Tuesday, May 31, 2016

Angela Mke Wangu...Yote Ulitaka Wewe

Disclaimer: Shairi hili limeandikwa kwa ushirikiano wa members kutoka blog ya Jamiiforums. Sehemu zilizoandikwa "Mentor" ni utunzi wangu.


Angela Mke Wangu, yote ulitaka wewe


Angela: "Bazazi wewe! Mwanaume Malaya, sijui unawafundisha nini watoto wako! Lione kwanza, lianaume sijui ulipe nini liridhike, najuuuutaaaa..."

Mentor:


Mke wangu mke wangu, kwanza punguza hasira
Nifungue moyo wangu, niieleze hadhira
Ulonitenda mwenzangu, kula vyako nikazira
Angela mke wangu, yote ulitaka wewe!

Tulikutana Majengo, ukiishi kwa mamayo
Mzuri huna mapengo, linikonga wangu moyo
Kakutoa tongotongo, la mapenzi bila choyo
Angela mke wangu, yote ulitaka wewe!

Mzuri kweli likuwa, umbo lako namba nane
Unang'aa kama hua, wanukia manemane
Piga simu nasifiwa, nikajiona senene
Angela mke wangu, yote ulitaka wewe!

Likuomba kakubali, uwe wangu wa maisha
sikutaka kwenda mbali, n'kawaacha kina Asha
pilau, ndizi na wali, likuwepo vya kutosha
Angela mke wangu, yote ulitaka wewe!

Ilikuwa tarehe 07/08/2009, Jumamosi yenye furaha tele. Nilikuvisha pete na mbele ya jamii nikasema 'Ndiyo'. Nawe kwa tabasamu la huba ukanitazama machoni, huku ukinivisha pete na ';Ndiyo' ukaniambia. Walipiga vigelegele vya furaha wote waliokuwepo. Ukanizalia mwana, Eddy, jina lake. Nikfurahi moyoni penzi nikaliongeza. Ndipo ukaanza badilika...

Ukaanza lalamika, bila sababu husika
Mwisho si hatujafika, vipi we wataka shuka
Asubuhi hijafika, naona wakunja shuka
Angela mke wangu, yote ulitaka wewe!

Tulimuajiri binti, kazi kutusaidia
wewe kakalia kiti, mwili kujitutumua
kazi afanye Mwasiti, vya ndani ukijilia
Angela mke wangu, yote ulitaka wewe!

Chumbani akaingia, kutandika na kudeki
Kiuno kaninamia, kaumbika kudadeki
Wewe nikikwangalia, -umbo- kama umepigwa jeki
Angela mke wangu, yote ulitaka wewe!

Kama hilo halitoshi, ukaanza lalamika
Kwa nini naenda Moshi, eti namfata Manka
Liniona kuni moshi, kila jiko mi napika
Angela mke wangu, yote ulitaka wewe!

Nikiongea kwa simu, kelele wazianzisha
hawara wako Saumu, jana alikuwa Sasha
Kila siku walaumu, kwa kweli unanichosha
Angela mke wangu, yote ulitaka wewe!


Angela ( lara 1):

Waungwana mwenzenu nipeni pole, Mwenzeu sipendwi kama upele
Wenzngu wamepata waume wapole, Mie nabakia napiga kelele
Mwanaume niajua ni mwenda pole, kumbe ndo mla nyama mwenda pole
Taraji langu la ndoa, limepotea kizani

Mwanaume mvuvi halisi, Wala huvui vingisi
Si kazi Huotea mifulusi, Majabi huya jalisi
Haogopi kaskazi wala kusi, Kutwa kuntia mie nuksi
Taraji langu la ndoa, limepota kizani

Niliamua niolewe na anenifaa, Mume mwenye kusfiwa
Niolewe mie ndoani nipate kuzaa, Kama vile nilivozaliwa
Mengi niliahidiwa mume kunituzaa, Zote ahadi hewa
Taraji langu la ndoa, limepota kizani

Nikavishwa johoza kifahari, Nikajua ndoa ni ya kheri
Mama yangu aliona fahari, Bintie kumlete uzeeni kheri
Nikajua nitaiepuka mibuzi shari, Nimtendee mume kila lakheri
Taraji langu la ndoa, limepota kizani

Mume wewe si mume tena, Bali gume gume aliokataza Mtume
Mume wanifoke mbele ya wana, Huna hata mswalie mtume
Kila siku wewe kunitukana, Hjui maana ya mume
Taraji langu la ndoa, limepota kizani

Wenzangu wapigwa na khanga, Mie najikaza nibaki kulea wana
Dharau zako kali kama upanga, Najitahidi hapa kwako kujibana
Nikiondoka nita tanga tanga, Pia nitawatesa wangu wana.
Taraji langu la ndoa, limepota kizani

Hali ngumu kulalama, ilihali washinda bar na kina salma
Watoto kutwa walalama, Mie nawambia wazi upo kwa Salma
Sijui kwanini hukumuoa Salma, Labda tu hamkukutana mapema
Taraji langu la ndoa, limepota kizani

Machahce nimeyasema uwazi ila mengi yako siyaweki wazi
Wadada kuolewa wala si kazi, Mda mwengine ni uduwanzi
Vimada wako ktwa wako zanzi, Mie ndani nakuna nazi
Taraji langu la ndoa, limepota kizani!

Mentor:

Mimi nitaendelea, hata ukinikatisha
Sio niliyekuoa, mwili wako wanitisha
Kitambi kimekolea, hunipi tena motisha
Angela Mke Wangu, yote ulitaka wewe!

Nikirudi mi nyumbani, unageuka redio
Eti umefanya nini, unanichosha mwenzio
-nikaona-
Shida yote hii ya nini, nianze kunywa kileo
Angela Mke Wangu, yote ulitaka wewe!

Pombe zilinikolea, ila nilizikinai
Nikampata Maria, kulalamika hajui
Nyumba nikampangia, kwako wewe situlii
Angela Mke Wangu, yote ulitaka wewe!

Nimewapitia wengi, Ana Amina Salama
Viuno nyigu si chungu, walivyopewa na mama
Kurudi kwako uchungu, paka wache kulalama
Angela Mke Wangu, yote ulitaka wewe!


Angela ( lara 1):


Mentor wangu mume jamani, Mbona unakuwa mbinafisi
Tangu tuoane sisi jamani, Kutwa waidhulumu Yangu nafsi
Ndoto unazo wewe tu jamani, Mkeo ndoto zake hazina nafasi
Vingi nafsini mwangu natamani, Utakalo wewe tu ndo lina nafasi
Mke nae mtu mmfikirie jamni, Ana yake binafsi pia nafsi
Taraji langu la ndoa, limepotea kizani

Kelele ni matokeo ya vingi vitu, Kichwani mwangu yakatiza mengi
Mwanaume hunisikii chochote kitu, Natamani nikurgoe kwa mengi
Kutwa waonekana bar na skitu, Unadhani walimwengu hawabongi
Nakereka ukisema huna kitu, Ilihali Sikutu umemuhonga vingi
Niamie mkeo huna kitu, Wahi nyumbani tujadili yetu mengi
Taraji langu la ndoa, limepotea kizani

Mwali wausakama kwani ulinioa hivi? Haya mtokeo ya wana nilikutuzaa
Mie sikutaa uwe mwanaume hivihivi, Nikaweka yangu maisha rehani kuzaa
Nikupe heshima uitwe baba Vivi, Kukuzalia kumenizulia kizaa zaa
Haya mambo yenu ya hivi , Vimada wenu asilani hawataki kuzaa
kuna kimada aliekuzalia hivi? Niheshimu japo mtoto kuzaa
Taraji langu la ndoa, limepotea kizani

Hadharani cheko kubwa nalitoa, moyoni maumivu makali naugulia
Kuolewa pongezi watu wanatoa, Ndani kwa ndani furaha naililia
Njikaza matatizo ya ndoa kutoyatoa, Uheshimike mimi navumilia
Waitamani yangu ndoa maombi watoa, sina nguvu za ukweli kuwamwagia
Sjui kwanini moyoni bado sijakutoa, naidangaya nafsi wema utaurudia
Taraji langu la ndoa, limepotea kizani

Hivi kwanini nyumbanii unarudi? Naogopa iko siku huko utapotelea
Iko siku mimi sitorudi, Usijitie kunitafuta niliko potelea
Kwanini huishi makusudi? Huoni unajana unakupotea
Uzeeni hutmuona hata Waridi, Ya nini kuonga akiba kukupotea
Mwanaume wewe ni hasidi, Maisha uliotea japo yatakupotea
Taraji langu la ndoa, limepotea kizani

Ingekuwa nikikuacha utaishi kwa furaha, zamani ningesha kutupa
Najua nikikuacha utaishia kuhaha, Na ushababi wako utakutupa
Nilikupenda sanaa kwa raha, Najikaza kwa shida kuto kutupa
Sijui lini utaacha karahaa, Na hizo zako nyingi pupa
Taraji langu la ndoa, limepotea kizani!

Mama wa Jirani ( mwallu):


Angela acha kulia, wajiumiza na familia
Mumeo kajitakia, shimoni kudumbukia
shetani limuachia, moyowe kujitwalia
Mwache atange na njia, machweo takurejea!


Ni mengi umepitia, jiranizo meshuhudia
Si wa kwanza nakwambia, h'tokua wa mwisho pia
Jifunze adabu kumtia, mambo yakimchachia
Mwache atange na njia, machweo takurejea!

Unamkumbuka Judi, bintie mzee Daudi
mumewe litia juhudi, dhulumu nafsi ya Judi
kuchukua hatua libidi, kulinda yake shadidi
Mwache atange na njia, machweo takurejea!

Jifanye kama hujali, hangaishwi zake pilka
Anza kuisaka mali, tunza mwili kwa hakika
fikiri watoto hali, mwanamke chakarika
Mwache atange na njia,machweo takurejea!

Angela ( lara 1 ):

mwallu hakika yote nimekusikia, Na pia ukweli nimeshawishika
Lakini bibie mie nakuapia, Hapa nilipo si pakujishika
Sheitwan mume huyu keshamuingia, Katu siwezi hata salimika
Nafsi yangu nyongo ishatumbukia, Navumilia tu wanangu kuwaweka
Ndoa yangu imegeuka ndoano shosti!

Mpita njia ( concious mind):

Mama itulize nafsi, bure usijewehuka,
kaamua jinafasi, hajui anatabika,
Upunguze wasiwasi, ishi nae kama kaka,
Huu ushauri bure, mapenzi si mashindano.

Waite wakubwa wenu, bayana uwaeleze,
Ndoa si hii ya kwenu, akutenda waeleze,
watamani rudi kwenu, usisite waeleze,
Huu ushauri bure, mapenzi si mashindano.

Bado wampenda sana, tatizo mbele huoni,
Umeshamuonya sana, mabadiliko huoni,
Na utashukuru sana, kibadilika mwandani,
Huu ushauri bure, mapenzi si mashindano


Mentor:

Angela mekusikia, kilio menifikia
Japo kijaniingia, huruma watafutia
Jirani meniitia, wambea wapita njia
Angela Mke Wangu, yote ulitaka wewe!

Hawaujui ukweli, wa yetu ndani nyumbani
Nje w'jifanya asali, ndani kwetu ni vitani
Maneno tu mi silali, lalamikacho sioni
Angela Mke Wangu, yote ulitaka wewe!

Muulize na Aneti, dada wetu wa nyumbani
Hadi kushushia neti, ulimwita kitandani
Kisa upo kwenye 'net', kutwa u mitandaoni
Angela Mke Wangu, yote ulitaka wewe!

Ndoa hii meichoka, nyumba ndogo sitoacha
Unaniona mi kaka, n'kikugusa w'sema "Acha"
Kuvuja kwake pakacha, mchukuzi hatoacha
Angela Mke Wangu, yote ulitaka wewe!

Ukweli nakuambia, hata uite ukoo
Ndiyo nitaitikia, kesho nipo kwa Ufoo
Usipo badilikia, Eddy ndo aniweka kwako
Angela Mke Wangu, yote ulitaka wewe!

Maneno ya majirani, endelea kusikiza
Waeleze mtaani, mbeleni watakuliza
Beti zo watazighani, wanifata kuki-giza
Angela Mke Wangu, yote ulitaka wewe!


Mpita njia ( concious mind):

mapenzi ni ya wawili, kidume umechemka,
usiwe kama tumbili, matatizo kuyaruka,
ongea na wako mwali, dawa yake si kutoka,
huu ushauri bure, mapenzi si mashindano.

kichwa dogo wa tumia, nje unaenda kuruka,
kinga usipotumia, mapema utakauka,
mwishoni utajutia, matatizo yashafika,
huu ushauri bure, mapenzi si mashindano.

eddy tabaki mkiwa, ubabe kiendekeza,
kamwe hutofanikiwa, kwa ubabe nadokeza,
mengi umeshaambiwa, mebaki kutekeleza,
huu ushauri bure, mapenzi si mashindano.

heri kelele hekima, kuliko liwazo ovu,
na bora ukayapima, usisubirie makovu,
nyumba ndogo sio dawa, kidogo kuwa mwelevu,
huu ushauri bure, mapenzi si mashindano.


No comments:

Post a Comment