisha wanatupa mayai. Au siku niliyopigwa teke na ng’ombe nikitaka kumkamua. Ni nyakati nzuri sana nikikumbuka.

Tulikuwa marafiki sana kipindi hicho (na hata sasa) hasa kwenye michezo ya utotoni ya kombolela, baba na mama, gololi, na zaidi sana mpira wa miguu. Kutokana na kuwa na uwanja wa Chuo cha Ushirika, sisi hatukutumia sana mipira ya kufuma kwa makaratasi (labda tu tulipokuwa shule) kwani wachezaji wengi wa timu ya veteran walikuwa marafiki zetu.

Katika kukua, kuna wale waliokuwa wajanja mapema na sisi ambao kwa kiasi ujanja tulikuja jifunzia ukubwani. Nicas ni mmoja wa wale walio ‘janjaruka’ mapema. Huyu jamaa ni wale tunaowaita, ‘players’ a.k.a ladies man…weka mbali na watoto wa kike.

Tukiwa shule ya msingi, Nicas alikuwa akitoroka nyumbani kwenda kufukuzia wasichana jambo ambalo kwa kipindi hicho hatukuwa tukielewa kinachomzingua ni nini hasa maana hao wasichana walikuwa kama dada zetu tu.

Miaka ikaenda miaka ikarudi, shule ya msingi ikahamia sekondari, sekondari ikahamia chuo nako huko hakuuacha mchezo huo mbaya wa kufukuzia kina dada. Stori zake kila siku zilikuwa hizo hizo. Hata nilipopigiwa simu kuwa kanywa simu, ama kwa hakika nilihisi tu kutakuwa na uhusiano na tabia yake hiyo.

Basi, kwa kuwa nilikuwa njiani kuelekea Moshi, nilisema nikifika nitaenda kumjulia hali.

November 23rd, Jumamosi 1730hrs

 Nilifika KCMC na kwenda moja kwa moja wodi alipolazwa Nicas. Nilimkuta mama yake akimalizia kumlisha chakula. Hakuonekana ana hali mbaya kama nilivyoambiwa na Aggrey ila macho yake yalionesha kukosa nguvu kabisa. Nilimsalimia mama yake na kumuomba kumsaidia kumalizia kumlisha. Alishukuru na kunipa bakuli la mtori kisha akatoka nje.

Nilimsalimia Nicas na yeye akaitikia kwa kutingisha kichwa. Hakuweza kusema chochote. Nilimalizia kumlisha mtori ule na haukupita muda mrefu muda wa kuona wagonjwa ukawa umekwisha. Hivyo nilifungasha vitu nikamngojea mama yake tukashuka wote kurudi nyumbani.

Novermber 24th, Jumapili 0530hrs

Kwa mchanganyiko wa mawazo, na ufukunyuku wangu, nilitamani sana kufahamu nini hasa kilimpata Nicas mpaka kufikia uamuzi wa kunywa sumu. Mama yake hakuwa akifahamu sababu hasa. Nilijiapiza kabla sijarudi jijini Dar es salaam, ni lazima nifahamu sababu hiyo. Hivyo niliamka mapema na kuamua kuwa siku hii nitaenda kusali Haggai Chapel, kanisa lililopo palepale ndani ya eneo la hospitali ya KCMC.

Baada ya ibada niliongea na mmoja wa wanafunzi wa udaktari pale, Alfred, na kumuomba anifanyie mpango niweze kuingia wodini. Alfred alikubali hivyo tukaenda wote hadi wodi alimolazwa Nicas. Kwanza nilishituka kumkuta na pingu mkononi. Hii sikuiona jana na sikuweza kufahamu ni tangu lini aliwekewa pingu ile.

Nilimkuta kajilaza lakini alikuwa macho. Hivyo nikamsalimia. Aliitikia kwa sauti nikafurahi. Alionesha nafuu kuliko jana. Alfred aliniaga na kwenda zake. Ndipo nikapata ujasiri wa kumuuliza Nicas kisa hasa cha kuwepo kwenye mkasa ule.

Alianza kwa kusema (huku machozi yakimlengalenga), “Mbe, ndo basi tena yani. Nishaadhirika mbe”

Ukweli, akili yangu iliwaza gonjwa hili la kisasa ila sikutaka sana kumuonesha kuwa ninamhisi vibaya kihivyo, hivyo nikamwomba anielezee kuwa ameadhirika vipi? Na nini? Ni nani kahusika? Kwa nini iwe basi tena?

Ndipo alipoanza kunihadithia…

Brenda, SMMUCo, 2012 Graduation day.

Ilikuwa graduation ceremony ya Jerry, [dogo mmoja ambaye tuliishi naye pia Ushirika lakini alikuwa mdogo kwetu. Ila kwa kuwa tuliishi nao pamoja na baadhi ya michezo tulikuwa wote, tulimchukulia kama rafiki.] Hivyo aliponiambia kuwa kungekuwa na graduation siku hiyo, na kunialika, sikusita kwenda kwani niliamini huko ningepata vimwana vipya.

Na kama ilivyokuwa. Katika pitapita za siku hiyo nilikutana na Brenda, 21, mwanafunzi mwaka wa pili BCOM. Ulimbwende wa binti huyu pamoja na sura yake ya upole vilinivutia zaidi kwake. Halafu zaidi siku kama hii alikuwa peke yake. Hivyo nikamfuata na kumjulia hali.

Nicas: “Mambo”

Brenda: “Poa”

Nicas: “Wakwe wako wapi?” (nikimaanisha wazazi wa Brenda)

Brenda: “Hawapo”

Nicas: “Basi tufanye mimi ndo nimekuja kukutembelea, twende ukanioneshe  vitabu vyako”

Brenda akacheka lakini bila kujitambua urafiki/mazoea yakazaliwa. Mwanzoni yote yalikuwa mema na tuliendelea kuwasiliana hata baada ya kumalizika graduation.
[Kwa kuwa Nicas alikuwa akisoma Postgraduate course ya Cooperatives chuoni Ushirika, ilikuwa rahisi wao hata kuonana kila walipopata nafasi.]

Kichwani kwa Brenda, alikuwa ameshaanza kujenga picha ya mahusiano yatakayodumu kwa muda mrefu. Alikuwa ameanza kuniamini kiasi cha kuwa anakuja kwangu na kukesha chumbani siku nzima. Akilini mwangu, nilikuwa nawaza mengine, ‘she is just another project!’ Kumbe sikujua nilikuwa najichimbia kaburi!
[Hapa Nicas alionesha kuumizwa sana na kumbukumbu ya kipindi hicho akaanza kulia hivyo ikabidi nimembeleze anyamaze ndipo aendelee kunihadithia.]*machozi*

Kutokana na maongezi yangu na Brenda nilikuja kugundua hajawahi kuwa na mahusiano yeyote ya kimapenzi na mwanaume hivyo nilifahamu kabisa jinsi ya kumpata ingekua tofauti kabisa na wale ninaokutana nao club au sehemu kama hizo.

Brenda alikuwa binti mchangamfu sana na nili-enjoy company yake. Ila nilitaka kumaliza mission yangu mapema niendelee na wengine. Tatizo, kila nilipochomekea habari za mapenzi Brenda alionesha sura ya kuhuzunishwa sana. Nilijua ni kwa sababu alikuwa akihofu kwani ni mara yake ya kwanza. Sikutaka kufanya haraka. Nilimpa muda wa kunizoea lakini kila mara nilipokumbushia hiyo hadithi Brenda alikuwa akiniomba tusifanye hilo tendo kabisa, kuna hadi kipindi alikuwa akilia kabisa ikitokea tumejikuta tunabusiana au tunatomasana. Alikuwa kama mtu aliyekumbuka jambo na kushtuka ghafla na kuchomoka kwangu. Akili yangu bado iliniambia alikuwa anaogopa kama walivyo wengi siku ya kwanza.

Miezi ilienda na alizidi kunitolea nje hadi juzi bro. Kulikuwa na mechi ya kufuzu kuwania kushiriki michuano ya kombe la dunia kati ya Portugal na Sweden. Nilikuwa na hamu mno ya kuiona na kwa kuwa kesho yake sikuwa na kipindi zaidi ya kumalizia thesis yangu nilijiapiza kuwa ni lazima ningeenda kuangalia mechi ile.

Nilimpigia simu Brenda ili kufahamu ratiba yake na kama bahati hakuwa na kipindi kesho yake hadi saa sita mchana hivyo nilipomuomba twende wote tukaangalie mechi alikubali kwa masharti kuwa niende kumchukua chuoni kwao.

Haikuwa shida hivyo mida ya saa mbili na nusu nilianza safari ya kwenda chuoni kwao kwani ni takribani dakika ishirini tu kutoka MUCCoBS kwa njia ya KCMC. Tulirudi na kuja kukaa Masikio Inn sehemu yangu maarufu kuangalizia mechi na kuagiza nyama choma huku tukingojea mechi ile. Kwa mara ya kwanza nilimshawishi Brenda akaonja pombe. Nilikuwa nimenunua pakiti ya Zanzi nikiichanganya na redbull. Ladha yake kwa kweli ilikuwa nzuri sana nikamshawishi aionje na kama nilivyotarajia aliipenda. Akawa akinywa kidogo kidogo lakini kama wahenga walivyokwisha kusema, ‘Kidogo kidogo…’

Nakumbuka mechi ile hata haikuisha, Brenda alikuwa amelewa na kuanza kusinzia kwa mbali. Aliniambia nimpeleke kwangu akapumzike nikitaka nirudi kuangalia mechi. Akili yangu ikapiga hesabu za haraka haraka nikajisemea moyoni, ‘Hao kina Ronaldo na Ibra wanafunga magoli wanaingiza zao hela mimi nikae hapa nipoteze golden chance ya kufunga goli pekee kwa Brenda!??’ Hivyo niliamka kwa haraka nikamshika mkono nikamyanyua huku nikimvuta kuelekea kwenye gari.

Tulifika nyumbani nikamsaidia kutoa nguo za juu…bro, asikuambie mtu Brenda ni mzuri mbe! Yani nilikuwa natamani nimmalize palepale mbe. Nilimpeleka hadi chumbani ambapo nilimlaza na kutaka kutoka kwenda sebuleni kuchukua juisi ya limao nimletee. Nilishituka aliponivuta na kunifanya nikose balance na kuangukia kitandani. Nilijua pombe inafanya kazi yake na mimi sikufanya ajizi nikajisogeza karibu yake.

Kwa muda wa kama dakika arobaini hivi niliishia kumbusu na kumtomasa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa ustadi wa hali ya juu. Alilegea kila mahali lakini alikuwa ni kama anayeshituka usingizini kila nikipeleka mkono kumtoa nguo ya ndani. Alinizuia huku akiniambia, ‘hapana Nic’ Nilijua ni uoga wake hivyo nikahamia plan B…nguvu!

Kwa kuwa alikuwa ameshalewa nguvu za kupingana na mimi hazikuwepo sana ila nakumbuka alikuwa akilia kabisa. Wakati huu nilihisi pombe zimemtoka kichwani kabisa na alikuwa akikataa. Nilijiambia akilini kuwa hii ni kama wengine tu niliowahi kuwapitia kwa mara ya kwanza na angenyamaza nikishaanza shughuli.

Mbe, alilia hadi wakati ninamaliza. Aliendelea kulia mpaka hofu ikaniingia bila kujua hasa nini sababu ya kilio chake. Nilipoona amelia sana ilinibidi nimletee tena zanzi ila niliichanganya kiasi na grants nikamlazimisha anywe. Ndipo alipokunywa na kusinzia. Nilikuwa na mawazo mengi kuliko furaha nakumbuka. Sikuwahi kuona kitu kama hiki alichokifanya Brenda. Nilibaki najiuliza, kwa nini alilia vile? Jibu lilikuwa likinisubiria asubuhi…

21st November 2013, Alhamisi

Sifahamu usingizi ulinipitia saa ngapi ila nilishtushwa na sauti ya mtu akilia. Alikuwa ni Brenda ameamka. Alikuwa akilia kwa kwikwi. Sikuelewa ni kwa nini alikuwa akilia vile. Nilimbembeleza aniambie nini hasa kilichokuwa kikimliza. Nilimdanganya kwa ahadi nyingi za mapenzi na hata ndoa alimradi anyamaze. Lakini kadri nilivyotaja hizo ahadi ndipo alipozidi kulia. Baada ya muda alinyamaza na kunielezea.

Kumbe Brenda alizaliwa akiwa keshaathirika na virusi vya UKIMWI. Wazazi wake walifariki miaka mitano iliyopita kwa ugonjwa huo. Nakumbuka aliwahi kuniambia kuwa yeye ni yatima na kuwa alikuwa akilelewa na mjomba wake. Lakini kamwe hakuwahi kuniambia sababu za wazazi wake kufariki.

Hivyo Brenda alikuwa akiishi na virusi hivyo kwa muda wote huo. Mbe, nilianza kukumbuka kila kitu nilichokifanya usiku wa siku hiyo nikajua tu nimeshaupata. Nakumbuka mchana wa hiyo siku nilinyoa mavuzi na kwa hakika kuna sehemu mbili tatu nilijikata. Nilikumbuka kuwa pia sikutumia kinga yoyote na kwa vile alivyokuwa akikataa lazima kutakuwa na michubuko ambayo ama kwa hakika nisingeweza kuiona kwa macho lakini ipo.

Ghafla kichwani nilipata picha iliyonipagawisha. Nilijiona nikiwa nimekonda hadi mbavu zinaonekana huku nikiwa nimetuliwa na nzi kila mahali na sina mtu anayenihudumia kwani kila aliyepita alikuwa akisema yake; ‘Huyu alikuwa player sana’ ‘amevuna matunda ya uhuni wake’ Hata mama yangu nilimsikia akiniambia, ‘huyu ndo mjukuu uliyeniletea mwanangu? UKIMWI?’

Bila kujielewa nilijikuta nikienda kwenye kabati la dawa na sifahamu hata nilichukua nini na nini ila nilimeza vidonge vingi nikashushia na konyagi. Nahisi ni Brenda ndiye aliniwahi na kunileta hospitali la sivyo ningeshaondoka mbe.


Nilipata wazo la kumuuliza huyu Brenda yupo wapi lakini ghafla nikamuona mama yake akiingia wodini na nilipotupia macho saa yangu ya mkononi ndipo niligundua imeshafika saa sita za mchana na muda wa kuwaona wangojwa ulikuwa umewadia. Nilimsalimia na kuwaaga huku nikibaki na maswali mengi kichwani ya kumuuliza Nicas.

Kwa bahati mbaya nilitakiwa kupanda ndege ya jioni ile na kurudi Dar es salaam kuendelea na majukumu ya kujenga nchi. Nikiwa kwenye ndege niliwaza sana na kuogopa sana moyoni. Hakuna aliye salama tena katika nyakati hizi. Hata yale mananasi yaonekanayo masafi na mazima kwa nje kumbe yameozea kwa ndani.

Wasalaam wapendwa,
Mentor.

No comments:

Post a Comment