MWANAYUMBA: PART II
Juni 2015
Ilikuwa siku ya Jumamosi, mwanzoni kabisa mwa mwezi huu wa sita.
Nilikuwa nikiendesha gari kutokea baharini kwa kupitia njia hii ya kati ya
Ikulu yetu ya Magogoni na Ikulu ndogo ya Zanzibar kama unaelekea hospitali ya
Ocean Road. Safari yangu ilikuwa ikielekea Chuo cha Utalii. Nilipofika eneo la
round about ile nikitaka kukunja kushoto kuendelea na safari yangu macho –
yasiyo na pazia – yalielekea upande wa kulia ambapo kuna lango la kuingilia
hospitali hiyo ya Ocean Road.
Niliiona sura ambayo ama kwa hakika haikuwa sura ngeni kabisa
machoni pangu. Kutokana na uharaka wa nilichokuwa nikikifuata huko chuoni
nilishawishika kutaka kuendelea na safari yangu. Wakati huo huo akili yangu iliniambia
niangalie tena kulia kwani ninamfahamu mtu huyo. Hapo ndipo nilipogundua kosa
nililokuwa ninalifanya. Kwa muda huo ambao akili yangu ilikuwa ikiwaza yote
hayo, gari lilikuwa likijiendesha lenyewe kwani niliposhtuka ilikuwa ni baada
ya madereva walio nyuma yangu kupiga honi zisizo na idadi, hawakujua nilitaka
kwenda upande upi. Nilijilazimisha kukunja kona ya nguvu na kuzunguka tena
round about ile na kisha kwenda kusimama mbele tu ya kibao cha hospitali.
Nilishuka kwa haraka na kwenda kumfuata binti yule huku akili
yangu ikiniambia kwa hakika yule ndiye. Kutokana na tukio lililotokea sekunde
chache kabla ya hapo, lilimfanya hata yule binti kusimama na kuhamaki huku
akinishangaa kama ambavyo wapita njia wengine walivyokuwa wakishangaa huku
wengine wakinitukana na kusema walichoweza kusema. Nilishuka kutoka kwenye gari
kwa haraka ili nimuwahi kabla hajaingia hospitalini ndani.
“Mwanay…!”
nilijikuta nimekatisha sentensi yangu baada ya kugundua kosa kubwa
nililolifanya. Hakuwa yeye! Lakini alifanana sana na Mwanayumba wangu. Duh
nilisikitika sana! Na kama kuongezea pilipli kwenye kidonda – au kama wahenga
wasemavyo, hakuna msiba usi na wenziwe – nikagundua kosa lingine nililolifanya.
Kumbe vijana wa fursa walipoona nimetoka kwenye gari ghafla
walikuja na kuniibia laptop na simu yangu iliyokuwa kwenye gari. Hapo hapo wale
wa kufunga tairi wakawa wamefika tayari kufunga tairi za gari langu kwa kuwa
nilipaki sehemu mbaya isiyoruhusiwa. Nilibaki nimeduwaa maana niliona
wakikimbia na sikujua kama mimi ndo nimeibiwa.
Nilimsalimia yule binti ingawa alionekana sasa na haraka ya
kuingia hospitalini. Nilipotaka kurudi kwenye gari ili nichukue kadi yangu
nimpatie ndipo nilipogundua hayo niliyoyaandika hapo juu. Ilinibidi nirudi
nichukue kalamu na karatasi na kumuandikia, “You remind me of a girl – 0784436***” Nikamuachia na kuondoka
kwenda kupambana na wazee wa Halmashauri. Hili tukio mpaka kesho sijawahi
kuelewa lilivyotokea; alinisubiri nikaenda kwenye gari pamoja na kwamba hakuwa
hata akinifahamu.
Ilikuwa mkasa juu ya mkosi mpaka nikajuta kupitia njia ile
kwani sikuwahi kuipitia kabla ya siku hii kwenda chuo cha utalii ambapo
nilikuwa nikienda kumpelekea laptop ‘mchumba wangu’ Happy. Laptop ambayo tayari
imeshaibwa na alikuwa akiihitaji kwani alikuwa na presentation baadaye siku
hiyo.
“Nisamehe mamii”
Nilianza kujitetea baada ya kufika chuoni hapo na kuonana naye.
“Nooo babes, usiniambie
umeisahau jamanii” alilalamika Happy. Nilitamani ingekuwa hivyo nikawaza
naanzaje kumuelezea laptop ilivyoibiwa?
“Unatakiwa kunipa pole
kwanza!” Nikaanza kuelezea ambavyo wakati nimetoka ferry nilivyokutana na
mgogoro pale usawa wa soko la samaki na wakati nikiangalia upande wa kulia
sekeseke lililokuwa likiendelea ndipo niliposhituka kuwa nimeshaibiwa simu na
laptop. Alikasirika sana Happy nakumbuka. Nami nilielewa kwani mimi sijawahi
kuwa mzembe kiasi kile.
Jioni nilipokea simu nisiyoitegemea. Ilikuwa kutoka kwenye
namba nisiyoifahamu na pamoja na kwamba nilikuwa nime-install application ya
‘true caller’ bado ilishindwa kunijulisha nani alipiga namba ile. Bado nilikuwa
na huzuni kwani tukio la mchana bado lilikuwa limeniacha na mchanganyiko wa
hisia na Happy aligoma kuja kwangu jioni hiyo.
Niliipokea kwa wasiwasi, “Hello”
“Hello Mentor.”
Ilikuwa sauti ngeni lakini si ngeni, sikutaka tena kujichosha kuwaza ni wapi
nimewahi kuisikia, nilisubiri ajitambulishe mwenyewe.
Naam, ilikuwa sauti ya Mwanayumba!!! Mwanayumba…uliipataje
namba yangu?
Kumbe, binti yule niliyemfananisha asubuhi alikuwa ndugu yake
na kwamba hata yeye mwenyewe alikuwa ndani hospitalini. Alinieleza kuwa baba
yake mzazi alikuwa mgonjwa na wapo Dar kwa ajili ya tiba ya baba.
Kumbe, binti yule alipofika ndani hospitali alimsimulia
Mwanayumba kisa chote kilichotokea nje hadi kumuonesha karatasi ile
nilipoandika namba yangu ya simu. Anasema aliikumbuka wakati uleule alipoiona
na kujua kuwa ni namba yangu, akaisave kwenye simu yake na ndo amenipigia.
Alinieleza jinsi gani baada ya sisi kukutana pale Shoprite
Arusha aliibiwa simu na tangu siku hiyo amejitahidi kunitafuta bila mafanikio.
Kiufupi, pamoja na mengine mengi, ameolewa na ana mtoto
mmoja, yeye na mumewe wanaishi Arusha. Hapo ndipo paliponirudisha mawazo kwa
ndugu yake! Niliumia moyo maana kusema kweli bado nilikuwa na hisia juu yake
lakini aliponieleza kuwa ameolewa moyo wangu ulivunjika. Ni kweli sikuwa
nimetegemea kuonana naye tena, na nilikuwa nimeshaanza mahusiano mengine lakini
kitendo cha kuisikia sauti yake nyembamba yenye kubembeleza kulinikumbusha
kipindi kile, 2003, wakati bado tupo kwenye mahusiano.
Nilimuambia asimueleze ndugu yake kama tunafahamiana na
akakubali maana tulikubaliana kuwa sasa mimi na yeye hatuna tena ‘future’
pamoja.
Baada ya hapo aliniambia atamshawishi ndugu yake anitafute na
kweli kuanzia siku iliyofuata tulianza kuwasiliana kwa ukaribu na huyo ndugu
yake bila huyo ndugu kufahamu mchezo aliochezewa.
Nilijikuta katikati ya pembetatu ambayo sikuifurahia.
Kwenye pembe moja alikuwa Happy ambaye nilianza kuanza kumbembeleza
anisamehe kwani lililotokea halikuwa uamuzi wangu, na ni jambo ambalo lingeweza
kumtokea mtu mwingine yeyote. Ilimchukua muda kunisamehe maana kazi zake za
shule nyingi zilikuwa mule na pamoja na kujitolea kumnunulia nyingine lakini
hakufurahia kabisa. Pamoja na hayo, bado alibaki kuwa ‘mchumba wangu’ (naweka
kwenye parandesi maana ni mchumba wa mjini, wazazi hawamfahamu, ila ninampenda!)
Uhusiano wetu ulipungua nguvu sana katika kipindi hiki jambo lililopelekea kukua
kwa pembe nyingine hizi mbili.
Kwenye pembe ya pili, alikuwa ndugu yake Mwanayumba. Huyu
tulianza kuwasiliana kimzaha mzaha. Alinielezea walivyonicheka siku niliyomuona
na mkasa ulionipata ila alinisifu maana nilionesha ujasiri wa kipekee. Yeye
alikuwa akisoma CBE hivyo yeye alikuwepo jijini hapa. Kidogo kidogo maongezi
yakaelekea kwingineko. Sitaki kutumia sababu ya ugomvi wangu na Happy kama
kigezo lakini ulichangia sana. Tulianza kukutana mara moja moja na siku ambazo
Happy alikwenda kumtembelea dada yake huko bara basi alikuja kwangu.
Kwenye pembe ya tatu alikuwa Mwanayumba. Tulikuwa na mambo
mengi ya kuzungumza hasa kwa kuwa ilikuwa takribani miaka saba tangu tuonane na
mengi yalikwisha tokea hapo kati. Alikuwa ameolewa na wamebahatika kupata mtoto
mmoja mpaka sasa. Alinieleza matatizo aliyokuwa nayo kwenye ndoa yake hasa kwa
kuwa mumewe hakupenda yeye ajiendeleze kielimu. Yaani ingekuwa ni uamuzi wa
mumewe huyo, basi angemwachisha kazi kabisa. Hatukuwahi kabisa kugusia kidonda
kilichokuwa kimeshaanza kupona cha mapenzi yetu.
Siku iliyobadilisha mwelekeo wa maongezi yetu ni siku ambayo
bila kukusudia wakati tunawasiliana kwa jumbe za simu tulijikuta sote tumetumiana
ujumbe unaofanana; “Ila nilikupenda,”
ulisomeka ujumbe huo.
Wakati hili linatokea
ilikuwa imeshafika mwezi wa nane kama sikosei. Mahusiano yangu na Happy
yalikuwa yakielekea kuzuri baada ya muda kutusahaulisha tukio la kuibiwa
laptop. Nadhani kilichosaidia zaidi ni kwamba walau alikuwa ameshamaliza chuo
na laptop niliyomnunulia; maana ilikuwa mara mbili zaidi bora kuliko yake ya
mwanzo…asante JK!
Kilichotokea
mwezi huu wa nane, Agosti 2015, ni ubinadamu…naomba msomaji wangu usinihukumu!
Nilichukua likizo ya dharura ya siku 14 tukaenda zetu
Morogoro kuwasalimia wazazi wa Happy. Tulikaa kwa siku nne mkoani huko na
kurudi zetu Dar wikiendi. Alikuwa akifanya kazi ya kujishikiza katika kampuni
moja ya binafsi na kwa kuwa alikuwa bado mgeni alipewa siku saba tu za ruhusa
yake hiyo. Hivyo mimi nilibaki na siku nyingine saba za mapumziko peke yangu. Tulipanga
mwezi wa kumi na mbili tungeenda wote Moshi na yeye akawafahamu wazazi na
baadhi ya ndugu zangu. Tulipanga mengi sana ikiwemo kuanza mipango ya ndoa yetu
ifikapo mwakani. Yaliyotugombanisha yalikuwa yameshasahaulika.
Wakati huo huo, nduguye Mwanayumba alikuwa ananisumbua sana
kutaka kupafahamu kwangu. Nyumba yangu – enzi za ujana wangu – nilikuwa nikiiita
‘kichinjioni’! Nikabaki najiuliza, ‘sawa
nimebadilika na niko kwenye kuelekea hatua kubwa sana maishani mwangu, lakini
je, nitaweza kujizuia akija kwangu?’
Niliamua liwalo na liwe, sikuwa na mpango wowote na yeye hivyo
hata likitokea sitakuwa na deni lolote kwake, nikamkaribisha siku ya Jumanne.
Kwa kuwa Happy alikuwa kazini sikuwa na hofu yoyote alipokuja. Sitaelezea
yaliyotokea ila yalitokea!
Jioni wakati namrudisha ferry ili aende kwake nilipokea
ujumbe wa simu ulionichanganya. “Mentor,
nipo njiani kuja Dar kuchukua dawa za baba. Sijawaambia ndugu zangu kuwa
ninakuja leo. Ninahitaji kuongea na wewe leo naomba uje kunipokea Ubungo,”
alikuwa Mwanayumba.
Na kama kuhakikisha kile alichoniambia, nduguye alijikuta
akisema tu kuwa Mwanayumba angekuja kesho, "anakuja kuchukua dawa za baba yake."
Safari ya ferry ikarefushwa kuelekea Ubungo. Huku nyuma
nikamwambia Happy kuwa nimevuka naenda kukutana na marafiki zangu na
nitachelewa sana kurudi hivyo tusingeonana siku hiyo. Hakuwa na wasiwasi na
mimi. Ingawa sikujua lengo la wito huu wa Mwanayumba lakini sikuwa na wasiwasi,
nilikwisha jiapia tangu miaka mingi kamwe kutojihusisha kimapenzi na mke wa mtu…hata
iweje! Nilijua tu kwa kuwa hakuwa na wakati mzuri na mumewe, alikosa mtu wa
kumsikiliza hivyo ni kweli alihitaji tu mtu wa kuongea naye. Sikwenda na
maandalizi yeyote!
Nilifika Ubungo na kumpigia simu ambapo aliniambia baada ya
kuona ujumbe wangu haujajibiwa aliamua kuchukua chumba na kupumzika. Alinielekeza
alipofikia nami bila hiyana niligeuza gari kuelekea kunako hoteli moja pembeni
mwa stendi ya mabasi yaendayo mikoani ya Ubungo. Ndiyo, ingawa siikumbuki jina,
nakumbuka ipo nyuma ya hostel ya chuo kikuu cha Dar es salaam ya pale Ubungo.
Kwa kuwa sikuwa nimekula na kwamba nilifika mida muafaka
kabisa ya kupata chakula cha jioni tuliagiza chakula cha jioni nikimuambia kuwa
tutaongea wakati tukila ili tuokoe muda niweze kurudi kwangu, tuue ndege wawili
kwa jiwe moja. Naye akapendekeza kama ni hivyo basi tupelekewe chakula chumbani
ili tuweze kuongea kwa uhuru. Sikuwa na hofu yeyote nilihisi tu yatakuwa ni
maongezi yenye kuhitaji faragha na asingependa watu pale wafahamu mambo yake ya
sirini, nikakubali.
Nadhani itoshe kusema kuwa tangu mlango wa kuingia chumbani
ulipofungwa nasi kujikuta chumbani wawili tu hadi wakati nilipoufungua mlango
kutoka muda wa saa tano ya usiku, sidhani kama tuliongea maneno zaidi ya kumi
chumbani humo. Niliondoka kwa aibu kubwa ya kitendo tulichokifanya, nilijijutia,
nilijichukia, niliichukia siku hiyo.
Nilirudi kwangu na tangu siku hiyo sikuwasiliana tena na
Mwanayumba! Ilikuwa afadhali kuishi hivyo, ilikuwa afadhali kipindi kile
nilipokuwa nikimtafuta bila mafanikio. Hata ndugu yake ilinibidi kumueleza
ukweli kuwa nina mchumba hivyo tulibaki kuwasiliana kishikaji tu pamoja na
kwamba alinikasirikia mwanzoni ila mara moja moja alikuwa akija tunacheza ‘video
games’ kwangu…he he he
2016, May 22,
Jumapili
Tulikuwa tumetoka ibada ya asubuhi mimi na mchumba wangu
Happy.
Tulirudi nyumbani kwake kwa ajili ya kupata staftahi. Ni wakati
huu nikiwa napeleka vihusika sebuleni kutoka jikoni ndipo ulipoingia ujumbe
kwenye simu yangu – niliyoiacha jikoni tulipokuwa tukipika na Happy wangu.
Nilirudi jikoni nikakuta ameshikilia simu huku uso wa simu
ukinielekea mimi ili nisome vyema ujumbe uliokuwa umeingia. (Kwa bahati mbaya
simu yangu ikiingia ujumbe huwa ujumbe una ‘pop up’ juu ya screen…sijui
nielezeeje vyema uelewe)
“From: nduguye Mwanayumba
Ujumbe: Mwanayumba amejifungua mtoto anafanana na weweeeeee….”
Ujumbe: Mwanayumba amejifungua mtoto anafanana na weweeeeee….”
Nilimuangalia Happy usoni kutaka kufahamu yuko kwenye hisia
ipi na sikufurahishwa na sura niliyoiona. Ilikuwa ni sura yenye kutaka maelezo.
Nitaanzaje kumuelezea! Mwanayumba ni nani? Huyu aliyetuma ujumbe huu ni nani? Kwa
nini aniambie kuhusu mtoto wa Mwanayumba? Nianze kumuelezea kutokea wapi? Niruke
sehemu ipi? Laptop yake?
Ngoja kwanza…MTOTO HUYU NI WA NANI? Akili ilihama ghafla hadi
kwenye chumba kile, siku ile Ubungo. Hapa ndipo nilipogundua kuwa kichwa cha
binadamu ni zaidi ya mashine maana bila kujigusa niliweza kuhesabu miezi na ndipo
hapo iliponiingia kichwani.
“HAIWEZEKANI!”
nilijikuta nikiropoka kwa nguvu.
“Haiwezekani nini
Mentor?” aliniuliza Happy. Nilishtuka kutoka kwenye lindi langu la mawazo
ya kujitakia na kugundua kumbe nipo na Happy na ninatakiwa kujibu maswali mengi
sana ambayo sijui naanzaje kuyaelezea.
Nilirudi sebuleni huku Happy akija nyuma yangu. Alitaka majibu!
Sikuwa na majibu! Ghafla nikaukumbuka wimbo wa zamani wa Shaggy – It wasn’t me! Nilitamani niutumie walau kwa wakati ule
niondoke pale nikapate uhakika kwanza wa habari zile. Lakini ningewezaje
kusema, “aaah babe atakuwa alikosea tu
mtu wa kumtumia ujumbe” wakati nilishapayuka mengine ya zaidi?
Baada ya lisaa lizima la kuelezea maneno yasiyoeleweka
nilifukuzwa – na njaa yangu – nikarudi kwangu. Lakini kwanza nikapitia mahali
nikapata supu nikampigia simu Mwanayumba lakini hakupokea simu yangu.
Nikampigia ndugu yake akanielezea ambavyo mtoto anafanana na mimi yani kama
angejua tunafahamiana basi angekuwa na uhakika kuwa mtoto ni wa kwangu. Jambo
jema ni hakujua kuwa mimi na Mwanayumba tulikuwa tukifahamiana hata kabla ya
yeye. Nilimuomba anitumie picha na akaniahidi atanitumia lakini hadi naandika
hapa hatajinitumia na hataki kupokea simu yangu tena.
Mwanayumba, kama utasoma hapa naomba ufahamu umeniumiza tena
kwa mara ya pili. Sikutegemea kufanya tulilolifanya lakini pia sikutegemea
kupata matokeo tuliyoyapata. Najua umeolewa hivyo sina haki wala dai juu yako
lakini ningependa tu kufahamu kama mimi ndiye nilihusika na ujauzito huo au la!
Mwanayumba umebadili na namba za simu na sijui umemuambia nini mdogo wako
hapokei tena simu zangu. Sijui njia nyingine ya kukupata lakini natamani
ningefahamu ukweli. Natamani ungeniweka wazi…au tusubiri tena miaka mingine
kumi hadi tutakapokutana tena katika mazingira yasiyoelezeka ndipo nitaufahamu
ukweli? Nilikupenda kweli ila umeniumiza, ni afadhali nisingekutana tena na
wewe…
Wasalaam
wapendwa,
Mentor.
No comments:
Post a Comment