Lakini mama...
09/23/2017..saa tano usiku
Ni saa tano usiku ambapo nimemaliza kufunga milango ya nyumba na kuzima taa moja baada ya nyingine kutokea sebuleni kuelekea chumbani kwangu huku akili yangu ikiwaza kwamba nitaenda kulala peke yangu, tena. Umri umesogea na ni mara kadhaa kwa siku za hivi karibuni nimekuwa nikiwaza kuhusu kutafuta binti ambaye nitatulia naye katika maisha ya ndoa. Tatizo kubwa nililokuwa nalo ni lile ambalo watu wengi wamekuwa wakisema kuhusu vijana wa kiume; kutafuta binti anayefanana na mama yake. Kwangu mimi nadhani, pamoja na kwamba sio kitu ambacho napenda kukikiri, lakini nahisi ninakumbwa na janga hili zaidi. Hata hivyo najipa moyo, huenda nitampata. Naingia kitandani kwangu na baada ya kusali najifunika shuka na kulala.
Ndipo nikaota ndoto…
Ilikuwa siku njema sana, ya nderemo na vifijo. Ni siku niliyofunga ndoa na mke wangu kipenzi. Ghafla harusi ikaisha na tukaelekea fungate. Ilikuwa wiki ya raha maana hatimaye tulikuwa pamoja. Tulijitahidi sana katika uhusiano wetu kabla ya ndoa kutoshiriki kimapenzi. Haikuwa kazi rahisi hasa kwa kuwa sote katika maisha yetu ya nyuma tulishawahi kuonja tunda lile. Lakini dhamira yetu ilikuwa njema na hatimaye wikii hii, hatukuwa na hofu tena. Sikumbuki kama kwenye ndoto yangu nilitoka hata kwenda kuogelea na kutembea nje maana nilikuwa na hamu ya kuwa na mke wangu huyu kila dakika. Ndoto ilikwenda haraka na kujikuta tumeanza maisha. Hapa ndipo nilipogundua ukiishi na mtu ni tofauti na mnavyokutana kila mwisho wa wiki. Ni tofauti kabisa. Nilikuwa nikiona makosa madogo madogo kwake ambayo sikuwa nikiyaona hapo kabla. Ama hakika na nikitaka kuwa mkweli na nafsi yangu, mara nyingi hayakuwa makosa yake.
Hamu ya kuwa na mke wangu ilipotea kadri siku zilivyozidi kwenda katika ndoto yangu. Sikujua kwa nini lakini nilidhani ni majukumu kazini, nilipandishwa cheo, nilikuwa nikisafiri mara kwa mara, akajifungua watoto, nikapata sababu ya kutokutoka naye. Wakati mwingine nilikuwa nikimfanyia visa tu na ikitokea kosa likawa lake basi nitaifanya kesi kuwa kubwa kuliko ilivyostahili. Ghafla ndoto yangu ilihama na kunipeleka nyuma miaka 30 hivi. Niliiona wazi kumbukumbu hii kwenye ndoto yangu kana kwamba ndiyo ilikuwa ikitokea wakati huo. Lakini nami nilikuwa kwenye hiyo ndoto ya pili. Nilikuwa mtoto…
1982
Nilizaliwa mtoto wa pili kwa wazazi wangu. Kwa ujumla mama yangu alijaliwa kujifungua watoto wanne. Mimi na kaka yangu ndio wale tunaosema tulizaliwa enzi za kuanza maisha. Ni kipindi hiki mama anatuhadithia kuwa tulilishwa mchicha mpaka tukaharisha kwa kuwa hali ya maisha haikuwaruhusu kutubadilishia mboga kila iitwapo leo. Alituambia pia tulikuwa tukinywa nusu lita ya maziwa watoto wawili. Lakini katika hali hiyo yote mama na baba na sisi tulikuwa na furaha. Nikiangalia picha zetu za utotoni ni dhahiri utaona furaha zilizokuwa nyusoni mwa wazazi wangu walipopiga picha pamoja. Pamoja na ugumu wa maisha wazazi wetu hawakuruhusu tukatembea uchi au kulala njaa. Baba alikuwa mchapa kazi haswa. Alilima bustani za mboga mboga nje ya nyumba waliyopanga. Mama alikuwa akipika maandazi na vitafunwa kama hivyo na kwenda kuuza shuleni alipokuwa akifundisha.
Mama yangu alikuwa mwalimu wa shule ya msingi. Kwa bahati mbaya, muda alioishi yeye ni ule ambao wazazi hawakuona faida ya kumsomesha mtoto wa kike. Lakini nikiangalia maisha aliyoishi mama yangu na jinsi alivyotufundisha, angepata fursa walizopata kaka zake basi angalikuwa mbali sana japo kielimu. Ila alipomaliza kidato cha nne kipindi hicho, baba yake alisema imetosha akae nyumbani ili kaka zake wakasome. Na alifaulu vizuri tu kumruhusu kuendelea na kidato cha tano. Ni hadi alipokuja kuletwa mjini kufanya kazi alipopata fursa ya kusoma na kwa kuwa alikuwa na matokeo mazuri ya kidato cha nne aliweza kwenda kusoma ualimu na kuwa mwalimu wa hisabati na sayansi.
Baba yangu alikuwa vivyo hivyo. Alikuwa na akili sana na hili limsaidia kuwa mbali kielimu. Alilelewa kijijini ambapo shule haikuwa kipaumbele zaidi ya kukata kuni, kufuga na kutengeneza mbege. Alifanya kazi zote hizi na bado kwa mwanga wa mbalamwezi au kijinga cha moto aliweza kusoma na kufaulu. Wakati anakutana na mama, alikuwa ameajiriwa mkoani Dodoma kama daktari. Walikutana walipoenda kutoa elimu ya afya kwa walimu shule anayofundisha mama. Kwa maelezo yake, alivutiwa na ulimbwende wake na sura yake ya upole (aibu?) tangu alipomtia machoni kwa mara ya kwanza. Hakuweza kusubiri hadi semina iishe na walipopata tu mapumziko ya mchana alimfuata na kuanza kuongea naye. Kwa adabu ya kijijini aliyokuwa nayo mama, hakuwa mwepesi kumzoea. Lakini tangu siku hiyo baba alidhamiria kumpata. Alimtumia zawadi, maua na mara moja moja alitumia gari la mganga wa wilaya kwenda kumsalimia shuleni kwake. Vishawishi hivi hatimaye vilifua dafu na muda si mrefu walifunga ndoa.
Kama alivyoanza kumfuatilia mama, maisha yao ya mwanzo ya ndoa ndivyo yalivyokuwa. Picha ninazoziona nyumbani zinanithibitishia hilo. Ni picha za mama akiwa na maua mkononi na tabasamu kubwa zuri usoni (sijapata kuona bado mwanamke mwenye tabasamu zuri kama la mama). Ni picha za baba na mama wakiwa mbugani walipochukua likizo yao ya kwanza baada ya ndoa. Hawakuwa na fedha nyingi lakini baba alijitahidi akajibana wakaweza kwenda mbugani. Kuna picha ya mama ambayo kila nikiiangalia inanipa tafsiri nyingi sana na tofauti kila ninapoitazama. Ni picha ya baba akichukua shoka kutoka mkononi mwa mama. Picha inaonesha kama mama hakuwa akitaka kumpa shoka lile na baba alikuwa akimlazimisha. Wote walikuwa wakitabasamu. Kwa pembeni wanaonekana bibi na babu yangu wakiwa wanacheka. Bibi alikuwa na mfuko mkononi. Hiki ndcho kinanionesha hii picha ilichukuliwa walipokwenda kwa wazazi wa baba yangu. Baba alituambia alikuwa ametoka mjini na alipofika na kupokelewa na bibi alimuona mama akipasua kuni. Aliwatania wazazi wake kuwa yani mkewe kaja juzi tu na leo wameshampa shoka. Kwa ambao umri hauwaruhusu kuelewa hili, mkasome lile shairi la siku kumi za mgeni ndipo mtaelewa kwa nini baba yangu alitoa utani huo.
Zaidi sana, wakati huo mama ndio alikuwa na ujauzito wa kaka yangu. Naangalia picha za kaka yangu, namuangalia baba, ndipo ninagundua aidha alikuwa na suruali tatu tu alizozipenda ama hizo ndizo suruali pekee alizokuwa nazo. Ninasahau kumuangalia mama. Labda kwa kuwa alikuwa amejitanda khanga katika baadhi ya picha. Lakini hata kama alikuwa na nguo moja, huwezi kujua wala kuona. Picha zote za mama zitakuvutia kuangalia kitu kimoja tu kwake; tabasamu. Ukimuangalia tabasamu lake hutoweza kujua kuwa tulikuwa tukishindia mchicha kila siku. Ndiyo, si kwamba baba na mama hawakuweza kubadilisha mboga lakini kwa wakati ule, ukienda shule ujue una ukoo mzima wa kuwasaidia. Na hili jukumu wazazi wangu hawakulikwepa. Hivyo, pamoja na kuwa na familia changa lakini bado wazazi na ndugu zako wengine wanakuangalieni. Na katika ugumu wote huu mama hakuacha kutabasamu.
1992
Baba alirudi kutoka shule. Alienda kusoma kozi ya kujiendeleza katika taaluma yake ya utabibu lakini pia alifanikiwa kusoma uongozi katika sekta ya afya. Baada ya kurudi alipandishwa cheo kazini na fedha zilianza kuonekana. Wakati huu familia yetu ilikuwa imekamilika. Tulikuwa watoto wanne tayari. Baba alikuwa na gari la kazini sasa. Ilikuwa raha kusema baba yetu alikuwa daktari. Zaidi ya hapo hatukuwa na faida kubwa sana ya kuwa naye. Maisha yetu na mama yalionekana kuwa vile vile kabla baba hajarudi au kupandishwa cheo.
Kutokana na kupandishwa cheo na majukumu, baba hakuwa akirudi nyumbani mapema tena. Kuna nyakati alikuwa bado akihitajika kutibu na nyakati nyingine alikuwa katika wadhifa wake wa uongozi. Mara nyingi tulikuwa tukila chakula cha jioni peke yetu na mama. Tabasamu la mama lilitufanya baada ya muda tuzoee na kusahau kumuulizia baba alipo. Tabasamu la mama lilitufanya hata tusikinai kupikiwa chakula kile kile kila siku. Ilikuwa raha kuwa na mama mezani jioni, kama hakufurahia sisi hatukujua, maana alitabasamu kila wakati.
Baba yangu hakuwa mgomvi wa kupigana kata kidogo. Ila nakumbuka kusikia mama akilalamika kila siku baba anaporudi usiku sisi tukiwa tumelala. Hakuwa akisema mengi zaidi ya ‘nimechoka! Nilikuwa kazini! Nilikuwa kwenye vikao!’ Kisha alielekea chumbani kulala. Nakumbuka hata siku niliyotoka chumbani kwenda kukojoa na kuwakuta mama na baba wakizozana, bado niliona mama alikuwa akitabasamu. Au nilikuwa na usingizi? Hapana, nakumbuka asubuhi nilipomuuliza kama walikuwa wakigombana usiku uliopita mama aliniangalia, kwa tabasamu, na kuniambia hapana.
Kadri baba alivyopanda cheo kazini ndivyo alivyozidisha umbali na familia yake. Wakati huu wote sisi watoto hatukujua lolote na bahati mbaya au nzuri kwetu tulikuwa tumeondoka nyumbani na tupo shuleni. Sote tulisoma shule za bweni. Tulirudi nyumbani nyakati za likizo na kukutana na tabasamu la mama yetu na giza la kutomuona baba. Tulijua bora zaidi ya kuuliza maana tabasamu la mama lilitufumba macho kujua yaliyokuwa yakiendelea. Naamini kipindi hicho tungeambiwa tumuelezee baba yetu, sote tungempa picha ya malaika ambaye anajitoa kwa taifa lake kama daktari na kiongozi na bado alihakikisha wanae tunaenda shule, tunavaa, tunakula na kulala. Ama hakika hatukujua kuwa zaidi ya kulipa ada ambayo nadhani alifanya kwa ajili ya kujiwekea heshima tu mtaani, hakuna cha zaidi alichofanya kwa fedha yake. Mama kwa mshahara ule wa mwalimu wa shule ya msingi alihakikisha tunakula na kuvaa, na hata pale ambapo tulijihisi kupungukiwa tukijilangisha na watoto wengine, tabasamu lake lilitufunika.
Baba aliacha kumtoa mama outing. Hata akipata tafrija ya kikazi ama kijamii atatafuta sababu tu aende peke yake. Mara nyingi alikuwa akisema ni tafrija ya kikazi na wake hawakualikwa. Mama hakuona shida kubaki nyumbani na kama aliona, basi tabasamu lake lilifunika hilo. Tulibaki wote tukila wali na marahage kwa siku ya tano mfululizo.
1999
Nilikuwa nimemaliza kidato cha sita na nilikuwa nikijiandaa kwenda chuo kikuu. Wakati huu wadogo zangu wote walikuwa shuleni na kaka yangu alikuwa akimalizia mwaka wake wa pili wa chuo. Nilibaki peke yangu nyumbani na mama. Umri ulikuwa umesogea na kwa kiasi tabasamu la mama halikutosha kunikinga kutokuona tabia ya baba. Mara nyingi alipokuwa akirudi nyumbani alikuwa amelewa na hakuwa akimjibu mama vyema. Nashukuru tu hakuwahi kumpiga mama na hata kama alimpiga sikujua na hata nilipomuuliza mama mwezi mmoja baada ya kugundua hilo hakuniambia, alitabasamu na kuniambia nisijali.
Bado baba alikuwa akitoka usiku mwenyewe, tulikula chakula cha jioni na mama peke yetu na aliporudi usiku nilimsikia baba akijitetea kuwa amechoka, alikuwa na kikao, mke wake hakualikwa, amechoka sana, amuache akalale tu. Nilikuwa nikichelewa kwenda kulala mara nyingi ili kusikia sababu za baba. Hakupaza sauti lakini kila siku alikuja na kisingizio kipya. Alianza kuuza baadhi ya mali alizonazo pia kwa ajili ya maisha yake aliyokuwa nayo huko nje. Kama si kuwa na gari la ofisini basi angeadhirika maana alifikia mahali aliuza hadi gari lake binafsi na hata nilipomuuliza mama kwa tabasamu aliniambia hajui limeenda wapi, lakini nisijali, yeye hana shida, ni gari la baba.
Niliondoka na kwenda chuo. Ndugu zangu wengine hawakujua yaliyokuwa yakiendelea au kama walijua basi hakuna aliyesema neno kwa mwenzake.
2002
Nilipomaliza chuo nilirudi nyumbani kidogo huku nikitafuta kazi ya kufanya. Kwa muda mfupi niliokuwa nyumbani nilikuwa nikifanya kazi za kujitolea na kuungaunga kwenye ofisi moja iliyokuwa karibu na nyumbani. Ilinibidi nifanye hivyo maana sikuwa na mahali pa kuishi kama ningeamua kubaki Dar es salaam. Nyumbani ningeweza kuishi bure na kupata uzoefu wa kazi wakati nikitafuta kazi itakayonilipa.
Jumatatu moja asubuhi mama alikuja chumbani kwangu huku akihema kwa nguvu. Ni wakati huu tu ndipo sikuliona tabasamu lake. Alikuwa ameshika kichupa cheupe. Aliniambia nimsomee vyema maandishi yaliyokuwa yameandikwa kwenye kichupa kile maana yeye alihisi haelewi vyema. Nakumbuka vyema maandishi yaliyokuwa kwenye kichupa kile. Nilianza kusoma Norvir, RITONAVIR huku nikiwa sielewi kwa nini hasa mama ameniletea kichupa kile nikisome. Mwanzo nilihisi ni jambo linalohusiana na mimi lakini sifahamu lolote kuhusu hiki kichupa. Kama mtoto, sikuwaza chochote zaidi ya kujiuliza ni nini uhusiano wangu na kichupa hiki, na kama utakuwepo, ni vipi nitaweza kujitetea? Ni hadi niliposoma kikaratasi cha ndani ndipo nilipoelewa kuwa vile vilikuwa vidonge vya kupunguza makali ya ukimwi (ARV). Nilimwangalia mama bila kuelewa hasa maana yake. Nilijua si mimi. Kwa mshtuko wake, nilijua pia si yeye. Sijui kwa nini ila mawazo yangu yalihamia kwa mdugu zangu. Mama aliondoka chumbani kwangu bila kunipa jibu la maswali yangu, hakuwa akitabasamu na kabla sijakusanya nguvu kuamka nilimsikia akifunga mlango na kuondoka.
Ni hadi aliporudi huku akitabasamu upya ndipo nilipojua ukweli. Alikuwa akifanya usafi chumbani kwao na kwa hiyo siku aligusa sehemu ambayo hakuwahi kugusa kwa muda mrefu. Ndipo alipokutana na kichupa hicho. Na alifahamu kabisa kuwa baba ndiye aliyekuwa akitumia dawa hizo hivyo alichofanya kwanza ni kwenda kupima kama ameathirika ama la. Kwa bahati nzuri alikutwa ni mzima. Alirudi nyumbani akitabasamu na kuniambia nisimueleze mtu yeyote. Alinifanya hadi nikaapa kutokumueleza mtu yeyote.
Hata baada ya baba kurudi, mama aliendelea kutabasamu na sijui ni wakati gani alimweleza kuwa anajua yote maana masikio yangu yalikuwa wazi wakati wote kusikiliza ugomvi utakaotokea. Siku, wiki, miezi, na miaka ilipita na mama alibaki nyumbani, na baba. Baba alizidisha tabia ya kulewa na kuuza vitu hadi kufikia wakati ilibidi kuficha baadhi ya hati ili asije kuuza kila kitu kuendeleza tabia yake. Baada ya baba kustaafu ilimbidi afanye hayo ili kuweza kuishi na ilimbidi astaafu kwa lazima kabla ya umri wa lazima wa kustaafu maana wakubwa wake walimuonea huruma kumfukuza. Hivyo alipofikisha miaka 55 alistaafu. Kuishi kwa pensheni na maisha aliyokuwa ameyazoea haikuwa rahisi.
Lakini la zaidi tulilokuja kulifahamu mwaka 2012 alipofariki baba ni kuwa tulizaliwa watoto wanne lakini wakati anazikwa tulikuwa watoto nane jumla. Hata watoto wote hawa walipojitokeza, mama hakukasirika. Alitabasamu na kuwakumbatia wote. Hakuwa na mali ya kuwagawia lakini alikuwa na tabasamu la kuwapa. Kile kidogo alichoweza kuficha baba asiuze hicho tuligawana wote. Hata wakati wadogo zangu wakilia kuwa hawakufahamu baba yetu alikuwa mume wa namna gani, mama aliwafuta machozi na kutabasamu huku akiwaambia aliwapenda na aliwalipia ada eti. Miaka 30+ ya ndoa, mama alitabasamu hata alipokosa vyote alivyostahili kwa baba na alibaki akitutunza sisi na kutufunika kwa tabasamu. Tabasamu la mama lilitufunika tusiyaone maovu ya baba. Kwetu na labda kwa kuwa hatukuwa tukimuona sana na tulipomuona hakuacha kutuambia alikuwa bize na kazi, tusome tuje kumsaidia kazi.
Siandiki kumshangaa au kumsimanga mama. Kwamba kwanini alivumilia yote hayo. Sijui na sasa siwezi kumuuliza tena. Siandiki kusema alikosea kwa kubaki katika ndoa ambayo haikuwa ndoa. Kwa kuvumilia kutofanyiwa aliyokuwa akifanyiwa kabla pesa na vyeo havijamkuta baba. Siandiki kusema pia alichokifanya mama kilikuwa sahihi. Hasa kwa kuwa baadaye nilikuja kujua aliyafahamu yote hata ya baba kuwa na watoto wa nje ya ndoa lakini alibaki kimya.
Siandiki kumsema vibaya baba. Kwetu sisi alikuwa baba mwema maana hakuwahi kututendea vibaya sisi. Tena kwetu sisi labda kwa kuwa tulifunikwa na tabasamu la mama, tuliona shule nzuri tuliyosoma na maisha tuliyoishi na ile raha ya kusema ‘baba yangu ni daktari’ vilitufanya tumuone baba tofauti na mama alivyomuona.
Bali nimetafakari nikagundua katika yote haya, mama hakuacha kutabasamu. Hata leo kwenye ndoto yangu, tabasamu lake lilikuwa dhahiri kuliko ndoto hadi nikahisi yupo nami chumbani. Nimeshtuka usingizini na kugundua nipo peke yangu na kwamba muda wote huu nilikuwa ninaota. Labda mama alikuwa akizungumza na mimi na kunionya kutokuja kuwa kama baba yangu.
Sijui, sitojua majibu ya kwa nini mama yangu hakuondoka katika yote hayo. Ninachojua ni, hata kwenye ndoto yangu, mama hakuacha kutabasamu!
Wasalaam wapendwa,
Mentor!
I don't have the kiswahili vocabulary to reply in it. Dude!!! Your mum is strong! Heed her warning though. The apple does not fall far from the tree oftentimes but through prayer and active participation, we overcome the odds.
ReplyDeleteYthera, nashukuru! Kama hata wewe umeelewa hadithi fupi hii basi nimefurahi sana. Kuhusu somo, mimi nimejifunza yangu..natumai nawe umepata la kujifunza kwako!
DeleteJina langu ni Lilian N.Hii ni siku ya furaha sana ya maisha yangu kwa sababu ya msaada wa Dragaguru amenipatia kwa kunisaidia kupata mume wangu wa zamani na uchawi na kupenda. Nilikuwa nimeolewa kwa miaka 6 na ilikuwa ni ya kutisha sana kwa sababu mume wangu alikuwa anajaribu kudanganya juu yangu na alikuwa akitafuta talaka lakini nilipoona barua pepe ya Dr.saguru kwenye mtandao juu ya jinsi amewasaidia watu wengi kupata zamani yao na kusaidia kurekebisha uhusiano. na kuwafanya watu wawe na furaha katika uhusiano wao. Nilielezea hali yangu kwake na kisha nikitafuta msaada wake lakini kwa kushangaza kwangu zaidi, aliniambia kwamba ataniunga na kesi yangu na hapa nimeadhimisha kwa sababu Mume wangu amebadilika kabisa kwa mema. Daima anataka kuwa na mimi na hawezi kufanya chochote bila ya sasa. Ninafurahia sana ndoa yangu, ni sherehe kubwa. Nitaendelea kutoa ushuhuda kwenye mtandao kwa sababu Dragaguru ni kweli harufu halisi ya spell. Je, unahitaji kupasa kuwasiliana na mkurugenzi SAGURU sasa VIA EMAIL: drsagurusolutions@gmail.com au +2349037545183 Yeye ndiye jibu pekee kwa tatizo lako na kukufanya uwe na furaha katika uhusiano wako.
Delete1 wapenzi SPELL
2 WIN EX BACK
3 FRUIT YA WOMB
4 PROMOTION SPELL
5 SPOTE YA KUJIBU
6 BUSINESS SPELL
7 JODA YA KIENDA
8 LOTTERY SPELL na COURT CASE SPELL.