Kidamali: Wewe Mwenyewe
Ndiye
Ilifika mahali sikuogopa
tena kuuliza ni kiasi gani walichohitaji kuhakikisha mipango yangu inakamilika.
Hali ilikuwa mbaya kiasi hicho. Rushwa haikuwa siri tena. Asiyetoa kitu kidogo
alikuwa mkosaji na aliyerefusha mkono wake japo kidogo alionekana sahihi na
kupata huduma haraka na kwa ukarimu wote. Ndivyo nilivyoweza kuukuza mtaji
wangu. Katika mizigo niliyokuwa nikiingiza nchini ni nusu tu ya mizigo hiyo
ndiyo ilikuwa imelipiwa ushuru. Nusu nyingine haikuhesabiwa. Nilikuwa mkarimu
kwa kutenga kabisa kiasi cha fedha kwa ajili ya kila mhusika. Kuanzia mamlaka
ya mapato, polisi hadi kwa mtumiaji wa mwisho. Sikusubiri kusimamishwa njiani
ndipo nianze kupiga simu kwa wahusika. Nilihakikisha taarifa zangu zimefika
muda kabla ya mizigo yangu kupita. Wakati huu, wasafirishaji wakubwa tulikuwa
wachache. Kutokana na kuwa mtoaji mzuri niliweza kupanua biashara zangu. Kila
mkoa uliokuwa na mpaka na nchi nyingine basi nilikuwa na ofisi hapo.
2015
Nikiwa na umri wa miaka
34 nilifikia maamuzi ya kufunga ndoa. Nilitamani nami niwe na mtu wa damu yangu
wa kuja kurithi na kuendeleza mali hizi. Nilikuwa nimepunguza kwa kiasi kikubwa
biashara za magendo. Nilijua nisingeweza kufanya hivyo kwa muda mrefu hivyo
niligawanya biashara zangu katika makundi mawili. Biashara moja ilikuwa ya
halali kabisa huku nikilipa kodi zote stahiki ingawa kwa kuwa hali ya rushwa
ilikuwa imekithiri haikuwa na faida yoyote. Hivyo, biashara hii ya pili ndiyo
ilikuwa inanipa faida ya kuweza kuishi mjini. Lakini pia, nilitaka kutulia
sehemu moja nisiwe nasafiri kila wakati. Niliyatamani maisha hayo. Ndani ya
wiki moja ninaweza kuwa nimetoka Mtwara na kukatiza mikoa ya kati yote na
kujikuta nipo Mwanza. Huo ndio ulikuwa mwenendo wa maisha yangu.
Haikuwa kazi rahisi
kuamua ni nani hasa angefaa kuwa mwenza wangu wa maisha maana kutokana na
kutokuwa na makazi maalumu, sikuwa na marafiki wa kudumu. Ni kweli, maisha
yangu yalinikutanisha na mabinti wa aina nyingi; wazuri, wakubwa kwa wadogo,
lakini wote hao niliishia kuwatumia tu na kuwaacha. Sikuwaza kama kuna siku
nitapata hamasa ya kutaka kuoa achilia mbali kuwa na familia na watoto.
Niliyaona maisha kwa lensi ya ujana. Kwa kweli, pesa iliongea. Nilijua hakuna
siku nitakosa mwanamke wa kunituliza moyo nitakapomhitaji na ndivyo ilivyokuwa.
Sijui ni mkoa gani sikuwa na wanawake si chini ya watano ambao muda wowote
nitakaofika ningeweza kupiga simu na tukaonana. Na, ni wa kada zote; wahudumu
wa bar, wanafunzi wa vyuo, hadi wafanyakazi serikalini, benki na wenye biashara
zao binafsi.
Hata hivyo nilifurahi
kuwa walau nimepata msukumo mwenyewe kutoka moyoni wa kutaka kuwa na familia.
Wazazi waliniuliza uliza wakati nimetimiza miaka 30 hivi ila baada ya muda nao
waliacha kuniuliza. Walijua sasa wajukuu watawapata kutoka kwa ndugu zangu tu,
kwangu walishakata tamaa. Pili, waliwaambia ndugu zangu nao wasiendelee
kuniuliza wakiogopa nisije kuoa kwa kusukumwa kisha nikafanya chaguzi mbaya.
Suala la kumpata binti
sahihi halikuwa rahisi maana sikuwa na binti niliyekuwa na mahusiano ya maana
naye. Ila baada ya muda nilifanikiwa. Kumpata kwake ni mkasa tosha
nitakaoulezea wakati mwingine. Tulifunga ndoa na kuianza safari hii pamoja.
Miaka miwili baadaye…
Ndoa! Ndoa! Ndoa! Maisha
ya ndoa yana changamoto nyingi kwa kweli. Unaweza kujiandaa kwa mengi kabla ya
ndoa lakini ukaja kukutana na mapya na mageni kabisa. Nilijiamini kuwa kutokana
na umri wangu na uzoefu wangu nisingepata shida katika ndoa. Niliamini pia kuwa
nimejijenga vya kutosha kifedha hivyo suala la mahitaji ya kifedha
lisingelikuwa tatizo kabisa kwetu. Zaidi nilijiamini kuwa, katika sekta muhimu
ile, nisingepata changamoto yoyote kwani nina uzoefu wa miaka nenda rudi. Kwa
hakika nilikuwa nimejidhatiti.
Miaka miwili hii
ilikatika bila changamoto kubwa zozote. Mengi yalikuwa ya kawaida na yaliweza
kutatulika, na hapa ndipo nilipojipa kichwa kuwa nilikuwa nimejiandaa vyema.
Sikujuta kuchelewa kuoa kama ambavyo jamii ilitaka kuniaminisha. Mke wangu
alikuwa akimalizia masomo yake ya uzamili na kwa kuwa tulikwisha liongea hata
kabla ya ndoa, tulikubaliana kuwa tusubiri hadi amalize shule kabla ya kutafuta
mtoto.
Siku moja nilishtuka
usingizini baada ya kusikia sauti bafuni. Mke wangu hakuwa kitandani nami.
Baada ya kusikiliza kwa makini nikagundua ni yeye yupo bafuni na alikuwa
akitapika. Niliamka ghafla na kwenda kumuangalia. Alisema alijisikia
kichefuchefu. Kichwani kwangu kengele ya hatari ikalia. Ilikuwa imetimia miezi
sita sasa tangu amalize shule hivyo siku yoyote tulitegemea hali kama hiyo.
Sikutaka kuendekeza wazo hilo nikaharakisha kwanza kumpa huduma ya kwanza na
kumpa maji ya kusukutua. Hakutumia dawa yoyote maana baada ya hapo alisema
anajisikia vyema na huenda ni chakula tu kilikataa. Tulirudi chumbani na
kuendelea na usingizi. Huenda naye alikuwa na wazo kama langu lakini hakuna
mmoja wetu aliyetaka kusema kwanza. Na sikutaka kujiaminisha sana maana kweli
alitapika chakula chote tulichokula usiku. Sikupata usingizi kwa muda nikaanza
kufikiria ambavyo mtoto wetu atakuwa. Nilipanga kumpa mema yote ya nchi.
Tulishapanga na jina la mtoto. Saa ya ukutani ililia kuashiria ni saa tisa
usiku. Sikuwa na hofu ya kuchelewa kuamka kwa kuwa sikupanga hata kwenda kwenye
miradi yangu hadi saa nne hivi. Kwa furaha niliyokuwa nayo nikajisemea hata gym
kesho sitokwenda. Raha ya kuwa bosi wako mwenyewe. Niliwaza kama akiniambia ni
mjamzito kweli tutakwenda safari Zimbabwe kuyaona maporomoko ya Victoria.
Alitamani kwenda huko siku nyingi. Naam, lazima nimpeleke huko. Ghafla saa
ikalia tena, saa kumi usiku. Nikajiambia, ‘sasa inakubidi ulale bosi’.
Nikatabasamu moyoni na kupotelea usingizini.
Saa tatu asubuhi
nilishtuka usingizini nikiwa nimebanwa na haja ndogo. Nakumbuka niliisikia
tangu nikiwa kwenye dimbwi langu la mawazo usiku lakini nikaona uvivu kuamka
tena. Nilipatwa na maumivu makali wakati wa kujisaidia. Baada ya tafakuri ya
haraka nikagundua kuwa sikuwa nimekunywa maji ya kutosha siku iliyotangulia na
nilikuwa nimeubana mkojo kwa muda mrefu hivyo nikajisemea hili litapita.
Niliamka na furaha sana na sikutaka hali ile inikoseshe amani. Mke wangu
alikuwa ameshaondoka kuelekea kazini. Nilijiandaa haraka haraka kuelekea kwenye
kikao cha saa nne na kabla sijaondoka nilikwenda tena kujisaidia na maumivu
yale yalijirudia. Niliishia kujishauri kuwa siku nyingine nisirudie kubana
mkojo kwa muda mrefu vile kisha nikaondoka.
Masaa machache baadaye
nilikuwa ofisi ya daktari nikimuelezea ambavyo maumivu yangu yalianza kimzaha
mzaha asubuhi ile na mpaka sasa hayajapungua. Nilifanyiwa vipimo vya UTI na
kukutwa safi. Daktari akaniambia anipime na STD ila nilitaka kukataa maana kwa
hakika baada ya ndoa yangu, sijawahi kuwa na mahusiano ya nje. Hata hivyo baada
ya ushawishi nilikubaliana naye kishingo upande. Majibu yalikuja kuwa niko safi
pia. Daktari alinipatia antibiotics (mpaka leo sijui kwa nini alinipa
antibiotics ilhali hakukuta tatizo lolote) na vidonge vya AZO kusaidia
kupunguza maumivu huku akiniambia baada ya kumaliza dozi niache hivyo vidonge
na mamumivu yakirudi basi nirudi hospitali. Nilirudi nyumbani na kuendelea na
maisha. Mke wangu aliniambia anajisikia vyema na hajatapika tena. Sijui kwa
nini, ila niliogopa kumuuliza kupima ujauzito maaana tulikuwa tunategemea hilo
muda wowote. Nilikaa kimya nami nikiendelea na dozi zangu bila kumuambia
kilichonitokea asubuhi. Sikutaka kuharibu furaha yetu.
Wiki mbili baadaye,
nilirudi nyumbani nikiwa na huzuni sana. Nilikaa kwenye kochi huku nikisubiri
mke wangu arejee. Nilikuwa kwenye hali ambayo yeye tu ndiye angeweza kunipa
neno la tumaini, neno la kunifanya niitamani kesho. Alirejea nyumbani na
tabasamu. Nililiona tangu alipofungua mlango maana nilikuwa nimekaa kwenye
kochi ambalo akiingia tu, ni lazima nitamuona.
Mke: “baby, baby….I
got news for you...” (aliongea na tabasamu kubwa usoni)
Kichwani kwangu nilikuwa
nimeshajiandaa na speech yangu kuwa “I need to tell you something” hivyo
sentensi yake ilinichanganya kabisa. Alianza kusakura kwenye pochi yake kama
atafutaye kitu. Alitoka na kikaratasi na kunikabidhi. Alikuwa na ujauzito.
Nilihisi kama jiwe kubwa limetuliwa begani mwangu. Nilinyanyuka nikamkumbatia
na kushindwa kujizuia, nikalia machozi kama mtoto mdogo. Naikumbuka ile siku
kama jana. Nakumbuka ambavyo alishtushwa na ‘reaction’ yangu maana alitegemea
ningefurahi. Lakini machozi yangu yalikuwa ya furaha pia. Ni furaha iliyofunika
huzuni iliyonitawala awali.
Baada ya kutulia
nilimuomba akae chini nami nimueleze yaliyonikuta siku hiyo. Baada ya kumaliza
dozi zangu na kuacha kutumia dawa zile za maumivu, bado maumivu wakati wa
kujisaidia hayakuisha. Nilikuwa nimerejea hospitali kwa ushauri zaidi. Baada ya
vipimo, daktari aliniambia kuwa siku ile walifanya testing ya mkojo tu ila
walihitaji kufanya culture kwa uchunguzi zaidi. Leo nilienda kupewa majibu.
Majibu yaliyonesha kuwa kulikuwa na chembechembe za ugonjwa ambao haukutibiwa
wote hapo awali. Nilikiri kuwa hapo nyuma niliwahi kupata maambukizi ya
kaswende (sijui ndo chlamydia?) lakini nilimhakikishia kuwa nilitumia dawa na
nilipona kabisa. Daktari aliniambia huenda ukawa umeniathiri zaidi ya
walivyoona lakini hakutaka kunipima wakati huo. Aliniandikia dawa na kunitaka
kurudi baada ya miezi miwili hivi kwa vipimo zaidi. Aliniambia nisiwe na
wasiwasi na ulivyonipa habari hizi basi nimesikia amani kugundua kuwa
sijaathirika kiasi cha kuharibu mfumo wangu wa uzazi. Nisamehe mke wangu kwa
kutokukueleza haya tokea mwanzoni. Hata hili la huu ugonjwa ni jambo
lililonikuta kabla hatujafahamiana na niliona nikufiche kwani sikutegemea kama
lingekuja kujitokeza mbeleni. Nilimueleza sababu ya mimi kulia ni mchanganyiko
wa hofu ya majibu niliyopewa kwa kuwa sikujua ni kwa kiasi gani ugonjwa ule uliniathiri
na furaha ya kugundua kuwa una ujauzito wangu.
Nilimuomba msamaha kwa
kutokumueleza yote hayo awali na hasa hilo la ugonjwa maana sikumbuki hata
ilikuwa wakati gani, ila kwa vyovyote vile ilikuwa kabla hatujakutana.
Alinisamehe na tukahamia kwenye kufurahia suala la ujauzito. Nilimshukuru Mungu
kwa yaliyotokea hata sikuweza kufikiri kukasirika kwa aibu iliyonikuta ama kwa
maelezo ambayo daktari aliniambia kuwa huenda nisingeweza kuzalisha tena.
Tuliendelea kuzungumza siku hadi siku juu ya yaliyotokea na kurudi katika hali
ya kawaida. Ulikuwa wakati mgumu lakini tuliuvuka vyema na ujauzito uliendelea
kukua.
2018
“Sitaki kumuona huyo
malaya, mhuni hapa kwangu! Naapa nitamuua..I hate her!” Naam, nakumbuka
nikiyatamka maneno hayo kwa hasira. Ni mke wangu. Nilijihisi kudhalilishwa kwa
hali ya juu. Alijifungua mwezi Disemba mwaka jana. Mtoto mzuri wa kike na
tukamuita Maila. Mtoto alifanana na mama yake kila kitu. Yani ilifika mpaka
kuanza kufananisha kisigino walau kutafuta ufanano na mimi. Nilijipa moyo kuwa
kama kachukua mwili kwa mama, basi atachukua akili kwa baba. Nilikuwa na furaha
isiyo kifani.
2018 March
Furaha yangu haikuchukua
muda mrefu kukatishwa. Wahenga walisema, “hakuna msiba usiokuwa na mwenzake.”
Sijapata kukutana na mwanamke katili namna hii duniani. Ama kweli nimefika
mahali nimeamini wanaowasema vibaya viumbe hawa wana haki hiyo. Viumbe wasiojua
wakitakacho. Nilitamani kumuondoa katika dunia hii kwa alilonitendea. Hata wewe
msomaji wangu naamini utakubaliana nami kuwa kwa alilofanya, hakustahili kuishi
hata siku moja ya ziada. Kwa lipi hasa alilokosa kwangu? Alikuwa na kila kitu.
Nilihakikisha anapata kila kilichokuwa ndani ya uwezo wangu. Kwenda kwake
kazini ilikuwa tu kama hobby. Alipenda alichokuwa akifanya nami sikuona sababu
ya kumzuia kisa tu nina pesa za kumtunza. Sikutaka pia kumlazimisha kuingia
kwenye biashara zangu. Nilimuahidi wakati tunafunga ndoa kuwa nitamsapoti kwa
ndoto zake zozote alizonazo na sitomlazimisha kufanya asichotaka kukifanya kisa
tu ni ndoto yangu. Kuwa, kuolewa na mimi isiwe sababu ya yeye kuua ndoto zake.
Niliahidi kutekeleza ahadi hiyo siku zote za uhai wangu na ndoa yetu. Lakini
kama wasemavyo, wao wenyewe hawajui wakitakacho. Women!
Nitakueleza
alichonifanyia kabla hujaaanza kunisema kwa kumhukumu vibaya. Msiba wa kwanza;
Maila hakuwa binti yangu! Naumia hata sasa kuyaandika haya. Nashindwa kujua
wapi nilipokosea. Nimefika mahali nikatamani hata nisingelijua hili, nimlee tu
mtoto kama wa kwangu. Lakini ndiyo nimeshajua. Sioni tena umuhimu wa kuendelea
kuishi na kutafuta mali. Vya kazi gani tena. Ili nani aje kuvifaidi?
Naam, msiba wa pili.
Baada ya uchunguzi zaidi wa hali yangu, iligundulika kuwa nilikuwa na uvimbe
ambao walikuja kugundua ni kansa. Daktari wangu aliniambia kuwa ni mara chache
sana hali kama hii kuwatokea wanaume maana sisi magonjwa ya zinaa yakitukumba hupatwa
na dalili mapema mno. Na kama tukitumia dawa bila ugonjwa kwisha, bado dalili
zitajitokeza tena. Zaidi sana, athari za ugonjwa huu kufikia hatua mbaya ya
kuathiri via vya uzazi ni ndogo sana kwa wanaume (mara nyingi kwa wanawake
ambao hawajatibu ugonjwa huu hupelekea kupatwa Pelvic Inflammatory Disease
ambayo huweza kuzuia kabisa uwezo wake wa kushika mimba). Nilimshukuru Mungu
kuwa wakati ninaanza matibabu mke wangu alikuwa mja mzito hivyo hata kama
mionzi ile itaniathiri basi walau Mungu amekuwa mwema kwangu akanijaalia kupata
mtoto mmoja wa damu yangu, kutoka viunoni mwangu. Nilishukuru kwa neema ile, na
ninaiita neema, kwa kuwa sikuistahili na niliona ni mavuno ya matendo yangu ya
zamani. Ninaapa kabisa, tangu nimpate mama Malia, sikuwahi kutokuwa mwaminifu
katika ndoa yangu hivyo sikutegemea madhambi yangu ya nyuma kuja kunifuata
huku. Ila sasa, mtoto si wangu. Nilimchukia sana mama Maila. Nimeangalia yote
mema niliyomfanyia, nimeangalia jinsi nilivyobadilika na kuwa mume mwema tangu
tuoane na sijaona sababu ya mimi kuyapitia haya.
2018 April 08, Jumapili
Ibadani...
“Na Mungu akamtuma Nathani kwa Daudi. Basi
akaja, akaingia kwake na kumwambia: “Palikuwa na wanaume wawili waliokuwa
katika jiji moja, mmoja alikuwa tajiri na yule mwingine alikuwa maskini. Yule mwanamume tajiri alikuwa na kondoo
na ng’ombe wengi sana; lakini yule mwanamume maskini hakuwa na chochote
isipokuwa mwana-kondoo jike mmoja, aliye mdogo, ambaye alikuwa amenunua. Naye
alikuwa akimhifadhi hai, na huyo kondoo alikuwa akikua pamoja naye na wanawe,
wote pamoja. Kondoo huyo alikuwa akila tonge lake, na kunywa kutoka katika
kikombe chake, naye alikuwa akilala kifuani pake, na kondoo huyo akawa kama
binti kwake. Baada ya muda, mgeni akaja kwa yule mwanamume tajiri, lakini
hakuchukua kutoka kati ya kondoo zake na ng’ombe zake ili kumwandalia yule
msafiri aliyekuja kwake. Kwa hiyo akachukua yule mwana-kondoo jike wa yule
mwanamume maskini, akamwandalia yule mtu aliyekuja kwake.”
Ndipo
hasira ya Daudi ikamwakia sana yule mwanamume, naye akamwambia Nathani: “Kama
Mungu anavyoishi, mtu huyo aliyefanya hivyo anastahili kufa! Na kuhusu yule
mwana-kondoo jike, atamlipa mara nne, kwa sababu yeye amefanya jambo hili na
kwa sababu hakuwa na huruma.”
Nikiwa
katika hali ya kufadhaishwa, aibu, hasira nilienda kanisani Jumapili hii. Kwa
kweli tangu mwezi jana nimekuwa na hasira na Mungu kwa nini ayaruhusu haya
yanipate mimi. Nimejiuliza ni kosa gani nilimfanyia binti huyu hadi Mungu
kuruhusu haya yanifike mimi. Hata kwenye biashara yangu, nilikuwa nimeachana
kabisa na magendo na kama ni rushwa basi sikuhusika moja kwa moja. Ni ngumu
kuendesha biashara bila rushwa. Kama si kodi zisizo na mantiki basi utawekewa
vikwazo vya kiutendaji. Kwa vyovyote vile utafanyiwa figisu ambazo kwa nje mtu
mwingine ataona ni utendaji wa kawaida lakini kwa ndani, kwa yule mfanyabiashara,
ndiye anayejua nini hasa kinachoendelea. Hata hivyo ni kwa kiasi kikubwa
nilikuwa nimeweza kujiepusha na hayo. Ni nini basi nilichokosea kustahili
fedheha hii? Kwa nini Mungu kaamua kuniadhibu mara mbili, hata yule niliyedhani
atanifuta machozi leo ninaambiwa si wangu. Nilijihisi kama maskini
aliyenyang’anywa kondoo wake na nilitamani kama walau kwa siku moja ningekuwa
na mamlaka ya mfalme Daudi, niliona hukumu aliyostahili mke wangu ni kifo tu.
Nilikuwa nimemkasirikia Mungu. Ndiyo nilikubaliana na aya ya mwisho ya neno
lililokuwa linasomwa, “...mtu huyo anastahili kufa!”
2012,
Kidamali Iringa
Mentor:
“Ayayayaya! Unaona ninachokiona lakini?” Niliongea huku nikimgusa
mwenzangu kuangalia upande niliokuwa nikiuangalia.
Rumbete:
“Ah! Ah! Ah! Mangi acha achia hapo hapo. Miaka 30 itakuhusu.”
Mentor:
“What!?? Yani ule mzigo wote bado ni under 18?”
Tulikuwa
tumefikia Kidamali katika shughuli zetu za biashara. Sijui siku hizi, enzi hizo
Kidamali ilikuwa kakijiji kadogo tu huko mkoani Iringa. Kwa sasa nadhani kipo
ndani ya jimbo la Kalenga. Hata sasa nakumbuka kanisa lile la Orthodox, sijui
lilijengwa mwaka gani. Ni hapa nilipomuona binti huyu, akiwa amevaa sketi
nyeusi ya marinda na kubeba ndoo ya unga kichwani akitokea mashine. Rumbete
alikuwa mwakilishi wa kampuni yangu mkoani Iringa hivyo wakati wote ninapokuwa
Iringa ilikuwa sina budi kusafiri naye. Rumbete ndiye aliyenionya kuwa binti
yule pamoja na umbo lake lile alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne tu na ndiyo
kwanza alikuwa ametimiza miaka 17. ‘Ama hakika watoto wa siku hizi wanakua
haraka,’ nilijisemea moyoni huku nikiendelea kummezea mate. Wakati huo yupo
kijijini, amevaa nguo zilizofubaa tu na bado hajakomaa vya kutosha lakini
anavutia vile. Pamoja na kwamba baada ya pale sikumueleza tena Rumbete lakini
moyoni niliendelea kummezea mate.
Tulirudi
Kalenga jioni ila akili yangu ya kipuuzi na kihuni haikutulia. Ilitaka
kumfahamu binti yule. Niliwasha gari na kurudi Kidamali kesho yake jioni kwenda
kumsaka. Haikunichukua muda kufahamu binti yule anapoishi baada ya kuwauliza
watoto waliokuwa wanacheza pale. Nilimpa mtoto mmoja shilingi mia na kumuambia
akamuite aje dukani. Kwa kuwa kulikuwa kumeshaingia kagiza niliweza kujificha
nisionekane na watu wengi. Nilikuwa nimeshaongea na muuza duka pale na ingawa
alijua lengo langu ni ovu, niliweza kumnyamazisha kwa fedha kidogo. Baada ya
binti kufika ilinichukua muda kumshawishi hata kunisikiliza lakini nilitumia
udhaifu wa dhiki zake kumshawishi. Nilimueleza kuwa ningerudi kesho yake
nimchukue twende Iringa mjini nikamnunulie nguo nzuri na mahitaji yake mengine.
Nilimuachia elfu kumi, fedha ambayo tangu azaliwe hakuwa amewahi kuimiliki.
Nilijua nimeshaweza kumteka. Tatizo la kutoroka kwao halikuwa kubwa kwani siku
iliyofuata ilikuwa siku ya shule. Tulikuwa tumeshazungumza mahali pa kumkuta na
kama ilivyokuwa nilimkuta. Sitaki kukumbuka sana maana ninapatwa na aibu.
Binti
wa watu alikuwa amejitunza na yuko bize na maisha yao ya dhiki akijitahidi
kufanya bidii shuleni lakini tamaa zangu zilikuwa zikikaribia kumfutia ndoto za
maisha mema na kumhukumu katika umasikini wa kudumu. Sikuliona hilo kwa wakati
huo. Nilifurahi kuokota dhahabu Kidamali, Iringa. Nilimuona tena kama mara
mbili au tatu zaidi na miezi miwili baadaye niliporudi pale aliniambia
anajihisi ni mja mzito. Hapo ndipo nilipoiona miaka 30 ikinitazama.
Nilimtafutia vidonge lakini havikusaidia chochote. Binti ilimbidi kusema kwao
kuwa ana ujauzito. Mtoto pekee kwa mama yake. Baba yake alikuwa mpita njia kama
mimi na hajulikani. Mama yake alikuwa akijitahidi kulima kumsomesha binti yake.
Alitishia kwenda kushitaki kwa mtendaji wa kijiji lakini wote hao niliwafumba
midomo kwa fedha. Nilimdanganya mama yake kuwa nitawahudumia kama
asiponishitaki polisi. Nilimuambia nikifungwa mimi basi hata wao maisha yao
yataharibika. Kwa kutumia dhiki ile ile nilifanikiwa kumnyamazisha mama yake
pia. Niliwatumia fedha japo kwa siri kubwa maana mimi mwenyewe niliona aibu kwa
nilichokifanya. Sikutaka mtu yeyote afahamu kwani sikutaka habari ile ifikie
mamlaka husika. Rumbete, kama utasoma hapa utaelewa sasa kwa nini nilizidisha
safari za Iringa na sikuwa nikikutafuta uambatane nami.
Kutokana
na umri wa binti, nilitaka pia kujiweka mbali nao. Hivyo baada ya muda nilianza
kupotea. Sikuwa na mpango wowote na binti yule zaidi ya tamaa za mwili tu. Neno
la mwisho nililolipata kupitia muuza duka ni kuwa binti alijifungua salama
lakini mfuko wake wa uzazi uliharibika. Asingeweza kushika tena mimba. Mama
yake alimpeleka kwa ‘wajomba zake mama yake’ huko mkoani Ruvuma. Hakujua zaidi ya
hilo. Baadaye mama yake naye alifariki na hakuna mtu mwingine tena pale kijjini
aliyekuwa akifahamu kuhusu binti yule.
“Ndipo
Nathani akamwambia Daudi: “Wewe mwenyewe ndiye yule mwanamume!” mchungaji alimalizia kusoma neno lile.
Nimelia
machozi baada ya kukumbuka tukio hili. Nimejiona jinsi gani nilikuwa kama
mfalme Daudi. Hapana, simaanishi alichofanya mke wangu ni sawa, lakini jinsi
ilivyokuwa rahisi kwangu kumhukumu bila kukumbuka kuwa nami nilifanya maovu
tena zaidi ya ya kwake. Jinsi gani ilikuwa rahisi kumhukumu tajiri aliyechinja
kondoo wa maskini na kusahau uuaji alioufanya kwa askari wake kisa tamaa ya
mkewe. Karma imerudi kunihukumu. Nipo hapa, mali nyingi lakini sina damu yangu
ya kuzirithi.
“Ndipo
Nathani akamwambia Daudi: “Wewe mwenyewe ndiye yule mwanamume!”
Wasalaam
wapendwa,
Mentor.
Kwa mara ya kwanza naomba niandike maelezo ya ziada;
ReplyDelete- Kisa hiki ni kisa cha ukweli kabisa (wahusika wamebadilishwa kuficha uhalisia)
- hata mimi mwandishi bado nipo kwenye dilemma ya kujua nani hasa ahukumiwe (au ahukumiwe zaidi).
Zaidi sana, ni lengo la mimi kuelezea mkasa huu;
- HUKUMU: Kabla hujamchukia na kumhukumu mtu kwa alilokufanyia, jichunguze kama hukuwahi kufanya kama yeye. Haimaanishi kwa kila kosa basi tunastahili adhabu lakini itatufanya kuwa wapole wakati mwingine tunapofikiria kumuumiza mtu mwingine. Mara nyingi, hasa kwenye mahusiano (na hii imewahi kunikuta) unamchukia mtu kwa kosa alilokufanyia. Unamtukana na kutumia maneno makali kuwa hakukupenda ndiyo maana akakufanyia A, B, C. lakini ukikaa kidogo ukafikiria 2012 huko Kidamali, Iringa, utagundua nawe uliwahi kumfanyia mwingine sawa (au zaidi) ya yale uliyofanyiwa. Ila kwa kuwa sasa kibao kimegeuka kwako, huuoni uovu wako ila wa yule aliyekutenda sasa. BIN ADAMU!
- HISTORIA: Uliyoyafanya kwa kificho, yatadhihirishwa mwangani siku moja. Mara nyingi tunafanya mambo kwa kuamini hayatakuja kutuumbua mbeleni. Kuna nyakati tunafanikiwa. Lakini, amin nakuambia, ipo siku uovu unaoufanya ukijua ni uovu utakuja kuku-haunt.
- NAFASI: Unayo nafasi ya kurekebisha na kuanza upya. Zaidi sana, unayo nafasi sasa ya kutafakari na kuishi sawa. Mfalme Daudi kwenye aya niliyoandika, alijuta na kutubu (kwa bahati mbaya kwake dhambi yake ilisababisha kifo/vifo) lakini alirejeshewa baraka zake. Alirekebisha mwenendo wake na Mungu akamrejeshea ufalme wake. Kwa kiingereza kuna mahali imeandikwa, "God considered him, a man after God's own heart." Inawezekana kurekebisha, inawezekana kuanza upya kwa usahihi na inawezekana kutafakari sasa na kuepuka kufikia kwa Daudi na Mentor. Usiendelee kuumia kwa uliyotendwa. Usiendelee kuumia kwa kuwaza uliyoyatenda. Unayo nafasi ya kuanza upya sasa. Itumie...
Wasalaam wapendwa,
Mentor.
Such a well composed true story!
ReplyDeleteTunayo nafasi @Mentor!
Thank you for this reminder...
Blessings! !
I very like reading through a post that can make people thinks. Also,
ReplyDeletemany thanks for permitting me to comment!scr888
Well done my friend and as the Bible says, "All have sinned and fallen short of the glory of God", which is why we have Jesus in our lives.
ReplyDeleteYou are right it is not so much what we have done, but what are we going to do about what we have done.
The longer I live the more I find it is my mistakes and failure rather than my successes that have shaped my character.
God Bless
Thank you for the very important additional comment. I am even more amazed at how you understood the story, it being in Swahili.
Delete