Karibu Mjini
Imeishazoeleka unaposafiri kutoka mkoani (najua wa mikoani hatupendi kweli kuitwa hivyo) kwenda jiji la wajanja, Daslam, lazima upewe mualiko wa kukukaribisha mjini. Ni kawaida sana kukutana na wajanja wa mjini wakakuibia ama kwa nguvu au kwa kutumia bongo tu ukajikuta umeuziwa sabuni badala ya simu. Na usiombe tukio hilo likukute ukiwa tu ndo umeshuka Ubungo na begi lako la BILABONG. Utapachukia sana.
Ni mwaka wa tano tangu niwasili kwenye jiji hilo lenye dhiki na adha nyingi lakini bado twapenda tu kujulikana twaishi humo. Lakini zaidi ya yote, sijawahi kuingizwa mjini kutapeliwa au kuibiwa muda wote huo. Hii imepelekea mimi kujiona kidume na siwezi tapeliwa tena maishani mwangu.
Hadithi hiyo ilibadilika nilipofika mkoani Katavi wilaya ya Mpanda.
03 Oktoba 2014, Ijumaa
Safari yangu ya utalii wa ndani ya nchi ilinifikisha Mkoa mpya wa Katavi kwenye wilaya ya Mpanda. Ni siku ya Ijumaa ambapo tuliwahi kufunga kazi hivyo kunipa wasaa wa kuweza kuzunguka kwenye viunga vya mji huu mkongwe ndani ya mkoa mpya. Ni hadi nilipofika eneo la Majengo ambapo kuna soko ndipo nilipatwa na tukio linalonilazimu kuandika kisa hiki kifupi.
Nilikuwa na mwenyeji wangu bwana Hemedi ambaye alikuwa akinionesha maeneo ya mji huo. Nahisi ni kutokana na kutumia sana vidole vyake kunionesha kila kitu ndipo kijana mmoja alipoweza kungamua kuwa sikuwa mwenyeji wa mahali hapa. Nilikuwa nimetupia uzi wangu wa Chelsea.
Ndipo alipokuja kijana mmoja akiwa kachangamka akanisalimia kama shabiki mwenzake. Mara anipe mkono mara ashike jezi yangu huku akitamka maneno ya kusifu sana chama letu. Mimi niliona kawaida sana wala sikushtushwa na lolote kwani nilikuwa najua wafipa (sina maana hiyooo) ni washamba washamba tu hakuna mtu anayeweza kuniibia. Ghafla akajifanya kugeuka kurudi tulikokuwa tukitokea.
MWIZI! Ndilo neno la kwanza lililonitoka baada ya kuhisi ghafla kuwa mfuko wa jeans umekuwa mwepesi. Sikuhitaji kuushika kuthibitisha kuwa wallet yangu haipo tena. Niligeuka na kumuona akikaribia kona moja aingie sokoni katikati ambapo ama kwa hakika akifanikiwa tu, sitoweza kumuona tena.
Watu walisikia nilivyoita mwizi mara ya kwanza na wote walikuwa macho kuona huyu mwizi yuko wapi. Nikatoka mbio huku nikimnyoshea mkono. Kabla hajakunja kona tu akakamatwa na kabla hata sijasema alichoiba wala kuthibitisha kwao kuwa ndiye au la, alianza kupokea kipigo. Nilimfikia na mimi kuanza kumshushia kipigo kabla hata ya kumdai wallet yangu kwani nilikuwa na uhakika ndiye.
Watu waliochelewa kujiunga na karamu ile nao wakaanza kusogea karibu huku wakiokota mawe na zana yeyote itakayofaa kumtia adabu kibaka yule. Sikumuonea huruma. Mara nyingi ninapoona mwizi anapigwa huwa nawaza kama ndiye kweli anayepigwa au huenda anayepigwa siye mwenye kosa. Kwa siku hii wala sikuwaza hivyo.
Ghafla akiwa mtu kati, akaongezeka na mtu mwingine pale kati, mzee wa makamo kiasi, akamkimbilia na kwenda kumkumbatia kibaka yule. Watu waliendelea kurusha mawe na fimbo hadi walipogundua kuwa zana hizo zinampiga mtu asiyehusika.
Wengi walianza kumtukana mzee yule na kumtaka aondoke kwani watamuua. Mzee yule hakusikia na ndiyo kwanza akazidi kumkumbatia kibaka. Wengi walidhani ni mwanaye au wana undugu Fulani. Ilibidi tusitishe zoezi la kumpiga mwizi na kumtoa yule mzee kwa Yule mwizi. Mzee akatuomba tusimpige mwizi kwanza hadi atuelezee kisa hasa cha kwanini hataki tumpige.
"Mimi nikiona mwizi anapigwa lazima nimuokoe," alianza kuelezea mzee yule. "Mwizi aliokoa maisha yangu."
"Ilikuwa ni mwaka 2001 mkoani Tabora. Nilikuwa afisa elimu wa Wiaya ya Tabora mjini. Kipindi hicho wanangu walikuwa likizo kwa bibi yao wilayani Kishapu. Tulibaki nyumbani na mke wangu.
Nakumbuka vyema usiku wa kuamkia siku ya tukio tulikuwa na mabishano ambayo hadi wakati tunaamka hatukuwa tumeyasuluhisha. Hatukufikia muafaka. Ni muda mrefu sasa tulikuwa tukibishana juu ya jambo lile. Nilijua sana kuwa mawazo yangu yalikuwa sahihi na hilo lilithibitika miezi michache baadaye kuwa alikuwa akibishana na mimi vile kwa kuwa alikuwa amempata mtu aliyekuwa akimdanganya. (kwa kipindi kile sikuweza kufahamu).
Niliamka na kwenda kazini ambapo kwa kawaida ya mji wa Tabora, siku ya Ijumaa watu hufanya kazi nusu siku. Nami ilipotimu mida ya saa sita unusu nilifunga ofisi na kuelekea nyumbani kwani sikuwa muumini. Nilifika nyumbani na kumkuta mke wangu akiwa nje anafua nguo. Nilitaka kutoka kwenda kupiga soga na wazee wenzangu kwani nilijua mchana huo siwezi msemesha mke wangu aniandalie chakula. Huko nje walau ningepata kahawa na visheti vya kutuliza njaa.
Kwa hali ya kushtua mke wangu alikuja na kunipa pole ya kazi kisha kunipokea mkoba na kunitaka kwenda kuoga ili nitakapotoka nikute chakula kiko tayari. Tulikuwa tumezoea kutaniana kutokana na aina ya chakula anachopika. Yaani kama angekuwa anapika cha muda mrefu angeniambia, mume wangu leo oga kimamtoni na kama ni chakula cha kuiva haraka angesema, baba nani leo kama unaoga uswahilini nyumba za kupanga aliniambia nioge kimamtoni zaidi hivyo nikajua chakula kitachukua muda kidogo kuiva.
Hivyo nilifanya taratibu alimradi baada ya dakika 45 ndipo nilipotoka chumbani kuelekea sebuleni. Sikutaka kuhoji mabadiliko yale maana sikutaka kutibua mabishano tena. Nilishaamua muda utasema vyema zaidi nani yuko sahihi kati yangu na yeye.
Nililetewa ugali kwa mlenda. Ama hakika alidhamiria kuimaliza hasira yangu huyu mwanamke. Hakuna chakula nilichokipenda kama hicho hasa niwapo na njaa kweli. Alinitengea kwenye sahani kisha kuvuta kiti akae. Nilikata tonge langu kubwa na kulimega mara mbili kisha kipande kimoja kukichovya ndani ya bakuli lenye mlenda. Nikiwa katika safari ya kuutoa mkono kwenye bakuli kuupeleka kinywani ilisikika sauti kutoka nyuma ya kochi ikisema tena kwa sauti ya hamaki- usile hicho chakula mzee.
Tulishtuka sote mimi na mke wangu. Tuligeuka kumuangalia kijana aliyekuwa amesimama sasa nyuma ya kochi. Alianza kuongea kwa haraka kabla hatujasema chochote. Samahani mzee, mimi kweli mwizi na nilikuwa nimekuja kuiba hapa kwako baada ya kugundua mlango wa mbele wa nyumba yenu uko wazi na mkeo alikuwa uani akifua nguo. Wakati natafuta kitu cha kuiba ghafla ukaingia na ndipo iliponibidi kujificha nyuma ya kochi hili. Lakini mzee wakati mkeo akikuandalia chakula nilimuona akikuwekea kitu kama sumu kwenye chakula chako ndo maana mzee nimeshindwa kujizuia.
MH! Moyo ulinilipuka kwa hofu. Akili ikawaza haraka haraka kuwa dakika chache baada ya hapa mimi ningeshakuwa marehemu. Wakati naendelea kutafakari hali ile mke wangu akadakia kupiga kelele za mwizi. Nilmpa kibao kimoja tu cha shavuni na kunyamazisha. Nikamwambia ale kile chakula. Alikataa katukatu na kunithibitishia alikuwa ameniwekea sumu.
Nilimfuata yule kijana na kumuuliza alitaka kuiba nini pale kwangu. Akaniambia chochote ambacho angeweza kuiba. Ndugu zanguni, vitu unaweza kununua lakini uhai je? Nilimwambia achukue chochote anachokiona atakachoweza kubeba.
Ghafla yule kibaka aliyekuwa ameniibia wallet yangu alinyanyuka kwa spidi ya radi na kuchomoka mbio ambazo zilituacha tumeduwaa kwa muda. Ni hadi nilipogundua kuwa bado alikuwa na wallet yangu ndipo niliponyanyuka kutaka kumfuatilia lakini hakuonekana hata alipopitia.
Hadithi ya yule mzee hata haikuninogea tena kwani nilianza kuwaza kadi zangu zote zilizomo mule zikiwamo na za benki.
Ni saa 23:21 sasa Jumamosi 04/10/2014 nimetoka kuongea na mwenyeji wangu ambapo amenikata maini kabisa kuniambia kuwa hana msaada wowote kwangu na hivyo nijipange kurudi Daslam na sina nauli.
Natanguliza shukrani.
Wasalaam wapendwa,
Mentor.
No comments:
Post a Comment