Huyu Ndiye!
Mimi alikuja siku moja jioni, baada ya chakula akaniambia, “Mume wangu! Ninajua nimekukosea, nisamehe. Nimekuwa na mahusiano ya kimapenzi na mfanyakazi mwenzangu. Niko tayari tuachane.”
Mh! Kwanza tukashtuka. Mbona Seba amebadilisha topic haraka hivi?
Ijumaa Februari 14, 2014
Ilikuwa siku moja kabla ya harusi ya rafiki yetu Kelvin. Siku hii tulikutana kwa chakula cha jioni na kutambulishana kabla ya kuelekea siku yenyewe ya harusi, yaani kesho yake, Jumamosi 15 Februari 2014.
Tulikutana sisi wasimamizi wa upande wa kiume (groomsmen) na wale wa kike (bridesmaids). Kutokana na kuwa wengi hatukuwa tukiishi mkoa mmoja, hatukuwa tunafahamiana. Tuliona lingekuwa wazo jema tukakutana siku moja kabla ya tukio kufahamiana japo kwa sura na majina ili kuepuka kuoneana aibu siku ya harusi.
Baada ya mazungumzo na chakula cha jioni kundi hili moja lilivunjika na kuwa makundi mawili. Wadada walijitenga pembeni na kuendelea kuzungumza ya kwao na sisi tukabaki peke yetu.
Mimi ndiye nilikuwa mdogo kiumri kwenye kundi lile na ambaye sikuwa nimeoa wakati ule. Tulikuwa wanaume watano; Kelvin – bwana harusi, Sebastian – best man, Morris, Phillip, na Mentor – mimi. Kwa kuwa wote walikuwa wameoa, niliwauliza swali ambalo lilikuwa likinisumbua kichwani kwangu wakati ule. “Ni nini kilikufanya ukajua kuwa huyo mkeo uliyenaye ndiye kati ya wanawake wote uliokuwa ukiwafahamu wakati huo?”
Philip:
Kaka Phillip alianza kujibu. Alikuwa mkaka mchangamfu na mstaarabu sana. Huyu nilimfahamu kitambo kidogo kwani alisoma na kaka yangu shule moja toka kidato cha kwanza hadi cha sita.
Alisema kuwa siku moja ya Ijumaa aliambiwa na bosi wake akamwakilishe kwenye kikao ambacho kingefanyika Jumatatu ya wiki iliyofuata. Hivyo alitakiwa kujibu barua pepe kwa kutuma jina lake na taarifa zake kadhaa. Hakuwa akipenda kwenda kwenye vikao hasa kikao ambacho hatokuwa na maamuzi yoyote na hakina malipo. Lakini kwa kuwa ni maelekezo ya bosi hakuwa na budi kwenda. Phillip alifanya kama barua pepe ile ilivyomwelekeza na Jumatatu alipofika kwenye ukumbi wa mkutano alikuta wameandaa vitambulisho kwa kila mshiriki. Kila mtu alitakiwa kuvaa kitambulisho kile mahali kitakapooenakana muda wote wa kikao.
Akiwa kwenye kikao aliangalia upande wa pili wa meza akamwona msichana. Binti mwenye sura ya upole, mzuri, mwenye ngozi angavu ambayo pamoja na kuwa alijipaka tu Vaseline lakini alikuwa anang’aa. Hapa tulicheka maana tulijua mapenzi upofu na Phillip yalishamkumba. Aliingia kwenye simu na kuingiza jina la yule binti kama lilivyokuwa limeandikwa kwenye kitambulisho chake. Akampata facebook. Akamtumia ‘friend request’. Kumbe binti yule naye wakati ule hakuwa hata akisikiliza kilichokuwa kinaendelea kwenye mkutano hivyo alivyoona ‘request’ ile akili yake ilimshtua kuwa sura hii inafanana na sura ambayo ameiona muda si mrefu. Aliponyanyua kichwa kuangaza kwenyue ukumbi ule wakakutana uso kwa uso. Binti akatabasamu! Phillip anaapa kuwa hapa na muda huu ndipo alipohisi kitu cha pekee kuhusu binti huyu. Macho yake ni kama yalikuwa mlango ulio wazi wa moyo wake. Tabasamu lake lilikuwa kama mwanga wa jua linapochomoza. Alivutiwa naye muda ule ule lakini alisita.
Phillip alikuwa mshiriki mkubwa sana wa makongamano na mikutano ya vijana na alikuwa akifundisha pia. Alikuwa akizungumzia mahusiano, urafiki na uchumba wa Kikristo. “Nilikuwa muumini mkubwa sana wa nadharia ya urafiki na uchumba wa muda mrefu,” alisema Phillip. Aliamini kuwa ili watu wawe na ndoa itakayodumu basi hawana budi kukaa katika urafiki na uchumba kwa muda usipoungua mwaka au miaka miwili. Aliamini watu lazima wafahamiane vyema kabla ya kuingia kwenye hii taaasisi ya ndoa. Lakini haikuwa hivi kwake.
Waliendelea kuchat facebook muda wote wa kikao na kabla hakijaisha walibadilishana namba na tayari walishakubaliana kukutana pamoja kwa chakula cha jioni siku ile ile. Baada ya kikao kile walitoka na yule binti ambaye baadaye alikuja kugundua kuwa naye alikuja kumuwakilisha bosi wake tu na hakuwa na ubia wowote na kikao kile.
Kulikuwa na sauti ndogo ikimkumbusha Phillip kuwa anaenda haraka sana tofauti na imani na mafundisho yake mwenyewe. Lakini kuna nguvu aliyoshindwa kuielezea iliyomfanya aendelee.
“Kabla hata chakula hakijaletwa nilikuwa nimeshajua akilini mwangu kuwa huyu binti nitamuoa!” alisema. “Unajua, tulikutana Januari na Disemba tulifunga ndoa.”
Alisisitiza kuwa ni miaka minne sasa na hajawahi kujutia maamuzi yale. Kabla sijapata muda wa kutafakari kisa kile na hata kuuliza maswali yoyote ya nyongeza, Morris alisema hadithi yake.
Morris:
“Mimi bana nilimuoa shangazi mapema sana,” aliongea kwa sauti yenye lafudhi nzito ya kichaga. Hapa na sisi tulikumbuka kuwa Morris huwa wanaitana ‘shangazi’ na mke wake na akatuahidi atatuelezea sababu.
Nilibahatika kumaliza Chuo Kikuu na kupata kazi hata kabla sijafanya mahafali. Niliajiriwa kuwa Mhasibu Hospitali ya Misheni ya St. Joseph, Peramiho huko Ruvuma. Mwanzoni niliona kama ni mbali na nyumbani lakini nikawaza watu wanaenda kuishi na kufanya kazi nchi za watu sembuse mimi hapa hapa Tanzania. Haikuwa mdahalo mkubwa kichwani na nilielekea Songea.
Likizo yangu ya kwanza nilirudi nyumbani Moshi, kijijini Marangu. Sikuwa na miradi wala chochote cha maana cha kufanya hivyo niliona ni heri nirudi nikae na wazazi nikipumzisha akili na kujipanga na mwaka mwingine kule kwa Wangoni.
Jumapili moja, Shangazi yangu alikuja pale nyumbani akanikuta peke yangu. Wazazi na ndugu wengine wadogo walikuwa wameenda kanisani. Mimi sikuwa mpenzi wa kanisani kivile si unajua Jumamosi tulitoka kupiga mbege na wazee nikarudi nimechoka, hivyo nilichelewa kuamka.
Shangazi alifika na kunitaka nivae nimsindikize ‘hapo tu’.
Tulicheka tukikumbuka ambavyo wazee wa zamani watakuambia ‘ni hapo tu’ halafu unaishia kutembea nusu siku.
Kwa bahati kwangu haikuwa hivyo. Ulikuwa mwendo wa kama lisaa limoja hivi. Tulipofika, shangazi alielekea kuzungumza na wenyeji wake na kuniacha nje nikipiga soga na watoto niliowakuta pale. Watu walikuwa ndiyo wanarudi majumbani kutoka kanisani na wale wavivu kama mimi ndiyo wanaamka kuandaa chai ya asubuhi. Nilikadiria kuwa ilikuwa imefika saa nne asubuhi.
Wakati nikizungumza na watoto wa eneo lile alitokea binti ambaye baada ya kuniamkia alielekea ndani. Ndiyo, aliniambia, “shikamoo kaka.” Sikuwa nimemtilia sana maanani. Baadaye alirudi na kunikaribisha chai. Nilitaka kukataa ila akaniambia shangazi hana dalili za kukaribia kumaliza mazungumzo. Hivyo nilimtania kuwa kama atakunywa chai na mimi, basi nitakunywa. Aliniambia nisubiri akawaandalie kina shangazi kisha aje tunywe wote.
Tulikunywa chai ya rangi na viazi vitamu vya kuchemsha lakini chai ile ilifungua mengi. Alikuwa ndiyo amemaliza masomo ya Uuguzi Chuo cha Afya cha Machame na alikuwa amerudi nyumbani akisubiri kupangiwa kituo cha kazi. Alisema bado hajafanya maamuzi kama aende kufanya kazi au aendelee na shule kusomea Shahada ya Uuguzi. Tulikubaliana kuwa ilikuwa changamoto, nzuri, lakini ya kufanyia maamuzi kwa wakati. Kabla hatujaendelea na mazungumzo shangazi aliniita kuwa nijiandae tuondoke.
Tulikubaliana kukutana Moshi Mjini siku iliyofuata tuzungumze zaidi na kumshauri. Hapo nilikuwa najiona mkubwa kweli.
Siku iliyofuata tulikutana mjini, nakumbuka tulikaa kwenye ngazi za kuingilia jengo la KNCU tukitafuna mahindi ya kuchoma. Tulizungumza kuhusu matamanio yake na kupima faida na hasara za kila wazo.
“Shangazi, kumbe ulikuja mjini na hukuniambia ningekutuma.” Ilikuwa sauti ya shangazi yangu. Hatukutegemea kuwa tungekutana naye mjini. Tulimsalimia na mazungumzo yetu yakaishia pale. Tukamsaidia kubeba mizigo aliyokuwa nayo kwenda stendi tukarudi nyumbani. Ile hali ilitufanya tutamani zaidi kuonana na kuzungumza maana tulihisi kama shangazi alitukatisha.
“Shangazi! Na leo tena unaenda mjini?” siku chache mbeleni tulikutana kwenye gari na shangazi yangu nikiwa naenda mjini kukutana na huyu huyu binti. Nilikaa kimya nikitamani kushuka kwani vituo vinne vitano mbele yule binti angeingia kwenye gari hilo hilo ili tuelekee wote mjini. Nilijikaza kwani tusingeonana angejisikia vibaya.
Tulikutana tena mara mbili mbeleni kabla ya kurudi Peramiho na itoshe kusema, miezi mitatu baada ya pale nilichukua likizo nyingine fupi na kuja kufunga ndoa na huyu binti. Kuanzia pale tulipokutana na shangazi kwenye gari basi tulianza kuitana ‘shangazi’ huku tukicheka na kuamini kuwa muda wowote shangazi atatokea hata pale ambapo tulikuwa tukienda nje ya mji.
Mimi na shangazi tupo kwenye ndoa mwaka wa tisa huu sasa. Sikumbuki hasa ni wakati gani nilihisi huyu ndiye lakini ni katika moja ya mazungumzo naye mjini maana hakika wakati ananisalimia na kunikaribisha chai nilimuona kama binti mdogo wa…
Sebastian:
Mimi alikuja siku moja jioni, baada ya chakula akaniambia, “Mume wangu! Ninajua nimekukosea, nisamehe. Nimekuwa na mahusiano ya kimapenzi na mfanyakazi mwenzangu. Niko tayari tuachane.”
Mh! Kwanza tukashtuka. Mbona Seba amebadilisha topic haraka hivi? Hata Morris hakuwa amemaliza hadithi yake vyema.
“Mimi haikuwa rahisi hivyo.” Aliendelea Seba.
I love! waiting for the second part!
ReplyDeleteIt's up! #refresh
ReplyDeleteKaka I wish to see my name there ����, a good story thou I’m inspired.
ReplyDelete