Nilipata fursa ya
kwenda nyumbani kwa ajili ya sikukuu ya pasaka. Haikuwa rahisi kupata ruhusa
hii ukizingatia uongozi wa sasa wa hapa kazi tu. Ila, bosi wangu hakuwa na budi
kuniruhusu maana nilimtoa kwenye shimo kubwa wiki moja kabla ya pasaka.
Jumatatu ya tarehe 21/03 nikamuambia anipe ruhusa niende nyumbani kwa ajili ya
pasaka; niondoke Jumatano na kurudi Jumanne, na isikatwe kwenye likizo yangu ya
mwaka huu. Kwa sababu za kiusalama sitotaja sehemu ninayofanyia kazi…maana sisi
ni masikini, masikini sana!
Niliukuta msalaba
nyumbani. Msalaba uliotundikwa ukutani, wenye urefu wa sentimeta 45 kwa ile
mbao ya kushuka na sentimeta 30 ile mbao ya kulala. Ulichongwa vizuri ila haukuwa
umepigwa nakshi yeyote. Lakini ulikuwa umetundikwa sebuleni. Kama usingekuwa ni
msalaba, basi usingefaa kuwa sebuleni, maana hauna urembo wowote. Lakini kwa
kuwa ulikuwa ni msalaba, basi sikuwa na cha kusema.
Hata hivyo, mama
yangu alinikuta nikiushangaa msalaba ule. Akaniuliza, “Unashangaa nini baba yangu (kwa mila za kichaga, mtoto wa pili wa
kiume anachukua jina la baba wa mama yake),” Nikamuuliza, “Mama, kwa nini huu msalaba msiupige rangi walau upendeze. Hamuoni
unaondoa urembo wa sebule?”
“Mwanangu,” alianza kusema mama, “Huo msalaba unanikumbusha mbali sana”
1977,
Dodoma
Nilikuwa nimemaliza
chuo na kupangiwa kwenda kufanya kazi Dodoma chini ya RTC (Regional Trading Company).
Nilikuwa binti mdogo bado, yaani sijaolewa, hivyo nyumba niliyopewa tulikuwa
tukiishi na mwenzangu, Asteria. Alikuwa ni binti aliyeokoka sana, yani ni wale
tunawaita kwa kimombo ‘smoking hot Christians’. Ndiye aliyenifundisha kuomba
kwa ajili ya mume unayemtaka. Na ndiye aliyenifanya nikapenda kwenda kanisani.
Simaanishi nilikuwa binti mbaya, ila nilikuwa makini na Mungu wangu zaidi baada
ya kukutana na Asteria.
Tulikuwa tukienda
kanisa la Kilutheri huko.
Mwaka 1978 mwanzoni
alikuja Mchungaji mwanafunzi kutoka chuo cha uchungai Makumira. Alikuwa kijana
wa umri wetu na nakumbuka tulizoeana naye haraka kwa kuwa Asteria ndiye aliyempeleka
kununua vifaa vichache kwa ajili ya nyumbani kwake. Alikuwa pia akimsaidia
kununua mahitaji ya jikoni kila aendapo sokoni. Asteria alijitoa sana kwa
kanisa na kumfanya mchungaji ajisikie kuwa yuko nyumbani.
Hivyo, tukawa
tumezoeana naye na mara nyingi alikuwa akija kwetu kwa ajili ya sala ya jioni
kwani nyumba yake ilikuwa upande wa pili wa barabara kutoka kwetu. Baada ya
miezi michache alituambia kuwa mkewe angekuja kumtembelea na kwamba angekaa
nayeye kwa miezi sita iliyobaki kabla yayeye kurudi chuoni Makumira kumalizia
mafunzo yake.
Alitueleza kuwa mwezi
mmoja kabla ya kuja Dodoma alikuwa ametoka kuoa. Tulimsaidia kufurahi na zaidi
hasa kwa kuwa mke wake angekuja tumwone maana alikuwa ni kijana mpole mno.
Akiongea kama humfahamu vyema unaweza kuhisi analalamika.
Hata siku mama
mchungaji anawasili Dodoma mjini, sisi ndio tuliompokea. Tulijitahidi kumfanya
ajisikie yuko nyumbani kwani mara nyingi tukitoka kazini tulikuwa tukienda
kwake kupiga naye soga. Ila hatukuweza kumzoea sana maana tulijua ni mama
mchungaji, si vizuri kumuuliza mambo mengi.
Jumapili
iliyofuata, ilitangazwa kwenye matangazo ya kanisa kuwa tutatambulishwa mama
mchungaji. Kila mtu alikuwa na hamu ya kumuona huyu mama mchungaji mwanafunzi.
Nakumbuka vyema alikuwa amekaa siti ya nyuma kabisa. Baada ya mahubiri
mchungaji alisimama mbele ili amwite mkewe washarika wamsalimie lakini
hakuonekana, alikuwa ametoka kanisani. Tuliporudi nyumbani
hatukuweza kumuuliza alienda wapi maana nimama mchungaji.
Wakati huo huo,
Asteria rafiki yangu alikuja nyumbaji jioni moja, akaniambia, “Mama Mentor (alitumia jina langu la kwanza),
leo nimekutana na jaribu.” Nikamdodosa aniambie ni nini kimemtokea.
Ndipo
akanieleza alikutana na mtu wakati akitoka kazini. Mkaka mrefu, mzuri,
mwanajeshi. Alimsimamisha na kumuambia kuwa amemuona mara kadhaa eneo lile na
angependa kumfahamu.
“Umeokoka?”
ndiyo swali la kwanza nililomuuliza huku moyoni nikitamani anijibu ‘ndiyo’.
“Nilikuwa nimeshaanza kujiona mke wa askari
mwenzangu,” aliendelea kuelezea. “Alinijibu
hapana ila yeye ni Mkristo. Moyo uliniuma lakini nilijikaza nikamwambia, ‘ukitaka
kunifahamu njoo kanisani’.”
Basi tukaachana naye ndipo nikaja nyumbani. “Hivi mama Mentor, kwa nini hawa vijana
wazuri hivi hawajampokea Yesu? Nitamuombea aokoke”
Nilijaribu kumuonya
kuwa makini na hisia zake lakini aliniambia atahakikisha anamuombea mpaka
aokoke.
Jumapili
iliyofuata, baada ya ibada kwisha na kama kawaida Mama mchungaji kututoroka
nilishangaa navutwa mkono. Kuhamaki ni Asteria ananipeleka upande ambao wanaume
huwa wanasimama. “Huyu anaitwa kaka
Masatu, ndiyo yule askari niliyekuambia nilikutana naye, amekuja kanisani!”
Nilishindwa kujua niseme nini nikaishia tu kumuambia, “Bwana Yesu asifiwe kaka” naye akaitikia kisha nikarudi kuendelea na
mambo yangu.
Niliwaacha pale
nikarudi nyumbani na Asteria aliporudi akaniomba nimruhusu Masatu aje
kututembelea kwa chakula cha mchana siku moja.
Tulikuwa tumekubaliana kuwa
hakuna wanaume kuja nyumbani kwetu na kwamba akija ni lazima sote tuwepo, hivyo
ombi lile ni ili nisipange ratiba yeyote siku hiyo waliyokuwa wamekubaliana
niwepo. Nilikubali ingawa niliona kama ni haraka sana.
Siku, wiki
zikasogea na hatimaye kuwa miezi mitano na kaka Masatu akampokea Yesu, akaokoa.
Alimtamkia Asteria kuwa anampenda na kwamba angependa kumuoa. Asteria kwa hamu
ya kuweka ushuhuda wa kuolewa na kijana aliyemsaidia kuokoa akamkubalia ila Masatu
alimwambia wafanye harusi ndogo tu na kwamba watafanya harusi kubwa siku
akienda kwao Mwanza. Kipindi kile alikuwa Makutopora kwa kozi maalum na mafunzo
ya utayari.
Jumatatu moja
jioni, alikuja nyumbani kwetu mchungaji mwanafunzi akiwa analia machozi. Ni
vigumu kuelezea kwa maneno ila alikuwa akilia kama mtoto. Tulijitahidi
kumbembeleza lakini ilikuwa kazi bure. Mwishowe tuliamua kusubiri anyamaze atuelezee
ni nini kilimsibu. Alikuwa anatia huruma sana!
Baada ya kunyamaza
alianza kutusimulia kuwa, usiku wa kuamkia siku hiyo, mkewe aliumwa sana tumbo.
Alimshauri waende hospitali – maana ilikuwa karibu tu na tunapoishi – lakini
mkewe alikataa. Hivyo aliamua kutulia mpaka asubuhi ili ampeleke hospitali ila
hawakuweza kulala kabisa.
Asubuhi na mapema
aliamka na kumwambia mkewe waende hospitali ila alikataa bado. Hivyo kwa uoga
aliamua kutoka na kwenda kumuita mama wa makamo wa jirani amsaidie baada ya kumuelezea mkasa mzima. Mama yule
akamuambia ampeleka hospitali bila hata ya kutoka ndani kwenda naye kwake.
Alimwambia, “usisahau kwenda na kadi ya
kliniki, si mlikuwa mnaenda? Usisahau kumchukulia na khanga na nguo chache”
Mchungaji alibaki anashangaa asijue cha kujibu kwani ni miezi mitano tu iliyopita
ndiyo mkewe alimwambia kuwa haoni siku zake hivyo alijua mama yule hataki tu
kumsaidia na kwamba mkewe hajafikia muda wa kujifungua.
Alirudi nyumbani
kwake bila msaada ila alipoingia ndani hakumkuta mkewe.
Akamfuata tena yule
mama kumueleza kuwa hajamkuta mkewe ndani. Yule mama akamwambia aende hospitali,
atangulie yeye anakuja nyuma.
Mchungaji akatoka
mbio kwenda hospitali akaanza kuzunguka kwenye wodi tofauti tofauti akimtafuta
mkewe bila mafanikio. Ni hadi anatoka wodi ya mwisho ndipo alipokutana na yule
mama wa makamo wa jirani aliyemwambia atangulie hospitali. Yule mama alishangaa
kumuona mchungaji anatoka wodi za wagonjwa wa kawaida ndipo akamshika mkono na
kumpeleka wodi ya wazazi. Kabla hata mshangao wake haujaisha, alipokelewa na manesi
wa pale wakimwambia, “hongera mchungaji,
umepata dume.” Akazimia!
Alipoamka bado
wakaendelea kumpa hongera kwani walihisi alizimia kwa furaha ya kupata mtoto.
Kumbe yeye anatafakari mtoto kapatikanaje. Akawauliza kama mtoto amezaliwa
akiwa katimiza muda wote – yaani miezi tisa - jibu ambalo lilimchosha zaidi. Akaingia
wodini akamkuta mkewe na mtoto anamnyonyesha.
Hapo ndipo ukweli ulipomuingia na ndipo alipoanza kulia na
kwamba ameshindwa kuelewa ilikuwaje.
Sisi nasi ndipo
tukaanza kufunguka macho kukumbuka yale maongezi aliyokuwa akitueleza yule mama
mchungaji, “Nyie ombeni tu Mungu lakini
ujue wakati mwingine unaweza kuolewa na mtu tofauti kabisa na unayempenda. Mimi
kuna mkaka nilikuwa nampenda jamani…” Na kwa ushamba wetu hatukujua kuwa
yule dada alikuwa na ujauzito. Kumbe wakati anakuja Dodoma alikuwa ana uja
uzito wa miezi takribani minne tayari.
Muda ule ule wazee wa
usharika wakaja na kuanza kuongea na mchungaji mwanafunzi huku wakimuuliza
maswali. Mchungaji yule alizidi kulia na kushindwa kuongea nao. Siku iliyofuata
mama mchungaji akaruhusiwa kurudi nyumbani baada yaa mtoto kupewa chanjo za
kwanza na mchungaji alienda kumchukua mke wake wakarudi nyumbani. Jumapili
iliyofuata mchungaji alitangazwa kuwa ametengwa na kanisa kwa kitendo
alichokifanya.
Ni hadi baadaye ndipo
alipokiri kuwa kabla ya ndoa hakuwahi kumfahamu mkewe kimapenzi. Hivyo wiki
iliyofuata tena mchungaji alirudishwa kanisani ila mkewe akatengwa. Wazee wa
kanisa na mwinjilisti waliwa na parish worker wakaanza kufurika wakipokezana kila
siku kwenda kwake kumpa neno kuwa amsamehe mkewe na kwamba hayo ndiyo majaribu
yatupatayo Wakristo na kwamba inatupasa kuyashinda.
Alirudi tena kwetu
akilia akatueleza hasa kilichokuwa kikimliza maana alikuwa akilia karibu kila
siku hasa akikutana na sisi.
Wakati anafika pale Dodoma, kazi yake ya kwanza
aliyopewa ilikuwa kwenda kuwapatanisha wanandoa watu wazima sana kwake ambao
mke wa bwana huyo aligundulika kuwa mtoto wake wa pili kati ya watatu aliozaa
na huyo bwana, sio wa mume wake wa ndoa. Mume alishindwa kumsamehe na hivyo
alitaka waachane. Mchungaji alimsihi sana yule mzee amsamehe mkewe maana wao ni
Wakristo na kwamba tumefundishwa kusamehe saba mara sabini. Alitusimulia
alivyomhubiria yule bwana kuwa amri pekee tuliyoachiwa na Bwana Yesu ni upendo,
na kwamba ni jinsi gani utakuwa umeonesha upendo wa dhati kama kumsamehe na
kumpokea tena mkewe.
Alimhubiria jinsi
gani Mungu alitufananisha sisi na mwanamke malaya, aliyetolewa kwenye madanguro
na kuolewa kisha akamtoroka mumewe usiku na kwenda kwenye umalaya wake. Lakini bado
mume – Mungu – alirudi na kumtafuta mkewe, kumfuata na kumrudisha nyumbani huku
akiwa amemsamehe. Alimueleza hata kwenye habari hiyo Mungu alisema tumezaa
watoto katika uasherati wetu lakini bado anatuita na anatupenda. Je, si zaidi
sisi tunawiwa kusamehe tunapokosewa na wapendwa wetu?
Aliumia maana aliona
ilivyo ngumu kusamehe katika hali ile na kwamba yeye alikuwa akimlazimisha mzee
yule kumsamehe mkewe.
Baada ya wiki mbili
tangu tukio lile, mchungaji alikuja kutuaga kuwa anarudi Makumira kuendelea na
mafunzo yake.
Alikuja na msalaba mmoja akatuachia akasema, “Dada zangu, huyu Mungu mnayemtegema
msimuache.”
Asteria alisikitika
sana mchungaji kuondoka maana angekosa harusi yake na Masatu lakini hakuwa na
budi kurudi chuoni. Asteria aliolewa mwezi uleule mchungaji alioondoka na baada
ya ndoa alihamia kwenye nyumba kambini alimokuwa akiishi Masatu, mumewe mpya.
Mwaka huo huo,
1978, ndipo kulipotokea vita vya Kagera wakati Idd Amin alipotuvamia. Masatu na
wenzake iliwabidi wajikusanye kuelekea vitani.
Hapo ilibidi
Asteria afungashe naye vitu vyake aende kijijini kwa Masatu mpaka vita
vitakapoisha ndipo arejee na yeye Dodoma. Hivyo ndivyo alivyoambiwa na Masatu,
mumewe. Hapo Asteria alikuwa na ujauzito tayari.
1979
Dodoma
Nilishtuka
nilipoufungua mlango wangu asubuhi ya saa kumi na mbili baada ya kusikia mtu
akigonga maana sikuwa nategemea kupata mgeni yeyote siku ile, hasa asubuhi yote
ile. Nilishtuka zaidi nilipokutana na sura ya mdada aliyekondeana na tumbo limejaa
kama vile ana utapiamlo; alikuwa Asteria! Nililia machozi tukakumbatiana
tukalia pamoja. Nakumbuka palepale kwenye ngazi za kuingia kwangu tulikaa
akanihadithia kilichotokea.
Kumbe, Masatu
alikuwa ameoa huko kijijini kwao hivyo alipofika alimkuta mke mkubwa na watoto
wawili tayari. Mke mkubwa hakufurahishwa kabisa na ujio wake hivyo alimtesa
sana. Ni hadi alipoweza kwenda kanisani na kukutana na mchungaji ambaye aliwahi
kuja kuhudumu pale kanisani Dodoma akamhadithia mkasa wote. Mchungaji yule
akajikusanya akampa nauli akatoroka na treni usiku ule ambapo ilimbidi kulala
stesheni kwani treni ilipita pale usiku sana. Alisafiri bila kula chochote
kwani pesa aliyopewa ilitisha tu kwa nauli na ndiyo amefika asubuhi ile baada
ya safari ya siku mbili.
Nilimkaribisha
ndani na kumuandalia uji mwepesi maana hata maji niliyompa aliyatapika. Wakati
huo ujauzito wake ulikuwa umefikisha miezi nane. Alikuwa amekonda sana na mwili
haukuwa na nguvu. Nadhani hiyo ndiyo iliyopelekea yeye kujifungua kabla ya
tarehe iliyotarajiwa ya kujifungua kwake. Kwa bahati mbaya Asteria alifariki
wakati akijifungua mtoto wake na mtoto wake pia alifariki.
“Sasa mama huo msalaba?” Niliuliza, maana
niliona mama ameshanipoteza kwenye mtiririko.
Ooh! Alirudi nao
Asteria hivyo nilibaki nao baada ya yeye kufariki. Huu msalaba ulinitesa sana
maana sikutaka kuolewa kwa muda mrefu sana. Na nikasema siufanyii chochote,
ndiyo maana unaona uko hivyo hivyo kama tulivyopewa na yule mchungaji
mwanafunzi!
Wasalaam wapendwa,
Mentor.
No comments:
Post a Comment