Mataa ya Ubalozi
Majengo, Moshi
Inafahamika kuwa mimi ni mwenyeji na mzaliwa wa Moshi. Nilizaliwa huko miaka ya 80. Napenda kuandika hivyo ili kujikumbusha ninazeeka sasa. Hilo si la muhimu kwa sasa. Wazazi wangu walikuwa wakiishi eneo la Majengo. Nilizaliwa mtoto wa tatu nikiwa nimetanguliwa na kaka zangu wawili. Wakati wazazi wangu wanaanza maisha hawakuwa na maisha mazuri sana. Hata hivyo, tulikuwa na uwezo wa kupata milo miwili na kama ukiipangilia vyema mitatu. Yaani asubuhi mnachemsha mihogo mingi ambayo mtaila na chai asubuhi, kisha mchana mnakatakata nyanya, kitunguu, pilipili, na hoho mnakula na mihogo ya asubuhi. Chakula cha jioni kilikuwa ni lazima. Kulikuwa na bustani ya mbogamboga nje ya nyumba hivyo ilisaidia kiasi.
Tuliishi nyumba ya kupanga. Kwa mwenyeji wa Majengo, nyumba nyingi zilikuwa zile za korido ndefu halafu vyumba vinaangaliana. Nyumba waliyopanga wazazi wangu ilikuwa ya vyumba viwili vya kulala na sebule. Jiko na vyoo vilikuwa nje.
Raha ya maisha yale ilikuwa kucheza na watoto wenzako. Tulijuana wote wa mtaa ule. Raha nyingine ilikuwa, unaweza kwenda kula popote alimradi kuna chakula. Sisi tulibahatika kuwa na uhakika wa chakula cha jioni, hivyo siku zote chakula cha jioni kilipikwa idadi kubwa kuliko tuliopo. Watoto wengine walikuwa wakija kula kwetu jioni na mama hakuwazuia.
Jirani yetu mmoja, mama Salehe, alikuwa akipika vitafunwa vya kuuza asubuhi. Ah, mama Salehe! Nakumbuka vyema alikuwa mtu wa Tanga. Mama alituambia ni mtu wa Tanga ndiyo maana anajua kupika eti. Alikuwa anajua kukarangiza yule mama. Nakumbuka tulikuwa tukihamia kwake kabisa zikifika siku za sikukuu za Eid. Ah mama Salehe! Kipindi hicho nilijisemea, ‘nikiwa mkubwa, nitaoa Tanga.’
Jirani yetu mwingine alikuwa mama Wilbadi (Wilbard). Huyu alikuwa na watoto wawili, Wilbadi na Pudensiana. Tulimwita tu Pude. Wilbadi alikuwa mbabe wa mtaa. Tulikuwa tukienda kucheza na watoto wengine hatuonewi kama Wilbadi yupo. Alikuwa ‘anavunja’ wote. Wilbadi alinizidi miaka miwili. Alikuwa amelingana na kaka yangu. Pude alikuwa mdogo kwangu kwa mwaka mmoja. Wote tulicheza pamoja michezo yote ya utotoni unayoijua. Kibaba-mama, kombolela, gololi, kuruka kamba, tobo kubitika. Kuna wakati tulikuwa tukicheza wote na wasichana bila kujali ilimradi tu namba itimie. Zilikuwa nyakati nzuri sana.
Hatukuwahi kumfahamu baba yao kina Wilbadi na Pude. Wao wenyewe walikuwa wakisema wana baba wawili, yaani kila mmoja alikuwa na baba yake. Kipindi hicho tuliona kama jambo zuri sana kuwa na baba wengi maana tuliamini ukiwa na baba wengi unapata zawadi nyingi zaidi ya sisi wenye baba mmoja watoto watatu. Lakini baba zao hawakuwahi kuja nyumbani. Hatukujua kwa nini. Mama yao alikuwa akifanya kazi usiku tu na mchana alikuwa analala mara nyingi. Kina mama walikuwa wakimsema ingawa sikumbuki hasa walikuwa wakisema nini kuhusu yeye. Ninajua tu hawakuwa wakimpenda sana. Hakuwa akifanya usafi siku za zamu yake mpaka asemwe au agongewe mlango. Hakuwa akituangalia pamoja na kwamba yeye ndo alikuwa akibaki na sisi mchana kama wazazi wetu hawapo. Nakumbuka tu tulikuwa tunasema, “Mama Wilbadi analala mchana kama watoto.” Maana nasi tulikuwa tukilazimishwa kulala mchana tukitoka shule.
Sikuwahi kufahamu mama Wilbadi alikuwa akifanya kazi gani kwa kweli. Alikuwa akiondoka jioni anawaacha Wilbadi na Pude peke yao au anakuja kumuomba mama wabaki na sisi mpaka watakaposinzia ndipo waende nyumbani kwao kulala. Sisi kama watoto tulifurahia hili ingawa huenda mama hakufurahishwa sana. Hii ilipelekea sisi kuwa karibu sana na kina Wilbadi na Pude.
Kazi ya mama yao iilibaki fumbo hadi wakati tunahama Majengo kwenda Rau. Ilikuwa siku ya huzuni sana. Niliumia kama mtu mzima. Nilijua ndiyo hatutaonana tena na marafiki zetu tuliozoeana. Tuliocheza pamoja. Tuliwaomba wazazi tusihame tuendelee kubaki au watuache hapo wao waende huko Rau. Kwa akili za utoto huamini kama huko unakokwenda utakutana na watoto wengine na utatengeneza urafiki mwingine. Pamoja na kwamba tulihamia nyumba nzuri zaidi. Nyumba ambayo ilikuwa inajitegemea yenyewe. Lakini tulikumbuka nyumba ya Majengo. Wakati huo kaka yangu wa kwanza alianza shule ya msingi Rau. Ilikuwa ni karibu sana na nyumbani tulipohamia. Huenda kwake ilikuwa faraja, sijui, nitamuuliza siku moja. Lakini kwangu, nilimkumbuka Wilbadi alivyokuwa ananilinda, sikuwahi kuonewa mtaani. Nilimkumbuka Pude maana tulikuwa tunaendana umri na tulicheza michezo mingi pamoja. Lakini ilibidi tuhame. Kidogo kidogo tukapata marafiki wengine, tukaanza kuwasahau kina Pude na Wilbadi.
Posta, Dar es salaam
Maisha. Maisha hakika ni safari ndefu. Sasa hivi nipo Dar es salaam. Nimehamia huku kabisa. Nimefikia hadi kuwa na mawazo ya kutafuta kiwanja nijenge. Mimi ambaye wakati nakuja huku nilipachukia kabisa. Hili joto na msongamano wake havijawahi kupungua wala kuwa na nafuu toka 2010 nikiingia jijini hapa. Nimeishi Sinza, Mbagala, Kigamboni, na sasa Tegeta na hakuna nilipoona pazuri. Ila sasa hivi sipakumbuki tena Moshi. Nikienda Moshi najiona mgeni. Ni kweli pamebadilika, ila vyovyote vile hapajachangamka kama Dar. Wakati nikiishi sinza, nilikuwa naweza kuamka saa tisa usiku kwenda kutafuta chakula na nikapata. Sijui kama kuna sehemu Moshi ninaweza kufanya hivyo. Lakini hilo si la muhimu kwa sasa.
Ijumaa, 18 Disemba 2020
Nilikuwa ninafanya mazoezi. Huwa nina tabia ya kukimbia kila jioni walau mara tatu au nne kwa wiki. Si mkimbiaji mashuhuri ila naona ni zoezi ambalo ninaweza kulifanya. Mara nyingi huwa ninakimbia kutoka Posta kupitia barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Mwisho wangu hutegemea hiyo siku nimeamkaje. Nimeshatangulia kusema mimi si mkimbiaji mashuhuri, msianze kunihukumu.
Ijumaa hii kama kawaida yangu nilijiondoa ofisini taratibu kwenda kubadili nguo. Nilikuwa na uvivu tu wa kwenda kukimbia. Sehemu ya akili yangu iliniambia, kuliko niende kukimbia ambako kutanilazimu kurudi nyumbani nioge kisha nitoke kwenda kupata moja moto, kwa nini nisitoke hivyo hivyo nilivyovaa nikapate head start. Akili yangu ilianza kunipa mawazo ya maeneo ambayo ningepata ‘happy hour’. Almanusura, sauti hii ishinde lakini nilifanikiwa kubadili nguo na kuanza kukimbia. Nilijua kwa kuwa nitapiga vinywaji vya kutosha wikiendi hii, basi nifanye zoezi la kutosha. Hesabu iliyokuwa akilini mwangu ni kama za kujumlisha na kutoa. Kama nitakunywa bia 10, basi nifanye mazoezi yatakayotosha kuondoa bia 10 mwilini. Kama kukopa vile.
Nilikimbia hadi kufika njia panda ya ubalozi wa Ufaransa, Mataa ya Ubalozi. Wengine hupaita Stanbic. Wengine hupaita njia panda ya kwenda Coco, mbele tu ya daraja la Selander. Kama umewahi kupita pale utagundua huwa kunakuwa na watu wa aina mbili. Kuna watu wanaouza vitu vidogo vidogo au matunda na wengine wanaomba tu bila kuuza chochote. Wateja wao wakubwa ni magari ambayo kwa foleni hii ya Dar es salaam hujikuta yamesimama pale muda mrefu.
Nilifika eneo lile nikiwa na mzuka kweli wa kukimbia, nilijisikia kuchangamka ghafla na kichwani mwangu nilijisemea hapa nitakimbia mpaka Morocco na kurudi. Uchovu wa awali ulishaanza kuondoka. Wakati nakatiza huku nikisikiliza nyimbo mpya hii ya Roma nikitafakari kama kweli ndiyo amestaafu muziki, siamini. Wakati huo pia, natafakari ujumbe ailouimba. Kwanza wimbo haufai kukimbilia ule, unakufanya uwaze sana, ila sikuwa na muda mwingine wa kuusikiliza nikiwa peke yangu bila bughudha. Ni katika dimbwi hili la mawazo nikajikuta nimegongana na katoto.
Nilishtuka na kutoka ghafla kwenye mawazo niliyokuwa nayo. Nilikasirika nikiamini hakustahili, hakutakiwa kuwa pale. Anafanya nini barabarani mtoto mdogo vile. Mama yake yuko wapi. Nilikasirika maana alinikata stimu ya kukimbia. Baada ya kugundua kuwa ni miongoni mwa omba omba ambao huwa eneo lile nilikasirika zaidi. Hasira hizi ni kutokana na imani yangu ya muda mrefu juu ya watu hawa. Kwa muda mrefu nimekuwa nikiamini kumpa omba omba shilingi elfu moja ni kumshawishi kesho arudi pale pale kuomba. Ni kumfanya aendelee kuwepo pale. Baadaye katika kukua tukawa tunaambiwa omba omba wengine ni usalama wa taifa. Hii ndiyo ilinifanya kabisa niache kuwasaidia. Na huu ulikuwa msimamo wangu kwa muda mrefu. Ndiyo maana mtoto huyu aliponigonga nilikasirika. Maana nilikumbuka yote haya.
“We mentor toka huko barabarani.” Ilisikika sauti ya kike ikiita. Nilishtuka. Nilishtuka kusikia mtoto huyo ombaomba aliyenigonga anaitwa jina kama langu. Sijui nilikasirika zaidi au nilishtuka tu. Nilitupia macho kule ile sauti ilipotokea. Alikuwa binti mwenye mtoto mwingine mgongoni. Nilishindwa nimgombeze kwa kumuita mwanaye jina kama langu au kwa kutomweka karibu mwanaye mpaka anasogea barabarani. Wakati ninamuangalia vizuri, na yeye akainua macho kunitazama.
Umeshawahi kukutana na mtu, mkaangaliana, kichwani kwako ukahisi umeshawahi kumuona mahali lakini huna uhakika. Nafsini mwako unajua kabisa sura hii si ngeni machoni pako. Ndivyo nilivyojisikia nilipomuona mama Mentor huyu ombaomba. Tulitazamana kwa sekunde kadhaa bila kuzungumza chochote. Nahisi na yeye akilini alikuwa akitafakari hii sura ameiona wapi. Nilikuwa wa kwanza kuacha kumuangalia na kupuuzia wazo lile. Kwani ni mimi peke yangu mwenye jina hili? Ndiyo si watu wengi wanalo, lakini. Au kinachoniuma ni kusikia mtoto wa ombaomba akiitwa jina kama langu. Kuhusu mama yake, nilijiaminisha simfahamu na kuwa huenda kwa kuwa nimepita hiyo njia mara nyingi, nimekuwa nikimuona bila kumtambua na akili inanichezea kuhisi ninamfahamu.
Niliendelea kukimbia, japo kichovu maana nilishapoteza dakika kadhaa hapo. Pili, unakimbia akili inawaza STRAVA yako ambayo hukuizima muda wote huo. Niliendelea kukimbia…
“Mentor!”, iliita sauti kwa upole, iliyoonesha kutokuwa na uhakika na hofu juu. Iliita kwa taratibu, ila niliiskia juu ya ‘earphones’ nilizokuwa nimevaa. Wakati huu nilikuwa nimeshakimbia na kurudi tena pale Mataa ya Ubalozi. Nilishtuka kuona aliyeniita ni yule dada, yule mama Mentor. Kwa haraka haraka nilijiaminisha alikuwa akimuita mwanaye. Nikakasirika tena huku nikijikumbushia kuwa hawatakiwi kuwa hapa mjini hawa omba omba. Aliniita tena nilipokuwa tu ninataka kuongeza mwendo. Nilisimama, nikatoa ‘earphones’ masikioni na kumsogelea.
“Wewe si Mentor! Uliwahi kuishi Moshi zamani.” Nilishangaa. Bado akili yangu ilitaka kuamini simfahamu mtu yule. Nikawaza, ‘au hawa ndo wale omba omba wa usalama’. Atakuwa anataka nini kwangu.
“Mimi ni Pude…hunikumbuki.”
Nilipatwa mshtuko usioelezeka. Moyo ulinilipuka baada ya kugundua ndiye. Nilijua kumbe sikuwa nimemfananisha. Pamoja na kuwa alikuwa amechoka kabisa, lakini sura yake ilibaki, nilimkumbuka vyema sasa. Nilizima mziki wangu na strava na kusogea pembeni kumsikiliza. Ilikuwaje Pude ukawa hivi?
Majengo, Moshi
Pude: Kipindi kile tukiishi Majengo, mama yangu alikuwa akijiuza. Ndiyo maana alikuwa akitoka usiku. Mimi mwenyewe sikuwa naelewa hili hadi nilipokuja kuwa mkubwa. Niliambiwa tu baba yangu alikuwa anaitwa Hubert Kimaro lakini sikufahamu zaidi. Sikuwahi kumuona.
Baada ya nyie kuondoka, kuhama, tulipata shida sana maana hatukuwa na mtu mzima wa kutuangalia. Mara nyingi nilimtegemea kaka Wilbadi kupika na kufanya kazi nyingine. Lakini naye alikuwa mdogo. Majirani hawakuwa wakitujali kama mama yako. Kutokana na hali ile, niliugua.”
Mimi: “Samahani, kwani hii ilikuwa lini? Hamkwenda shule?”
Pude: “Tulienda, ila mimi niliishia darasa la pili. Kaka Wili yeye aliishia la nne. Baada ya kufanya mitihani hakurudi shule tena.”
Pude: “Kutokana na hali tuliyokuwa tukiishi bila uangalizi wa mtu mzima, na
mimi mtoto wa kike, niliugua. Nakumbuka hapa nilikuwa na miaka 9 au 10 tu. Mama
alinipeleka hospitali ya Majengo lakini wakaelekeza nipelekwe Mawenzi. Nilipewa
dawa lakini baada ya muda nilirudia ugonjwa ule. Wakati huu wenzangu
walishaanza darasa la tatu. Kwa kuwa mama hakuwa anatutunza, kaka Wilbadi ndiye
aliyekuwa anakaa na mimi nyumbani. Hivyo naye hakuendelea na shule.
Hali yangu ya kiafya iliendelea kutetereka. Baadaye nilipelekwa KCMC. Madaktari walishindwa kujua shida yangu ilikuwa nini. Nilirudi nyumbani kuendelea na dawa zile zile ambapo zilipunguza tu maumivu kwa muda. Sikuwa naweza kulala usiku. Nilijua muda wowote ningekufa.
Wakati huu pia, mama alianza kuleta wanaume nyumbani, hata nyakati za mchana. Majirani hawakufurahia hali hii. Walimsema sana. Akawa anakaa muda, kisha anarudia tena. Siku moja mama aliondoka na hakurudi tena. Tulimsubiri bila mafanikio. Kaka Wilbadi alisema anaenda kumtafuta. Naye aliondoka kama mama bila kurudi.
Nilianza kuwa nazurura tu mtaani mchana, kisha narudi nyumbani usiku. Hapo ndipo nilianza kuwa omba omba. Sikuwa na njia nyingine ya kupata chakula. Sikuwa na njia yoyote ya kujisaidia. Nilikuwa nikiwaza chakula, mama, na kaka Wilbadi. Sikujua pa kwenda kuwatafuta. Majirani ni kama hawakuwa wakiniona. Walizuia watoto wao kucheza na mimi.
Siku moja, alikuja mbaba mmoja nyumbani akimuulizia mama. Nilimwambia sifahamu alipo. Aliniangalia akagundua nina njaa. Aliondoka akaja na chakula. Akaingia ndani, akanivua nguo, akanibaka. Baada ya hapo alikuja tena mara kadhaa zaidi akifanya vile vile. Nilikuwa nikiumia lakini sikujua ni nini alikuwa akinifanyia. Nilijisemea, walau ninapata chakula.
Alikuja siku moja akaniachia pesa. Akaniambia anasafiri. Alisema anakwenda Dar es salaam. Kuna mji mkubwa huko na maisha mazuri. Alisema atakuwa huko kwa muda. Aliondoka.
Nilianza kusikia maumivu ya tumbo mwezi mmoja baadaye. Nilipata ujauzito. Nilipojifungua tu nilifukuzwa pale nyumbani. Kodi ilikuwa imeisha na walikuwa wanaogopa tu kunifukuza. Wakati nimelazwa Mawenzi, walitoa vitu vyote nje na kufunga nyumba. Nilirudi na kukuta vyombo na nguo zote nje.
Nilibaki mtaani nikimhudumia mwanangu kwa kuomba omba.
Siku moja nilikutana na mbaba akaniambia anaendesha malori na kwamba alitaka kunipeleka Dar es salaam. Niliwaza, labda nitaenda kukutana na baba wa mwanangu. Aliniambia nijiandae na kwamba angenipitia pale stendi ya Majengo jioni. Hakukuwa na simu. Hivyo ilibidi niwepo pale mapema. Nilimchukua mwanangu na vinguo vichache nilivyokuwa navyo na kwenda stendi. Baada ya muda kweli lilikuja lori na alishuka yule mbaba. Niliingia kwenye lori na safari ya kwenda Dar es salaam ilianza.
Alinihadithia mambo mengi njiani kuhusu Dar es salaam. Alinieleza juu ya majengo yake makubwa na ya kifahari, juu ya wanawake wake wazuri, wasafi na wenye kuvaa vizuri. Alinisifia kuwa kwa uzuri wangu, nikipata matunzo, nitaweza kuwa kama wao. Nitapata pesa na nitakuwa na maisha mazuri. Lakini kwanza, tusimame hapa njiani nipumzike. Hakusimama mahali ambapo malori mengine yalisimama. Alisogea mbele na kwenda eneo la peke yake, pembeni mwa barabara.
Usiku ule alinibaka. Sikuweza kumkatalia wala kumzuia. Aliniahidi atanitunza tukifika Dar es salaam. Huu ulikuwa mwaka 2007. Nilikuja Dar es salaam nikaenda kuishi naye maeneo ya Keko. Alinitambulisha kama mtoto wa nduguye, mpwa wake. Lakini usiku alikuwa akinilala. Nilikuwa nikiumia sana, ila hakuelewa hata nilipomuambia.
Nilianza kufanya kazi ndogo ndogo za mikono. Nilikuwa nikifanya usafi kwa watu wananilipa. Mambo mengi yalinitokea hapo katikati Mentor hata sitaki kukumbuka. Mwanangu alifariki kwa maradhi. Nililia lakini sikuwa na chochote cha kufanya. Kichwani kwangu niliwaza chakula, mama, na Wilbadi.
Mwaka 2011 mwishoni nilimtoroka. Alikuwa ameanza kuleta marafiki zake nyumbani na kuwaambia wakimpa pesa atawaruhusu walale na mimi. Sikumuelewa lakini nilikuwa nimeshakuwa mdada mkubwa. Nilielewa alichokuwa ananifanyia. Mwishoni mwa mwaka huo yalinipata makubwa ndani ya siku moja.
Nilienda kufanya usafi nyumba moja ya mtu. Siku ile nilimkuta baba wa ile nyumba. Alinitamani na aliponieleza adhma yake nilikataa pamoja na kwamba aliniahidi pesa zaidi. Nilitaka kuondoka, akanitishia kuwa nikiondoka atasema nimeiba nikakimbia. Niliogopa. Sikujua cha zaidi cha kufanya. Alinilala. Niliumia sana. Sikujua kama mtu msafi vile angevutiwa na mimi hata kutaka kunifanyia vile. Jioni ya siku ile, yule bwana alirudi nyumbani na marafiki zake wakiwa wamelewa. Kama kawaida yake aliwaambia wampe fedha walale na mimi. Nilitaka kutoroka lakini walinizidi nguvu. Nilitaka kupiga kelele wakatishia kuniua. Nilikaa kimya. Walinibaka wote, walikuwa wanne jumla.
Walipoondoka nilichukua nguo zangu na kutoroka. Nilikuja kuishi Sinza. Kuna dada nilikutana naye wakati nafanya usafi naye alikuwa akifanya kazi hizo, akanikaribisha kwake. Alisema yeye hawezi kujiuza, hivyo anajishughulisha na kazi hizo za mikono.
Miezi michache baadaye niligundua nina uja uzito. Sikujua ni wa nani kati ya wote wale. Ndipo nilipojifungua huyu Mentor. Nilimwita hivyo maana ndilo jina pekee la kiume lililobaki nililokuwa nalifahamu.”
Ilibidi nimkatishe kuzungumza maana giza lilikuwa linaingia. Sikuwa na chochote mfukoni kwani nilikuwa kwenye mazoezi. Nikamuahidi kuwa kesho yake ningekuja kumuona.
Niliogopa kumuuliza maswali mengi maana sikuwa na msaada wowote wa kumpa wakati ule. Sikuwa na fedha yoyote mfukoni. Huenda angekuwa mwenyewe angeshaomba fedha na kusaidiwa.
Niliondoka na mawazo sana juu ya Pude. Nilijiuliza, je, huyo mtoto wa mgongoni ni wake pia? Amempataje? Kama Pude hakuweza kwenda shule, je Mentor anaenda? Ngoja kwanza, Wilbadi alienda wapi? Mama yake je, alikuja kufahamu walipo?
Nilijiuliza, kwa mtu kama huyu, je, ni omba omba au mhitaji? Nilijihoji juu ya msimamo wangu wa kutowasaidia. Bado sikuwa na majibu, na hata wakati ninaondoka, na kumuahidi kurudi kesho yake, bado sikujua nikirudi nitafanya nini. Nitamsaidiaje? Nilivuka mataa ya Selander kurudi Posta nikiwa kwenye lundo la mawazo almanusura nigongwe na gari. Nakumbuka yule dereva alinitukana, akiamini ni mkimbiaji tu nimefanya makusudi. Sikumjibu, nilikuwa nawaza, nawazua.
Jumamosi, 19 Disemba
Nilirudi pale kwenye mataa ya Ubalozi na kupaki gari pembeni. Nilitembea kwenda pale nilipokutana na Pude. Sikumkuta. Nilimuulizia, wakasema hayupo. Hakuna aliyeonekana kumjali mwenzie pale.
Jumatatu, Disemba 21
Siku nzima ya leo nimekaa ofisini nikitafakari. Ninapanga kurudi mataa ya Ubalozi kumtafuta Pude. Sijui kama nitamkuta. Mpaka sasa sijui hata nikimkuta nitafanyaje. Nitamsaidiaje. Sijui, ila nitamtafuta. Ngoja nijiandae kutoka, nikazungumze naye. Huenda nitajua cha kumsaidia. Huenda nitapata majibu ya maswali yangu. Ni mpaka nitakapokutana na Pude, ila kwa sasa, naelekea Mataa ya Ubalozi.
Wasalaam wapendwa,
Mentor.
Maisha ni fumbo, na mawazo ni sehemu ya maisha. Vitu vingi, hata uwaze na kuwazua vipi havina majibu mpaka ushirikishe upande wa pili. Hata ikiwa wewe umefanya maamuzi kuna vingine utahitaji mchango wako.
ReplyDeleteKwa kuamua kurudi, kumsaka na kufikiria kurudi pia tena, kwa uchache wake hiyo ni nia ya kutaka kuelewa, sio lazima utatue kila kitu na sio lazima ujitwishe mzigo wote pia. Kuna watu wenye nia ila hawafahamu, kuwajuza nako ni ushirikishaji wa kusaidia kuwaza.
Pude hayuko peke yake kwenye hili na wewe hauko peke yako kwenye hili, Mungu hajawaacha nyote, kwakua kwa uwezo wake mmekutana basi kwa uwezo wake utatuzi utafikika.
Mwanzo huwa eiza mgumu au mraisi ila nia thabit huwa inasaidia kwa kiasi kikubwa kufahamu au walau kutabiri mwisho wa jambo. tupo pamoja
Woow...!! ��
ReplyDeleteBlessed hands, flow with the mind.